Jun 1, 2012

AMADOU TOUMANI TOURE: Apinduliwa wiki chache kabla hajaachia madaraka

* Alipo kwa sasa ni kizungumkuti


Amadou Touman Toure

BAMAKO,
Mali

HIVI karibuni wanajeshi nchini Mali waliupindua uongozi wa nchi hiyo uliokuwa chini ya Amadou Touman Toure. Kadhalika waasi wanaoongozwa na Watuareg wamezidi kuteka maeneo mengine ya nchi hiyo na wamesonga mbele katika maeneo ya Kaskazini ya Mali, eneo kubwa wanalodai liwe huru.

Hali ya wasiwasi inazidi kuongezeka kuhusu harakati za makundi ya wapiganaji wa Kiislamu Kaskazini ya Mali baada ya waasi hao wanaoongozwa na Watuareg kuyateka maeneo makuu ya eneo hilo wiki iliyopita.

Waasi hao wakiongozwa na makamanda Watuareg wameteka maeneo zaidi katika mkoa wa kati wa Mopti kwa mujibu wa wakazi wa eneo hilo. Wameingia katika mji mdogo wa Hombori ulio kilometa 300 Kaskazini mwa mji mkuu wa mkoa wa Mopte bila ya mapigano yoyote.

Awali walisema mji wa Homboni hauko katika eneo la Azawad wanalodai liwe huru. Hakuna ishara yoyote kama watasonga mbele kuelekea Kusini. Wapiganaji wa kundi la Waislamu la Ansar Eddine wameanza kutekeleza kanuni za sheria za Kiislamu katika miji mikuu mitatu iliyotekwa na waasi mwishoni mwa wiki iliyopita.

Taarifa kutoka Kidal Gao na Timbuktu zanaeleza kuwa wapiganaji wa Ansar Edinne walishambulia baa zinazouza pombe na kupiga marufuku kucheza muziki wa nchi za Magharibi katika vituo vya redio. Shirika la Utamaduni la umoja wa mataifa limeelezea wasiwasi wao kuwa maeneo ya kale katika Timbuktu huenda yakaharibiwa na uasi huo.

Hata hivyo, kiongozi wa Mali aliyepinduliwa, Toure, japo hajulikani yuko wapi, amenukuliwa akisema yuko huru na salama kabisa. Toure amekanusha habari kuwa anashikiliwa na wanajeshi ambao siku ya tarehe 22 walipindua serikali yake.

Kupinduliwa kwa Rais huyo wa Mali kulitokea kukiwa kumesalia wiki tano peke yake ili uchaguzi mkuu ufanywe. Lakini mara tu baada ya kumtimua madarakani Rais Toure, Baraza la Jeshi linaloongoza nchi lilitangaza kuahirishwa kwa uchaguzi huo kwa muda usiojulikana.

Katika taarifa yake fupi kwa njia ya simu kwa shirika la habari la AFP Toure alisema lililo muhimu kwa wakati huu ni kufahamisha watu kuwa yuko huru wala hazuiliwi kama inavyodaiwa.

“Nafuatilia kwa makini sana yale yote yanayotokea nchini. Kwa moyo wangu wote nataka amani na demokrasia”, Toure alisema.

Historia yake

Amadou Toumani Touré amezaliwa tarehe 4 Novemba 1948. Alikuwa Rais wa Mali kuanzia 2002 hadi 2012. Alimwangusha Rais Moussa Traoré katika mapinduzi ya kijeshi ya Machi 1991 na kuongoza serikali ya mpito kwa mwaka mzima kabla ya uchaguzi wa vyama vingi; alikabidhi madaraka kwa mamlaka za kiraia mnamo Juni 1992.

Miaka kumi baadaye, baada ya kustaafu kutoka katika jeshi, aliingia katika siasa kama raia na kushindi uchaguzi wa urais wa mwaka 2002. Alichaguliwa tena kirahisi mwaka 2007 kwa muhula wa pili na wa mwisho. Miezi tu kabla ya kuachia ngazi kufuatia uchaguzi uliopangwa kufanyika, wanajeshi wa Mali wenye kinyongo walipindua nchi na hivyo kumlazimisha aende mafichoni

Maisha ya awali

Amadou Toumani Touré alizaliwa tarehe 4 Novemba 1948, katika eneo la Mopti, ambako alihudhuria masomo ya shule ya msingi. Kati ya 1966 na 1969, alihudhuria masomo ya sekondari katika shule ya Badalabougou iliyopo Bamako ili aje kuwa mwalimu. Hatimaye, alijiunga na jeshi na kujiunga na chuo cha Kijeshi cha Kati. Akiwa mmoja wa wanaanga, alipanda haraka akipitia safu na kozi mbalimbali za mafunzo katika Umoja wa Kisovieti na Ufaransa, na kuwa kamanda wa kikosi cha parachute Commandos mwaka 1984.

Siasa na kazi ya kijeshi

Mwezi Machi mwaka 1991, baada ya ukandamizaji wa kutumia nguvu wa maandamano dhidi ya serikali, Toure alishiriki katika mapinduzi yaliyoelekezwa dhidi ya Rais Moussa Traoré, na kuwa kiongozi wa Kamati ya Mpito kwa ajili ya Ustawi ya Watu na kiongozi wa nchi katika jitihada ya kamati ya mpito kuipeleka serikali ya nchi hiyo kwenye demokrasia.

Aliandaa mkutano wa kitaifa kati ya Julai 29 na Agosti 13, 1991 kuandaa Katiba ya Mali na kufanyika kwa uchaguzi wa wabunge na rais wa mwaka 1992. Baada ya matokeo ya uchaguzi kujulikana, Toure alikabidhi madaraka kwa rais mpya aliyechaguliwa, Alpha Oumar Konaré. Kutokana na kuondoka kwake madarakani kwa hiari, alipata jina la utani la "Askari wa Demokrasia."

Juni 2001, Toure alifanya kazi kama mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, wa Jamhuri ya Afrika, baada ya jaribio la mapinduzi lililoshindwa nchini humo.

June 2002, Mwezi Septemba 2001, aliomba na kustaafu kutoka jeshi, akaingia katika siasa kama mgombea katika uchaguzi wa mwaka 2002. Katika duru ya kwanza ya kupiga kura, alikuwa wa kwanza kwa asilimia 28.71 ya kura, wakati katika raundi ya pili alishinda kwa asilimia 64.35 ya kura, akimshinda mgombea wa ADEMA, waziri wa zamani wa baraza la mawaziri, Soumaïla Cissé, ambaye alipata asilimia 35.65. Touré aliapishwa tarehe 8 Juni 2002.

Urais wake umekuwa ukitazamwa na waangalizi wa mambo kama si wa kawaida, kwa sehemu kutokana na ukweli kwamba si mwanachama wa chama chochote cha siasa na kwamba amekusanya wanachama wote kutoka vyama vyote vya kisiasa nchini humo katika serikali yake. Kufuatia uchaguzi wake wa 2002, aliwateua Ahmed Mohamed AG Hamani kama Waziri Mkuu, lakini tarehe 28 Aprili 2004, nafasi yake ilichukuliwa na Ousmane Issoufi Maiga, ambaye naye kwa upande alilirithiwa na Modibo Sidibé tarehe 28 Septemba 2007.

Touré pia alianzishwa shirika la watoto lililoitwa Fondation pour l'enfance - jina lililokuwa likitumiwa pia shirika kama hilo lililoundwa na Danielle Mitterrand, mke wa rais wa Ufaransa, François Mitterand. Shirika hili hivi karibuni limekuwa likisimamiwa na mke wa Rais Toure, Lobbo Traore, akiliongoza kama wakala wa Touré.

Touré alitangaza mnamo 27 Machi 2007, kuwa angegombea kwa awamu ya pili katika uchaguzi wa rais wa Aprili 2007. Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangaza tarehe 12 Mei, Toure alishinda uchaguzi kwa asilimia 71.20 ya kura. Mpinzani mkuu, Rais wa Bunge, Ibrahima Boubacar Keïta, aliambulia asilimia 19.15; Chama cha Front for Democracy and the Republic; umoja huo ikiwa ni pamoja na Keïta na wagombea wengine watatu, waliyakataa matokeo rasmi. Waangalizi wa Nje, hata hivyo, waliukubali uchaguzi kama huru na wa haki. Touré akaapishwa kwa muhula wake wa pili kama Rais tarehe 8 Juni 2007, katika sherehe iliyohudhuriwa na marais wengine saba ya Afrika.

Kutokana na katiba ya Mali, ambayo inataja vipindi viwili vya urais, Toure alithibitisha katika mkutano wa vyombo vya habari tarehe 12 Juni 2011, kwamba hataweza kusimama katika uchaguzi wa rais wa 2012 .

Mapinduzi ya kijeshi 2012

Kwa miezi kadhaa mwaka huu, wanajeshi wa Mali wameipinga serikali ya Touré na kufanya uasi katika eneo la Kaskazini mwa Mali. Tarehe 21 Machi, askari walifanya jaribio la mapinduzi baada ya kuteka maeneo kadhaa Bamako, ikiwa ni pamoja na ukumbi wa rais, makao makuu ya televisheni ya nchi, na baadhi ya kambi za kijeshi. Kisha wakaanzisha mamlaka ya awali ya kiserikali, Kamati ya Taifa ya Matengenezo ya Demokrasia na Nchi (CNRDR), na kutangaza kwamba wameuangusha utawala wa Touré, kwa shutuma kuwa serikali yake ilitawaliwa na uzembe. Touré hakufungwa gerezani na waasi.

Mahali alipo Touré kwa sasa hapajulikani na wanejeshi hao wanaotawala nchi (CNRDR) hawajaonesha kuwa yupo chini ya ulinzi wao.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.


No comments:

Post a Comment