Jun 1, 2012

JOYCE BANDA: Kutoka mwanamke aliyenyanyaswa na mume hadi Rais

Joyce Banda

LILONGWE,
Malawi

ALIYEKUWA makamu wa Rais wa Malawi, Joyce Banda, amechukua madaraka ya kuiongoza nchi hiyo ya Kusini mwa Afrika Jumamosi ya Aprili 6, mwaka huu  kufuatia kifo cha Rais Bingu wa Mutharika.  Banda ambaye hana undugu na Rais wa kwanza wan chi hiyo, Hayati Dk. Kamuzu Banda anakuwa rais wa kwanza  mwanamke Kusini mwa Jangwa la Sahara, na aliapishwa mbele ya bunge katika mji mkuu wa Malawi, Lilongwe.

Banda, ambaye alikuwa makamu wa rais tangu mwaka 2009, alishangiliwa na kupigiwa makofi kabla na baada ya shughuli hiyo. Mutharika, 78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alhamisi, ingawa kifo chake hakikuthibitishwa hadi Jumamosi.

Kuchelewa kutangazwa kifo chake kulisababisha wasiwasi kuhusu nani anaongoza nchi hiyo. Kulikuwa na tetesi kuwa watu wa karibu wa Rais Mutharika walikuwa wakitaka kubadili katiba ya nchi ili kumzuia Banda kuchukua madaraka, na badala yake kumpa ndugu wa rais, Peter Mutharika ambaye ni waziri wa mambo ya nje wadhifa huo.

Katiba ya Malawi inataja kwamba makamu wa rais atachukuwa madaraka ya nchi iwapo rais amefariki dunia lakini ilionekana kwamba Mutharika alikuwa akimuandaa mdogo wake Peter kuwa mrithi wake.

Banda alifarakana na Rais Mutharika mwaka 2010 na kisha kuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wake. Alifukuzwa kutoka chama cha DPP na kuunda chama chake cha Peoples Party.

Hofu ya kuzuka kwa mapambano ya kuwania nafasi ya kumrithi rais huyo imeanza kupungua kutokana na asasi za kitaifa kuunga mkono makabidhiano ya madaraka kwa kuzingatia katiba. Serikali imethibitisha rasmi kifo cha Mutharika mwenye umri wa miaka 78 hapo Jumamosi ikiwa ni siku mbili baada ya kufariki kwake dunia kutokana na mshtuko wa moyo.

Banda mwenye umri wa miaka 61 alikuwa na mkutano na waandishi wa habari katika mji mkuu wa Lilongwe ambapo alitangaza siku 10 za maombolezo rasmi ya Mutharika ambaye aliitawala Malawi kwa miaka minane. Ameamuru bendera za taifa kupepea nusu mlingoti na shirika la utangazaji la taifa kupiga muziki wa kuhuzunisha.

Ametowa wito kwa Wamalawi kuwa watulivu na kudumisha amani katika kipindi hiki cha maombolezo. Banda alikuwa akizungumza huku akiwa ameandamana na mwanasheria mkuu wa serikali na wakuu wa jeshi na polisi.

Kabla ya kuchukua rasmi madaraka hayo aliulizwa na mwandishi wa habari iwapo alikuwa anachukuwa madaraka ya urais, Banda mwanaharakati wa haki za wanawake alijibu "kama unavyoona, katiba inafaya kazi".

Banda anatazamiwa kuiongoza nchi hiyo hadi uchaguzi ambao umepangwa kufanyika hapo mwaka 2014. Ofisi ya rais na baraza la mawaziri vimetoa taarifa yenye kuwahakikishia raia na jumuiya ya kimataifa kwamba katiba ya Jamhuri ya Malawi itaheshimiwa ipasvyo katika kuongoza kipindi cha mpito.

Historia yake

Joyce Hilda Banda ni mwelimishaji na mwanaharakati wa haki za jinsia kwa watu wa chini. Alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi kuanzia mwaka 2006 hadi 2009 na Makamu wa Rais wa Malawi kuanzia Mei 2009 kabla ya kuukwaa urais Aprili 7,  2012. 

Pia alikuwa Mbunge na Waziri wa Jinsia, Mambo ya Watoto na Huduma za Jamii. Kabla ya kushiriki kikamilifu katika siasa alikuwa mwanzilishi wa Taasisi ya Joyce Banda (Joyce Banda Foundation), mwanzilishi wa Chama cha Taifa cha Wafanyabiashara Wanawake (NABW), Mtandao wa Viongozi Vijana Wanawake na Mradi Njaa. Alitajwa katika jarida la Forbes mwaka 2011 kama mwanamke wa tatu mwenye nguvu zaidi na ushawishi katika Afrika.

Ni mwanzilishi na kiongozi wa Chama cha Watu (People's Party) kilichoundwa mwaka 2011, na kabla ya kifo cha Bingu wa Mutharika alionekana kuwa na uwezekano wa kugombea Urais wa Malawi katika uchaguzi mkuu wa 2014. People's Party wamepanga kuwa na mkataba baadaye mwaka huu, pamoja na uwezekano wa kuthibitishwa kwa Joyce Banda kuwa kiongozi wa chama.

Maisha ya awali

Banda anatokea Malemia, kijiji katika Wilaya ya Zomba nchini Malawi. Ana cheti cha Cambridge. Ana Shahada ya Sanaa katika Elimu ya Mafunzo kutoka Chuo Kikuu cha Columbus, na Diploma katika Usimamizi aliyopata nchini Italia. Katika umri wa miaka 25, alikuwa na watoto watatu na alikuwa akiishi mjini Nairobi, Kenya. Mwaka 1975, harakati za wanawake nchini Kenya zilimtia moyo Banda na aliwachukua watoto wake na kuachana na ndoa yake ya kwanza ya unyanyasaji. Kati ya 1985 na 1997 Banda alianzisha biashara na makampuni mbalimbali ikiwa ni pamoja na Ndekani Garments, (1985), Akajuwe Enterprises (1992), na Kalingidza Bakery (1995). Mafanikio yake yalimuongoza kuwasaidia wanawake wengine kufikia uhuru wa kifedha na kuvunja mizunguko ya kunyanyasika na umaskini. 

Ni dada wa Anjimile Oponyo, Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya Raising Malawi Academy for Girls iliyoanzishwa na Madonna. Ameolewa na Richard Banda, aliyekuwa Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Malawi.

Maisha ya Siasa (2004-2009)

Kabla ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Makamu wa Rais na baadaye Rais, alikuwa Mbunge wa jimbo la Zomba-Malosa. Pia alikuwa Waziri wa Huduma za Jinsia, Ustawi wa Watoto na Jumuiya kabla ya kuteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Rais Bingu wa Mutharika Juni 1, 2006. Kama Waziri wa Jinsia, Ustawi wa Watoto na Huduma za Jamii alipigania hadi kutungwa Sheria ya Unyanyasaji wa kijinsia, ambayo ilishindwa kwa miaka saba kabla. Aliunda Jukwaa la Taifa la Usaidiaji wa Yatima na walio kwenye mazingira magumu na Kampeni ya Kutovumilia dhidi ya unyanyasaji wa watoto.

Makamu wa Rais (2009-2012)

Banda alikuwa mgombea mwenza wa urais wa chama cha Democratic Progressive (DPP) katika uchaguzi wa Rais Mei 2009, akigombea sambamba na Mutharika, mgombea urais wa DPP.  Kwa mshangao ndani ya DPP, Joyce Banda na makamu wa pili wa rais, Khumbo Kachali, walifukuzwa kama makamu wa Rais wa DPP tarehe 12 Desemba 2010 kwa kile kilichojulikana 'kupambana na chama hicho’. Katika majaribio ya kumdhoofisha, rais aliendelea kutoa majukumu ambayo awali yalikuwa chini ya Banda na kuyakabidhi kwa Callista Mutharika ambaye aliingizwa katika baraza la mawaziri mwezi Septemba 2011.

Uhusiano kati yake na Rais wa Malawi uliendelea kuwa wa wasiwasi kwa sababu ya Rais kujaribu kumpa nafasi ndugu yake, Peter Mutharika kama mwandamizi wa chama na rais mtarajiwa. Ingawa Banda alitimuliwa kutoka nafasi ya Makamu wa Rais wa DPP pamoja na Makamu wa Rais wa pili Khumbo Kachali, aliendelea kuwa Makamu wa Rais wa Malawi kama ilivyoainishwa katika katiba ya Jamhuri ya Malawi. Hatua hii ilisababisha wengi kujitoa DPP na kuunda mitandao ambayo ilimsaidia makamu wa rais ili kusaidia ugombea wake wa urais wa Malawi katika uchaguzi mkuu wa 2014. DPP ilikanusha kujitoa kwa wengi na kusisitiza kwamba waliojitoa walikuwa wachache tu.

Urais

Baada ya kifo cha Mutharika, kulikuwa na hofu ya kugombea madaraka kufuatia taarifa ya Waziri wa Habari na Elimu ya Uraia, Patricia Kaliati, kuwa "mwenendo wa Joyce Banda ni katika kutengeneza chama chake cha upinzani kimsaidie katika kufanikiwa urais." Shirika la habari la Ufaransa lilitoa taarifa kuwa rais wa zamani wa Malawi, Bakili Muluzi,  kusisitiza “utaratibu wa kufuata katiba,” akisema makamu wa rais lazima achukue madaraka moja kwa moja kwa mujibu wa katiba. “Natoa wito kufuata kikatiba, kwa ajili ya amani kuendelea na utaratibu. Sheria za Malawi ziko wazi kabisa kuwa makamu wa rais anachukua madaraka” pale ambapo hayupo rais. Tunatakiwa kuzuia hali ambapo kuna machafuko. Hebu tufuate katiba. Hatuna chaguo zaidi ya kufuata katiba. Ni muhimu sana kuwepo amani na utulivu,” alisema.

Vikosi vya Usalama vya Malawi pia vilitaka katiba ifuatwe. 

Chama cha wanasheria wa Malawi pia kilithibitisha kuwa chini ya kifungu cha 83 (4) cha katiba ya Malawi, Banda ndiye mrithi halali wa Urais. Aliapishwa kama rais mwanamke wa kwanza nchini humo Aprili 7, na kutoa wito kwa umoja wa kitaifa. Alipongezwa na Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe .

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment