Feb 17, 2011

Kanali Dk. Kiiza Besigye: Swahiba wa Museveni aliyegeuka adui kwa kuutaka urais wa Uganda

Kanali Dk. Kiiza Besigye

Kampala
UGANDA

KAMPENI za Urais nchini Uganda ambazo zilikumbwa na matatizo madogo ya hapa na pale kuwahusu wagombeaji wa kiti hicho zimehitimishwa juzi tarehe 16 Februari, na leo tarehe 18 Februari ndiyo siku ya kupiga kura kumchagua rais atakayeiongoza Uganda kwa kipindi kingine cha miaka mitano.

Uchaguzi huu wa rais wa Uganda unaofanyika leo, jumla ya wagombea 8 akiwemo rais wa sasa, Yoweri Museveni wanagombea urais. Hii itakuwa ni mara ya nne kwa Museveni kugombea urais tangu mwaka 1986, na Kizza Besigye tangu ajiingize kwenye kinyang'anyiro ndiye amekuwa mshindani mkubwa wa Museveni.

Rais Museveni aliyechukua hatamu za uongozi wa nchi hiyo mwaka 1986 katika kipindi cha utawala wa chama kimoja. Aliruhusu mfumo wa vyama vingi mwaka 2005 kufuatia mashinikizo ya ndani na kimataifa.

Huku mgombea mmoja ambaye ni mwanamke pekee, Betty Oliva Kamya wa chama kipya cha Uganda Federal Alliance, akiwa hospitalini baada ya kufanyiwa upasuaji wengine waliendelea na mikutano ya kampeni japo walikuwa wanasumbuliwa katika mikutano hiyo, mfano mgombea mmoja alizomewa na vijana wa upinzani na vijana hao kukamatwa. Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Uganda, vikimnukuu msemaji wa Polisi Bi Judith Nabakooba, watu sita walipelekwa rumande katika magereza yaliyoko katika wilaya jirani ya Mpigi.

Watu hao inasemekana walimzomea Rais Museveni wakati akifanya mkutano wa kampeni katika soko moja eneo la Buwama. Vyombo vya habari vilimnukuu afisa polisi aliyeshuhudia mkasa huo akisema kundi la vijana waliodhaniwa wa vyama vya upinzani, walianza kumzomea punde tu alipoanza kuhutubia mkutano huo. Miongoni mwa maneno waliokuwa wakitumia ni kama tumekuchoka, umekuwa madarakani kwa muda mrefu na mengine.

Wagombea wengine ni Nobert Mao wa DP, Jaberi Bidandi Ssali wa PPP, Dk Abed Bwanika wa PDP, Olara Ottunu wa UPC, mgombea wa kujitegemea Walter Samuel Lubega na Dk. Kiiza Besigye wa IPC.

Kumekuwepo madai ya kufanyika mizengwe na udanganyifu katika uchaguzi mkuu wa Uganda. Hayo yalibainishwa na Akbar Hussein Godi, Mbunge wa eneo la Arua katika bunge la Uganda aliyemtuhumu Jenerali Aronda Nyakairima, Kamanda Mkuu wa Jeshi pamoja na makamanda kadhaa wa jeshi hilo kwamba walikutana tarehe 20 Januari na mmoja wa wakuu wa Tume ya Uchaguzi ya Uganda na kupanga njama ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi mkuu.

Kwa mujibu wa madai ya mbunge huyo, Jenerali Nyakarima alimtaka afisa huyo wa tume ya uchaguzi awashawishi wenzake ili waruhusu askari wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wanaoishi katika eneo lake la ubunge washiriki katika uchaguzi huo ambao unafanyika leo, kwa maslahi ya Rais Yoweri Museveni.

Mbali na madai ya mizengwe pia kulikuwepo madai ya kuwepo kwa vitendo vya rushwa kama ilivyo kwa nchi za Afrika. Katika utafiti uliofanywa hivi karibuni na gazeti la New Vision la nchi hiyo, imebainika kuwa baadhi ya wagombea wa nafasi hizo wanatoa rushwa ili kuwarubini wananchi wawapigie kura. Utafiti huo uliofanyika kati ya Novemba 22 na Desemba 23, mwaka jana, unaonesha kuwa asilimia 14.5 ya wananchi waliohojiwa wamekiri kupokea rushwa kutoka kwa baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali kwenye maeneo yao.

Kuhusu kukithiri kwa rushwa, imesemwa ujinga na umasikini miongoni mwa wananchi ni chanzo cha kuwepo kwa vitendo hivyo.

Pia kwenye uchaguzi huu, Waziri wa Habari na Mwongozo wa Taifa wa Uganda, Bibi Kabakumba Masiko amesema kuwa serikali ya Uganda imechukua hatua za kuimarisha usalama ili kuepusha tukio lolote la kimabavu kutokea.

Pamoja na kuwepo kwa vuta nikuvute, wabashiri wa mambo wanasema Rais Museveni ana nafasi kubwa ya kuendelea kuongoza taifa hilo pamoja na kukabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mpinzani wake mkuu, Kanali Dk. Kiiza Besigye.

Hata hivyo, mpinzani huyo wa Rais Museveni ameikosoa serikali ya sasa ya National Resistance Movement –NRM, kwa kupuuza malengo yaliyosababisha vita vya msituni ambavyo hatimaye vilisababisha kundi la uasi baada ya NRM kutwaa madaraka miaka 30 iliopita.

Aliyasema hayo katika mkutano na waandishi habari mjini Kampala, wakati akitoa ujumbe kwa jeshi hilo lilipokuwa likijiandaa kusherehekea miaka 30 ya kuasisiwa.

Katika kile kinachosemwa kutumika jeshi kumpendelea mpinzani wake, Rais Yoweri Museveni, Besigye amewaonya wanajeshi kutotumiwa na watu ambao wanataka kuwakatisha tamaa wananchi wa Uganda.

Historia ya Besigye
Kizza Besigye Warren Kifefe alizaliwa Aprili 22, 1956, eneo la Rukungiri, Uganda. Ni kanali wa zamani wa Jeshi la Uganda, mwenyekiti wa Forum for Democratic Change (FDC), na amegombea katika uchaguzi wa rais nchini Uganda mwaka 2001, 2006 na mwaka huu 2011.

Maisha ya awali na kazi
Besigye, mtoto wa pili katika familia ya watoto sita, alisoma shule ya msingi Kinyasano na Mbarara Junior. Wakati akiwa shule ya msingi, wazazi wake wote walifariki. Alimaliza elimu ya sekondari katika shule ya Kitante na baadaye sekondari ya juu katika shule ya Kigezi.

Mwaka 1975 alijiunga na Shule ya Tiba ya Chuo Kikuu cha Makerere na kufuzu shahada ya udaktari mwaka 1980.

Baada ya kufanya kazi ya kutibu katika Hospitali ya Aga Khan ya Nairobi, aliacha na kuchukua mafunzo ya kijeshi kwa kujiunga na National Resistance Army kati ya mwaka 1980-1986 kwenye vita vya msituni dhidi ya serikali ya Milton Obote. Alikuwa akiwajibika kuangalia afya za wapiganaji na hasa Mwenyekiti, Yoweri Museveni.

Yoweri Museveni alipokuwa Rais mwaka 1986, Besigye, wakati huo akiwa na umri wa miaka 29, aliteuliwa Waziri wa Mambo ya Ndani. Mwaka 1988, aliteuliwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, na Kamisaa wa Siasa za Taifa.

Mwaka 1991, alikuwa Kamanda wa Kikosi cha kisasa wa Masaka, na mwaka 1993 akawa Mkuu wa ugavi na Uhandisi. Kabla ya kustaafu kutoka jeshi muda mfupi kabla ya uchaguzi wa 2001, Besigye alikuwa amefikia cheo cha Kanali na alikuwa Mshauri Mwandamizi wa Jeshi na Wizara ya Ulinzi.
Mwaka 1998, Besigye alimuoa Winnie Byanyima, aliyekuwa Mbunge wa Manispaa ya Mbarara na mwanamke wa kwanza kuwa mhandishi mwanaanga nchini Uganda. Anselm Besigye, kijana wa kiume alizaliwa na Kizza Besigye na Winnie Byanyima, Septemba 1999.

Uchaguzi 2001
Kabla ya uchaguzi wa rais mwaka 2001, Besigye alijitokeza kuwa mpinzani wa sera za NRM ya Museveni na mfumo wa serikali wa “hakuna chama”, akiamini kuwa uongozi ulikuwa “haurekebishiki”, na kwamba “alitakiwa mtu kuchukua hatua na kuweka mambo sawa”. Alitaka kutazamwa upya kwa mfumo wa vuguvugu, na kubaki na utaratibu wa mpito, badala ya kuuhalalisha kama mfumo mbadala wa siasa.

Uchaguzi wa mwaka huo, Besigye, alionekana ndiye mpinzani pekee wa Museveni, alikuwa mmoja wa wagombea sita, wakati wa kampeni zilizokuwa na unyanyasaji mkubwa. Museveni alishinda uchaguzi wa urais, na matukio ya vurugu yalitokea baada ya kutangazwa kwa matokeo.

Kurudi toka uhamishoni na kukamatwa
Oktoba 26, 2005, Besigye alirejea Uganda kutoka Afrika Kusini, alikokuwa akiishi baada ya kuondoka Uganda. Maelfu ya wafuasi wake walijipanga mitaani kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe hadi mji mkuu, Kampala.
Alikamatwa Novemba 14, 2005, akituhumiwa kwa uhaini na ubakaji. Kesi ya uhaini ilimhusisha na madai yake ya kuhusishwa na waasi wa vikundi vya LRA na PRA, na mashtaka ya ubakaji ilihusishwa na madai ya tukio la Novemba 1997 kati yake na binti wa rafiki yake.

Kukamatwa kwake kulifuatia maandamano na vurugu jijini Kampala na miji nchini kote. Waandamanaji waliamini kuwa mashtaka yaliundwa kumzuia Besigye kugombea rais katika uchaguzi wa 2006.

Februari uchaguzi 2006
Uchaguzi mkuu wa 2006 ulishuhudia chama cha FDC kama chama kikuu cha upinzani na Besigye kama mpinzani kuu dhidi ya Museveni kwenye urais. Museveni alichaguliwa kwa kipindi kingine cha miaka mitano, kwa asilimia 59 dhidi ya asilimia 37 za Besigye. Besigye, aliyakataa matokeo kwa madai ya kuwepo udanganyifu.

Mahakama Kuu ya Uganda ilitoa maamuzi kuwa uchaguzi huo ulikuwa umefunikwa na vitisho, vurugu, kuwagawa wapigakura, na makosa mengine. Hata hivyo, Mahakama ilimpitisha Museveni kwa kura 4-3 kuzingatia matokeo ya uchaguzi.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaasda wa vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment