Jan 27, 2012

Kinachotafutwa ni vazi la taifa au kitambaa cha taifa?

Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi akiwa na wajumbe wa kamati ya kutafuta vazi la taifa, ofisini kwake jijini Dar es Salaam

 Wa-Nigeria wanaopigiwa mfano


Wanawake wa Kimasai wakiwa katika mavazi rasmi ya kabila lao

BISHOP HILUKA

Dar es SalaamWIKI iliyopita katika kituo kimoja cha televisheni nilishuhudia mdahalo kuhusu vazi la taifa, mdahalo ulinivutia kiasi cha kuamua kuandika makala hii. Hoja zilizotolewa katika mdahalo huo na nyingine ambazo nimekuwa nikizisikia zimeshindwa kunishawishi kukubaliana na hiki kinachoitwa vazi la taifa. Hoja hizo zimeniacha na maswali kadhaa ambayo ningependa wahusika wajitokeza kuyatolea ufafanuzi ili kutushawishi wote wenye mashaka kama yangu.Mtaniwia radhi kama nitaonekana si mzalendo, lakini mimi pia nina mtazamo wangu katika jambo hili. Mwanzoni nilidhani kinachotafutwa ni vazi la taifa, lakini siku chache hata kabla ya mdahalo huo nilishangazwa na kauli za wahusika wakuu wa mchakato huu kuhusu mwenendo mzima wa kupata kile kinachoitwa vazi la taifa. Wahusika hao, kwa nyakati tofauti nimewasikia wakiongelea aina ya kitambaa, ubora wake na rangi gani inafaa!Hapa pana mkanganyiko, wanaposema eti kitambaa kitakuwa na ubora tofauti kulingana na hadhi ya mvaaji, wakitolea mfano wa wabunge, ambao wanaweza kuchagua suti waipendayo kutokana na kitambaa hicho! Kumbe mawazo yao yamejikita kwenye kitambaa na ubora wa kitambaa na si vazi kama dhana nzima ilivyoelezwa mwanzo! Je, kwa wananchi wengi, hususan vijijini ambao hawamudu bei za vitambaa madukani na kimbilio lao kubwa ni mitumba tunawaambia nini? Pia hapa sijajua, hoja ni vazi au kitambaa cha taifa?Hata hivyo, vazi la taifa halitafutwi na halijawahi kutafutwa! Wamasai walitafutiwa na nani? Au hizo nchi zinazotolewa mfano; Ghana, Nigeria, Afrika Kusini au China hawajawahi kuwa na kamati ya kutafuta vazi. Kwanza si kweli kwamba wana mavazi ya taifa, hayo tunayodhani kuwa ni ya taifa ni mavazi yanayovaliwa na makabila makubwa. Nina wasiwasi kwamba tutatumia pesa nyingi katika kitu kisicho na tija kwa maana kuwa mwisho wa mchakato vazi halitakuwepo.Sikubaliani na sababu zinatolewa eti vazi hili litazidisha uzalendo, litaleta maendeleo, litatangaza utamaduni, vivutio na utambulisho wa nchi! Nijuavyo, vazi la taifa kama ni utamaduni basi utamaduni hauundiwi mezani kama tunavyotaka kuaminishwa.Ieleweke kuwa lengo la makala hii ni kutoa changamoto na kuibua mjadala zaidi katika kuangalia namna nzuri ya kurudisha maadili, uzalendo na kuutangaza utamaduni wetu katika kazi za sanaa na changamoto zinazotukabili juu ya namna ya kukuza au kudhibiti wimbi la mapokeo ya sanaa zinazokiuka mila, desturi na maadili yetu ya Ki-Tanzania, badala ya kufikiria kuwa kitambaa pekee kitatusaidia.Hebu tujiulize ni nchi gani duniani ambayo kuendelea au kutokuendelea kwake kumetokana na kuwa ama kutokuwa na vazi la taifa? Je, ni kitu gani cha muhimu ambacho kama taifa tumekikosa kwa miaka 50 kwa sababu ya kutokuwa na kipande cha nguo kinachoitwa vazi la taifa? Ni kweli uzalendo umepungua nchini kwa sababu ya kukosa vazi la taifa? Je, vazi la taifa ni sawa na vazi la heshima ambalo ndicho kitu cha msingi sana kama tunaangalia udumishaji wa mila?Nafikiri tuna changamoto nyingi ambazo hata tukileta hilo vazi haliwezi kuziondoa, tunapaswa kukabiliana na mmomonyoko wa maadili kwenye jamii yetu ambao unaletwa na utamaduni tunaoiga toka nje, huku wizara inayoratibu mchakato wa kitambaa kinachoitwa cha taifa ikiwa kimya na haijawahi kuunda kamati kuushughulikia. Tunashuhudia mmomonyoko mkubwa katika jamii hii, kupitia nyimbo za matusi, filamu na nyimbo za mapenzi au zisizo na asili yetu zilizonakili vitendo na maudhui ya jamii za nje. Je, wizara husika iko wapi katika hili?Sanaa kama nguzo muhimu ya utamaduni hukua na pia hufa. Hivi sasa sanaa zetu zipo katika chumba cha wagonjwa mahututi na tusipochukua juhudi za ziada tutazika uasili wa sanaa zetu tulizoachiwa na wazee wetu zilizodumu kizazi hadi kizazi. Hili linazigusa sanaa zote kuanzia filamu, muziki, sanaa za maonesho na kazi za mikono. Ni kweli njia tunayoenda nayo katika kazi zetu za sanaa inatupeleka kwenye msingi wa waliotutangulia au tumepotea na wimbi la utandawazi? Je, hili vazi litasaidiaje kuzifanya sanaa zetu zisife?Tuna tatizo kubwa la maadili katika sanaa na udhibiti wa kazi chafu, jambo ambalo limekuwa gumzo. Mbona wizara haijawahi kuandaa kamati ya kutafuta alama ya muziki wetu? Mbona haitafuti alama ya filamu au chanzo cha wasanii kuiga filamu zisizo na maadili? Au mbona ubunifu wa mitindo yetu ya kucheza muziki wetu na sanaa nyinginezo ni wa kuiga? Kwa nini vazi la taifa?Nimewahi kusoma kuwa fani ya muziki inaporomoka kwani wanamuziki walio wengi wamepotea njia kwa kutofuata miiko katika tungo zao, miundo, mitindo na maudhui kulingana na uasili, mila, desturi, mapokeo, historia na urithi tulioachiwa. Haya yote yakiwa yanaashiria kuporomoka kwa fani hii.Kadri muda unavyozidi kwenda tunawapoteza wapiga ala kama ngoma, marimba, zeze, Saxophone na kadhalika, huku idadi lukuki ya waimbaji bandia wasio na msingi na kanuni za fani ya uimbaji na utunzi wakiongezeka na kusababisha muziki wetu kuchuja katika muda mfupi, hapo hapo teknolojia ikimaliza vipaji vya wapiga ala kwa kuwa kila ala siku hizi ipo studio kwenye mashine (computer). Mbona wizara haiundi kamati kunusuru hili?Tumekuwa mahodari wa kushabikia sanaa za kutoka nje ya nchi. Kuanzia kwenye jamii hadi ngazi ya taifa, jambo linalotufanya kuwa wasindikizaji kwa kupokea sanaa na mitindo toka nje. Haya yanajitokeza katika fani za unenguaji, filamu, muziki wa injili na hata fani nyinginezo za sanaa. Bila kujua tumekuwa tunapandikiza mbegu mbaya katika jamii kwa kutopenda cha kwetu. Je, katika mazingira haya uzalendo na moyo wa kuipenda nchi utabadilishwaje na kitambaa tunachoita vazi la taifa?Mwisho, tujiulize maswali haya; je, vipaumbele vyetu kama taifa ili kujiletea maendeleo na kudumisha maadili ni muhimu kuwa na vazi la Taifa leo? Tunapoangalia ubora na rangi ya vitambaa katika nchi hii ya wavaa mitumba, je, serikali kupitia wizara husika haikuona umuhimu wa kuunda kwanza tume ya kusaidia wakulima wa pamba ili pamba yao iwe katika kiwango bora badala ya kukimbilia kuunda tume ya kutafuta vazi la Taifa?Je, kuna mkakati gani hadi sasa wa kuongeza thamani ya pamba yetu ili tuiuze kama malighafi nje ya nchi? Kwa nchi ambayo haina viwanda vya nguo, leo tunaunda tume ya kutafuta vazi la Taifa, hivi kama vazi hilo likipatikana ni kiwanda gani hapa nchini kitashona nguo hizo za vazi linaloitwa la Taifa? Au tutaanza tena mchakato wa kutafuta mzabuni wa kutushonea nguo katika nchi kama China, India, Pakistani na kwingineko?


Naomba kuwasilisha…


LEON MUGESERA: Mtuhumiwa wa mauji ya kimbari aliyerudishwa Rwanda baada ya kukwepa kwa zaidi ya miaka 16

Leon Mugesera

QUEBEC
Canada

MTUHUMIWA wa mauji ya kimbari, Leon Mugesera, aliyekuwa anahitajika sana nchini Rwanda kwa madai ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu yenye uhusiano na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambayo yalishuhudia ukatili mkubwa ulioongozwa na Wahutu kwa mamia ya maelfu ya watu, hasa wa kabila la Watutsi.

Madai ya uchochezi yanahuswa na hotuba ya Mugesera aliyoitoa mwaka 1992 akitoa wito kwa Wahutu kuwaondoa nchini Rwanda Watutsi, aliowaita "mende."

Serikali ya Canada imeamua kumrudisha Rwanda mtuhumiwa huyo wa mauji ya kimbari. Mahakama hiyo ya Canadian imekataa ombi la rufaa kutoka kwa mshukiwa huyo aliyepinga kurudishwa nchini Rwanda akisema kuwa hatapata haki nchini huko.

Mugesera ambaye anakabiliwa na mashtaka hayo ya kutoa matamshi ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu, inasemekana alitoa hotuba ya kichochezi mwaka 1992, mbele ya wanachama wa kilichokuwa chama tawala cha wahutu (MRND), na anadaiwa kusema kwamba Watutsi wanapaswa wauawe huku akiwaita 'mende'.

Mwenyewe amekanusha madai hayo akisema kuwa matamshi yake yametafsiriwa vibaya. Mugesera, mwanataaluma na mwanaharakati wa kisiasa ambaye alikuwa akiishi katika jiji la Quebec, alipigania bila mafanikio kwa muda wa miaka 16 katika mahakama kadhaa - ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu ya Canada mwaka 2005 - ili kuepuka kurejeshwa nchini Rwanda.

Kufuatia hukumu, ambayo mahakama ilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Mugesera ndiye alichochea mauaji dhidi ya Watutsi, hatimaye serikali ya Canada mnamo Novemba mwaka jana ilipitisha uamuzi wa kufukuzwa kwa Mugesera.

Wakili wa Mugesera alikuwa ameomba apewe muda zaidi ili Kamati ya Umoja wa Mataifa inayopinga vitendo vya unyanyasaji na mateso ichunguze kwanza na itoe hakikisho kuwa hatapatwa na kadhia hiyo akiwa Rwanda lakini mahakama ilitupilia mbali ombi hilo. Mugesera na wanasheria wake walisema kuwa atateswa au kuuawa kama atarudishwa Rwanda na kupambana na kesi hiyo, kwa vile yeye ni adui wa Rais Paul Kagame. Wameonesha shaka katika utawala wa nchi hiyo wa sheria au uwezo wa Mugesera wa kupata hukumu ya haki mbele ya mahakama nchini humo.

Serikali ya Rwanda imefurahishwa na uamuzi huo.

Historia yake

Leon Mugesera amezaliwa mwaka 1952, ni mzaliwa wa Rwanda, ambaye alikuwa anaishi katika jiji la Quebec, Canada tangu mwaka 1992, kabla hajatakiwa kuondoka nchini Canada kwa sababu ya kesi inayomkabili ya uchochezi dhidi ya Watutsi kutokana na hotuba yake ambayo wakosoaji wanadai ndiyo iliyochochea mauaji ya kimbari nchini Rwanda ya 1994.

Akiwa Rwanda

Mugesera wa kabila la Kihutu, amekuwa mwanachama wa chama kikubwa cha Kihutu cha MRND, ambacho kilikuwa na mahusiano ya karibu zaidi na jeshi la nchi hiyo. Alikuwa Makamu Mwenyekiti wa MRND katika mkoa wa Gisenyi.

Katika hotuba yake iliyotolewa Novemba 22, 1992 nchini Rwanda, inadaiwa Mugesera aliwaambia wanachama 1000 wa chama chake kwamba "sisi watu wa Kabila la Hutu tuna wajibu wa kuchukua jukumu wenyewe na kufuta hili povu" na kwamba wanapaswa kuwaua Watutsi na "kuitupa miili yao katika mito ya Rwanda". Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Kufuatia hotuba hii, Waziri wa Sheria wa Rwanda wakati huo, Stanislas Mbonampeka, alitoa kibali cha kukamatwa dhidi ya Mugesera kwa kuchochea chuki za kikabila. Mugesera alikimbia na familia yake, kwanza katika jeshi la Rwanda na kisha katika jiji la Quebec, Canada. Muda mfupi baadaye, Mbonampeka alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Sheria kufuatia maandamano.

Canada

Nchini Canada, Mugesera na familia yake waliwasili kama wakimbizi, na walipatiwa haraka nyaraka za ukazi wa kudumu. Mugesera akapata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Laval.

Mashtaka ya uhalifu wa kivita

Philip Gourevitch, mwandishi wa “We Wish to Inform You That Tomorrow We Will Be Killed With Our Families”, alidai kwamba hotuba ya Mugesera ya mwaka 1992 ilisababisha kasi na mhemko wa watu wasio wa kabila la Watutsi ambayo ndiyo ilisababisha mauaji ya kimbari, akisema kuwa "(Mugesera) alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kabisa kwenda kwenye vyombo vya habari kutoa hotuba kwa umma na kusema, ‘Angalieni, makosa yetu katika siku za nyuma yanavyotugharimu kuruhusu Watusi wachache kuendelea kuishi. Lazima tuwamalize’”. Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Mchakato wa kufukuzwa

Mwaka 1995, wanasheria wa serikali ya Canada walianza kusikiliza shauri dhidi ya Mugesera. Mahakama mbili za uhamiaji ziliamuru kuondoshwa kwake na kurudishwa Rwanda, hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho la Canada ilitengua hukumu hizi. Jaji Robert D├ęcary, aliiandikia Mahakama, kwamba kulikuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuunganisha hotuba ya mwaka 1992 na mauaji ya kimbari ambayo yalitokea miaka miwili baadaye. Katika kesi zote, Mugesera aliwakilishwa na mwanasheria wa Quebec, Guy Bertrand.

Tarehe 1 Agosti, 2001, Mugesera alitoa taarifa, na kuomba kesi ifutwe chini ya Sheria mpya za Canada dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho baadaye ilitoa uamuzi wa 8-0 kuhusiana na Mahakama Kuu ya Canada mnamo Juni 28, 2005, ambayo awali iliidhinisha kufukuzwa nchini humo kwa Mugesera.

Kufukuzwa kwa Mugesera kulicheleweshwa kwa sababu ya wasiwasi juu ya uwezekano wa kukabiliwa na adhabu ya kifo nchini Rwanda. Hata hivyo Rwanda ilipiga marufuku adhabu ya kifo mwaka 2007. Mugesera ndipo akaanza kupigania asihamishwe Canada kutokana na hofu kuwa atateswa akiwa nchini Rwanda. Serikali ya Canada ilisita kumfukuza nchini mtu ambaye angeweza kukabiliwa na mateso, lakini Kigali waliihakikishia Canada "dhamana ya kidiplomasia" kuhusu hali ya baadaye ya Mugesera.

Uamuzi wa Jaji wa Mahakama ya Juu, Michel Delorme, wa kukubali hoja zilizotolewa na serikali ya shirikisho, ambayo ilisema ni Mahakama Kuu tu ndiyo ina mamlaka katika masuala ya uhamiaji. Delorme aliendelea zaidi kwa kusema kuwa Kamati ya Umoja wa Mataifa haina nguvu kisheria kuilazimisha serikali katika maamuzi yoyote.

Wanasheria wa Idara ya Sheria pia walisema kuwa tayari walishafanya utafiti wa muda mrefu na kugundua kuwa hakuna hatari yoyote wala mateso katika kesi ya Mugesera awapo nchini Rwanda na kwamba hali nchini Rwanda kwa sasa ni salama.

Jumatatu ya Januari 23, 2012, Jaji wa Mahakama Kuu ya Quebec alikataa jitihada za Leon Mugesera za kuzuia kufukuzwa nchini humo. Mugesera aliondolewa nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Montreal siku hiyo hiyo ya Jumatatu, saa 10 jioni.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Jan 19, 2012

Kuna maisha bora kwa kila Mtanzania kwa gharama hizi?

  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Harun Masebu, akizungumza na waandishi wa habari

Makao Makuu ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco)
yaliyopo Ubungo jijini Dar es Salaama

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza tena kupanda kwa gharama za umeme. Mwaka jana ilitangaza ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 18.5. Mwaka huu imeongeza bei ya umeme kwa zaidi ya asilimia 40 kuanzia Januari 15 huku mgao wa umeme ukiendelea ingawa hata huo upatikanaji wa umeme ni wa mashaka, huku chini ya asilimia 15 ya Watanzania wote ndiyo wanaopata umeme! Kupanda kwa bei ya umeme hakika kunazidisha ugumu wa maisha ambao upo hasa kwa wananchi walio wengi ambao ni wenye kipato cha chini.

Pamoja na Tanesco kupandisha gharama ya umeme, lakini shirika hilo bado halijafanya maboresho ya mitambo kwa kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta madhara makubwa ikiwemo kuunguza vitu majumbani na maofisini.

Hatua ya kupandisha gharama hizi inazidi kuwaongezea umaskini Watanzania ambao tayari wana maisha magumu mno kwa sababu hata bei ya awali wengi walikuwa hawaimudu. Jumatano asubuhi kwenye kipindi cha asubuhi cha moja ya vituo vyetu vya televisheni nilimsikia mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Siraji Kaboyonga akitetea ongezeko hili la bei, lakini haikuniingia akilini kutokana na sababu alizozitaja.

Kupandisha bei bado hakuwezi kuwa suluhisho au kuifanya Tanesco ijiendeshe kwa ufanisi kwani kinachotakiwa ni mbinu za kiutendaji na ubunifu katika kuliendesha shirika. Mbona mapato Tanesco yako mengi, isipokuwa imekosa mbinu na mikakati ya kuzuia wizi wa umeme unaofanywa na watumiaji wengi wa umeme.

Mfano eneo ninaloishi na hata maeneo mengi ninayotembelea, wezi wanaotumia umeme wa wizi bila malipo ni wengi, tena wanashirikiana na wafanyakazi wa Tanesco na wala hakuna jitihada za makusudi kuwazuia vishoka. wanapandisha bei ya umeme wakati hata huduma zenyewe hazijaboreshwa!

Kupanda kwa bei hakika kunapunguza watumiaji wa umeme na kuwarudisha watu katika utumiaji wa vibatari na mishumaa kwa sababu ya kuogopa gharama ya umeme. Hali hii imefika hapo ilipo kutokana na mfumo wa nchi hii kuegemea zaidi kwenye siasa kuliko kujali utaalamu. Siyo siri kuwa wananchi wa Tanzania kwa sasa wanaishi kwenye kiza kinene baada ya kujitokeza jinai ya kugawiwa umeme wakati huu.

Ni aibu kuendelea kutegemea chanzo cha maji kuzalisha umeme wakati tuna vyanzo mbadala. Uchumi wa Tanzania unaporomoka kwa kasi kubwa kutokana na ukosefu wa nguvu ya umeme wa uhakika pamoja na kuwa madini ya Uranium yanayotengeneza nishati ya nyuklia yanapatikana kwa wingi Tanzania. Madini ambayo kwa nchi kama Iran na Korea yanatumika kwenye uzalishaji nguvu za umeme kwa njia ya nyuklia.

Moja ya tatizo ambalo tumekuwa nalo kipindi kirefu sasa, Watanzania wengi tunategemea nishati hii kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa ya maji. Miundombinu bado haijaboreshwa halafu linakuja suala la kuongeza bei ambalo ni kumwongezea mwananchi mzigo mkubwa usiobebeka na hiyo ni hatari kwa taifa, kwani itashusha hata uzalishaji na uchumi wa taifa utashuka.

Kwa nini tusiachane na vyanzo hivi na kuangalia vyanzo mbadala, kwani siku zote ambazo mabwawa hayo hupungua kina cha maji au kukauka, tumekuwa tukishuhudia mgao mkali, jambo ambalo tunaamini sasa umefika wakati wa serikali kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hii.

Hebu fikria ni biashara ngapi zinaathirika kutokana na mgao huu wa umeme. Hata kama ni biashara ya mwananchi wa kawaida ya kuuza barafu au juisi bado ina mchango katika ujenzi wa taifa changa
kama Tanzania. Kukosekana umeme wa uhakika katika mgao wa siku ni pigo kubwa kwa taifa kwani shughuli nyingi za uzalishaji zinasimama.

Mgao huu wa umeme licha ya kudhoofisha uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja unasababisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Majenereta yanayofanya kazi mchana kutwa mijini yamekuwa yanachafua mazingira kwa moshi na hata kelele. Mgao wa umeme mbali na kusababisha kuparaganyika kwa uchumi pia ni chanzo cha rushwa. Mara nyingi sehemu za wenye pesa na vigogo serikalini huwa haziathiriki na kadhia kama hizi. Hii ni kwa vile ama wenye nazo wanahonga watendaji wa Tanesco, au wenye madaraka wanapendelewa kwa vile wameshikilia kila kitu katika nchi hii.

Inaposemwa eti ongezeko hili haliwagusi wenye kipato kidogo naona kama kuwafanya Watanzania mbumbumbu. Kwani ongezeko linapovikumba viwanda basi hata bidhaa zitapanda bei na watumiaji ni hawa hawa walalahoi.

Gharama hizi za umeme ni kama muendelezo na mzigo mkubwa wanaotwishwa wananchi baada ya matatizo mengi yanayowakabili, huku ikisemwa kuwa serikali ndiye mdaiwa sugu lakini sidhani kama inaguswa. Kwa gharama hizi hakika ile kaulimbiu ya Rais Kikwete ya maisha bora kwa kila Mtanzania itabaki kuwa ndoto nzuri ya mchana.

Alamsiki…

MUKESH KAPILA: Ailaumu Sudan baada ya kufukuzwa nchini Chad

Mukesh Kapila

N'DJAMENA
Chad

WIKI hii kulikuwa na habari za afisa misaada mwandamizi wa Uingereza kufukuzwa nchini Chad wakati alipojaribu kutembelea kambi ya wakimbizi ambao bado wanaishi mashariki mwa nchi hiyo.

Afisa huyo, Mukesh Kapila, alikuwa mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Sudan aliyezungumza wazi wakati mgogoro wa Darfur ulipoanza miaka tisa iliyopita. Waziri wa mambo ya ndani wa Chad alimuamuru afisa huyo kuondoka nchini humo.

Kapila mwenyewe amesema sababu za kufukuzwa kwake kunahusiana na ushirikiano wa karibu uliopo kati ya serikali ya Sudan na Chad ambao amewatuhumu kuhusika na mauaji ya kimbari.

Hii ilikuwa ni ziara ya kwanza ya Kapila kuzuru eneo hilo tangu alipoondolewa katika nafasi yake mwaka 2004 akiwa amechanganyikiwa na kushindwa kuwashawishi jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kwa hali iliyokuwepo wakati huo Darfur, aliamua kuzungumza kwa umma alipozungumza na Shirika la Habari la Uingereza, BBC. Kapila anatishiwa na kivuli chake mwenyewe baada ya kushindwa kuzuia mauaji Darfur.

Kapila alitembelea makambi ya wakimbizi mashariki mwa nchi ambako watu 200,000 bado wanaishi. "Nilichanganyikiwa, nimehuzunishwa sana na kukasirishwa mno," aliiambia BBC alipojua kuwa amefukuzwa nchini humo.

Mukesh Kapila amefanya kazi sana na alishauri katika mgogoro na usimamizi wa migogoro, masuala ya kibinadamu, ahueni baada ya vita na maendeleo, na VVU na UKIMWI. Kapila bado anafanya kazi Chini ya Katibu Mkuu wa Taifa wa Maendeleo ya Jamii na Maarifa katika Shirikisho la Kimataifa la Msalaba na Mwezi Mwekundu (IFRC).

Historia ya Kapila imejikita katika tiba, afya ya umma na, hatimaye, maendeleo ya kimataifa na masuala ya kibinadamu.  amehitimu kutoka Vyuo vya Oxford na London.

Akiwa mtumishi wa umma wa ngazi ya kati mwaka 1994, alikuwa sehemu ya timu ya kwanza ya Uingereza kuangalia matokeo ya baada ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda hasa baada ya Rwanda Patriotic Front kuidhibiti Kigali.

Alikuwa Naibu Mkurugenzi wa programu ya Taifa ya UKIMWI nchini Uingereza katika miaka ya 1990.

Aliwahi kuwa Mkuu wa Migogoro na Mambo ya Kibinadamu wa Uingereza kitengo cha Idara ya Maendeleo ya Kimataifa kuanzia 1998 hadi 2002. Kuanzia 2002 hadi 2003, Kapila alikuwa Mshauri Maalum wa Umoja wa Mataifa, kwanza kwa Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu nchini Afghanistan na kisha kwa Kamishna wa Haki za Binadamu. Mwaka 2003 hadi 2004 Kapila alikuwa Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa wa Kibinadamu, na Mwakilishi Mkazi wa Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa kwa Sudan.

Alipokuwa Sudan, alishutumu vikali ukiukwaji wa haki za binadamu uliofanywa katika jimbo la Magharibi la Darfur. Harakati yake ilianza baada ya mwanamke wa Darfur aliyekuja ofisini kwake kumwambia jinsi gani yeye, binti yake na wanawake wengine 200 katika kijiji cha Tawilla walivyobakwa na makundi na wengi kuuawa na askari wa serikali na wanamgambo. Ripoti yake juu ya vita ya Darfur wakati huo ilifutwa na Serikali ya Sudan kwa madai kuwa "ni ya uongo", ingawa walifanikiwa kuileta Darfur katika sura ya vyombo vya habari vya dunia kwa mara ya kwanza. Kapila hatimaye alihamishiwa nje ya Sudan mwezi Aprili 2004, miezi 13 tu katika miezi 24 ya mkataba wake.

Akizungumza mwaka 2006 katika kipindi cha BBC, Kapila alisema:
“Kuna mjadala kuhusu kama tuliwahi kuwa na mauaji ya halaiki katika jimbo la Darfur au la, lakini kwa hakika katika akili yangu, na mawazo ya watu wengi, wengi, nadhani kuna shaka kidogo sana kwamba kile kilichotokea katika jimbo la Darfur mwaka 2003 na mwanzoni mwa 2004 hakika kilikuwa ni mauaji ya kimbari. Tunaweza kusema maneno, lakini ambayo hayatakuwa na faraja kwa watu wote ambao wameathirika.
Hivyo hatimaye niliendelea kusema kuhusu hilo hadharani, baada ya kujaribu njia mbalimbali za kidiplomasia na ustawi, na nilijikuta haraka  nikikokotwa kwenye ndege na kutupwa nje ya Khartoum. Na nilipotazama yaliyojitokeza nyuma, nilijiuliza kwamba kulikuwa na mauaji ya kwanza ya karne ya 21 - ni mahali katika historia ambapo hutotaka kuwepo.

Kapila ameshinda tuzo kadhaa kwa kazi yake ya kibinadamu na maendeleo. Mwaka 2003, alitunukiwa tuzo na Malkia Elizabeth II na kutajwa kuwa Kamanda wa Order wa Dola ya Uingereza kwa huduma yake ya kimataifa. Mwaka 2007 alipokea Tuzo Kimataifa ya ijulikanayo kama Dk Jean Mayer Global Citizenship Award of the Institute for Global Leadership.

Aliwahi kuwa Mkurugenzi katika Idara ya Afya inayohusiana na migogoro ya Shirika la Afya Duniani kuanzia 2004 hadi 2006. Mfanyakazi wa Serikali ya Uingereza, alikuwa ameazimwa kufanya kazi kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa. Alikuwa mshauri wa Benki ya Dunia juu ya masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, amewahi kuushauri Umoja wa Mataifa katika Mkakati wa Kimataifa wa Kupunguza Maafa (UN /ISDR), na Shirika la Kimataifa la Kazi Duniani. Alikuwa mtendaji mkuu wa PHG Foundation katika Cambridge, Uingereza kuanzia Septemba 2003 hadi Agosti 2004.

Kabla ya kuteuliwa kuwa chini ya Katibu Mkuu kwa kazi ya Maendeleo ya Taifa ya Jamii na Maarifa, Kapila aliwahi kuwa Mwakilishi Maalum wa VVU na UKIMWI, na hatimaye kama Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa IFRC. Wakati akiwa IFRC, Kapila alikuwa chombo katika maendeleo duniani kote "ushirikiano wa kimataifa" ya Msalaba Mwekundu na Mwezi Mwekundu kama vile VVU na kupunguza hatari ya maafa, ambapo mafanikio kidogo yamekuwa na mafanikio. Hivi karibuni, amekuwa na wajibu wa kuandaa Mkakati wa mwaka 2020 – visheni ya Shirikisho la Kimataifa kwa muongo ujao.

Aliwahi kutumikia nafasi ya Mshauri wa Bodi wa Kituo cha Geneva kwa ajili ya Udhibiti ya Kidemokrasia wa Vikosi vya Jeshi (Democratic Control of Armed Forces), na wa Minority Rights Group International, na Mjumbe Mtendaji wa Kamati ya Utekelezaji ya Muungano wa moja kwa moja dhidi ya ubakaji katika Migogoro na migongano (AllianceDARC).  Amekuwa mjumbe wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti (UNITAR), Kituo cha Amani cha Kimataifa na Mratibu wa mfumo wa Tathmini ya Majanga Umoja wa Mataifa.
Dk Kapila kwa sasa ni mjumbe mwandamizi wa Hughes Hall College, Chuo Kikuu cha Cambridge, nchini Uingereza. Pia ni Mshiriki Mweza katika Taasisi ya kukabiliana na Migogoro ya Kibinadamu, katika Chuo Kikuu cha Manchester, Uingereza.

Kapila anaishi Uingereza na Uswisi.  Ameoa na ana watoto watatu.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

Jan 11, 2012

ANWAR IBRAHIM: Upinzani dhidi ya serikali wamfanya kubambikwa mashtaka ya ulawiti

Anwar Ibrahim

KUALA LUMPAR
Malaysia

KIONGOZI wa upinzani nchini Malaysia, Anwar Ibrahim ameondolewa makosa ya ulawiti katika kesi iliyochukua karibu miaka miwili. Mwanasiasa huyo alituhumiwa kufanya ngono na aliyekuwa msaidizi wake wa kiume. Hata hivyo jaji wa mahakama hiyo alisema uchunguzi wa DNA haukutoa ushahidi wowote.

Punde baada ya mahakama kutangaza uamuzi huo, jamaa wa Anwar walionekana kububujikwa na machozi ya furaha huku wafuasi wake wakishangilia uwamuzi huo. Wafuasi wa mwanasiasa huyo waliokusanyika nje ya mahakama mjini Kuala Lumpar wamekuwa wakisisitiza kwamba kesi hiyo haikufaa kufunguliwa tangu kuwasilishwa kwa tuhuma za ulawiti.

Hii ni mara ya pili Anwar ameshtakiwa kwa kufanya ulawiti. Kesi dhidi yake zimesababisha kuwepo na msisimko mkubwa wa kisiasa nchini Malaysia kwa zaidi ya muongo mmoja. Anwar Ibrahim ametaja kesi hiyo kama iliyochochewa kisiasa japo serikali imekanusha kuhusika kwa vyovyote.

Huku uchaguzi mkuu ukitarajiwa karibuni, chama tawala ambacho kimekuwa madarakani kwa zaidi ya nusu karne kinakabiliwa na upinzani mkali kutoka mrengo wa upinzani unaoongozwa na Anwar.

Historia yake

Anwar Ibrahim amezaliwa 10 Agosti 1947 ni mwanasiasa wa Malaysia ambaye aliwahi kuwa Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia 1993 hadi1998. Mapema katika kazi yake, Anwar alikuwa mshirika wa karibu wa Waziri Mkuu, Mahathir Mohamad, lakini baadaye alijitokeza kama mkosoaji maarufu wa serikali ya Mahathir.

Mwaka 1999, alihukumiwa kifungo cha miaka sita jela kwa rushwa, na mwaka 2000, miaka mingine tisa kwa kulawiti. Mwaka 2004, Mahakama Kuu iliipindua hukumu yake ya pili na kumuachia. Julai 2008, alikamatwa kwa madai ya kumlawiti mmoja wa wasaidizi wake wa kiume, lakini aliachiwa huru mwaka 2012.

Tarehe 26 Agosti 2008, Anwar alishinda tena uchaguzi wa Pauh Permatang na kurejea Bungeni kama kiongozi wa upinzani wa Malaysia. Amesema ipo haja ya kuwepo uhuru, ikiwa ni pamoja na mahakama huru na vyombo vya habari huru, ili kupambana na rushwa iliyotapakaa ambayo anaona inaisukuma Malaysia kwenye umasikini.

Kuanzia 1968 hadi 1971, akiwa mwanafunzi, Anwar alikuwa rais wa chama cha wanafunzi wa Kiislamu. Alikuwa pia mmoja wa waasisi wa kamati ya Vuguvugu la Vijana wa Kiislamu wa Malaysia, ambayo ilianzishwa mwaka 1971. Pia alichaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Vijana wa Malaysia. Mwaka 1974, Anwar alikamatwa wakati wa maandamano ya wanafunzi dhidi ya umaskini na njaa vijijini. Hii ilitokana na tetesi kuwa familia ilikufa kutokana na njaa katika kijiji cha Baling, katika jimbo la Kedah, pamoja na ukweli kwamba haikuwahi kutokea. Alifungwa jela chini ya Sheria ya Usalama wa Ndani, inayoruhusu kuwekwa kizuizini bila kufunguliwa mashitaka, na alikaa kizuizini kwa miezi 20 katika Kituo cha Kamunting.

Mwaka 1968-1971, alilelewa katika Umoja wa Kitaifa wa Wanafunzi wa Kiislamu wa Malaysia ​​akiwa rais wa Muungano. Mwaka 1982, Anwar, aliyekuwa kiongozi mwanzilishi na rais wa pili wa chama cha vijana wa Kiislamu, aliwashangaza wafuasi wake kwa kujiunga na United Malays National Organisation (UMNO), iliyoongozwa na Mahathir Mohamad, aliyekuwa waziri mkuu mwaka 1981. Alipanda safu ya kisiasa haraka: kazi yake ya kwanza ilikuwa ni Waziri wa Vijana, Utamaduni na Michezo mwaka 1983, baadaye, aliongoza wizara ya kilimo mwaka 1984 kabla ya kuwa Waziri wa Elimu mwaka 1986. Kwa wakati huo, uvumi ulienea kuwa Anwar kupanda hadi nafasi ya Naibu Waziri Mkuu kitu kilichokuwa jambo la kawaida nchini Malaysia kwa Waziri wa Elimu kushika nafasi ya Naibu Waziri Mkuu.

Kipindi cha uongozi wake kama Waziri wa Elimu, Anwar alianzisha sera mbalimbali katika mitaala ya shule kitaifa. Moja ya mabadiliko makubwa aliyofanya ni kuipa jina jipya lugha ya taifa kutoka Bahasa Malaysia na kuwa Bahasa Melayu, moja ya makabila nchini Malaysia kitendo kilichokosolewa na wasio wa kabila hilo.

Mwaka 1991 aliteuliwa kuwa Waziri wa Fedha. Mwaka 1993, akawa Naibu Waziri Mkuu wa Mahathir baada ya kushinda Unaibu Rais wa UMNO dhidi Ghafar Baba. Kuna taarifa Anwar alitumia fedha nyingi ili kuungwa mkono. Ilidaiwa pia alitumia fedha za siasa ili kupata nafasi yake kama makamu wa rais wa UMNO.

Mwishoni mwa miaka ya 1990, hata hivyo, uhusiano wake na Mahathir ulianza kuzorota, ulisababishwa na kutofautiana juu ya utawala. Wakati Mahathir hayupo, Anwar alijichukulia hatua kali za kuboresha mifumo ya uongozi wa nchi hiyo ambayo ilikuwa tofauti na sera za Mahathir za kibepari.

Matarajio ya Kisiasa

Novemba 2006, Anwar alitangaza mpango wa kugombea ubunge mwaka 2008. Anwar amekuwa mkosoaji wa sera za serikali tangu kuachiliwa kwake kutoka gerezani, hasa utata wa Sera Mpya ya Uchumi, ambayo inatoa usawa wa kijinsia kwa Bumiputras. Sera zinazoweka idadi maalum ambayo lazima ifikiwe. Pia ni Mshauri wa Parti Keadilan Rakyat, chama ambacho mke wake, Dk Wan Azizah ni rais.

Tarehe ya uchaguzi wa 2008, hata hivyo, ilipangwa kuwa Machi 8, 2008, na kuzua mzozo ambapo chama cha Barisan Nasional kilitoa wito wa kufanyika uchaguzi huo mapema kwa nia ya kuzima mipango ya Anwar kutaka kurudi Bungeni. Mke wa Anwar, Wan Azizah Wan Ismail, alitangaza kuwa angejiuzulu ili kurejesha kiti chake cha ubunge wa Permatang Pauh ili kulazimisha uchaguzi ambao Anwar atagombea. Alipoulizwa kuhusu uwezekano wa Anwar kuwa Waziri Mkuu ajaye, kiongozi wa zamani, Tun Dr Mahathir, alijibu kwa vijembe, "Labda awe Waziri Mkuu wa Israel".

Madai ya ngono

Katika Baraza Kuu la UMNO, kitabu, "Sababu 50 Kwanini Anwar Hawezi Kuwa Waziri Mkuu" kilisambazwa chenye picha pamoja na shutuma za rushwa dhidi ya Anwar. Kitabu kimeandikwa na Khalid Jafri, mhariri wa zamani wa gazeti la serikali, ‘Utusan Malaysia’ na aliyekuwa mhariri mkuu wa gazeti wa jarida lililoshindwa la Harian National. Anwar aliomba amri ya mahakama kuzuia usambazaji zaidi ya kitabu na kufungua kesi dhidi ya mwandishi kwa kashfa. Polisi walimshtakiwa mwandishi wa kitabu kwa kuchapisha habari za uongo. Miongoni mwa madai katika kitabu ni kwamba Anwar ni shoga. Polisi waliamuriwa kuchunguza ukweli wa madai hayo. Katika kile gazeti la Sydney Morning Herald liliita "ukweli wa kisiasa uliopangwa", Anwar alishtakiwa kwa kulawiti, alikutwa na hatia na kuhukumiwa miaka 15 jela.

Mwaka 1999, Anwar alifungua kesi dhidi ya Waziri Mkuu Mahathir ya kashfa, kwa madai ya kutamka shutuma za vitendo kinyume na maadili na kumwita Anwar shoga katika mkutano wa waandishi habari nchini Malaysia. Hukumu hii iligeuzwa mwaka 2004, na Anwar akatoka gerezani. Mwandishi wa kitabu alikufa mwaka 2005 kwa ugonjwa wa kisukari, lakini si kabla ya Mahakama Kuu kumkuta na hatia ya kashfa na kutakiwa kulipa fidia ya mamilioni. Mahakama Kuu, Machi 8, 2010 ilitoa uamuzi kuwa kutimuliwa kwa Anwar mwaka 1998 kutoka Baraza la Mawaziri kulikofanywa na Mahathir kulikuwa halali kikatiba.

Tarehe 29 Juni 2008, iliripotiwa kuwa msaidizi wa Anwar Ibrahim alitoa ripoti polisi ya madai kuwa alilawitiwa na Anwar. Anwar alisema kuwa uwezekano wa hukumu ya kifungo jela kutokana na madai inaweza kuwa jaribio la kumuondoa kwenye nafasi ya kiongozi wa upinzani kufuatia kuongezeka kwa wafuasi wake na ushindi katika uchaguzi. Pia alisaini kuwa hana hatia na alitoa ushahidi katika mfumo wa taarifa za matibabu.

Kesi hii imefutwa tarehe 9 Januari 2012, karibu miaka miwili baada ya kesi kuanza, baada ya Jaji Mohamad Zabidin Mohd Diah, kumuona Anwar hana hatia ya kulawiti. Jaji aligundua kuwa ushahidi wa DNA uliowasilishwa na upande wa mashtaka haukuwa sahihi, na kumwachia huru Anwar.

Madai ya mkanda wa ngono uliofichwa

Machi 21, 2011 video ya ngono ilionekana ambayo ilidaiwa kumshirikisha Anwar Ibrahim. Siku moja baadaye, Anwar Ibrahim alifungua malalamiko polisi. Polisi kwa sasa wanafanya uchunguzi dhidi ya watu watatu ambao waliionesha video hiyo. Watu hao ni waziri kiongozi wa zamani wa Malacca, Tan Sri Abdul Rahim Thamby Chik, mfanyabiashara Datuk Shazryl Eskay Abdullah na mweka hazina wa zamani wa Perkasa, Datuk Shuaib Lazim.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.