Jun 22, 2011

Hili la posho ya vikao ni aina nyingine ya ufisadi

Waziri Mkuu, Mizengo Pinda

Wabunge katika Bunge la Jamhuri mjini Dodoma

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KWA watu wenye uelewa wanafahamu fika kwamba ufisadi nchini mwetu umekua na kustawishwa na mfumo uliohalalishwa na watawala, japo tuna serikali inayojivuna kupambana na ufisadi. Kwa utamaduni huu waliojiwekea watawala wetu wa posho za vikao hata kwa mikutano ya kikazi ya idara katika mfumo mzima wa serikali na mashirika yake hauna tofauti kabisa na ufisadi tunaoupigia kelele.

Inashangaza sana hata pale kiongozi tunayemfahamu kwa uadilifu wake anapoinuka na kutetea/kuhalalisha ufisadi huu kwa kisingizio kwamba upo kisheria! Anasahau kwamba Watanzania wa leo si wa jana na wameishavuka kiwango cha kudanganywa kwa hoja dhaifu kama hizo zinazotolewa na wateule hao kuhalalisha ufisadi.

Serikali inapoamua kuhalalisha mtu alipwe mishahara miwili kwa kazi moja - kwa maana ya mshahara halisi na “mshahara posho”, ni sawa na kushiriki katika kujenga misingi ya ufisadi ambayo inapambana nayo. Bahati mbaya tumefika mahali ambapo wahusika hawawezi kuona soni kuhalalisha ufisadi kwa kuwa wanaamini kuwa wanachofanya ni halali.

Bajeti ya Serikali ya Tanzania kwa mwaka wa fedha 2011/12, imepita huku serikali ikitangaza kodi na tozo ambazo imezipunguza katika bidhaa ya petroli ili kuhakikisha bidhaa hiyo inashuka bei na kutoa ahueni ya maisha kwa wananchi.

Akihitimisha hotuba ya Bajeti ya Serikali bungeni, Waziri wa Fedha, Mustafa Mkulo alisema, Serikali imekubaliana na ushauri wa Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi na ushauri wa wabunge wengine kuondoa kodi na tozo kwa bidhaa hiyo ya petroli.

Kwa upande wa posho, Waziri Mkulo alisema kuwa uamuzi wa kuzifuta na kuzirekebisha baadhi ya posho hizo umefikiwa na Serikali yenyewe. Alisema katika hotuba yake alisisitiza kuwa ili kupunguza matumizi yasiyo ya lazima, Serikali itapunguza posho zisizo na tija na safari za nje ambazo hazina tija, jambo ambalo kwa mtazamo wangu ni habari njema kwa Watanzania endapo itatekelezwa na si maneno matamu ya kisiasa.

Pia waziri Mkulo alisema suala la posho limekuzwa isivyo kawaida na kwa kutumia takwimu ambazo si sahihi, huku akisisitiza kuwa posho zingine haziwezi kuondolewa kwani zipo kisheria hivyo hazifutwi na akatoa mfano wa posho za joho la jaji au posho za madaktari.

Pamoja na maelezo hayo ya Mkulo, Kambi ya Upinzani iliikataa Bajeti hiyo kwa madai kuwa hoja zao hazijazingatiwa hata baada ya baadhi kuelezwa na Mkulo kuwa zilikuwa za uongo. Kutokana na madai hayo, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe, alitangaza kurejesha gari 'shangingi' alilopewa na Bunge ili lipigwe mnada.

Mbowe pia alilitaka Bunge kufanya uamuzi mgumu wa kukubali kufutwa kwa posho ya vikao, kufutwa kwa matumizi ya magari ya kifahari kwa baadhi ya viongozi na kupambana na ufisadi katika manunuzi ya umma. Binafsi nakubaliana na Mbowe kwa asilimia mia moja kwa kuwa haiwezekani Serikali ijidai kuwa inapambana na ufisadi wakati huohuo ikipalilia na kustawisha mfumo wa ufisadi huu wa kupeana posho hata katika mazingira ambayo si sawa.
Mbowe pia alisema wamemwandikia Katibu wa Bunge kumweleza kuwa wabunge wa Chadema hawatasaini fomu za posho pamoja na kuwepo madai ya kuwa baadhi ya wabunge wa chama hicho hawakupenda kususia posho. Aliongeza kuwa baadhi ya wabunge wameitafsiri vibaya hoja hiyo ya kutaka kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge kwa kudhani kuwa wabunge wa Chadema wanashinikiza ili posho zote za wabunge zifutwe.

Mbowe aliwataka wabunge bila kujali itikadi za siasa kuungana pamoja na kukubali kushinikiza kuchukuliwa kwa uamuzi huo mgumu wa kufutwa kwa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wote wa serikali ili kuliokoa taifa.

Na alibainisha kuwa yapo maeneo ambayo viongozi wa serikali wamekuwa wanalipana hadi kati ya Shilingi milioni 1.5 na Shilingi milioni mbili kama posho za kuhudhuria vikao, hatua ambayo imewalemaza viongozi wengi wa serikali na wakati mwingine kususa kushiriki vikao wanavyoona havina posho. Hii ni hatari sana kwa ukuaji wa uchumi wa nchi hii.

Kwa hali hii, kuna jambo moja nimekuwa nikijiuliza mara kwa mara, kama mfumo huu wa posho uliwekwa kwa nia njema kama ambavyo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameutolea kauli ya kuuhalalisha, basi afahamu kuwa nia hiyo imegeuka kuwa ufisadi, na tunatakiwa kuubadilisha.

Na kama kweli suala hili la posho lilikuwa na lengo zuri kama ambavyo imesemwa basi limetumiwa vibaya kwa maslahi ya wachache wenye hulka ya ubinafsi. Ni ufisadi ambao wanaonufaika nao hawataki kukiri au kuuona kuwa ni ufisadi bali wanatumia maneno haya na yale kuuhalalisha uendelee kuwepo.

Ndio maana nimekuwa na mashaka na hiki kinachoitwa 'Utawala Bora' kwa kuwa kwa walio wengi kimegeuka kuwa wimbo mtamu unaoimbwa na kufanyiwa semina elekezi ilimradi wateule walipane posho zao, na kushibisha matumbo yao basi!

Naomba kuwasilisha...

FREDERICK CHILUBA: Kutoka urais, kushtakiwa kwa ufisadi hadi mauti yake

 Frederick Chiluba
 
Frederick Chiluba na mkewe enzi za uhai wao
 
LUSAKA
Zambia
RAIS wa zamani wa Zambia, Frederick Chiluba, amefariki, akiwa na umri wa miaka 68. Msemaji wa rais huyo mstaafu alisema kuwa Chiluba kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa kwa matatizo ya moyo na figo ambayo ndiyo yamesababisha kifo chake.

Chiluba aliingia madarakani kwa kishindo katika uchaguzi wa 1991 wakati Afrika ikiwa inaanza kuingia katika demokrasi ya vyama vingi, katika uchaguzi wa kwanza wa mfumo wa vyama vingi akichukua madaraka hayo toka kwa rais wa zamani wa nchi hiyo, Kenneth Kaunda aliyemkosoa kwa sera zake za kushindwa kukuza uchumi wa taifa hilo wakati wa mfumo wa vyama vingi ulipoanza.

Aliingia kupitia chama cha Movement for Multiparty Democracy (MMD) ambapo aliiongoza nchi hiyo hadi mwaka 2001 alipoachia madaraka. Kabla ya hapo alikuwa kiongozi wa wafanyakazi.

Aliingia madarakani wakati Zambia ilikuwa imeshafilisika, naye alipoondoka aliacha rushwa ikistawi. Mara baada ya kuingia madarakani Chiluba alibinafsisha zaidi ya makampuni 250 ya serikali hatua iliyokosolewa vikali na wapinzani wake ambao baadaye aliwakamata na kuwafungulia mashtaka.

Aling'atuka madarakani mwaka 2001 baada ya kushindwa jaribio lake la kutaka kubadili katiba ya nchi hiyo na kuiongoza nchi hiyo kwa miaka mitatu na hatimaye kumpisha marehemu Levy Mwanawasa ambaye baada ya kushika madaraka alimfungulia mashtaka ya rushwa kiongozi huyo na kupatikana na hatia.

Mwaka 2007 mahakama kuu nchini Uingereza ilitangaza kuzuia mali zote za kiongozi huyo wa zamani wa Zambia zilizokuwa na thamani ya zaidi ya dola za marekani bilioni 4. Pia Chiluba alilaumiwa sana kwa kupenda maisha ya anasa.

Akiwa madarakani Chiluba pia aliweza kushinda jaribio la kutaka kupinduliwa mwaka 1996 na wanajeshi waasi ambapo aliwakamata viongozi kadhaa wa upinzani akiwemo Kenneth Kaunda na baadhi ya waandishi wa habari akiwashutumu kuhusika na upangaji njama wa kufanya mapinduzi.

Historia yake

Frederick Jacob Titus Chiluba alizaliwa Aprili 30, 1942 na alikuwa mwanasiasa wa Zambia ambaye alikuwa Rais wa pili wa Zambia kuanzia 1991 hadi 2001. Chiluba, kiongozi wa chama cha wafanyakazi, alishinda katika uchaguzi wa rais wa vyama vingi mwaka 1991 akiwa mgombea wa Movement for Multiparty Democracy (MMD), akimwangusha rais wa muda mrefu, Kenneth Kaunda.

Alichaguliwa tena kuiongoza Zambia mwaka 1996. Kwa kuwa hakuweza kugombea katika awamu ya tatu mwaka 2001, aliyekuwa Makamu wa Rais, Levy Mwanawasa aligombea badala yake kwa chama cha MMD. Baada ya kuondoka madarakani, Chiluba alikuwa chini ya uchunguzi wa muda mrefu na kesi kuhusu madai ya rushwa, hatimaye aliachiwa huru mwaka 2009

Maisha ya awali

Alizaliwa na wazazi Jacob Titus Chiluba Nkonde na Diana Kaimba na kukulia Kitwe, Zambia. Chiluba alioa mara mbili. Frederick Chiluba alisoma katika Shule ya Sekondari Kawambwa katika eneo la Kawambwa, ambapo alifukuzwa akiwa mwaka wa pili kwa kujishughulisha na mambo ya kisiasa. Alifanya kazi ya ukondakta wa basi na baadaye akawa dereva wa basi.

Ni wakati huo ndipo alipoufahamu uwezo wake wa kuwa mwanasiasa kutokana na haiba yake. Baadaye alifanya kazi kama diwani kabla ya kuwa msaidizi wa mweka hazina wa Atlas Copco, na kupanda hadi, mjini Ndola ambako alijiunga na Umoja wa Kitaifa ya Ujenzi.

Maisha binafsi

Frederick Chiluba na mke wake wa kwanza, Vera Tembo, ambaye amezaa naye watoto tisa, walitalikiana mwaka 2000 baada ya miaka thelathini na mitatu ya ndoa. Tembo aliamua kuendelea na kazi ya kisiasa kivyake, na kuwa Mwenyekiti wa MMD wa Mambo ya Wanawake, alichaguliwa katika Bunge la Zambia, na kuwa naibu Waziri wa Mazingira mwaka 2006. Mei 6, 2002, Chiluba alioa mke wa pili, Regina Mwanza, Mwenyekiti wa zamani wa masuala ya wanawake wa MMD, mjini Lusaka.

Chiluba siku zote alionekana nadhifu sana katika umbo lake fupi (akiwa na mita 1.5). Kuhusiana na madai ya rushwa kwa nchi za Ulaya dhidi yake katika miaka ya 2000 mwishoni, iligundulika kwamba duka la Uswisi lilizalisha jozi 100 za viatu namba 6 kwa ajili yake vikiwa na visigino inchi mbili, vingi vikifanana. Muonekano wake makini na suti nzuri vikawa ndiyo nembo yake, na vilibainishwa wakati wa kesi yake ya rushwa.
Katika mfano mkali, mwandishi wa gazeti la Zambia Post, Roy Clarke ambaye ni mwandishi wa safu ya mara kwa mara ambayo ilimshutumu Rais wakati alipokuwa madarakani alimfananisha kama "kazi bure, msalaba-wenye mavazi, mvaa-visigino virefu, mgoni, kibete".

Wapinzani wake wa kisiasa walimbeza wakati wakikosoa utawala wake. Michael Sata, kwa mfano, alimshutumu Chiluba kwamba "uwezo wake wa kufikiri ni mrefu kama kimo chake... hatuibi fedha, hatuteki nyara, hatununui suti, hatununui viatu. Hatuhongi wasichana nyumba..."
Kaunda aliyejulikana kwa Chiluba kama "kibete mwenye futi nne" wakati wa kupanda kwa Chiluba katika ulingo wa siasa za upinzani. Chiluba aliachiwa huru kutokana na mashitaka ya rushwa mwezi Agosti 2009. Chiluba alielezewa na BBC kama "Mkristo motomoto aliyezaliwa mara ya pili... ambaye "...maisha yake binafsi yalikuwa kiini cha uvumi mwingi."

Vyama vya Wafanyakazi

Chiluba alishinda uenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zambia (ZCTU). Yeye na viongozi kadhaa katika ZCTU waliwekwa kizuizini mwaka 1981 na Rais Kenneth Kaunda kwa kuanzisha mgomo mkubwa uliopoozesha zaidi uchumi wa Zambia. Viongozi hao wa vyama waliachiwa baada ya Jaji kusema kuwekwa kwao kizuizini ilikuwa kinyume cha katiba. Mwaka 1987, alifanikiwa kuleta changamoto ya uenyekiti wake wa NUBEGW, ambao uliiweka nafasi yake ZCTU katika hatari.

Siasa

Mwaka 1990 alisaidia kuundwa kwa Movement for Multiparty Democracy (MMD), chama ambacho, Chiluba kama mgombea wake wa urais, kilifanikiwa na kuleta changamoto kubwa katika utawala wa Kaunda katika uchaguzi wa 1991. Chiluba alikuwa mzungumzaji mzuri mwenye kipaji cha asili. Chiluba aliingia madarakani Novemba 2 mwaka huo. Alishinda tena katika uchaguzi huo kwa kipindi cha pili cha miaka mitano mwaka 1996, licha ya kesi ya kuhoji uzawa wake.

Chiluba alijaribu kumfukuza nchini humo Kaunda kwa madai kuwa alikuwa na asili ya Malawi. Alifanya marekebisho ya katiba ili kuzuia wananchi wenye asili ya kigeni kugombea urais, kwa lengo la kumfanya Kaunda asigombee. Baadhi ya wagombea katika uchaguzi wa rais wa 1996 walidai Chiluba hakustahiki, kwa madai kwamba yeye au baba yake alizaliwa Zaire. Hata hivyo, hakuna shaka kwamba alilelewa katika eneo la Copperbelt la Zambia.

Mwishoni mwa 2001, Chiluba alimtaliki mke wake, Vera, ambaye wamezaa watoto tisa; Helen, Miko, Hortensia, Castro, Chongo, Kaindu, Hulda, Frederick Jr na Verocia. Kwa mke wake mwingine wana watoto, Tito na Nikombe.

Baadaye alimuoa Mwenyekiti wa Wanawake wa MMD, Regina Mwanza, aliyekuwa katalikiwa. Pamoja na chama chake kushinda kwa wingi katika bunge, alishindwa kuungwa mkono katika jitihada zake za marekebisho ya katiba kuruhusu kugombea awamu ya tatu. Hakuna mbunge aliyeongoza msukumo kufanyia marekebisho katiba ya nchi, serikali haikuwahi kuwasilisha pendekezo lolote juu ya jambo hilo wala hapakuwa na kura ya maoni ya kurekebisha katiba ya nchi.

Mjadala mrefu wa tatu ulikuwa kati ya makundi mbalimbali ndani na nje ya chama cha MMD. Chiluba mwenyewe alikuwa kimya kuhusu hilo. Aliachia ngazi mwishoni mwa muhula wake siku ya Januari 2, 2002, na nafasi yake kuchukuliwa na Levy Mwanawasa, makamu wake wa rais. Chiluba katika uongozi wake alianza kama mjamaa, lakini akikubali mageuzi kadhaa ya kiuchumi.

Ufisadi

Baada ya kuondoka madarakani, Chiluba alikuwa shabaha ya kampeni za Mwanawasa dhidi ya rushwa: Februari mwaka 2003, alishtakiwa pamoja na wakuu wake wa zamani wa usalama, mawaziri wa zamani kadhaa na viongozi waandamizi, kwa makosa 168 ya wizi wa jumla ya zaidi ya dola 40m.

Ilidaiwa kuwa fedha zilihamishwa kutoka Wizara ya Fedha hadi akaunti iliyopo tawi la London la Benki ya Biashara ya Zambia (Zanaco). Chiluba alisema akaunti hiyo ilitumiwa na huduma za usalama wa nchi kufadhili shughuli za nje ya nchi. Mashtaka mengi yaliyofunguliwa dhidi yake baadaye yalifutwa, lakini mengine yalibaki. Aidha, mke wake Regina alikamatwa kwa kupokea bidhaa za wizi.

Kifo

Chiluba amefariki Jumamosi ya Juni 18, 2011, muda mfupi baada ya usiku wa manane. Msemaji wake, Emmanuel Mwamba, alitangaza kifo chake. Mwamba alisema kuwa Chiluba alikuwa na siku ya kawaida Juni 17, na hata alikuwa na muda wa kukutana na baadhi ya wanasheria wake. Baadaye alianza kulalamika kuhisi maumivu ya tumbo.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari ya kimataifa

Jun 15, 2011

Tuhuma za kuwadhalilisha wasanii wa kike zinaichafua tasnia ya filamu



 Picha hizi za juu zinawaonesha baadhi ya 
wasanii wa kike wanaounda Bongo Movie Club
 

 Hatmann Mbilinyi, mwenyekiti wa Bongo Movie Club

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KATIKA karne hii ya 21 vyombo mbalimbali vya mawasiliano, kama vile, magazeti, simu, redio, kinasa sauti, runinga, video, mtandao na kadhalika, vinachangia sana katika kuifanya dunia yetu kuwa ndogo sana. Vinachangia pia katika kuuendeleza utandawazi, na katika usambazaji wa utamaduni wa Kimagharibi kwa nchi zetu.

Vyombo hivi vimekuwa vikitumika kwa ajili ya kujielimisha na kujiburudisha, na maendeleo ya vyombo hivi yanakua kila siku kutokana na kuvumbuliwa kwa teknolojia mpya na rahisi kutumia.

Hali hii imetufanya sisi vijana kuvutiwa sana na mambo mapya (hasa ya kigeni), hata maendeleo ya vyombo vya mawasiliano yamekuwa yanatushangaza sana. Sisi vijana tunapenda pia kuunganika daima na vijana wengine kwa njia ya kuvitumia vyombo hivi.

Dunia ya mawasiliano imeweza kuchochea ubunifu wa vijana. Imeweza kutusaidia kujielimisha na kujiburudisha. Kwani wakati mwingine huhitaji kusafiri ili kujua kile kinachoendelea Barani Ulaya au Marekani, bali kwa kutumia mawasiliano ya kiteknolojia. Aidha, imeweza kwa kiasi kikubwa kuleta mabadiliko ya kiutamaduni hasa kati yetu vijana.

Mabadiliko haya, ingawa sehemu nyingine ni chanya, lakini kwa upande mwingine yameanza kutuletea athari mbaya na tunaonekana kuelekea uelekeo ambao Wazungu wanajitahidi kuondoka kwa kuwa umeshawaletea matatizo makubwa sana.

Juzi Jumatano nilibahatika kuusoma ujumbe mmoja uliotumwa na msanii muigizaji wa filamu mmoja wa kike (jina nalihifadhi) ambao ulikusudiwa kwenda kwa viongozi wa Shirikisho la Filamu Tanzania (TAFF) akiwalalamikia kwa kutochukua hatua kutokana na kile alichodai unyanyasaji wanaofanyiwa na baadhi ya viongozi wao wa klabu inayokutana kwenye viwanja vya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, maarufu kama Bongo Movie Club.

Ujumbe huo ulikuwa ukiwataarifu viongozi wa shirikisho la filamu kuwa kumekuwepo unyanyasaji mkubwa kwenye Club, huku ngono, majungu na ufisadi vikitawala, na ikaelezwa kuwa msanii mmoja wa kike (jina tunalo) alifanyiwa unyanyasaji na mmoja wa vigogo wa club (jina tunalo) walipokuwa ziarani Mwanza ambako walicheza na timu ya waandishi wa habari.

Hata hivyo, ujumbe huo uliendelea kueleza kwamba kiongozi mmoja wa club amekuwa na tabia ya kuwafanyia unyanyasaji mabinti na tayari ameshawafanyia vitendo kama hivyo wasanii wawili (majina tunayo), na bado kuna wengine anawahitaji, tena kwa kutishia kuwa wasipoonesha ushirikiano watapotezwa kabisa kwenye soko la filamu.

Ujumbe huo haukuishia hapo bali ulielezea pia tabia mbaya inayooneshwa na viongozi wengine wawili ambao wameamua kuigeuza Club hiyo kuwa sehemu ya kujipatia pesa kwa vigogo maarufu kama 'mapedeshee'.

Pia yapo madai kuwa club hiyo imeundwa mahsusi ikichukua sura ya danguro kwani wasanii wa kike wanaonekana kama wapo sokoni wakinadiwa kwa 'mapedeshee' na wakubwa.

Wakati leo, Ijumaa, Bongo Movie wanatarajiwa kucheza mechi yao na Wabunge mjini Dodoma, huku Dar es Salaam wameacha skendo hii ambayo hata hivyo wamejitahidi sana kuizima isijulikane kwenye vyombo vya habari kabla hawajacheza na wabunge.

Taarifa za kuaminika zinabainisha kuwa kwa siku mbili mfululizo walikuwa na vikao kwa ajili ya kuweka mambo sawa ili kuhakikisha kuwa habari hii haisambai. Hata waandishi wa habari waliowafuata kutaka ukweli walinyimwa kabisa ushirikiano!

Baada ya kupata taarifa hii nilijaribu kuwapigia simu baadhi ya waathirika wa vitendo hivi waliotajwa kwenye ujumbe huo ambao hata hivyo walisita kuniambia chochote kwa kuwa hawakuruhusiwa kabisa kuongea na vyombo vya habari, na nilipomtafuta mmoja wa viongozi anayetuhumiwa kwa unyanyasaji simu yake ilikuwa haipatikani.

Sikuishia hapo, nilimtafuta rais wa shirikisho la filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba, ambaye alikiri kupokea ujumbe huo na kuniambia kuwa hata yeye alishangazwa na kile kinachoendelea pale na kuahidi kufuatilia ili kujua ukweli. Hadi tunakwenda mitamboni sikuwa nimepata taarifa zaidi.

Niseme tu kuwa sina uhakika na habari hizi lakini kama ni kweli basi itanisikitisha sana kuona tabia kama hizi zikijitokeza kwa watu ambao jamii inawaamini, waliopaswa kuwa mfano mzuri kwenye jamii yetu. Pia ikumbukwe kuwa mimi ni mdau muhimu kwenye tasnia hii, kwa kuwa nimekuwa naandika miongozo ya filamu, naongoza filamu na wakati mwingine nashirikishwa hata kuigiza sehemu ndogo ndogo za kupita.

Nawaheshimu sana wasanii kwani ni watu muhimu sana kwenye jamii yoyote kwa kuwa huwa wanawakilisha ujumbe mahsusi kuhusu mila, desturi na tabia za jamii hiyo kwenye jamii zingine, hivyo huchangia kwa kiasi kikubwa katika suala zima la kuwaonesha wananchi njia nzuri ya kupita, hasa katika dunia ya sasa ya utandawazi.

Sitegemei kama watu ambao jamii inawaamini kuwa kile wanachokiigiza kina mafundisho mazuri kwao leo hii ndiyo wawe wa kwanza kukengeuka, tena kwa kiwango cha kustaajabisha kinachotia kichefuchefu hata kukielezea!

Nachukua nafasi hii kuishangaa serikali kwa kuonekana kukikumbatia kikundi cha watu kadhaa ambacho hakina hata usajili wowote kwa maana ya kutambulika kisheria, lakini ndiyo kimekuwa kikipapatikiwa, kikikaribishwa na kuchukuliwa kama nembo ya tasnia ya filamu, nadhani kwa sababu tu ya umaarufu wa wahusika.

FAZUL MOHAMMED: Kifo chake chaleta ahueni katika Afrika Mashariki

 Fazul Abdullah Mohammed

MOGADISHU
Somalia

KUUAWA kwa kiongozi wa Al Qaeda katika Afrika Mashariki, Fazul Abdullah Mohammed, mjini Mogadishu Somalia, kumewafanya wakazi wa kanda hii kupumua kidogo. Serikali ya mpito ya Somalia ilisema kuwa Fazul Mohammed aliuawa kwa kupigwa risasi siku ya Jumatano Juni 8, 2011, na ukaguzi wa DNA umethibitisha kuwa ni yeye.

Kifo chake kinafuatia shutuma alizokuwa akipewa na Marekani kuwa alipanga mashambulio ya kigaidi ya mwaka wa 1998 dhidi ya balozi za Marekani nchini Kenya na Tanzania, na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 224.

Mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa habari, Ahmed Rajab, amekaririwa akisema: “Si ajabu kuwa Fazul ameuawa mjini Mogadishu, kwa sababu kwa muda mrefu akijulikana kuwa alikuwa kamanda wa kikundi cha wapiganaji wa Somalia, al Shabab. Lakini tukumbuke kulikuwa na taarifa zamani kwamba aliuliwa na Marekani, na taarifa hizo zikawa si za kweli”.

Kikundi cha al-Shabab kimekanusha taarifa na kusema kuwa Fazul Mohammed hakuuawa.

Rais wa Somalia, Sheikh Sharif Sheikh Ahmed, ametoa maelezo zaidi kuhusu kuuawa kwa kiongozi huyo wa Al Qaeda Afrika Mashariki. Rais huyo alisema kuwa Marekani ilisaidia kuthibitisha utambulisho wa Mohammed, na ukaguzi ulifanywa nje ya nchi.

Aliwaonesha waandishi wa habari, ile ambayo alisema, ni hati ya kuzaliwa ya Fazul Mohammed, picha za familia yake, na ramani ya pengine malengo ya kushambulia mjini Mogadishu.

Waziri wa Mashauri ya Nchi za Nje wa Marekani, Hillary Clinton, amevipongeza vikosi vya serikali ya Somalia kwa kufanikiwa kumuua mtu huyo ambaye ni mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ugaidi waliohusika na mlipuko wa mabomu katika balozi za Tanzania na Kenya mwaka 1998. Clinton alikuwa Tanzania na kuweka shada la maua kwenye jengo la ubalozi wa Marekani, lililoshambuliwa kwa bomu na Al Qaeda mwaka 1998.

Clinton amesema kuuawa kwa Mohammed ni ushindi kwa nchi ya Somalia na dunia kwa ujumla wakati huu ambapo dunia inapambana kutokomeza vitendo vya ugaidi duniani.

Clinton aliyasema hayo muda mfupi baada ya kuwasili katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es slaam Tanzania kwa ziara ya siku tatu. Mohammed amekuwa akisakwa kwa udi na uvumba na serikali ya Marekani kuhusiana na kushiriki kupanga njama za kulipua ubalozi wa Marekani nchini Tanzania na Kenya.

Mara baada ya kutekeleza shambulio hilo Mohammed alikimbilia Somalia ambako mwaka 2007 alinusurika katika shambulio la vikosi vya Marekani na hakuonekana tena mpaka alipouawa na vikosi vya Somalia mjini Mogadishu.

Msemaji wa polisi mjini Mogadishu amesema kuwa Mohammed aliuawa alipokuwa akijaribu kuwatoroka polisi ambapo kulitokea majibizano ya risasi kati yao na baadaye kufanikiwa kumuua.

Afisa huyo ameongeza kuwa awali hawakubaini kama ni Mohammed hadi walipofanikiwa kupekua begi alilokuwa amebeba na kukuta ana pasi ya kusafiria ya Afrika Kusini yenye jina la Daniel Robinson. Mbali na mtuhumiwa huyo kukutwa na pasi hiyo ya kusafiria ya Afrika Kusini pia walimkuta na kiasi cha dola za Marekani elfu arobaini.

Historia yake:

Fazul Abdullah Mohammed alizaliwa Agosti 1972, au Februari 25, 1974, au 25 Desemba 1974. Alikuwa mwanachama wa al-Qaeda, na kiongozi katika Afrika Mashariki kuanzia Novemba 2009. Mohammed alizaliwa visiwa vya Moroni, na alikuwa na uwezo wa kuongea lugha za Kingereza, Kifaransa, Kiswahili, Kiarabu na Kingazija.

Nafasi katika al-Qaeda

Mohammed na watu wengine kadhaa walikuwa wanakabiliwa na mashitaka nchini Marekani kwa madai ya kushiriki katika mashambulizi ya balozi za Marekani mwaka 1998 Afrika ya Mashariki. Mohammed alikuwa kwenye orodha ya FBI ya magaidi wanaosakwa zaidi tangu kuanzishwa kwake Oktoba 10, 2001. Yalitangazwa malipo kwa ajili ya kumtafuta Mohammed ya dola za Marekani milioni 5.

Nchini Kenya, Mohammed aliwahi kuwa katibu, na kuishi katika nyumba moja na, Wadih el-Hage. El-Hage alishtakiwa na amekutwa na hatia. Kuna barua ilioneshwa iliyoandikwa kwenda kwa el-Hage, ilidhaniwa kutoka kwa Mohammed.

Mohammed alitumia muda wake mwingi akiwa Mogadishu akipanga mipango ya kuandaa lori lenye mabomu dhidi ya Umoja wa Mataifa ulioanzishwa nchini humo, na alikuwepo mjini hapo Oktoba 3, 1993, wakati wanamgambo wa Somalia walipoziangusha helikopta mbili za Marekani na kuua wanajeshi 18 wa kikosi maalum.

Vita dhidi ya ugaidi:

Mohammed anatuhumiwa kuhusika katika mashambulizi mawili mjini Mombasa, Kenya mnamo Novemba 26, 2002. Shambulio moja likihusisha lori lililotegwa bomu katika hoteli ya Paradise, ambapo 15 waliuawa. Jingine ni lile la uzinduzi wa makombora mawili kwenye shirika la ndege la Israel; hakukuwa majeruhi.

Mei 26, 2004, Mwanasheria Mkuu wa Marekani, John Ashcroft na Mkurugenzi wa FBI, Robert Mueller walitangaza kuwa ripoti ilionesha kuwa Mohammed alikuwa mmoja kati ya watu saba wanachama wa al Qaeda waliokuwa na mipango ya kigaidi wakati wa majira ya kiangazi mwaka 2004.

Kulingana na ripoti ya mahojiano ya FBI, mmoja wa washirika wake alikiri kwamba wapiganaji hao walipewa mafunzo na al-Qaeda na Osama Bin Laden nchini Afghanistan. Ahmed Ghailani, pia katika orodha hiyo, alikamatwa nchini Pakistan mwezi mmoja baadaye. Mara baada ya hapo, vyombo kadhaa vya habari vikatoa taarifa, vikidai vyanzo rasmi vya Umoja wa Mataifa na Marekani, vilielezea ushiriki wa wanachama kadhaa wa al-Qaeda, wakiwemo Mohammed na Ghailani, kujihusisha na harakati na kununua almasi nchini Liberia.

Wakati meli ya MV Bukoba ilipozama katika Ziwa Victoria mwaka 1996, na kusababisha kifo cha mwanzilishi mwenza wa al-Qaeda, Abu Ubaidah al-Banshiri, Mohammed ndiye aliyepelekwa eneo hilo la ajali na al-Qaeda, ili kuthibitisha kwamba Abu Ubaidah alikuwa amekufa.

Mwaka 2007, wakati wa Vita ya Somalia, inaaaminiwa kuwa Mohammed alikuwa katika mpaka karibu na eneo la Ras Kamboni akishirikiana na Muungano wa Mahakama za Kiislamu. Januari 8, 2007, ndege ya kivita ya Marekani, AC-30 iliwashambulia al-Qaeda katika eneo hilo.

Kuna uwezekano kuwa yeye ndiye aliyekuwa mlengwa, kama Pentagone walivyosema: "Mlengwa alikuwa ni kiongozi muhimu wa al-Qaeda katika kanda." Viongozi wa serikali ya Somalia walisema kuwa kifo chake kilithibitishwa katika ripoti ya kiusalama iliyokabidhiwa Somalia na mamlaka ya Marekani. Hata hivyo, katika mahojiano na Shirika la Habari la Uingereza, BBC, balozi wa Marekani nchini Kenya, Michael Ranneberger, alikana kwamba Mohammed hakuwa ameuawa katika mashambulio ya anga, na alisema kuwa msako wa watuhumiwa watatu wa al-Qaeda bado unaendelea.

Mashambulizi hayo yalisababisha vifo vya raia wasiopungua 70 na wengine wengi kujeruhiwa zaidi wakati walipokuwa wakitafuta chanzo cha maji usiku. Akasema kuwa mabaki ya Mohammed, kama yakipatikana yanaweza kutambuliwa kwa msaada wa sampuli ya DNA nchini Comoro.

Mmoja wa wake wa Mohammed na watoto wake walikamatwa wakijaribu kutorokea Kenya wakitokea Somalia. Walikamatwa katika eneo la Kiunga na kupelekwa Nairobi kwa ajili ya mahojiano. Kabla ya mke wa Mohammed kurudishwa Somalia na serikali ya Kenya, kompyuta aliyokuwa nayo ilidhaniwa kuwa ya Mohammed na kwamba kulikuwa na uwezekano "ilikusanya taarifa muhimu za kigaidi juu ya mafunzo na ukusanyaji wa taarifa za kiusalama ikiwa ni pamoja na upelelezi." Mohammed aliaminika "kuwa mtaalamu mzuri katika kompyuta".

Wakati ikiwa haijathibitishwa kama Mohammed alitoroka mapigano nchini Somalia au alikuwepo huko wakati machafuko yakitokea, gazeti kubwa la nchini Madagascar, Midi Madagasikara, liliripoti mnamo Februari, 2007, kwamba Mohammed alikuwa akiishi katika kisiwa cha taifa hilo. Hii ilikuwa tofauti na taarifa za Abdirizak Hassain, akisema kwamba Mohammed aliuawa katika vita ya Ras Kamboni na mashambulizi ya anga ya Marekani. Likinukuu taarifa za kijeshi na "vyanzo vingine," gazeti lilidai kuwa alikuwa katika mji wa Mahajanga.

Agosti 2, 2008, Mohammed aliwatoroka polisi huko Malindi, Kenya, lakini wasaidizi wake wawili walikamatwa. ilisemekana kuwa alipelekwa Kenya kutoka Somalia siku chache kabla, kwa matibabu ya matatizo ya figo. Polisi walitaifisha pasipoti zake mbili na laptop, miongoni mwa mali nyingine. Operesheni ya polisi ilifanyika siku kadhaa kabla ya kumbukumbu ya maadhimisho ya miaka 10 tangu mabomu ya Ubalozi 1998.

Novemba 11, 2009 Mohammed alisimikwa kuwa kamanda katika sherehe ya wazi Kusini mwa Somalia katika mji wa Kismayo, kulingana na tafsiri iliyopokewa na kuchapwa na jarida la The Long War, na tovuti inayowaunga mkono waasi, inayoendeshwa na ukoo wa Kisomalia, wa Hawiye. Kwa mujibu wa tovuti hiyo, alitoa "hotuba yake ndefu".

Akizungumzia kuteuliwa kwake na Osama Bin Laden na kumsifu mtangulizi wake, Saleh Ali Saleh Nabhan, aliyeuawa na kikosi maalum cha majeshi ya Marekani katikati ya mwezi Septemba, Mohammed alikubali jukumu lake wakati wa mabomu ya ubalozi wa Marekani mwaka 1998 ya Kenya na Tanzania. Aliahidi kuwa al-Qaeda na Shabaab watapambana na nchi jirani. Na kuapa kuwa "Baada ya Somalia tutaendelea Djibouti, Kenya na Ethiopia."

Baada ya mashambulizi ya Kampala, Julai 2010 nchini Uganda, yaliyowalengwa watu waliokuwa wakiangalia fainali ya Kombe la Dunia, kiongozi wa kiroho wa al-Shabaab, Sheikh Mukhtar Abu Zubayr alitishia kufanya mashambulizi zaidi katika ardhi ya kigeni, hasa Burundi na Uganda, kutokana na kuwepo kwa askari wa kulinda amani kutoka nchi hizo huko Somalia.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

Jun 8, 2011

Bado kuna utata mkubwa kuhusu demokrasia ya kweli Barani Afrika

Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe

Mpinzani wa Mugabe, Morgan Tsvangirai

Kiongozi wa Kambi rasmi ya Upinzani Tanzania,
Freeman Mbowe

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

RIPOTI iliyotolewa na shirika moja linaloheshimiwa sana nchini Afrika Kusini inayoonesha kuwepo orodha ya wapiga kura hewa milioni 2.6, kwa dhamira ya kuendeleza udanganyifu, katika daftari la kudumu la wapiga kura nchini Zimbabwe, inatuthibitishia kuwa demokrasia ya kweli barani Afrika bado ni kitendawili.

Orodha hiyo inaashiria kuwepo zaidi ya watu elfu 41 walio na umri wa zaidi ya miaka 100 - hii ikiwa ni mara nne zaidi ya idadi ya watu hao nchini Uingereza, ambayo ina idadi kubwa zaidi ya watu na muda mrefu wa kuishi ikilinganishwa na Zimbabwe.

Hii imekuja wakati Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akiitisha uchaguzi ufanyike mwaka huu, huku mpinzani wake na Waziri Mkuu katika serikali ya mseto, Morgan Tsvangirai, akisema kuwa uchaguzi huo unapaswa kuandaliwa mwaka 2012 baada ya katiba mpya kuidhinishwa ili kuhakikisha kuwa kuna uhuru na haki.

Wastani wa umri wa kuishi miongoni mwa raia wa Zimbabwe umeteremka hadi miaka 49, lakini kumeripotiwa kuwa na wapiga kura 41,100 wanaodaiwa kuwa na zaidi ya umri wa miaka 100.

Serikali za Kiafrika zimekuwa na tabia ya 'kuchakachua' ili ziendelee kutawala, na kuna uwezekano kuwa nchi nyingi za Afrika pamoja na kujidai kuwa na chaguzi huru huwa zinatawaliwa kwa mabavu na si kwa ridhaa ya wananchi, kutokana na uchakachuaji kama huu wa kura.

Naamini kwamba kwa mustakabali wa nchi yoyote, vyama vyote vya siasa vina haki sawa mbele ya katiba ambayo pia inawapa wananchi haki na uwezo wa kuchagua chama chochote kati ya hivyo vilivyopo na kukiweka madarakani.

Ni kutokana na ukweli huo, sheria na kanuni za uchaguzi zinahitaji kuwepo na mazingira sawa kwa vyama vyote vinavyoshiriki uchaguzi. Mazingira hayo ni muhimu ili kutoa fursa ya mshindi kupatikana katika misingi ya kidemokrasia ambayo hustawi katika uchaguzi ulio huru na wa haki.

Kwa msingi huo, Serikali nyingi za Kiafrika zinapaswa kujenga utamaduni wa majadiliano ya kina, kukuza na kudumisha demokrasia pamoja na kuwashirikisha watu katika mchakato mzima wa kujiletea maendeleo yao, jambo ambalo litasaidia kwa hakika kujenga na kuimarisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu.

Lakini hii demokrasia, hasa kwa nchi za Afrika ni neno ambalo kwa miaka mingi sasa limekuwa likipita masikioni mwa watu wengi hali ya kuwa wengi wao hata hawajui maana na uzito halisi wa neno hilo. Kwa lugha rahisi, neno hili linatafsiriwa kama aina ya uongozi wa watu kwa ajili ya watu. Uongozi huo hupatikana kwa kufanyika uchaguzi ambao unatakiwa uwe huru na wa haki.

Uchaguzi huru na wa haki unamaanisha kwamba wananchi wagombee nafasi za uongozi wanazotaka ikiwa wana sifa zinazostahili, wawe na uhuru wa kuongea na wananchi wenzao kuhusu sera na mipango yao pindi watakapopewa dhamana ya kuwaongoza ikiwa ni pamoja na kuukosoa uongozi uliotangulia bila uwoga wa aina yoyote kwa kueleza ukweli waziwazi kuhusu 'madudu' yaliyofanywa na uongozi huo na jinsi gani wao wataweza kufanya marekebisho na kuboresha hali ya maisha ya wananchi wenzao pamoja na nchi kwa ujumla.

Pia wawe huru kuwachagua viongozi wanaowataka bila woga wala vitisho, wala kununuliwa hati zao za kupigia kura kwa kilo mbili za sukari na upande wa khanga kutokana na hali zao kimaisha kuwa duni kiasi kwamba hawawezi hata kukumbuka ni lini ilikuwa mara ya mwisho kwao kunywa chai yenye sukari!

Katika hili nchi za Afrika zinatakiwa kuacha unafiki wa kujifanya zinafuata demokrasia na utawala bora wakati sio kweli. Sasa wakati umefika kwa viongozi wa Afrika kuyafanya kwa vitendo wanayohubiri na kuondokana na mfumo wa utawala jeuri na wa kibabe, kwa ajili ya mafao na maendeleo ya watu wa Afrika, Bara ambalo kwa miaka mingi linaendelea kukumbana na kinzani, migogoro na hali ngumu ya maisha.

Wakati umefika kwa nchi za Kiafrika kujenga na kuimarisha misingi ya haki jamii, ugawaji bora zaidi wa rasilimali ya nchi, utengenezaji wa fursa za ajira kwa kuboresha mazingira ya wananchi wanaoishi vijijini ili waweze kutumia ardhi waliyonayo kwa ajili ya maboresho ya hali ya maisha yao. Serikali hizi zina changamoto ya kuondokana na ubinafsi, uroho wa mali na madaraka, mambo ambayo yamelitumbukiza Bara la Afrika katika kinzani, migogoro na vita ya wenyewe kwa wenyewe.

Uongozi ni dhamana nzito ambayo inatakiwa iwe kwa ajili ya watu na nchi husika kwa ujumla na si kwa ajili ya maslahi binafsi ya wachache kama wafanyavyo wengi katika nchi za Afrika, ambao wengi wao wanaingia madarakani kiujanjaunjanja au kinyume na misingi ya demokrasia.
Pia kuwepo matumizi ya nguvu na vitisho katika nchi ni dalili ya ung'ang'anizi wa madaraka na hivyo kuondoa maana halisi ya demokrasia! Ung'ang'anizi huu mara nyingi unaashiria kwamba viongozi wetu hawana sifa ya kupewa dhamana hiyo.

Vitisho na hasa matumizi ya nguvu kwa wapinzani wa serikali ni dalili ya kufilisika kwa ushawishi, kwani huambatana na kimbilio la vitisho kama njia ya kujihami! Serikali kutumia vitisho kwa watu binafsi si haki, kwani mtu unayemzidi uwezo huwezi kumtishia kwa sababu hakutishii au hakusumbui.

Bara la Afrika halina budi kusoma alama za nyakati, kwa kutambua mabadiliko ya uongozi, nafasi na dhamana ya vijana katika kuleta mabadiliko, bila kusahau athari za matumizi ya vyombo vya mawasiliano ya jamii, yanayoiwezesha dunia kuwa kama ulimwengukijiji.

DIMEJI BANKOLE: Spika wa Nigeria anayeonja chungu ya ufisadi

 Dimeji Bankole

 Dimeji Bankole baada ya kutiwa nguvuni

ABUJA
Nigeria

MMOJA wa wanasiasa mashuhuri wa Nigeria amekamatwa na polisi wa kupambana na ufisadi. Spika wa bunge la wawakilishi linalomaliza muda wake, Dimeji Bankole alizuiliwa kuhusiana na madai ya ubadhilifu wa mamilioni ya dola,fedha za serikali ya nchi hiyo.

Alikamatwa baada ya makao yake katika mji mkuu wa nchi hiyo, Abuja kuzingirwa.

Alipoapishwa kuchukua madaraka wiki iliyopita, Rais wa Nigeria, Goodluck Jonathan aliahidi kukabiliana na ufisadi uliokita mizizi nchini Nigeria kwa nguvu zake zote.

Taarifa zilizomkariri mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), Jonah Fisher, zilisema kukamatwa kwa Bankole si suala ambalo halikutarajiwa, baada ya wiki kadhaa za tetesi zilizochapishwa katika magazeti ya nchi hiyo kwamba atakamatwa.

Msemaji wa tume ya kukabiliana na uhalifu wa kiuchumi na kifedha nchini humo (EFCC), alisema kuwa tume hiyo ilipokea taarifa kwamba Dimeji Bankole alikuwa akipanga kutoroka nchini humo.

Sawa na wabunge wengine, muhula wa spika huyo, Dimeji Bankole, ulimalizika Ijumaa iliyopita, na bunge jipya linatarajiwa kuapishwa Jumatatu.

Bankole alipoteza kiti chake katika uchaguzi wa mwezi Aprili, taarifa ya EFCC inasema kuwa Spika huyo anatafutwa kujibu shutuma zinazomkabili za ufisadi.

Miongoni mwa shutuma hizo ni pamoja na matumizi mabaya ya dola milioni 60, na kuchukua dola milioni 65 kama mkopo binafsi akitumia akaunti ya bunge kama dhamana.

Awali msemaji wa Bankole, Idowu Bakare, alitoa taarifa kuwa spika huyo "hakuwahi kunufaika" kwa kutumia nafasi yake. Liliripoti shirika la habari la AP.

Historia ya Dimeji Bankole

Oladimeji Sabur Bankole amezaliwa Novemba 14, 1969. Ni mwanasiasa wa Nigeria na Spika wa Baraza la Wawakilishi anayemaliza muda wake Ijumaa hii. Ni mtoto wa Chifu wa Abeokuta, Alan Bankole, alikuwa mfanyabiashara kabla ya kuchaguliwa kuwa Spika wa Bunge. Alichaguliwa katika umri wa miaka 37, na hivyo kuweka historia ya kuwa Spika mdogo katika historia ya Bunge la Nigeria.

Maisha ya awali, elimu, na michezo

Bankole alizaliwa katika eneo la Abeokuta, ambalo sasa ni sehemu ya Jimbo la Ogun, Novemba 14, 1969. Wazazi wake ni Alan Bankole, mfanyabiashara, na Makamu Mwenyekiti wa zamani wa Taifa wa chama cha All Nigerian Peoples (ANPP) na Seriki Jagunmolu wa Egbaland, na mke wake, Atinuke Bankole, Ekerin Iyalode wa Egbaland.

Gazeti la moja la Thisday liliwahi kubainisha elimu ya Bankole kuwa alisomea shule ya Baptist Boys High School, iliyopo Abeokuta alipoanza mwaka 1979, Chuo cha Albany, kilichopo London, Uingereza kuanzia 1985, Chuo Kikuu cha Reading, kilichopo Reading, Uingereza kuanzia 1989, Chuo Kikuu cha Oxford, kilichopo Oxford, Uingereza mwaka 1991; na Chuo Kikuu cha Havard, Cambridge, Massachusetts, Marekani mwaka 2005.

Mtandao wa All African.com ulitoa taarifa kuwa Bankole ana cheti cha kitaaluma katika usimamizi wa Fedha za Umma kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, Marekani.

Bankole alibainisha kuwa hajawahi kwenda chuo cha kijeshi cha Sandhurst lakini alichukua mafunzo ya maafisa wa kijeshi katika Chuo Kikuu cha Oxford ambapo alikuwa katika Kikosi cha Mizinga.

Bankole ni mchezaji wa mchezo wa wapanda farasi wa kupiga tufe kwa fimbo (polo), na ni mwanachama wa chama cha mchezo huo maaruf kama Lagos Polo Club, ambapo nafasi yake katika mchezo ni ya ulinzi. Pia huwa anafurahia sana mchezo wa soka.

Kazi ya Biashara

Bankole alikuwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Wakala wa Ndege Nigeria, kuanzia mwaka 1995 hadi 1998, Mkurugenzi Mtendaji wa Uendeshaji wa kampuni ya Chuma ya Afrika Magharibi (West African Aluminium Products Ltd) kuanzia mwaka 1998 hadi 2003 na Mkurugenzi wa kampuni ya ASAP Limited kuanzia mwaka 2000 hadi 2003. Pia yeye ni mchumi.

Kazi ya kisiasa

Mwaka 2002, Bankole alichaguliwa kwenye Baraza la Wawakilishi kwa tiketi ya People's Democratic party (PDP) kuwakilisha eneo la Abeokuta Kusini katika Jimbo la Shirikisho la Ogun. Alikuwa Naibu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Fedha wakati Amim Bello Masaari alipokuwa Spika, (Farouk Lawan alikuwa Mwenyekiti wa kamati) na aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi ya Usafiri. Kamati zingine alizopitia ni ya Ulinzi, Mambo ya Ndani na Benki, na Fedha.

Bankole alichaguliwa tena mwezi Aprili 2007. Alichukulia utashi wake katika ubunge kuuhusha na ulinzi na fedha.

Baraza la Wawakilishi

Uspika: Mwezi Septemba 2007, kamati ilimhoji Spika, Patricia Etteh kuhusu matumizi yake ya milioni 628 (dola milioni 4.8) kwa ajili ya ukarabati wa nyumba na magari.

Spika huyo alikana makosa hayo, lakini wawakilishi wengi hawakuwa na furaha kutokana na jitihada zake za kujitetea mwenyewe, juhudi zikazidishwa na wawakilishi hao katika kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa. Rais wa zamani, Olusegun Obasanjo na wanachama ngazi za juu wa PDP waliendelea kumuunga mkono Etteh, lakini sehemu kubwa ya chama, wakiongozwa na Lawan na pamoja na Bankole, walimtaka ajiuzulu. Kulikuwa na taarifa kwamba Bankole, alikuwa ni miongoni mwa wagombea wengine, waliokuwa na matumaini makubwa ya kumrithi Etteh mwezi Oktoba 5, 2007.

Baada ya Etteh kujiuzulu nafasi ya uspika mnamo Oktoba 30 (pamoja na naibu wake, ambaye pia aliingizwa kwenye kashfa hiyo), mwanachama wa Kundi la waadilifu (waliompinga Etteh), Terngu Tsegba akawa Spika wa mpito. Samson Osagie wa Jimbo la Edo alimpendekeza Bankole kuwania nafasi ya Spika, na Lynda Ikpeazu wa Jimbo la Anambra akaunga mkono pendekezo hilo.

Tarehe 1 Novemba, Bankole alichaguliwa kushika nafasi iliyoachwa wazi na Etteh. Mpinzani wake mkubwa alikuwa ni Mwakilishi wa Jimbo la Osun, George Jolaoye, ambaye alimshinda kwa kupata kura 304 dhidi ya kura 20 (na kura 4 hazikupigwa).

Etteh alikuwa ni miongoni mwa wale ambao hawakumpigia kura Bankole. Naibu Spika mpya alikuwa Usman Nafada Bayero.


Wakati wa kuchaguliwa kwake, Bankole alisema "Nachukua vazi la uongozi katika wakati mgumu sana, lakini hizi ni nyakati ngumu, tunahitaji kujenga imani tena na kuwahakikishia watu kwamba sisi bado ni wawakilishi wao. Nahitaji kuwa na Bunge huru ambalo Wanigeria watajivunia, hii ni kazi yangu ya kwanza."

Wiki moja tu baada ya kuchaguliwa, wapinzani wake wa kisiasa walidai kuwa Bankole hakukamilisha mafunzo yake ya Jeshi la Vijana la Kujenga Taifa (National Youth Service Corp, NYSC), ambayo ni ya lazima kwa Wanigeria wote wanaohitimu Chuo Kikuu wakiwa chini ya umri wa miaka thelathini, na wakataka ajiuzulu kwa sababu ya suala hilo. Uongozi wa Jimbo la Bankole wakatoa uthibitisho wake wa kumaliza NYSC, na kukomesha uvumi.

Mnamo Juni 22, 2010, Bankole aliwasimamisha wawakilishi 11 wa Bunge kwa muda usiojulikana kwa kuonesha utovu wa nidhamu na kupigana ndani ya Bunge.


Kashfa ya 2009

Mwaka 2009, Bankole alishitakiwa kwa matumizi makubwa ya zaidi ya Naira bilioni 52 zilizotumika kama gharama za usafiri, kitendo kilichoelezwa na wajumbe wengi wa Baraza la Wawakilishi kama 'ubinafsi na ulaghai', kwa kuzingatia kiwango cha sasa cha umaskini miongoni mwa asilimia kubwa ya wakazi wa Nigeria.

Kukamatwa 2011

Dimeji Bankole anatiwa mbaroni na kikosi cha polisi cha kupambana na rushwa kwa tuhuma za wizi wa mamilioni ya pesa za serikali. Bankole alitiwa mbaroni muda mfupi baada ya kuwepo taarifa za kutaka kutoroka nchini.

Msemaji wa taasisi ya kuzuia rushwa nchini Nigeria alisema kuwa alipata taarifa kwamba Bankole alikuwa na mipango ya kutoroka nchini humo ndiyo maana wameharakisha kumkamata. Spika huyo anadaiwa kukopa zaidi ya dola za Marekani milioni 60 benki kwa kutumia jina la Bunge wakati mkopo huo ulikuwa ni binafsi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.


Jun 3, 2011

UNYWAJI MAZIWA: Tunakatishwa tamaa na wachakachuaji

 Bidhaa za Kiwanda cha Tanga Fresh katika maonyesho hayo

 Baadhi ya wanafunzi wa shule mbalimbali za msingi za Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wakiandamana kwenye barabara ya Kawawa kuadhimisha kilele cha wiki ya uhamasishaji unywaji wa maziwa

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii ilikuwa ni ya maadhimisho ya wiki ya unywaji maziwa ambapo Bodi ya Maziwa Tanzania kwa kushirikiana na Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi iliandaa maadhimisho ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa Kitaifa yaliyofanyika mkoani Dar es Salaam kuanzia tarehe 28 Mei mpaka 31 Mei, 2011.

Maadhimisho hayo ya kitaifa yalihusisha uhamasishaji wa unywaji maziwa yaliyoambatana na maonesho ya bidhaa zitokanazo na maziwa yanayozalishwa Tanzania, pamoja na Mkutano wa mwaka wa Baraza la Wadau wa maziwa

Kaulimbiu ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa mwaka 2011 ilikuwa ni Kunywa maziwa kwa afya yako; Jenga uchumi wa nchi yako’.

Madhumuni ya Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa yalikuwa na lengo kuu la kuhamasisha unywaji wa maziwa kwa afya ya binadamu kwa kuwa maziwa ni chakula bora kwa watu wa rika zote na kutoa taarifa kuhusu changamoto na fursa za sekta ya maziwa katika kuondoa umasikini kwa Watanzania.

Pamoja na hayo Wiki ya Uhamasishaji wa Unywaji wa Maziwa inachangia katika kuboresha soko la maziwa na bidhaa zake na pia kutoa fursa kwa wadau kukutana na kubadilishana uzoefu katika kuendeleza sekta ya maziwa.

Imekuwa ikisemwa kuwa pamoja na kuwa Tanzania ni nchi ya tatu kwa wingi wa mifugo katika Bara la Afrika, lakini Watanzania wengi hawana kabisa utamaduni wa kunywa maziwa, kula mayai na nyama kama wenzao wa Uganda na Kenya!

Kwa maana hiyo, kwa kuwa hatuna utamaduni wa kunywa maziwa, wananchi wa Kenya ndio wanaoongoza kwa kunywa maziwa wakifuatiwa na Uganda na Rwanda ingawaje sisi tumejaaliwa kuwa na mifugo wengi ambao wangetosheleza mahitaji yetu ya vyakula hivyo.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali zilizofanywa, unywaji wa maziwa nchini uko chini sana na inasemwa kwamba mtu mmoja anakunywa lita 40 tu za maziwa kwa mwaka, tofauti na viwango vilivyowekwa na Shirika la Chakula Duniani (FAO), ambapo viwango vya FAO vinataka kila mtu anywe maziwa lita 200 kwa mwaka.

Napenda niseme wazi kama mwananchi na Mtanzania kuwa mimi ni mmoja wa watu wanaopenda sana wanywe maziwa, nikiwa nayahitaji maziwa kwa sababu kuu mbili: kwanza nayahitaji maziwa kwa ajili ya afya yangu, hasa ikizingatiwa kuwa nina vidonda vya tumbo na maziwa hunipa ahueni kubwa, na sababu ya pili ambayo ni ya kiafya vilevile kutokana na kutumia muda mwingi kwenye kompyuta, ambapo kuna madhara ya mionzi tunashauriwa kunywa maziwa kila mara ili kuepuka madhara hayo ya mionzi.

Si kwambwa hatupendi kunywa maziwa bali kuna mambo kadhaa kama nitakavyoyaeleza baadaye; moja ya matatizo makubwa yanayotukatisha tamaa ni kwamba maziwa mengi yanayouzwa maeneo ya mijini hususan Dar es Salaam si maziwa halisi kama wafanyabiashara wa maziwa wanavyotaka tuamini, kwa kuwa wafugaji tayari huwa wamekwishayachakachua kwa kuongeza maji ili yawe mengi.

Na haiishii hapo tu kwani yakishafika kwa wafanyabiashara nao hupenda kuchukua maziwa hayo kiasi kidogo na kuchanganya na maziwa ya unga au wakati mwingine hata unga wa ngano, kisha wanatia mafuta kidogo ili kupata utando wa mafuta juu yake.

Maziwa ya moto yanayouzwa kwenye vibanda vingi jijini Dar es Salaam, pindi ukiyatia mdomoni huwezi kuisikia ile radha ya maziwa, na pia huwa yana utando wa mafuta ambao si wa kawaida hasa kwa mtu anayeyafahamu vizuri maziwa halisi.

Lengo la wafanyabiashara kuamua kuchakachua maziwa ni ili wapate faida kubwa bila kujua kwamba wanajiharibia soko na wakati huohuo kuhatarisha afya za watumiaji kwani hata hayo maji wanayotumia kuchakachua sidhani kama ni maji salama.
Sababu nyingine inayosababisha Watanzania kuonekana kuwa hawapendi kunywa maziwa ni kutokana na kuendelea kwa umasikini na hali ngumu ya kiuchumi katika ngazi za kifamilia na kitaifa, hali hii imefanya afya za wananchi ziendelee kuwa hatarini kutokana na ugumu wa maisha na hivyo kufanya hata baadhi ya vyakula muhimu ikiwemo maziwa kuwa anasa kwa Mtanzania wa kawaida.

Kauli mbalimbali zinazotolewa na baadhi ya viongozi na watafiti kwamba eti Watanzania wafundishwe (waelimishwe) kuhusu umuhimu wa kula nyama, mayai na kunywa maziwa, kwangu mimi nahisi kama hiki ni kichekesho cha mwaka! Ni kichekesho kwa kuwa sidhani kama kuna Mtanzania asiyejua umuhimu wa vyakula hivyo kwa mwili wa binadamu!

Wanapodai kuwa tuelimishwe, wanatuelimisha katika lipi wakati tuna kliniki zimejaa nchini takriban kila kijiji, ni nani ambaye hajawahi kufundishwa au ambaye mama yake hajafundishwa umuhimu wa vyakula hivyo? Inaposemwa kuwa Watanzania hawanywi maziwa, hawali nyama na mayai sio kwa sababu hawana elimu ya umuhimu wa lishe hiyo bali hawana imani na maziwa yanayouzwa na wafanyabiashara wetu na pia hali ya kiuchumi haiwaruhusu kufanya hivyo!

Maziwa pekee yanayoonekana kuaminika miongoni mwa jamii zetu au kuwa halisi ni yale yanayosindikwa viwandani ambayo hata hivyo kwa hali halisi ya kiuchumi ya Watanzania wengi ni sawa na anasa kuyanunua.

Naomba, maadhimisho haya ya wiki ya kunywa maziwa, wahusika pia wangetumia fursa hiyo kunyoosheana kidole kwa kujiharibia soko kwa kuchakachua maziwa. Lakini pia ni jukumu la Serikali kuchukua hatua na kuangalia jinsi ya kudhibiti uchakachuaji huu ili kulinda afya za Watanzania na kwa kufanya hivyo, biashara hiyo itakuwa kubwa na hata Serikali itapata mapato kupitia kodi.