Rais wa Senegal, Abdoulaye Wade
RAIS wa Senegal, Abdoulaye Wade, mwenye umri wa miaka 85 sasa na akiendelea kuongoza taifa hilo kwa miongo kadhaa anajiandaa kugombea tena kwa kipindi cha tatu baada ya uamuzi wa Mahakama Kuu kutolewa. Hukumu hiyo imesababisha vyama vikuu vya upinzani kufanya maandamano makubwa ya kupinga hatua ya Rais Wade kugombea nafasi yake kwa kipindi cha tatu mfululizo.
Jopo la Majaji watano ndilo lililoamua hatima ya Rais Wade kwenye harakati za kusaka kuwania kiti hicho kwa mara nyingine huku shinikizo kubwa likitaka kiongozi huyo asuruhusiwe kuvunja katiba.
Rais Wade amewasihi wananchi ambao wameonekana kukerwa na kitendo chake cha kuendelea kutaka kusalia madarakani, wawe watulivu baada ya maandamano ya ghasia kuzuka kufuatia uamuzi wa mahakama kutoa uamuzi wake. Rais Wade alisema kuonesha hasira kwa fujo hakutaleta tija yoyote.
Alitokeza kwenye televisheni huku ghasia zikiwa zinatapakaa katika miji kadhaa ya Senegal . Katika mji mkuu, Dakar , vizuizi viliwekwa, magari yalipinduliwa na maduka kadhaa yalichomwa moto. Kuna taarifa za askari polisi kuuawa.
Mpinzani maarufu wa Wade, mwimbaji Youssou N'Dour, ameonya kuwa hukumu ya Mahakama ya Katiba haitakubalika. Mahakama hayo yalitupilia mbali ombi la Youssou N'Dour kutaka kugombea urais katika uchaguzi wa mwezi ujao. Uchaguzi wa Senegal unatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu ambapo ndiyo hatima ya uongozi nchini humo utabainika.
Historia yake
Abdoulaye Wade amezaliwa Mei 29, 1926, ingawa baadhi wanadai alizaliwa miaka kadhaa nyuma. Ni rais wa tatu wa Senegal , aliyeingia madarakani mwaka 2000. Pia ni Katibu Mkuu wa Chama cha Kidemokrasia cha Senegal (PDS) alichokiongoza tangu kilipoanzishwa mwaka 1974. Amekuwa kiongozi wa muda mrefu wa upinzani, akiwa amewania urais mara nne, kuanzia 1978, kabla ya kuchaguliwa mwaka 2000.
Maisha kabla ya siasa
Wade alizaliwa katika eneo la Kebemer nchini humo. Alisoma na kufundisha sheria katika Shule ya Lycee Condorcet nchini Ufaransa. Ana shahada mbili za udaktari katika sheria na uchumi. Alikuwa pia Mkuu wa Kitivo cha sheria na uchumi katika Chuo Kikuu cha Dakar nchini Senegal . Amemuoa Viviane Wade mwenye asili ya Uzungu.
Mtoto wao wa kiume, Karim Wade, alikuwa mkuu wa zamani wa wakala wa Taasisi ya Kitaifa ya Kiislam na alifanya kazi tangu Mei 2009 kama Waziri wa Ushirikiano wa Kimataifa, Mipango Miji na Mikoa, Usafiri wa Anga, na Miundombinu. Binti yao , Sindjely Wade, ni Msaidizi Maalum wa Rais ambaye alishiriki katika mikutano ya kampeni mingi ikifanyika Paris na Dakar .
Kazi ya siasa
Katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Nchi Huru za Kiafrika (OAU) mjini Mogadishu, mwaka 1974, Wade alimwambia Rais Leopold Senghor Sedar kwamba alitaka kuanzisha chama kipya, na Senghor alikubali. PDS ilianzishwa tarehe 31 Julai 1974. Chama ambacho awali kilikuwa na lengo la Uliberali mwaka 1976 kutokana na kuanzishwa kwa sheria ya kuruhusu kuwepo kwa vyama vitatu tu na itikadi tofauti tatu, mbili zilichukuliwa na vyama vingine (uliberali ndo' chaguo pekee lililobakia).
Wade aliwania urais mwezi Februari 1978 dhidi ya Senghor, na kupata asilimia 17.38 ya kura. Pia mwaka huo, Wade alichaguliwa kuwa mbunge, alioutumikia hadi 1980. Aliwania pia urais katika uchaguzi wa 1983 na 1988 na kuchukua nafasi ya pili kila wakati, nyuma ya mrithi wa Senghor wakati huo, Abdou Diouf. Kufuatia uchaguzi wa 1988, alikamatwa kutokana na maandamano na alisimamishwa asigombee. Baada ya hapo alikwenda Ufaransa na kurudi mwaka 1990.
Mwezi Aprili 1991, Wade na wanachama wengine wanne wa PDS walijiunga na serikali ya umoja wa kitaifa pamoja na chama tawala cha Kisoshalisti (PS); Wade akawa Waziri wa Nchi asiye na wazara maalum. Oktoba 1992, yeye na mawaziri wengine wa PDS walijiondoa serikalini kutokana na malalamiko kuhusu namna ambayo PS ilikuwa ikiidhibiti serikali. Katika uchaguzi wa rais wa Februari 1993, Wade alikuwa wa pili tena, akiwa na asilimia 32 ya kura, nyuma ya Diouf, aliyeshinda kwa asilimia 58.
Kufuatia mauaji ya Makamu wa Rais wa Baraza la Katiba Mei 1993, Babacar Seye, Wade, pamoja na viongozi wengine wa PDS , walihojiwa na polisi. Oktoba 1, Wade, mke wake, na wabunge wawili wa PDS (Abdoulaye Faye na Ousmane Ngom), walishtakiwa kwa makosa ya mauaji, ingawa hawakuwa chini ya ulinzi au kufunguliwa kesi. Kufuatia maandamano mwezi Februari 1994, Wade alikamatwa pamoja na wengine wengi kwa tuhuma za kutishia usalama wa serikali. Mashtaka ya kushiriki katika mauaji ya Sèye yakafutwa Mei 1994, na Wade na washitakiwa wenzake walianza mgomo wa kutokula mnamo Juni 30. Yeye na washitakiwa wenzake waliachiwa Julai 4, na mashtaka yaliyosalia yalifutwa mnamo Agosti 30, 1994.
Wade alijiunga tena na serikali kama Waziri wa Nchi mwezi Machi 1995, lakini yeye na mawaziri wengine wa PDS walijiondoa tena Machi 1998. Ingawa alichaguliwa katika Bunge la Taifa katika uchaguzi wa Februari 1998 wa bunge, alitangaza kujiuzulu katika Bunge la Taifa mwishoni mwa Julai 1998, akisema kuwa kulikuwa na "wasaidizi wa kutosha kufanya kazi katika nafasi yangu".
Uchaguzi wa 2000 na muhula wa kwanza
Wade aliishi kipindi cha mwaka nchini Ufaransa, na kurejea tena Senegal tarehe 27 Oktoba, 1999. Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais 2000, uliofanyika Februari 27, alikuwa katika nafasi ya pili tena, kwa kupata asilimia 31 ya kura, lakini kwa mara ya kwanza, Diouf hakuwa amefikia asilimia zinazomfanya atangazwe mshindi katika raundi ya kwanza, hivyo mzunguko wa pili ulifanyika Machi 19. Wade alishinda kwa asilimia 58.49 ya kura, baada ya kuungwa mkono na wagombea kutoka duru ya kwanza, ikiwa ni pamoja na mgombea aliyeshika nafasi ya tatu, Moustapha Niasse. Wade akawa Rais tarehe 1 Aprili, 2000, na kumteua Niasse kuwa Waziri Mkuu wake muda mfupi baadaye.
Katiba mpya ilipitishwa mwaka 2001, na kupunguza kipindi cha urais kuwa miaka mitano baada ya Wade kukamilisha muda wake wa miaka saba mwaka 2007.
Uchaguzi wa 2007 na awamu ya pili
Oktoba 15, 2006, Wade aliteuliwa kuwa mgombea urais wa PDS kwa uchaguzi wa urais wa Februari 2007. Mmoja kati ya wapinzani wa Wade katika uchaguzi huu alikuwa waziri mkuu wake wa zamani, Idrissa Seck, ambaye mwanzoni alichukuliwa kuwa mfuasi wa Wade, lakini alikamatwa mwaka 2005. Matokeo ya mwisho yaliyotolewa Machi 11, 2007, yalionesha Wade kashinda katika raundi ya kwanza kwa asilimia 55.9 ya kura, kwa mbali dhidi ya wapinzani wake wa karibu, Seck asilimia 15 na kiongozi wa Socialist Party, Ousmane Tanor Dieng, asilimia 13.6. Dieng na mgombea mwingine wa upinzani, Abdoulaye Bathily, walikata rufaa kuhusu uchaguzi, lakini ilikataliwa na Baraza la Katiba. Wade aliapishwa kwa kipindi chake cha pili mnamo Aprili 3 katika Uwanja wa Leopold Sedar Senghor jijini Dakar , na viongozi wengi wa Afrika na watazamaji 60,000 walihudhuria.
Vyama vikuu vya upinzani havikukubali ushindi wa Wade wa mwaka 2007 na kuhoji uhalali wake kama Rais; waligomea uchaguzi wa Bunge la Taifa na Seneti baadaye mwaka huo. Wade alihitimisha kwa kusema katika mahojiano yaliyochapishwa na ‘Le Soleil’ mnamo Mei 19, 2008, kwamba hakukuwa tena na uwezekano wa mazungumzo na upinzani isipokuwa kwanza atambuliwe kama Rais halali. "Waacheni wafanye wanachotaka, hainisumbui," alisema, "mradi tu waheshimu sheria na utaratibu."
Julai 2007, Umoja wa Afrika katika mkutano wa kilele mjini Accra , Ghana , Wade aliunga mkono kuundwa haraka kwa mapendekezo ya Umoja wa Afrika na alisema: "Kama tunashindwa kuungana, tutakuwa dhaifu, tukiishi kila nchi pekee yake katika nchi ambazo zimegawanywa, tutakabiliwa na hatari ya kuangukia katika nchi kubwa zilizoungana kiuchumi".
Uchaguzi wa 2012 na awamu ya tatu
Julai 2008, Bunge la Taifa lilipitisha mabadiliko ya katiba na kuongeza muda wa urais kwa miaka saba, kama ilivyokuwa kabla ya kupitishwa kwa katiba ya mwaka 2001. muda huu hautahusu kipindi cha uongozi wa Wade cha 2007-2012, lakini Waziri wa Sheria, Madické Niang, alisisitiza kuwa Wade ana uwezekano wa kugombea uchaguzi wa mwaka 2012 kama bado ana afya. Baadaye, Septemba 17, 2009 Wade alithibitisha kuwa alipanga kugombea awamu ya tatu mwaka 2012 "kama Mungu atanipa maisha marefu". Wade, katika hotuba ya 14 Julai 2011 kwa wafuasi, alitumia lugha ya Wolof “Ma waxoon waxeet” (nilisema, naweza kugombea tena) katika kueleza uamuzi wake wa 2007 wa kutogombea kwa kipindi kingine.
Januari 27, 2012 Abdoulaye Wade alipitishwa rasmi na Baraza la Katiba (linalojumuisha majaji wakuu watano) kugombea kwa muhula mwingine wenye utata wa tatu na wa mwisho. Kufuatia tamko hili, hasira za umma ziliwatuma kushiriki katika maandamano. Pia kumekuwepo na taarifa kuwa Wade ni mwanachama wa Freemason.
Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.
No comments:
Post a Comment