May 18, 2011

Mauaji ya Nyamongo na serikali inayodai kufuata utawala bora





 Picha mbalimbali zinazoonesha eneo la mgodi wa Nyamongo kulikofanyika mauaji


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii vyombo vya habari vilitawaliwa na habari ya mauaji ya watu sita na wengine kadhaa kujeruhiwa katika mgodi wa dhahabu wa kampuni ya African Barrick Gold (ABG), wanaodaiwa kuvamia mgodi huo, yaliyofanywa na Jeshi la Polisi wilayani Tarime.

Mauaji haya yanazidi kujitokeza wakati Serikali ya Awamu ya Nne ikiwa imejivika joho la utawala bora na kudai kuwa imebobea na kuitekeleza dhana ya utawala bora kwa vitendo.

Wakati makala haya yakiandikwa kulikuwa na taarifa za kutatanisha kuhusu idadi kamili ya watu waliofariki wakati polisi waliokuwa doria katika eneo hilo walipowarushia risasi za moto watu waliokuwa karibu na eneo la hifadhi ya mgodi huo kwa lengo la kuokota mchanga wa dhahabu.

Taarifa za vyombo vya habari zilimkariri Mwenyekiti wa kijiji cha Kewanja kilichopo kwenye mji mdogo wa Nyamongo, kuwa watu watano waliuawa katika vurumai hiyo iliyotokea Jumatatu saa 11 alfajiri.

Hata hivyo taarifa hizo zilitofautiana na zile za Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Tarime/Rorya ambapo lilithibitisha vifo vya watu watatu kutokana na risasi za moto, wanaodaiwa kuwa miongoni mwa kundi la wananchi waliotaka kuvamia mgodi huo. Kulikuwa pia na taarifa kuwa waliokufa ni sita.

Nilidokezwa kuwa eneo la kijiografia la mgodi huo ndilo linaloshawishi wananchi kuingia mgodini kwani halijulishi yepi ni makazi ya watu na lipi eneo la mgodi. Ndiyo maana nikawa najiuliza kwamba, hata kama wananchi walivunja sheria na kuingia eneo la mgodi polisi hawakuwa na ruhusa ya kuwaua, kwanza wananchi wenyewe hawakuwa na silaha walitakiwa kutumia mbinu nyingine kuwatawanya, kuua si suluhisho.

Ikumbukwe kuwa nchi yetu imetia saini mkataba wa kimataifa wa haki za binadamu na haikubaliki kumwadhibu mtu anayedaiwa kuvamia mgodi kwa kumuua, badala yake anapaswa kufikishwa katika vyombo vya sheria.

Hali hii ya mauaji ya raia kwenye maeneo ya migodi inatuashiria hatari ya upanuzi wa matabaka na iko wazi kwa kila mtu. Hatujui, kwa mfano, hata suala la wachimbaji wadogo wa madini waliowahi kupigwa risasi katika mgodi wa Mererani, kama wale wachimbaji wakubwa waliowapiga risasi walifikishwa mbele ya vyombo vya sheria.

Wachimbaji hawa wakubwa walistahili kufikishwa mahakamani kujibu suala hili kama ilivyo kwa polisi hawa walioua raia juzi kule Nyamongo wanavyopaswa kuchukuliwa hatua, kwa sababu jambo hili lina dalili zote za uenezi, unyanyasaji kwa watu wasio na uwezo, uhalifu na mauaji.

Hoja ya kwamba polisi walizidiwa kutokana na wananchi waliovamia mgodi kuwa zaidi ya mia nane bado ni hoja dhaifu katika kuhalalisha mauaji kwani wananchi hawakuwa na silaha. Ikiwa raia hawatalindwa na kutetewa na Taifa lao au hawataandaliwa mazingira mazuri ya kutafuta riziki yao kwa njia za halali katika nchi yao, sasa waende wapi?

Kwa kweli katika mauaji haya waliosababisha wana wajibu wa kuwajibika. Uwajibikaji ndiyo kiini na msingi wa utawala bora kwa serikali yoyote. Uwajibikaji hauwezi kusimamiwa kikamilifu na kudaiwa pasipokuwa na uwazi na utawala wa sheria.

Pamoja na kwamba viongozi wetu wamekuwa wakizungumzia sana suala la utawala bora, na hata kuona kuwa ni silaha ya pekee ya kuzuia migogoro ndani ya Taifa, lakini bado pengine uwajibikaji hujapewa uzito unaostahili. Ndiyo maana tunashuhudia mauaji yanayofanywa na Jeshi la Polisi na wahusika hawachukuliwi hatua kwa kisingizio cha habari za kiintelijensia.

Si kwa sababu viongozi hawajali sehemu hii ya utawala bora, bali pengine, hawatambui kwamba kutokuwajibika ndiyo chimbuko hasa la matatizo ya kiuchumi yanayotoa nafasi kubwa sana ya kuendeleza umaskini uliokithiri katika Taifa letu.

Utawala bora una maana ya utendaji wa wazi na unaowajibika juu ya rasilimali yote kwa usawa na juu ya jamii ya watu wake. Rasilimali ya nchi ni pamoja na rasilimali watu (elimu, ujuzi na ufundi), maliasili na uwezo wa ndani na nje wa kiuchumi na kifedha na hii ni pamoja na misaada ya maendeleo kutoka nje.

Kumekuwepo malalamiko ya muda mrefu kuwa wawekezaji huwanyanyasa raia katika eneo la mgodi huo kwa kuwatumia polisi, kuwalaumu tu wananchi bila kutoa elimu ya uraia ili wawe na wigo mpana wa kujua mipaka yao sanjari na wanachopaswa kukifanya pasi na kuvunja sheria za nchi bado hatuwasaidii.

Pale ambapo sheria inapiga marufuku jambo fulani lisitendeke, ni wajibu wa serikali kuwahamasisha raia wake wasitende jambo hilo sanjari na kuweka mfumo wa watendaji wenye taaluma na weredi wa kutosha ili kuwawajibisha wakiukaji wa sheria hizo.

Serikali haina budi kuwa makini kuyaangalia matatizo na changamoto zinazoendelea kujitokeza nchini hasa baina ya wananchi na wawekezaji kwa kukazia zaidi upatanisho, haki na amani sanjari na mikakati ya maendeleo endelevu ili kuepusha damu zaidi kumwagika.

Kwa mtazamo wangu nadhani kuna mambo makuu matatu ambayo serikali inapaswa kuyafanyia kazi kwa ajili ya ustawi wa watu wake ili kusiwepo machafuko zaidi: Utawala bora, wanawake na ujenzi wa amani. Hakuna maendeleo, ikiwa kama misingi ya haki, amani na upatanisho imebomolewa.

Utawala Bora unahitaji ushirikiano wa dhati katika ngazi mbalimbali za maisha. Bajeti za Serikali zilenge zaidi katika mafao ya wengi pamoja na kuwa na matumizi bora ya misaada inayopatikana kutoka nje ya nchi.

Wanawake: wanapaswa kushirikishwa katika mchakato wa utoaji wa maamuzi katika hatua mbalimbali za maisha ya kijamii, kwani hawa ndio wadau wakuu katika jitihada za ujenzi wa upatanisho, haki na amani.

Wajenzi wa amani: Viongozi wa madhehebu ya dini wanapaswa kuwa ni wadau wakuu katika harakati za ujenzi wa misingi ya haki na amani katika maeneo yake, kwa kukazia majadiliano ya kina, mawasiliano ndani na nje ya miundo ya madhehebu. Haki na amani ni masuala yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee katika ajenda za maisha.

Mungu ibariki Tanzania

No comments:

Post a Comment