Feb 17, 2011

Serikali haiwezi kuendelea kukwepa suala la katiba

 Waziri wa Sheria na Katiba, Celina Kombani

Katiba ya Jamhuri ya mwaka 1977
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KWA miaka 18 sasa kumekuwa na madai ya wazi kupitia majukwaa ya siasa, wanaharakati na hata viongozi wa dini kuwa nchi hii inahitaji katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Katiba ya sasa inatajwa kuwa imejaa vipengele ambavyo havilingani kabisa na mazingira ya sasa ya mfumo wa vyama vingi.

Ni kwa mantiki hiyo, katiba yetu ya hivi sasa haihitaji tena marekebisho kama viongozi wa chama tawala wanavyotaka tuamini, kwani imefanyiwa marekebisho mengi mno kiasi kwamba kama ingekuwa ni nguo basi hata rangi yake ya asili ingekuwa imepotea kabisa kutokana na kujaa viraka.

Ipo haja ya kuwepo kwa mjadala mpana wa kitaifa ambao utawashirikisha pia wananchi kwani suala hili ni la jamii nzima na wala si la wasomi na wanaharakati pekee. Suala la kudai Katiba mpya halikuanza leo bali tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi lakini hadi leo hakuna kilichofanyika.

Lakini pia ieleweke kuwa suala la elimu ya uraia linapaswa kupewa kipaumbele zaidi kwani madai ya katiba mpya hayataeleweka vizuri iwapo wananchi wengi hawaijui hata hiyo katiba inayodaiwa kuwa ina kasoro. Nimewahi kusikia habari za kushangaza sana kuwa eti asilimia kubwa ya walimu wa shule za msingi na sekondari hawajawahi hata kuiona katiba! Kama walimu hawajawahi kuiona wala kuisoma, tunategemea nini kwa wanafunzi? Hivi ni wananchi wangapi wanaielewa katiba? Kuielewa katiba ni mkakati wa awali wa mafanikio ya madai ya katiba mpya.

Kilio cha Watanzania kutaka katiba mpya kilipewa nguvu na taarifa ya Tume ya Jaji Charles Nyalali iliyopendekeza kufutwa kwa vipengele 40 ambavyo vinakiuka haki za binadamu, taarifa iliyoamsha kilio cha kutaka katiba mpya mwanzoni mwa miaka ya tisini.

Wanasiasa, wanaharakati na viongozi wa dini walianza kudai katiba mpya wakitaka sheria mbaya 40 zilizopo katika katiba ziondolewe wakisema kuwa zilikuwa zinapigana na haki za bidamamu.

Hata hivyo, mbali ya viongozi wa dini na wanasiasa kutaka katiba mpya, aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Jaji Kiongozi Mstaafu, Amir Manento naye aliwahi kusema kuwa kuna kila sababu kwa Watanzania kuwa na mikakati ya kuidai katiba mpya kwa sababu iliyopo imepitwa na wakati.

Moja ya mambo muhimu yanayotakiwa kuangaliwa na kufanyiwa kazi kwa haraka iwapo tutakuwa na katiba mpya ni kulitenganisha bunge na serikali, ili kulipa nguvu bunge ambalo sasa linaonekana kuipoteza baada ya kuzidiwa nguvu na serikali.

Imekuwa ikisemwa kuwa muundo wa serikali na idadi kubwa ya mawaziri waliopo bungeni umelifanya bunge kushindwa kusimamia vyema uwakilishi wa mawazo ya wananchi, hivyo kujikuta likisimamia zaidi maamuzi ya mawaziri na serikali iliyopo madarakani na kulifanya liwe la kupitisha hoja bila kupingwa.

Pia mamlaka ya Rais katika suala la uteuzi wa nafasi mbalimbali, ikiwamo kumteua Waziri Mkuu ambaye lazima athibitishwe na wabunge, huku katiba hiyo ikiacha nafasi ya uteuzi wa mawaziri wengine mikononi mwake ni jambo la kuangaliwa pia.

Pia mamlaka ya Rais kumteua mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya katiba inasababisha malalamiko mengi kuwa wateule hao wamekuwa hawatendi haki kwa watu wenye itikadi tofauti na wao.

Naamini serikali ya Chama Cha Mapinduzi ni sikivu na yenye kuwajali watu wake, kwa nini hailioni hili kama kweli inataka kuendelea kudumisha mshikamano na amani ya nchi? Madai ya Katiba mpya yasisubiri machafuko yatokee kama ilivyokuwa Kenya bali serikali ikubali kuanzisha mchakato wa Katiba sasa.

Inashangaza kuona kuwa watawala ama wamekuwa wakitoa majibu ya kejeli au wamekaa kimya. Walichoona kwenye marekebisho ya katiba ni kutamka tu kwamba nchi ni ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.

Matatizo kibao yaliyomo ndani ya Katiba ya nchi ni mengi na yanahitaji kuangaliwa upya, sidhani kama watawala hawayaoni. Wanayaona lakini wanayaacha yaendelee kuwemo kwa kuwa kama inavyosemwa; yanawasaidia kubaki madarakani.

Mfano halisi wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977. Ibara 41 (7). Inasema:
Iwapo mgombea ametangazwa na Tume ya Uchaguzi kwamba amechaguliwa kuwa Rais kwa mujibu wa ibara hii, basi hakuna mahakama yoyote itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.”

Kwa kutaka kumwalinda watawala waliopo madarakani ndiyo maana ibara ikasukwa ndani ya katiba, kwamba pale mtu atakapokuwa ametangazwa kuwa rais, isiwepo mahakama yoyote ile “itakayokuwa na mamlaka ya kuchunguza kuchaguliwa kwake.” Kwa nini kuwe na katiba inayoruhusu mwanya wa kutenda uhalifu? Kwa nini kuwe na katiba inayotilia mashaka nguzo muhimu ya dola – mahakama – katika usimamizi wa haki?

Kila baada ya uchaguzi mkuu, waliochaguliwa wamekuwa wakiapa kulinda katiba hiihii inayotiliwa mashaka; ambayo ina uwezekano wa kuleta viongozi waliopatikana kwa njia chafu lakini hawawezi kuhojiwa mbele ya mahakama.
Inaaminika kuwa kiini cha migogoro mingi katika nchi za Kiafrika ikiwamo kuibuka vita vya wenyewe kwa wenyewe chanzo chake ni katiba. Viongozi wengi wa kiafrika wamekuwa wakitumia katiba kama silaha yao ya kuwachapia wale ambao wanamezea mate madaraka ya kuongoza nchi.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment