Feb 15, 2012

Kwa kudharau Kiswahili tutaendelea kuwa wasindikizaji

Mwalimu Julius Nyerere, alikipigania Kiswahili ambacho kwa sasa kinapuuzwa

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

“VIONGOZI wamekuwa wakitupiga fiksi miaka yoote, ooh Kiswahili lugha ya taifa, ooh tujivunie Kiswahili, ooh tukienzi… Haya sasa nimejifunza Kiswahili kwa bidii na cheti nimekipata. Nakaa nasubiri kazi, matangazo yote kwenye magazeti yetu yanatoka kwa Kimombo. Kina fulani wanapata kazi, mimi naambiwa …we need English!...” Kijana mmoja anawaeleza wenzake walipokuwa kijiweni.

“Acha mambo yako, Wabongo ndivyo mlivyo, mnapenda kulalamika wakati nyinyi wenyewe hamtaki hata kujishughulisha! Nafasi zipo lakini hamzitumii matokeo yake mnalalamikia Kiswahili, kinahusiana nini na hayo?” kijana mwingine anaingilia kati.

“Hivi wewe uko nchi gani?” anajibu kwa ghadhabu yule kijana wa kwanza, “Tujishughulishe vipi? Ina maana huoni kinachoendelea nchini? Wamekuwa wanatuongopea eti Kiswahili ndiyo lugha ya taifa wakati wao wanapeleka watoto wao Ulaya na kwenye shule za English Medium, si hivyo tu hata tenda zote nzito nzito kwenye magazeti zinaandikwa kwa Kiingereza. Nasikia hata Kanumba alipokwenda kule Big Brother alienda huku akiwa anajivunia lugha yake ya Kiswahili, unajua nini kilichotokea? Akaambiwa …we need English

“Kweli bradha, Watanzania sasa tumeshtuka, tena tumeshtuka ile mbaya. Hizi fiksi tumegundua zinatulostisha kabisa. Wengi wameshtuka sasa, ndiyo maana hata huku Uswahilini sasa hivi shule zenye majina kama Tujitegemee, Tuungane, Umoja au Mwongozo huzikuti. Na ukizikuta ujue hazina tena soko. Usishangae siku hizi kusikia shule kama Santa Paul ya Manzese, New World Academy ya Gongolamboto, Galaxy International School ya Kiwalani na nyingine kibao… tumeshtuka!” Alidakia kijana mwingine.

Haya ni baadhi ya mazungumzo kwenye kijiwe kimoja huku mtaani kwetu niliyobahatika kuyanasa wakati nikipita eneo hilo. Ingawa niliyachukulia kama mzaha tu wa vijana wasio na kazi wanaopenda kulalamika, lakini yameendelea kujirudia akilini mwangu kiasi kwamba nadhani ni muhimu ikawekwa wazi ili Watanzania tuufahamu ukweli.

Inaeleweka kabisa kuwa kila nchi ina lugha yake ya taifa, lugha ambayo inatumika katika shughuli zote za kiserikali. Mfano mzuri ukienda Kenya, lugha yao ya taifa ni Kiswahili na Kiingereza na ndio maana katika shughuli zote za mambo ya serikali, wanatumia lugha hizo za Kiingereza na Kiswahili. Ukienda hospitali, mahakamani, shule na hata katika vyuo vya elimu ya juu, lugha inayotumika ni Kiingereza tu.

Hebu tujiulize hapa kwetu Tanzania ni ipi ni lugha ya taifa? Kila mara napata wakati mgumu, ninapoona viongozi wakichanganya lugha - yaani Kiswahili na Kingereza (Kiswanglish au Kiswakinge)!

Lugha ni utambulisho wa jamii na kwa kutumia lugha watu hupashana habari, hujenga uhusiano kwa kufahamiana, kuelimishana na kupatana au kufarakana. Lugha ndiyo njia kuu ya mawasiliano. Ni sehemu ya utamaduni, ni amali ya jamii inayoizungumza na ina alama ya umoja wa kitaifa. Kwa kweli suala la mila na utamaduni wetu huwa linachanganya kidogo. Tunapoongelea utamaduni na mila za Watanzania katika Tanzania yenye zaidi ya makabila 120 ambayo kila moja lina mila na utamaduni wake, tujiulize utamaduni na mila za Watanzania ni zipi?

Hapa ndipo Serikali na Watanzania wote kwa ujumla wetu tunapokuwa na jukumu la kuhakikisha tunalinda tamaduni zetu na kuwa urithi bora kwa vizazi vijavyo nao wataposherekea miaka mia moja ya uhuru wawe na vitu cha kujivunia kutoka kwenye jamii yao ya asili. moja ya vitu hivi ni lugha ya Kiswahili.

Ieleweke kuwa maendeleo ya sekta zote, yawe ni maendeleo ya kiuchumi, kisiasa, kijamii na kitamaduni yanahusisha lugha katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku. Hivyo sekta zote zinapaswa kuhimiza matumizi ya Kiswahili, iwe ni kwa mazungumzo au kwa maandishi.

Kwa njia ya lugha, maisha ya jamii yanaakisiwa na kuifanya kuwa kioo cha jamii, bila lugha ingekuwa vigumu kuurithisha utamaduni wa kizazi kimoja hadi kingine. Kwa maana hiyo, Kiswahili kitaendelea kuwa kielelezo cha utamaduni wa Watanzania na njia kuu ya mawasiliano ya wanajamii wa Tanzania. Tunapaswa tukitunze na kukienzi badala ya kuendelea kupiga porojo kuwa ni lugha ya taifa wakati hatukithamini.

Kiswahili ni lugha ambayo ni kielelezo cha ndani cha jamii ya Watanzania, kimekuwa kikitumika kuelezea mila na desturi ambazo ni nguzo muhimu za utamaduni wa Tanzania. Utamaduni (kupitia lugha) ni kielelezo cha uhai na utashi wa taifa na ni mama na baba wa sekta nyingine za jamii; siasa na uchumi. Lugha ni nyenzo muhimu sana katika kuuelezea utamaduni wa Taifa kwani haiwezi kuwa utambulisho wa taifa bila kuelezea utamaduni wake.

Ni ukweli ulio dhahiri kuwa lugha ya taifa hapa nchini ni Kiswahili, lakini cha ajabu watu hawakitumii inavyostahili, kutokana na madai eti wakiongea Kiswahili, wataonekana si wasomi! Hii imedhihirishwa hat kwa watunga sera wetu kwa kuandaa sera na mambo muhimu (sheria, kanuni) yanayomgusa mwananchi wa kawaida kwa Kingereza badala ya Kiswahili.

Kama walivyokuwa wakisema vijana wa kijiweni huku mtaani kwetu, Kiswahili kimekuwa hakipewi umuhimu, ingawa ndio lugha ya taifa; na badala yake hata viongozi wamekuwa na tabia ya kuchanganya Kiswahili na Kingereza! Hali hii imeigwa na wasanii wa filamu ambako sasa kuchanganya Kingereza na Kiswahili limekuwa jambo la kawaida.

Wasomi wetu, imekuwa ni jambo la kawaida kuchanganya Kiswahili na Kingereza, Wakiamini kufanya hivyo ni kujitambulisha katika jamii, kuwa wao ni wasomi wa elimu ya juu! Wakisahau kuwa Kiingereza ni kama lugha zingine tu, na kujua Kingereza haimaanishi kuwa wewe ni msomi, kwani Kingereza ni lugha kama Kijita, Kingoni au Kizaramo, tofauti yake ni kwamba lugha hii inazungumzwa na Wazungu! Kwa nini hatutaki kujifunza toka nchi za dunia ya kwanza kama China ambao lugha yao imewasaidia katika maendeleo? Unapokwenda kusoma China ni lazima ufahamu lugha ya Kichina na utafundishwa kwa lugha hiyo.

No comments:

Post a Comment