Jun 1, 2012

DIONCOUNDA TRAORÉ: Rais wa mpito nchini Mali anayekabiliwa na shinikizo

Dioncounda Traore


BAMAKO,
Mali

WAKUU wa serikali nchini Mali wamesema kuwa Rais wa Mpito wa nchi hiyo, Dioncounda Traore, amepelekwa eneo salama baada ya kupigwa hadi kuzirai na mamia ya waandamanaji nchini humo.

Mamia ya waandamanaji walimshambulia Rais Traoure wakipinga mkataba ulioafikiwa na Tume ya kiuchumi ya nchi za Magharibi mwa Afrika, ECOWAS, ambapo Traoure ataendelea kutawala kwa hadi mwaka mmoja badala ya siku 40 pekee zilizokubaliwa miezi miwili iliyopita.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, amesema kuwa shambulio hilo litawashtua wanadiplomasia waliokuwa wakifanya kila juhudi kurejesha amani na utangamano nchini humo. Muda wa kuongoza aliopewa kiongozi huyo, Djouncounda Traore, ulitarajiwa kukamilika Jumatatu.

Lakini viongozi wa nchi za Magharibi mwa Afrika, waliafikia mkataba na kiongozi wa mapinduzi, Kapteni Amadou Sanogo, kwamba Traore asalie mamlakani ili aweze kuongoza harakati za uchaguzi na kumaliza harakati za waasi wa Tuareg.

Mkataba huo pia ulijumuisha mpango wa kukubalia Sanogo atajwe kama kiongozi wa zamani alipwe mshahara wa rais na apewe nyumba ya kifahari.

Mapinduzi hayo pamoja na harakati za waasi kuteka maeneo ya Kaskazini mwa Mali, yamesababisha maelfu ya watu kutoroka makwao. Mashirika ya misaada wanasema wana wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya kibinadamu nchini Mali nchi ambayo pia inakumbwa na baa la njaa.

Mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Uingereza, BBC, mjini Bamako, Martin Vogl amesema kuwa wanajeshi waliwaruhusu baadhi ya waandamanji kuingia katika ikulu ya rais ingawa rais huyo wa mpito hakuwepo wakati huo.

Historia yake

Dioncounda Traoré amezaliwa tarehe 23 Februari, 1942, ni mwanasiasa wa Mali ambaye amekuwa Rais wa Mali katika kipicha cha muda mfupi tangu mwezi Aprili mwaka 2012.  Amekuwa Rais wa Bunge la Mali tangu mwezi Septemba 2007, na Rais wa chama cha kisiasa kinachojulikana kama Alliance for Democracy in Mali-African Party for Solidarity and Justice (ADEMA-PASJ) tangu mwaka 2000. Pia alikuwa Rais wa Alliance for Democracy and Progress (ADP), muungano wa vyama ambavyo viliunga mkono uchaguzi wa marudio wa Rais Amadou Toumani Touré mwaka 2007.

Kazi ya siasa

Traoré alizaliwa katika eneo la Kati. Baada ya kusoma nje ya nchi katika Umoja wa Kisovyeti, katika Chuo Kikuu cha Algiers, na katika Chuo Kikuu cha Nice, alifundisha nchini Mali katika Chuo cha Walimu (ENSUP) kati ya 1977 na 1980. Kisha alikamatwa kwa kujishughulisha na harakati za mambo ya muungano wa vyama vya kibiashara na kupelekwa Ménaka kaskazini mwa Mali.

Baada ya hapo, akawa mkurugenzi mkuu wa Shule ya Taifa ya Uhandisi. Alishiriki katika mapambano kwa ajili ya demokrasia ambayo yalisababisha kuangushwa kwa Rais Moussa Traoré mnamo Machi 1991. Alikuwa mwanachama mwanzilishi wa ADEMA, na katika mkutano wake wa Katiba, uliofanyika mnamo Mei 25 na 26 mwaka 1991, alichaguliwa kuwa Makamu wa Pili wa Rais wa ADEMA, wakati Alpha Oumar Konaré alichaguliwa kuwa Rais wa chama hicho na Mohamed Lamine Traoré alichaguliwa kuwa Makamu wake wa kwanza wa Rais.

Baada ya Konaré kuchaguliwa kuwa Rais wa Mali katika uchaguzi wa rais wa mwaka 1992, Traoré aliteuliwa kuwa Waziri wa Utumishi wa Umma, Kazi, na Utawala mnamo tarehe 9 Juni 1992, katika serikali ya kwanza chini ya rais wa Konaré. Baadaye aliteuliwa kuwa Waziri wa Nchi kwa ajili ya Ulinzi mnamao tarehe 16 Aprili 1993, ameshika nafasi hiyo hadi alipokuwa Waziri wa Nchi kwa ajili ya Mambo ya Nje mnamo tarehe 25 Oktoba 1994. Katika mkutano wa kwanza wa ADEMA wa kawaida, uliofanyika Septemba 1994, Traoré alichaguliwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa chama hicho, wakati Ibrahim Boubacar Keïta alichaguliwa kuwa Rais wake.

Alichaguliwa kuwa Naibu katika Bunge akitokea Nara mwaka 1997 na kujiuzulu nafasi yake ya Waziri wa Mambo ya Nje mnamo tarehe 24 Agosti 1997 ili kuchukua kiti chake cha ubunge. Katika Bunge, akawa Rais wa Kundi la Wabunge wa ADEMA, kufuatia kujiuzulu kwa Keïta katika nafasi ya Urais wa ADEMA mnamo Oktoba 2000, Traoré alichaguliwa kuwa Rais wa ADEMA kwa mara ya kwanza katika Mkutano wa chama wa dharula, uliofanyika Novemba 25 hadi 28, 2000. Katika uchaguzi wa mwaka 2002 wa bunge, Traore alishindwa katika jimbo la Nara na kupoteza kiti chake.

Katika uchaguzi wa wabunge mnamo Julai 2007, Traoré aligombea tena katika akiwemo orodha ya ADEMA katika jimbo la Nara, ambapo viti vitatu vilikuwa hatarini. Katika raundi ya kwanza, orodha yake ilishinda kwa asilimia 39.59 ya kura, na katika raundi ya pili ilishinda kwa asilimia 58.41 ya kura. Wakati Bunge jipya la taifa lilipofanya mkutano wake wa kwanza tarehe 3 Septemba 2007, Traoré alichaguliwa kuwa Rais wa Bunge, akipata kura 111 dhidi ya kura 31 za Mountaga Tall wa National Congress for Democratic Initiative (CNID), mwanachama mwingine wa ADP.

Kufuatia mapinduzi ya kijeshi mnamo Machi 2012, ambayo yalisababisha kuwekwa vikwazo vya kiuchumi na Jumuiya ya Kiuchumi ya nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) dhidi ya Mali, mpango huo, ulioandaliwa katika nchi ya Burkina Faso na Rais Blaise Compaoré chini ya mwamvuli wa ECOWAS, ulisainiwa tarehe 6 Aprili 2012 ambao ulitarajiwa kuona mkuu wa serikali hiyo ya kijeshi, Kapteni Amadou Sanogo, akiachia madaraka kwa Dioncounda Traoré ili ashikilie madaraka ya urais katika serikali ya mpito hadi uchaguzi utakapofanyika. Traoré alikuwa ameondoka nchini humo kufuatia mapinduzi ya kijeshi, lakini alirudi mnamo Aprili 7.

Traoré aliapishwa kuwa Rais katika sherehe iliyofanyika mnamo tarehe 12 Mei 2012. Aliahidi "kufanya vita" juu ya uasi wa Tuareg katika upande wa kaskazini mwa Mali isipokuwa kama wataachia udhibiti wa miji ya kaskazini mwa Mali na kutangaza kuwa ni nchi ya Azawad.

Shambulio la Mei 2012

Tarehe 21 Mei 2012, askari waliruhusu kundi la waandamanaji wanaounga mkono mapinduzi ndani ya ofisi ya Traoré katika mji wa Bamako. Waandamanaji, ambao walikuwa wamebeba jeneza likiwa limeandikwa kimasikhara jina la Traoré juu yake, wakamshambuliwa, hadi akapoteza fahamu. Alipelekwa katika Hospitali ya Point G lakini hakuwa na fahamu wakati akipelekwa hapo, inaonekana alikwa anaosumbuliwa na majeraha ya kichwa. Waandamanaji watatu waliuawa na wengine kujeruhiwa wakati wana usalama wa Traoré walipowafyatulia risasi.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment