Jan 27, 2012

LEON MUGESERA: Mtuhumiwa wa mauji ya kimbari aliyerudishwa Rwanda baada ya kukwepa kwa zaidi ya miaka 16

Leon Mugesera

QUEBEC
Canada

MTUHUMIWA wa mauji ya kimbari, Leon Mugesera, aliyekuwa anahitajika sana nchini Rwanda kwa madai ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu yenye uhusiano na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, ambayo yalishuhudia ukatili mkubwa ulioongozwa na Wahutu kwa mamia ya maelfu ya watu, hasa wa kabila la Watutsi.

Madai ya uchochezi yanahuswa na hotuba ya Mugesera aliyoitoa mwaka 1992 akitoa wito kwa Wahutu kuwaondoa nchini Rwanda Watutsi, aliowaita "mende."

Serikali ya Canada imeamua kumrudisha Rwanda mtuhumiwa huyo wa mauji ya kimbari. Mahakama hiyo ya Canadian imekataa ombi la rufaa kutoka kwa mshukiwa huyo aliyepinga kurudishwa nchini Rwanda akisema kuwa hatapata haki nchini huko.

Mugesera ambaye anakabiliwa na mashtaka hayo ya kutoa matamshi ya kuchochea mauaji ya halaiki na uhalifu dhidi ya binadamu, inasemekana alitoa hotuba ya kichochezi mwaka 1992, mbele ya wanachama wa kilichokuwa chama tawala cha wahutu (MRND), na anadaiwa kusema kwamba Watutsi wanapaswa wauawe huku akiwaita 'mende'.

Mwenyewe amekanusha madai hayo akisema kuwa matamshi yake yametafsiriwa vibaya. Mugesera, mwanataaluma na mwanaharakati wa kisiasa ambaye alikuwa akiishi katika jiji la Quebec, alipigania bila mafanikio kwa muda wa miaka 16 katika mahakama kadhaa - ikiwa ni pamoja na Mahakama Kuu ya Canada mwaka 2005 - ili kuepuka kurejeshwa nchini Rwanda.

Kufuatia hukumu, ambayo mahakama ilisema kuwa kuna ushahidi wa kutosha kuonesha kuwa Mugesera ndiye alichochea mauaji dhidi ya Watutsi, hatimaye serikali ya Canada mnamo Novemba mwaka jana ilipitisha uamuzi wa kufukuzwa kwa Mugesera.

Wakili wa Mugesera alikuwa ameomba apewe muda zaidi ili Kamati ya Umoja wa Mataifa inayopinga vitendo vya unyanyasaji na mateso ichunguze kwanza na itoe hakikisho kuwa hatapatwa na kadhia hiyo akiwa Rwanda lakini mahakama ilitupilia mbali ombi hilo. Mugesera na wanasheria wake walisema kuwa atateswa au kuuawa kama atarudishwa Rwanda na kupambana na kesi hiyo, kwa vile yeye ni adui wa Rais Paul Kagame. Wameonesha shaka katika utawala wa nchi hiyo wa sheria au uwezo wa Mugesera wa kupata hukumu ya haki mbele ya mahakama nchini humo.

Serikali ya Rwanda imefurahishwa na uamuzi huo.

Historia yake

Leon Mugesera amezaliwa mwaka 1952, ni mzaliwa wa Rwanda, ambaye alikuwa anaishi katika jiji la Quebec, Canada tangu mwaka 1992, kabla hajatakiwa kuondoka nchini Canada kwa sababu ya kesi inayomkabili ya uchochezi dhidi ya Watutsi kutokana na hotuba yake ambayo wakosoaji wanadai ndiyo iliyochochea mauaji ya kimbari nchini Rwanda ya 1994.

Akiwa Rwanda

Mugesera wa kabila la Kihutu, amekuwa mwanachama wa chama kikubwa cha Kihutu cha MRND, ambacho kilikuwa na mahusiano ya karibu zaidi na jeshi la nchi hiyo. Alikuwa Makamu Mwenyekiti wa MRND katika mkoa wa Gisenyi.

Katika hotuba yake iliyotolewa Novemba 22, 1992 nchini Rwanda, inadaiwa Mugesera aliwaambia wanachama 1000 wa chama chake kwamba "sisi watu wa Kabila la Hutu tuna wajibu wa kuchukua jukumu wenyewe na kufuta hili povu" na kwamba wanapaswa kuwaua Watutsi na "kuitupa miili yao katika mito ya Rwanda". Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Kufuatia hotuba hii, Waziri wa Sheria wa Rwanda wakati huo, Stanislas Mbonampeka, alitoa kibali cha kukamatwa dhidi ya Mugesera kwa kuchochea chuki za kikabila. Mugesera alikimbia na familia yake, kwanza katika jeshi la Rwanda na kisha katika jiji la Quebec, Canada. Muda mfupi baadaye, Mbonampeka alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Sheria kufuatia maandamano.

Canada

Nchini Canada, Mugesera na familia yake waliwasili kama wakimbizi, na walipatiwa haraka nyaraka za ukazi wa kudumu. Mugesera akapata kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Laval.

Mashtaka ya uhalifu wa kivita

Philip Gourevitch, mwandishi wa “We Wish to Inform You That Tomorrow We Will Be Killed With Our Families”, alidai kwamba hotuba ya Mugesera ya mwaka 1992 ilisababisha kasi na mhemko wa watu wasio wa kabila la Watutsi ambayo ndiyo ilisababisha mauaji ya kimbari, akisema kuwa "(Mugesera) alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kabisa kwenda kwenye vyombo vya habari kutoa hotuba kwa umma na kusema, ‘Angalieni, makosa yetu katika siku za nyuma yanavyotugharimu kuruhusu Watusi wachache kuendelea kuishi. Lazima tuwamalize’”. Kauli hii haipo katika tafsiri rasmi ya hotuba, kama iliyotolewa katika hati ya kisheria mbele ya Waziri wa Uraia na Uhamiaji wa Canada tarehe 8 Agosti 2003.

Mchakato wa kufukuzwa

Mwaka 1995, wanasheria wa serikali ya Canada walianza kusikiliza shauri dhidi ya Mugesera. Mahakama mbili za uhamiaji ziliamuru kuondoshwa kwake na kurudishwa Rwanda, hata hivyo, Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho la Canada ilitengua hukumu hizi. Jaji Robert D├ęcary, aliiandikia Mahakama, kwamba kulikuwa hakuna ushahidi wa kutosha kuunganisha hotuba ya mwaka 1992 na mauaji ya kimbari ambayo yalitokea miaka miwili baadaye. Katika kesi zote, Mugesera aliwakilishwa na mwanasheria wa Quebec, Guy Bertrand.

Tarehe 1 Agosti, 2001, Mugesera alitoa taarifa, na kuomba kesi ifutwe chini ya Sheria mpya za Canada dhidi ya ubinadamu na uhalifu wa kivita.

Mahakama ya Rufaa ya Shirikisho baadaye ilitoa uamuzi wa 8-0 kuhusiana na Mahakama Kuu ya Canada mnamo Juni 28, 2005, ambayo awali iliidhinisha kufukuzwa nchini humo kwa Mugesera.

Kufukuzwa kwa Mugesera kulicheleweshwa kwa sababu ya wasiwasi juu ya uwezekano wa kukabiliwa na adhabu ya kifo nchini Rwanda. Hata hivyo Rwanda ilipiga marufuku adhabu ya kifo mwaka 2007. Mugesera ndipo akaanza kupigania asihamishwe Canada kutokana na hofu kuwa atateswa akiwa nchini Rwanda. Serikali ya Canada ilisita kumfukuza nchini mtu ambaye angeweza kukabiliwa na mateso, lakini Kigali waliihakikishia Canada "dhamana ya kidiplomasia" kuhusu hali ya baadaye ya Mugesera.

Uamuzi wa Jaji wa Mahakama ya Juu, Michel Delorme, wa kukubali hoja zilizotolewa na serikali ya shirikisho, ambayo ilisema ni Mahakama Kuu tu ndiyo ina mamlaka katika masuala ya uhamiaji. Delorme aliendelea zaidi kwa kusema kuwa Kamati ya Umoja wa Mataifa haina nguvu kisheria kuilazimisha serikali katika maamuzi yoyote.

Wanasheria wa Idara ya Sheria pia walisema kuwa tayari walishafanya utafiti wa muda mrefu na kugundua kuwa hakuna hatari yoyote wala mateso katika kesi ya Mugesera awapo nchini Rwanda na kwamba hali nchini Rwanda kwa sasa ni salama.

Jumatatu ya Januari 23, 2012, Jaji wa Mahakama Kuu ya Quebec alikataa jitihada za Leon Mugesera za kuzuia kufukuzwa nchini humo. Mugesera aliondolewa nchini humo kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa Montreal siku hiyo hiyo ya Jumatatu, saa 10 jioni.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment