Jun 1, 2012

Kama tunataka kuulinda muungano turuhusu mjadala wa wazi

Mwalimu Nyerere akichanganya mchanga kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania, Aprili 26, 1964

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania ulizaliwa Aprili 26, 1964 na hivyo Alhamisi ya Aprili 26 mwaka huu muungano wetu umetimiza miaka 48. Nilishuhudia sherehe za Muungano kupitia televisheni, na hali imeendelea kubainisha kuwa tunalazimisha kusherehekea huku kukiwa na manung’uniko kutoka kwa wananchi na hata baadhi ya viongozi wa kisiasa wakionekana ama kuupinga mfumo wa Muungano au kutoutaka kabisa Muungano huu.

Wazanzibar wanalalamika wamemezwa na Tanzania Bara, Watanzania Bara (Watanganyika) wanalalamika kuwa wameipoteza Tanganyika yao na wananyonywa kupitia mwamvuli wa Muungano wa Tanzania, lakini wachache katika serikali yetu wameapa kuwa wataulinda muungano huu kwa nguvu zote!

Ni ajabu sana kuwa kila upande unalalamika! Inashangaza sana katika vuta nikuvute hii eti kuna kundi linasema litaulinda Muungano kwa nguvu zote! Katika kuulinda huu Muungano kumekuwepo tafsiri ambayo inahitaji ufafanuzi; kuulinda kwa nguvu zote maana yake nini?

Wafuatiliaji wa masuala ya siasa wanaiona kauli ya kuulinda ni kuzuia watu wasiujadili. Kutoruhusu uvunjike. Huku wengine (nikiwemo mimi) tukijiuliza, ya nini kuwa na muungano bila kuujadili? Inafaa nini kuishi kwa mazoea? Na kwa faida ya nani? Huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akisema kuwa jambo pekee wanalopaswa wananchi kujadili kuhusu Muungano ni kuuboresha! Inawezekanaje watu waboreshe kitu ambacho hawajakubaliana umuhimu wake?

Rais amesahau kuwa Watanzania walio wengi leo hii ni vijana waliozaliwa baada ya Muungano. Ingawa wamesoma habari za Muungano katika vitabu vya historia lakini hawauelewi vyema, ndiyo maana hata shamrashamra za serikali na wananchi juu ya Muungano zimeshuka siku hizi. Tunachoshuhudia ni wananfunzi kulazimishwa kwenda kwenye sherehe hizi bila ridhaa yao.

Kama vijana hawaujui vyema Muungano wetu, kwa nini sasa wanataka kunyimwa fursa ya kuujadili? Fursa imejitokeza lakini viongozi wanatuzuia? Hivi kweli wanautakia mema Muungano huu?

Hapa sijui kama kweli kuna nia ya dhati ya kuuboresha. Kutoujadili? Kutorusu uvunjike? Hivi tunayafanya haya kwa faida ya nani? Wananchi ambao ndiyo wenye nchi yao wanataka kuandika upya historia yao tena kwa nyakati zao
lakini viongozi wanataka kuwaenzi waasisi kinafiki! Nani mwenye nchi? Wananchi au viongozi?

Siandiki haya kwa kuwa labda siutaki Muungano, hasha! Nautakia mema ndiyo maana napenda tukae mezani kuujadili, tuangalie kasoro zote zilizopo na kuzirekebisha ili hatimaye tuingie kwenye Muungano uliopata ridhaa za wananchi wa pande zote. Ni kufilisika kimawazo kudhani kwamba anayehoji Muungano ana nia ya kuuvunja. Badala yake, ni kuchochea mjadala mpana na wa kina kuhusu umuhimu wa Muungano. Hatutakuwa na muungano imara kama viongozi wataendelea kutulazimisha bila kusikiliza hoja na manung’uniko yetu.

Hata hivyo, kuvunjika kwa muungano si jambo la ajabu, kama hatutaruhusu mijadala ya wazi tunaweza kuishia walikoishia wengine. Tusidhani kuwa sisi tuna akili zaidi au tumebarikiwa zaidi ya wengine. Tuna kipi cha ajabu? Kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa mojawapo ya waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia iliyotengana na Eritrea, muungano wa Senegambia ulishindikana kwa kuwa wananchi hawakushiriki na hatimaye walitengana na kubaki nchi mbili za Senegal na Gambia, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo sasa ni nchi mbili za Rwanda na Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.

Inashangaza sana kuona kuwa kundi dogo linataka kubinafsisha mawazo ya walio wengi, vijana na wasomi wa taifa hili wanashindwa kuhoji mambo kwa mapana yake. Tunapaswa tujiulize, hivi kwa nini tuliungana? Huu si wakati tena wa kuleta sababu dhaifu eti tunaleta umoja au eti kwa vile sisi ni ndugu. Mbona hatuungani na Wakenya wakati nchi zote hizi zina undugu?

Kwa nini hatupewi nafasi ya kuhoji nini sababu hasa ya muungano huu? Wenye majibu wote kwa sasa hawapo na yaliyobaki ni majibu ya kufikirika tu, nafasi ya uongo ni kubwa. Bila majibu haya, ni vigumu ni bora watu wakajadili na wakaja na aina ya muungano wanaoutaka.

Hali ya mashaka inaugubika Muungano huu, inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.

Habari zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya mustakabali wa nchi yao.

Ndiyo maana nafikiri kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.

Ukiuangalia Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima na hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.

Kwa kuwa tupo katika kipindi cha kuandika Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.

Hofu za viongozi wetu zinatoka wapi? Mbona Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na Muungano, wanaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.

Kero hizi ni pamoja na mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka kuuboresha Muungano. Muundo wa Muungano, hata kama chama tawala kimekuwa kikidai kuwa sera yake ni ya serikali mbili, linatakiwa liwe jambo litakaloamliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa wa mambo 11 kama ambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa kinyemela.

Hata hili la ushirikiano wa kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na ndiyo maana Zanzibar waliamua kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.

Kero nyingine ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili limeondolewa bila ya kura ya maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote

Miaka ya hivi karibuni zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibar kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia ikilalamikiwa. Haya yanahitaji muungano kuhojiwa kwa uwazi ili majibu ytaolewe. Kama kutakosekana majibu ya maana, itakuwa ni kazi bure kutumia maneno makali kwani wananchi wataukataa.

No comments:

Post a Comment