Feb 17, 2012

Serikali itamke wazi kuwa imeshindwa kudhibiti udanganyifu katika mtihani

Katibu Mtendaji wa NECTA, Dk. Joyce Ndalichako

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI karibuni Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kumaliza sekondari mwaka jana 2011, ambao watahiniwa 3,303 wamebainika kuufanya kwa zaidi ya mara 10 ya mwaka juzi, hali inayotufanya tuamini kuwa udanganyifu huu umekuwa gonjwa lililokosa tiba kwa serikali yetu.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk. Joyce Ndalichako, alisema kuwa Baraza limefuta matokeo ya watahiniwa hao, ambao kati yao, 3,301 ni wa Mtihani wa Kidato cha Nne na wawili ni wa Maarifa (QT). kila mwaka msamiati huu wa udanganyifu umeendelea kutawala, si tu kwa matokeo ya kidato cha nne, bali hata darasa la saba au kidato cha sita. Hii inatufanya tuingiwe na wasiwasi kwa kuwa hawa waliohusika ndiyo watakaokuwa viongozi wa kesho, je, tutegemee nini kutoka kwa serikali watakayoiongoza?

Kila mwaka, nyakati kama hizi wakati matokeo ya mtihani kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya sekondari yanapotangazwa huambatana na baadhi ya wanafunzi kushangilia hali wengine wakibaki wameduwaa. Matokeo hayo huleta huzuni kwa walio wengi ambao hawakupata matokeo mazuri. Pia hili suala la baadhi yao au shule kadhaa kufutiwa matokeo kwa sababu za udanganyifu katika mtihani limekuwa ni sehemu ya matokeo hayo. Binafsi sishangai kila linaposikika.

Limekuwa la kawaida kwa kuwa matokeo haya hutumika kuwakejeli watoto wa mafukara na wazazi wao kwa kuwa wamewekwa kando na mfumo wa kijamii – kiuchumi unaowapendelea, kuwajenga na kuwaendeleza wachache huku ukiwapuuza, kuwachuja na kuwatupa walio wengi.

Mfumo wa kijamii – kiuchumi nchini umejengwa kitabaka, hautumiki kuleta usawa katika jamii bali unatumika kuzidisha tabaka kati ya matajiri na masikini. Enzi za Mwalimu Nyerere, matarajio na malengo ya mfumo wa elimu ilikuwa kwanza kupiga vita ujinga. Lengo lilikuwa kuhakikisha kila Mtanzania anajua kusoma na kuandika ili kuweza kujitegemea.

Huo ndio ulikuwa msingi ambao ulijengwa na Serikali ya Awamu ya Kwanza. Baada ya Mwalimu, awamu zilizofuata zilipaswa kuendeleza mambo muhimu yanayohitajika katika mfumo wa elimu bora. Hivi sasa tunajivuna kutimiza miaka 50 ya Uhuru, lakini bado hatujautazama upya mfumo wetu wa elimu unamsaidiaje Mtanzania wa karne hii ya sayansi na teknolojia, ikiwa ni pamoja na kutafuta tiba hii ya udanganyifu katika mitihani.

Hivi tunadhani tunajenga taifa la aina gani,
kama kila mwaka tutaendelea kushuhudia “maafa” haya ya udanganyifu kwa vijana ambao tunataraji siku moja watakuwa viongozi wa nchi hii? Hivi hata huu mfumo tulionao unamjengaje kijana wa Kitanzania kushindana na kijana wa Kikorea, Kihindi au Kimexico kama si kuhamasisha wizi wa mitihani?

Kwa mujibu wa Dk. Ndalichako, kama alivyonukuliwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu aina za udanganyifu, alisema kuwa ni pamoja na wanaokamatwa na wasimamizi ndani ya chumba cha mitihani wakiwa na ‘notes’, wanaofanyiwa mitihani na watu wengine, wanaosajiliwa kufanya mitihani kwa kutumia majina ya wengine wakati walishafanya mtihani na wanaokuwa na karatasi za majibu zenye miandiko tofauti au kuwa na miandiko tofauti katika karatasi ya somo moja.

Nyingine ni kubadilishana karatasi za maswali/vijitabu vya kujibia mtihani ili kuandikiana majibu, au kujadiliana ndani ya chumba cha mtihani, watahiniwa kukamatwa na booklet zaidi ya moja ambapo booklet moja hawakupewa na msimamizi na watahiniwa kubainika kuwa na kesi mbili tofauti; kama vile mfanano wa majibu, notes, kijitabu cha kujibia zaidi ya kimoja na kubadilishana karatasi za majibu au kijitabu cha kujibia mtihani.

Yote haya yanasababishwa na mfumo tulionao unaoangalia zaidi matokeo ya mtihani na si uelewa, huku tukitumia mfumo wa miaka saba ya elimu ya msingi, miaka mine ya sekondari na miwili ya sekondari ya juu kabla mwanafunzi hajakanyaga chuo chochote kupata mafunzo anayoweza kuyatumia.

Kwa maana hiyo, kijana anatumia miaka 13 akiwa hana ujuzi wowote! Je, katika miaka hii 13 anakuwa ameandaliwa kushindana na vijana wenziwe kutoka nchi nyingine kama hatafanikiwa kuingia chuo chochote?

Na huu mfumo wa mtoto kuanza elimu ya msingi akifundishwa masomo yote kwa Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza kwa miaka yote saba, kisha anapoanza sekondari masomo yote kufundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili hatudhani kuwa ndiyo chanzo cha udanganyifu huu, kwa kuwa unayafanya masomo kuwa magumu zaidi na yasiyoeleweka kwa wanafunzi? Hatuoni kuwa mwanafunzi kujifunza mambo mageni kwa lugha ya kigeni ndiyo sababu ya wizi huu?

Mimi naamini kuwa mfumo huu unazalisha vijana wenye uwezo wa juu wa kukariri na si vijana wenye uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo. Kama matarajio yetu ni kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitihani, basi tumepiga hatua kumi kurudi nyuma kwa kuwa kijana wa Kitanzania huandaliwa ili afanye mtihani, na hii ndiyo sababu ya udanganyfu tunaoulalamikia kila mwaka!

Tangu lini ubora wa elimu ukapimwa  kwa kushindanisha shule zipi zinatoa wanafunzi wengi wa daraja la kwanza, na si shule zipi zinatoa wanafunzi wenye uwezo wa juu wa kufikiri na kuchambua mambo?

Badala ya kuwapa watoto elimu ya kuwafanya wajitambue na kuendeleza vipawa vyao tunatumia muda mwingi kuwafanya wafaulu mitihani kitendo kinachohamasisha wizi wa mitihani. Mfumo wa kutathmini vipawa vya watoto kwa mitihani ya siku chache katika kipindi kirefu cha masomo hautufai na ndiyo sababu ya udanganyifu huu. Hivi hili serikali hailioni?

Nadhani sasa wakati umefika serikali iamue moja; kubadilisha mfumo wa elimu na kuwawajibishwa na kuwachukulia hatua kali wote waliohusika, au itangaze kuwa imeshindwa katika vita hii.

No comments:

Post a Comment