Jan 19, 2012

Kuna maisha bora kwa kila Mtanzania kwa gharama hizi?

  Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura), Harun Masebu, akizungumza na waandishi wa habari

Makao Makuu ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco)
yaliyopo Ubungo jijini Dar es Salaama

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza tena kupanda kwa gharama za umeme. Mwaka jana ilitangaza ongezeko la bei ya umeme kwa asilimia 18.5. Mwaka huu imeongeza bei ya umeme kwa zaidi ya asilimia 40 kuanzia Januari 15 huku mgao wa umeme ukiendelea ingawa hata huo upatikanaji wa umeme ni wa mashaka, huku chini ya asilimia 15 ya Watanzania wote ndiyo wanaopata umeme! Kupanda kwa bei ya umeme hakika kunazidisha ugumu wa maisha ambao upo hasa kwa wananchi walio wengi ambao ni wenye kipato cha chini.

Pamoja na Tanesco kupandisha gharama ya umeme, lakini shirika hilo bado halijafanya maboresho ya mitambo kwa kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta madhara makubwa ikiwemo kuunguza vitu majumbani na maofisini.

Hatua ya kupandisha gharama hizi inazidi kuwaongezea umaskini Watanzania ambao tayari wana maisha magumu mno kwa sababu hata bei ya awali wengi walikuwa hawaimudu. Jumatano asubuhi kwenye kipindi cha asubuhi cha moja ya vituo vyetu vya televisheni nilimsikia mbunge wa zamani wa Tabora Mjini, Siraji Kaboyonga akitetea ongezeko hili la bei, lakini haikuniingia akilini kutokana na sababu alizozitaja.

Kupandisha bei bado hakuwezi kuwa suluhisho au kuifanya Tanesco ijiendeshe kwa ufanisi kwani kinachotakiwa ni mbinu za kiutendaji na ubunifu katika kuliendesha shirika. Mbona mapato Tanesco yako mengi, isipokuwa imekosa mbinu na mikakati ya kuzuia wizi wa umeme unaofanywa na watumiaji wengi wa umeme.

Mfano eneo ninaloishi na hata maeneo mengi ninayotembelea, wezi wanaotumia umeme wa wizi bila malipo ni wengi, tena wanashirikiana na wafanyakazi wa Tanesco na wala hakuna jitihada za makusudi kuwazuia vishoka. wanapandisha bei ya umeme wakati hata huduma zenyewe hazijaboreshwa!

Kupanda kwa bei hakika kunapunguza watumiaji wa umeme na kuwarudisha watu katika utumiaji wa vibatari na mishumaa kwa sababu ya kuogopa gharama ya umeme. Hali hii imefika hapo ilipo kutokana na mfumo wa nchi hii kuegemea zaidi kwenye siasa kuliko kujali utaalamu. Siyo siri kuwa wananchi wa Tanzania kwa sasa wanaishi kwenye kiza kinene baada ya kujitokeza jinai ya kugawiwa umeme wakati huu.

Ni aibu kuendelea kutegemea chanzo cha maji kuzalisha umeme wakati tuna vyanzo mbadala. Uchumi wa Tanzania unaporomoka kwa kasi kubwa kutokana na ukosefu wa nguvu ya umeme wa uhakika pamoja na kuwa madini ya Uranium yanayotengeneza nishati ya nyuklia yanapatikana kwa wingi Tanzania. Madini ambayo kwa nchi kama Iran na Korea yanatumika kwenye uzalishaji nguvu za umeme kwa njia ya nyuklia.

Moja ya tatizo ambalo tumekuwa nalo kipindi kirefu sasa, Watanzania wengi tunategemea nishati hii kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa ya maji. Miundombinu bado haijaboreshwa halafu linakuja suala la kuongeza bei ambalo ni kumwongezea mwananchi mzigo mkubwa usiobebeka na hiyo ni hatari kwa taifa, kwani itashusha hata uzalishaji na uchumi wa taifa utashuka.

Kwa nini tusiachane na vyanzo hivi na kuangalia vyanzo mbadala, kwani siku zote ambazo mabwawa hayo hupungua kina cha maji au kukauka, tumekuwa tukishuhudia mgao mkali, jambo ambalo tunaamini sasa umefika wakati wa serikali kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hii.

Hebu fikria ni biashara ngapi zinaathirika kutokana na mgao huu wa umeme. Hata kama ni biashara ya mwananchi wa kawaida ya kuuza barafu au juisi bado ina mchango katika ujenzi wa taifa changa
kama Tanzania. Kukosekana umeme wa uhakika katika mgao wa siku ni pigo kubwa kwa taifa kwani shughuli nyingi za uzalishaji zinasimama.

Mgao huu wa umeme licha ya kudhoofisha uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja unasababisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Majenereta yanayofanya kazi mchana kutwa mijini yamekuwa yanachafua mazingira kwa moshi na hata kelele. Mgao wa umeme mbali na kusababisha kuparaganyika kwa uchumi pia ni chanzo cha rushwa. Mara nyingi sehemu za wenye pesa na vigogo serikalini huwa haziathiriki na kadhia kama hizi. Hii ni kwa vile ama wenye nazo wanahonga watendaji wa Tanesco, au wenye madaraka wanapendelewa kwa vile wameshikilia kila kitu katika nchi hii.

Inaposemwa eti ongezeko hili haliwagusi wenye kipato kidogo naona kama kuwafanya Watanzania mbumbumbu. Kwani ongezeko linapovikumba viwanda basi hata bidhaa zitapanda bei na watumiaji ni hawa hawa walalahoi.

Gharama hizi za umeme ni kama muendelezo na mzigo mkubwa wanaotwishwa wananchi baada ya matatizo mengi yanayowakabili, huku ikisemwa kuwa serikali ndiye mdaiwa sugu lakini sidhani kama inaguswa. Kwa gharama hizi hakika ile kaulimbiu ya Rais Kikwete ya maisha bora kwa kila Mtanzania itabaki kuwa ndoto nzuri ya mchana.

Alamsiki…

No comments:

Post a Comment