Jun 1, 2012

FRANCOIS HOLLANDE: Japo ilionekana kuwa ni safari ndefu hatimaye katua Ikulu

Francois Hollande


PARIS,
Ufaransa

TAREHE 6 Mei 2012, Ufaransa imempata rais mpya kupitia chama cha kisoshalisti, Francois Hollande, ambaye amemshinda rais aliyekuwa madarakani akitarajia kupata kipindi kingine cha uongozi, Nicolas Sarkozy, katika uchaguzi wa marudio uliofanyika mwishoni wa juma lililopita.

Hollande anakuwa rais wa kwanza wa kisoshalisti nchini Ufaransa kwa kipindi cha miaka 17; na amekuwa wa kwanza kumshinda rais aliyetumika kwa muhula mmoja tu, tangu mwaka wa 1981.

Wasoshalisti wanasema kazi ya mwanzo ni kufanya majadiliano tena juu ya sera za kiuchumi za Umoja wa Ulaya. Punde baada ya kura za awali kuonesha matokeo, Rais Sarkozy alikiri kuwa ameshindwa, na alimpigia simu Hollande kumtakia heri.

Historia yake

François Gérard Georges Hollande alizaliwa Agosti 12, 1954. Aliwahi kuwa katibu wa kwanza wa chama cha Socialist cha Ufaransa kuanzia 1997 hadi 2008 na Naibu wa Bunge la Ufaransa wa Jimbo la Corrèze 1 tangu mwaka 1997, na hapo awali aliwakilisha kiti cha ubunge kuanzia 1988 hadi 1993. Alikuwa Meya wa jiji la Tulle kuanzia mwaka 2001 hadi 2008, na alikuwa Rais wa Baraza Kuu la Corrèze kuanzia 2008 hadi 2012.

Maisha ya awali

Hollande alizaliwa katika eneo la Rouen, Seine-Maritime, Upper Normandy, katika familia ya kati. Mama yake, Nicole Frédérique Marguerite Tribert (1927-2009), alikuwa mfanyakazi wa jamii, na baba yake, Georges Gustave Hollande, alikuwa daktari wa koo, pua na masikio ambaye "aliwahi mara moja kugombea katika siasa za mitaa". Ubini wa "Hollande" "unaaminika kutoka kwa mababu waliotoroka Holland (Netherlands) katika karne ya 16 na kuchukua jina la nchi yao ya zamani." Hollande alilelewa katika dhehebu la Katoliki.

Elimu

Alisoma katika shule ya Saint Jean-Baptiste de La Salle, baadaye HEC Paris, shule ya utawala ya École, na Taasisi ya Mafunzo ya Siasa ya Paris. Alimaliza mwaka 1980. Aliishi nchini Marekani katika majira ya joto ya 1974 alipokuwa mwanafunzi wa chuo kikuu. Mara baada ya kuhitimu, alifanya kazi kama Diwani wa Mahakama ya Ukaguzi.

Kazi za mwanzo za kisiasa

Baada ya kazi za kujitolea kama mwanafunzi, François Mitterrand hatimaye alishindwa katika kampeni za uchaguzi wa rais 1974, Hollande alijiunga na Chama cha Kisosholisti miaka mitano baadaye. Haraka alionwa na Jacques Attali, mshauri mwandamizi wa Mitterrand, ambaye alipanga Hollande agombee katika uchaguzi wa Bunge la Taifa la Ufaransa mwaka 1981 katika jimbo la Corrèze dhidi ya aliyekuja kuwa rais, Jacques Chirac.

Hollande alishindwa na Chirac katika raundi ya kwanza, ingawa baadaye alikuwa Mshauri Maalum wa Rais mpya Mitterrand, kabla ya kufanya kazi chini ya Max Gallo, msemaji wa serikali. Baada ya kuwa Diwani wa Manispaa wa Ussel mwaka 1983, aligombea katika jimbo la Corrèze kwa mara ya pili mwaka 1988, wakati huu alichaguliwa kuingia katika Bunge.

Katibu wa kwanza wa Chama cha Kisosholisti

Mwisho wa kipindi cha Mitterrand madarakani ulivyokaribia, Chama cha Kisoshalisti kilipasuka kutokana na mapambano ya makundi ndani ya chama, kila kundi likitaka kushawishi mwelekeo wa chama. Hollande aliomba upatanisho ili chama kiungane nyuma ya Jacques Delors, Rais wa Tume ya Ulaya, lakini Delors alitangaza nia yake ya kugombea Urais wa Ufaransa mwaka 1995, na kusababisha Lionel Jospin kuanza upya mbio za uongozi wa chama.

Jospin alimchagua Hollande kuwa msemaji rasmi wa chama, na Hollande akagombea katika jimbo la Corrèze kwa mara nyingine tena mwaka 1997, alifanikiwa kurudi katika Bunge. Mwaka huo, Jospin akawa Waziri Mkuu wa Ufaransa, na Hollande akashinda na kuwa Katibu wa Kwanza wa chama cha Socialist wa Ufaransa, nafasi ambayo alishikilia kwa miaka kumi na moja. Kwa sababu ya nafasi kubwa sana ya Chama cha kisoshalisti ndani ya Serikali ya Ufaransa wakati wa kipindi hiki, nafasi ya Hollande iliwafanya baadhi kumuona kama "Makamu wa Waziri Mkuu". Hollande alichaguliwa kuwa Meya wa Tulle mwaka 2001, alishikilia nafasi hiyo kwa miaka saba.

Kujiuzulu mara moja kwa Jospin katika siasa kufuatia mshtuko wake wa kushindwa na mgombea Jean-Marie Le Pen katika raundi ya kwanza ya uchaguzi wa rais mwaka 2002 kulimlazimisha Hollande kutizamwa na umma wa chama kwa uchaguzi wa 2002 wa wabunge, ingawa aliweza kuzuia kushindwa na alichaguliwa tena katika jimbo lake mwenyewe, Chama cha Kisoshalisti kiliopoteza ushindi kitaifa.

Ili kujiandaa kwa Mkutano wa Chama mwaka 2003 katika eneo la Dijon, alipata msaada wa watu wengi mashuhuri wa chama na alichaguliwa tena kuwa Katibu wa Kwanza dhidi ya upinzani kutoka mrengo wa kushoto. Baada ya ushindi wa kushoto katika uchaguzi wa mwaka 2004 wa kikanda, Hollande alitajwa kuwa mgombea urais, lakini chama cha kisoshalisti kiligawanyika kuhusu Katiba ya Ulaya, na nguvu ya Hollande kwa nafasi ya "ndiyo" katika kura ya maoni ya Ufaransa kwa Katiba ya Ulaya iliyosababisha msuguano ndani ya chama. Ingawa Hollande alichaguliwa tena kama Katibu wa kwanza katika mkutano wa Le Mans mwaka 2005, mamlaka yake kwenye chama yalianza kushuka.

Hatimaye mwenzi wake wa ndani, Segolene Royal, alichaguliwa kuwakilisha Chama cha Kisosholisti katika uchaguzi wa rais wa 2007, ambapo alipoteza kwa Nicolas Sarkozy. Hollande alilaumiwa sana kwa kushindwa kwa Chama cha Kisoshalisti katika uchaguzi wa 2007, na alitangaza kuwa hatagombea mhula mwingine kama Katibu wa Kwanza. Hollande alitangaza hadharani kumuunga mkono Bertrand Delanoë, Meya wa Paris, ingawa ni Martine Aubry aliyefanikiwa kushinda mwaka 2008.

Kufuatia kujiuzulu kwake kama Katibu Kwanza, Hollande mara moja alichaguliwa kuchukua nafasi ya Jean-Pierre Dupont kama Rais wa Baraza Kuu la Corrèze mwezi Aprili 2008, nafasi aliyoishika hadi anachaguliwa kuwa rais.

Kufuatia kuchaguliwa kwake tena kama Rais wa Baraza Kuu la Corrèze Machi 2011, Hollande alitangaza kwamba atagombea katika uchaguzi ujao wa awali kuchagua mgombea wa chama cha kisoshalisti wa urais. Kufuatia kukamatwa kwa Strauss-Kahn kwa tuhuma za unyanyasaji wa kijinsia jijini New York Mei 2011, Hollande alionekana kuanza kuongoza kura ya maoni. Nafasi yake kama mgombea ilianzishwa na Strauss-Kahn aliposema hatatafuta nafasi ya uteuzi katika kinyang’anyiro hicho. Baada ya mfululizo wa mijadala mwezi wote wa Septemba, Hollande aliongoza katika kura katika duru ya kwanza iliyofanyika Oktoba 9 kwa asilimia 39 ya kura, dhidi ya Martine Aubry, aliyekuwa wa pili kwa asilimia 30 ya kura.

Uchaguzi wa pili ulifanyika Oktoba 16, 2011. Hollande alishinda kwa asilimia 56 ya kura kwa 43 za Aubry na hivyo akawa mgombea rasmi wa chama cha kisoshalisti wa urais kwa mwaka 2012. Baada ya matokeo ya awali, aliungwa mkono mara moja na wagombea wengine wa chama kwa ajili ya uteuzi, ikiwa ni pamoja na Aubry, Arnaud Montebourg, Manuel Valls na mgombea wa 2007, Segolene Royal.

Kampeni za urais za Hollande zilisimamiwa na Pierre Moscovici na Stéphane Le foll, Mbunge ambaye pia ni Mbunge wa Ulaya. Hollande alizindua kampeni zake rasmi na mkutano wa hadhara na hotuba kubwa katika eneo la Le Bourget Januari 22, 2012, mbele ya watu 25,000.

Tarehe 26 Januari iliainisha orodha kamili ya sera katika ilani yenye maazimio 60, ikiwa ni pamoja na mgawanyo wa shughuli za rejareja kutoka biashara za uwekezaji za kibenki; kupandisha kodi kwa makampuni makubwa, mabenki na matajiri; kutengeneza ajira za kufundisha 60,000; kurudisha umri rasmi wa kustaafu kutoka 62 hadi 60; kuanzisha ajira za ruzuku katika maeneo ya uhaba mkubwa wa ajira kwa vijana; kukuza zaidi viwanda nchini Ufaransa kwa kujenga uwekezaji wa benki za umma; kupitisha ndoa na haki za kuasili mtoto kwa wanandoa za jinsia moja, na kuwaondoa askari wa Kifaransa nchini Afghanistan mwaka 2012. Februari 9, alielezea kwa kina sera zake hasa kuhusiana na elimu katika hotuba kubwa katika eneo la Orleans.

Tarehe 15 Februari, Rais Nicolas Sarkozy alitangaza kugombea kwa awamu ya pili na ya mwisho, akikosoa vikali mapendekezo ya Hollande na kudai kuwa ataleta "maafa ya kiuchumi ndani ya siku mbili baada ya kuchukua madaraka" kama akishinda.

Katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi kwa ajili ya kampeni zake, alitembelea Berlin, Ujerumani, Desemba 2011 kwenye mkutano wa Shirikisho wa Chama cha Kidemokrasi cha Kijamii, ambapo alikutana na Sigmar Gabriel, Peer Steinbrueck, Frank-Walter Steinmeier na Martin Schulz; pia alisafiri hadi Ubelgiji kabla ya kwenda Uingereza mwezi Februari 2012, alikokutana na kiongozi wa upinzani, Ed Miliband, na hatimaye Tunisia mwezi Mei 2012.

Duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais ilifanyika 22 Aprili. François Hollande aliongoza kwa asilimia 28.63 ya kura, na kumkabili Nicolas Sarkozy katika duru ya pili. Katika mzunguko wa pili Jumapili iliyopita ya Mei 6, 2012, François Hollande alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Ufaransa kwa asilimia 51.7 ya kura.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment