Jun 1, 2012

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ziangalieni kasoro hizi

Mshindi wa ubunge Jimbo la Arumeru, Joshua Nassari

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

KWANZA kabisa nachukua nafasi hii kumpongeza Joshua Nassari wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa ushindi wake wa kishindo alioupata katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki hivi karibuni. Uchaguzi huo mdogo wa ubunge katika Jimbo la Arumeru Mashariki ulifanyika kufuatia jimbo hilo kuwa wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Jeremiah Solomon Sumari.

Naamini kuwa kwa sasa uchaguzi umepita na wahusika wanafanya tathmini ya yaliyotokea, lakini binafsi umeniacha na maswali ambayo sina majibu yake na ninadhani Tume ya Taifa ya uchaguzi (Nec) inapaswa kutafuta majibu ili kutuondolea shaka hii, kwani naamini si mimi peke yangu mwenye shaka.

Natumaini kuwa hivi sasa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (Nec) watakuwa wameanza kufanya tathmini ya utendaji wa chombo hicho katika muktadha wa usimamizi wa sheria, kanuni, taratibu, maadili ya uchaguzi na mwenendo mzima wa uchaguzi huo.

Tukiachana na kasoro kadhaa zilizojitokeza katika uchaguzi wa Arumeru na hata katika chaguzi zingine zilizoambatana na huo za udiwani katika maeneo kadhaa ya nchi, mojawapo ya kasoro hizo ilihusu uvunjifu wa amani na kusababisha wabunge wawili wa Chadema kucharangwa mapanga katika mkesha wa uchaguzi wa diwani katika Kata ya Kirumba, jijini Mwanza.

Ninachokikusudia hapa ni kuieleza hii kasoro ya idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura kuwa kubwa mno ikilinganisha na idadi ya watu wanaojitokeza kupiga kura.

Inaonekana kuwa suala hili la takwimu katika idadi ya wapiga kura walioandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura limekuwa ni tatizo sugu nchini. Mi’ nadhani kazi kubwa inayoikabili Nec kwa sasa ni kuhakiki upya Daftari hili la Kudumu la Wapiga kura ambalo naamini limesababisha wananchi wengi kutokuwa na imani na chaguzi zinazosimamiwa na kuendeshwa na tume hiyo.

Takwimu hizi ni jinamizi linalousumbua mfumo mzima wa uchaguzi katika nchi yetu kwani sidhani kama Nec yenyewe wana uhakika na idadi ya wapiga kura walioorodheshwa katika daftari hilo.

Wakati wa uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010 nilianza kuingiwa shaka pale ilipokuwa ikitajwa kuwa idadi ya wapiga kura katika daftari la kudumu ilikuwa ni watu milioni 20,137,303, na hata baada ya uchaguzi kauli kubadilika na kuwa watu milioni 19! Hii ikiambatana na idadi ndogo ya watu milioni 8,626,283 tu sawa na asilimia 42.84 waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi huo.

Nilianza kupata wasiwasi hasa baada ya kusoma chapisho lenye takwimu zinazochapishwa na majarida ya kimataifa, kuwa Tanzania, Afrika na nchi zinazoendelea duniani zinaonesha watu wenye umri kati ya siku moja hadi chini ya miaka 18 ni kati ya asilimia 65 hadi 70.

Wenye umri wa kuanzia miaka 18 na kuendelea ni kati ya asilimia 30 hadi 35. Na ikasisitizwa kuwa haijapata kutokea katika nchi yoyote ya dunia ya tatu ikiwemo Tanzania kukuta idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura ikazidi asilimia 25 ya idadi ya wananchi katika nchi husika.

Lakini mwaka 2010, Tanzania iliyo katika kundi hili la nchi za dunia ya tatu, eti ikawa na idadi ya watu waliojiandikisha kupiga kura karibu asilimia 55 ya wananchi wake! Hii ilikuwa ni rekodi ya aina yake na ilipaswa kuingizwa kama maajabu kwenye kitabu cha kumbukumbu za dunia, Guinness Book Encyclopedia.

Kama hiyo haitoshi, mwaka jana katika uchaguzi mdogo wa ubunge katika Jimbo la Igunga, idadi ya waliopiga kura ilikuwa ni watu 53,672 tu kati ya waliosemwa kuwemo katika daftari la kudumu la wapiga kura ambayo ni watu 171,019! Ieleweke kuwa hapo sikuwa nimetia shaka kabisa katika uchaguzi huo wa Igunga kwa kuwa niliamini kuwa wengi hawakujitokeza kupiga kura kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vitisho vilivyokuwa vimetawala wakati wa kampeni.

Lakini hili la Arumeru limenifanya nione kuwa hapa kuna kiini macho kuhusu idadi ya watu katika daftari la wapiga kura, kwani naamini kuwa wakazi wa Jimbo la Arumeru walikuwa wamehamasika mno katika uchaguzi huu, na hata vyama vilivyochuana, hususan CCM na Chadema vilikuwa vikiwahamasisha na kuwahimiza kujitokeza kupiga kura siku ya tarehe Mosi Aprili. Cha ajabu bado tumesikia yaleyale ya idadi ndogo ya wapiga kura ikilinganishwa na waliojiandikisha!

Ni watu 60,699 tu waliopiga kura kati ya watu 127,455 waliojiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura kwa mujibu wa Nec. Hapa kuna maswali mengi kuliko majibu.

Kwa nini Nec haifanyi uhakiki kila mwaka kujua ni wangapi waliofariki au kuhama kutoka sehemu moja kwenda nyingine? Hivi haioni kuwa kutofanya hivyo ni kuiminya demokrasia? Nasmea kuiminya demokrasia kwa kuwa ikumbukwe pia kuna vijana wengi ambao mwaka 2010 (miaka miwili nyuma) hawakuwa wametimiza miaka 18 inayowaruhusu kupiga kura kwa mujibu wa sheria lakini mwaka jana na hata mwaka huu wametimiza umri wa kupiga kura. Hivyo walikuwa na haki ya kupiga kura katika chaguzi ndogo lakini wamenyimwa fursa hii. Hivi hali hii inaendelea hadi lini?

Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment