Jun 1, 2012

Hii ndiyo Dini inayoenea kwa kasi kubwa nchini Tanzania


Charles Ekerege, Mkurugenzi Mkuu wa TBS

Machinjio ya ng'ombe


BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

MAJUZI nilikutana na dokezo moja kutoka kwa Profesa Mbele alilolitoa kwenye blogu yake, kuwa ufisadi ndiyo dini inayoenea kwa kasi nchini Tanzania. Kwangu mimi hii ilikuwa ni habari kubwa mno. Japo ilikuwa ni kama dokezo tu (fupi mno) la kawaida, lakini ilinifanya kufikiria kwa kina huku nikilinganisha na hiki kinachoendelea kutokea nchini mwetu. Kwa kifupi nakubaliana na Profesa Mbele kuhusu hilo.

Profesa Mbele aliandika hivi: “Mara kwa mara ninawasikia watu wakiongelea suala la dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania, Afrika au duniani kwa ujumla. Kila mtu ana mtazamo wake. Wengine wanatoa pia takwimu, ambazo sijui kama ni za kweli au ndoto. Ni mchezo wa kuringiana nani zaidi kwa kutumia takwimu, wakati dini ni suala la mtu binafsi. Wala hutaingia ahera kwa msingi kuwa dini yako hapa duniani ilikuwa na wafuasi wengi kuliko dini nyingine.

“Kwa mtazamo wangu, dini inayoenea kwa kasi kuliko zote Tanzania ni ufisadi na ushirikina. Ufisadi na ushirikina huo unaendelea kushamiri kiasi kwamba unajitokeza hata kwenye nyumba za ibada za dini mbalimbali. Hebu tutafakari hilo.”

Ni maneno machache lakini yaliyobeba ujumbe mkubwa mno na unaweza kuyaelezea kwa kurasa zaidi ya elfu moja. Binafsi nadhani kuenea kwa dini (ufisadi) hii kumesababishwa na nchi hii kuitupa misingi iliyoongozwa na Azimio la Arusha, kufumbia macho vitendo vya rushwa na kukubali wafanyabiashara ambao wengi wao historia zao binafsi katika suala zima la uadilifu zinafahamika waziwazi ndani ya jamii na zimekuwa zinatiliwa shaka sana kupewa nafasi kwenye vyama vya siasa, hasa chama tawala.

Wafanyabiashara hawa wakubwa wenye kashfa mbalimbali za kuhujumu Taifa wamekuwa wakijitokeza kugombania nafasi mbalimbali za kisiasa, wanapokosa huwa wanaamua kupandikiza watu wao katika uongozi ili kuhakikisha dili zao na biashara zao zinakaa sawa.

Kinyume na ilivyokuwa katika awamu ya kwanza na kipindi cha kwanza (1985-90) cha awamu ya pili ya uongozi wa nchi hii, uongozi wa Tanzania kwa sasa si dhamana tena kama tulivyokuwa tukifundishwa shuleni kwamba 'cheo ni dhamana'. Uongozi sasa hivi umegeuka kuwa njia ya kumfanya mtu mambo yake yamnyookee, uongozi umekuwa biashara 'bab kubwa' isiyo na hasara. Zamani uongozi ulikuwa ni mzigo lakini siku hizi uongozi ni ‘kuula’ kwa maana ya dhiki kutoweka kabisa.

Kuenea kwa dini hii ni matokeo ya wimbi la wafanyabiashara kujiingiza kwenye siasa na kuviteka vyama huku wakipandikiza watu wao kwenye uongozi. Inashangaa hata pale wataalamu wa fani tofauti wanapoacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa. Hebu fikiria maprofesa, madaktari, wahandisi, na wataalamu wa fani mbalimbali wanaacha kazi zao walizosomea na kupigania kwenda kusinzia bungeni au kwenye mikutano ya halmashauri!

Wafanyabiashara hawa wana nguvu kubwa sana ndani ya vyama na hata serikalini, ndiyo maana sasa tunashuhudia wakisamehewa kodi kila mwaka huku ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2009/10 aliyoitoa hivi karibuni ikionesha kwamba katika kipindi hicho misamaha ilifikia shilingi trilioni 1.2 (asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali).

Kibaya zaidi, mawaziri na wabunge wetu ni miongoni mwa vigogo wanaojinufaisha na Sheria ya Msamaha wa Kodi kinyume cha taratibu. Orodha ya majina ya watu waliosamahewa kodi na Serikali katika mwaka wa fedha 2009/2010 inaonesha majina ya baadhi ya mawaziri, wabunge na wakuu wa taasisi za Serikali wakiwa wamenufaika na misamaha hiyo.

Viongozi hawa wameshiriki katika kuidhinisha shilingi bilioni 31 kununua bidhaa kwa matumizi ya Serikali pasipo kutolewa ufafanuzi, shilingi bilioni 8 kutumika bila kufuata utaratibu maalumu na shilingi milioni 143 kutumiwa na serikali kulipa mishahara kwa wafanyakazi hewa, watoro na waliostaafu! Yaliyomo kwenye ripoti hiyo yanasikitisha na kutisha sana.

Matokeo ya kushamiri kwa dini hii yamesababisha wataalamu wa wanyama, afisa afya na watendaji wa majinchio ya Vingunguti jijini Dar es Salaam kuruhusu kuletwa utumbo na nyama iliyooza na kuuzwa kwa wananchi, kitendo kilichovuka hata mipaka ya ubinadamu!

Ni nani atabisha kwamba dini hii haina nguvu na haijaenea nchini? Hata kama nchi inanuka rushwa na ufisadi, lakini ndiyo iwe kwa kiwango cha namna hii? Kwa hali ya kawaida, haihitaji kuwa msomi sana kubaini kuwa bidhaa ya kuoza kama ile italeta madhara makubwa sana kwa watu na pengine hata ndugu wa karibu wa wahusika.

Hii pia haina tofauti na ile habari Shirika la Viwango Nchini (TBS) kuruhusu bidhaa feki zitumike nchini. Tukubali au tukatae, hii ni dini inayoenea kwa kasi kutokana na kukumbatia rushwa, kuruhusu wafanyabiashara watawale mfumo wa uongozi kwa kupandikiza watu wao, na kutochukuliwa hatua thabiti kwa wanaobainika kufanya ‘madudu’.

Kushamiri kwa dini hii kumesababisha pia kuwapo habari kuwa vibali bandia 480 vimetolewa na kuidhinishwa na kigogo mmoja wa Idara ya uhamiaji mkoani Kilimanjaro. Vibali hivyo vimeisababishia Serikali hasara ya Sh 231 milioni. Serikali pia ilipata hasara ya Sh 86 milioni kutokana na vibali vingine bandia 84 vilivyokamatwa mwaka jana katika kiwanda kimoja wilayani Mwanga, huku kinara mkuu akidaiwa kuwa uraiani.

Hayo na mengine mengi yanatufanya tuamini kuwa sasa hii ndiyo dini iliyoshamiri nchini. Ni kipi kitatufanya tusiamini kuwa dini hii ndiyo inayoenea kwa kasi nchini?

No comments:

Post a Comment