Jun 1, 2012

JIM YONG KIM: Aukwaa urais wa Benki ya Dunia licha ya shinikizo

Jim Yong Kim

Marekani

BODI ya Benki ya Dunia imemchagua mwanazuoni wa Marekani, Jim Yong Kim, kuwa rais wa Benki hiyo. Hii ni licha ya shinikizo kutaka nafasi hiyo kumuendea raia asiye Mmarekani. Dk. Kim ni mtaalamu wa Afya akiwa na uzoefu wa nchi zinazoendelea.

Kim alikuwa akipambana na Waziri wa fedha wa Nigeria Ngozi Okonjo-Iweala. Waziri huyo aliungwa mkono na nchi kadhaa zinazoendelea. Hata hivyo alikabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wajumbe wanaopiga kura ambao wengi hutoka Ulaya na Marekani.

Rais wa sasa, Robert Zoellick, anamaliza mhula wake wa miaka mitano hapo mwezi Juni.

Historia yake

Jim Yong Kim amezaliwa tarehe 8 Desemba 1959, ni daktari Mmarekani mwenye asili ya Korea na Rais wa 17 wa Chuo cha Dartmouth. Zamani alikuwa Mwenyekiti wa Idara ya Afya na Tiba ya Jamii katika Shule ya Tiba ya Harvard, na alikuwa mmoja wa waanzilishi na mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Washirika Katika Afya (PIH). Machi 2, 2009, Kim aliteuliwa kuwa rais wa Chuo cha Dartmouth. Kim pia ni Mmareka wa kwanza mwenye asilia ya Asia kushika nafasi ya rais katika taasisi ya Ivy League.

Machi 23, 2012, Rais Barack Obama alitangaza kuwa Marekani itamteua Kim kama Rais wa Benki ya Dunia ajaye. Aprili 16, Kim alichaguliwa kuwa rais na ataanza kazi Julai 1.

Alizaliwa jijini Seoul, Korea ya Kusini, Jim Yong Kim na familia yake walihamia Marekani akiwa na umri wa miaka mitano na kukulia Muscatine, katika Jimbo la Iowa. Baba yake alifundisha somo la afya ya meno na kinywa katika Chuo Kikuu cha Iowa, wakati mama yake alipata shahada yake ya uzamivu (Ph.D.) katika falsafa. Kim alipata masomo ya juu katika shule ya Muscatine. Baada ya mwaka mmoja na nusu katika Chuo Kikuu cha Iowa, alihamishiwa Chuo Kikuu cha Brown, ambapo alihitimu shahada ya kwanza mwaka 1982. Alihitimu shahada ya udaktari kutoka Shule ya Tiba ya Harvard mwaka 1991, na shahada ya uzamivu (Ph.D.) kutoka Chuo Kikuu cha Harvard, Idara ya anthropolojia (elimu ya binaadamu), mwaka 1993.

Kazi

Jim Yong Kim, pamoja na Paul Farmer, Todd McCormack, Thomas J. White na Ophelia Dahl, walianzisha Taasisi ya Washirika Katika Afya (PIH) mwaka 1987. Shirika lililenga katika mpango wa huduma za afya ya jamii nchini Haiti, ambao ulilenga kutoa tiba kulingana na mahitaji ya ndani na mafunzo ya jamii kuyatekeleza. Mwanzoni mwa miaka ya 1990, mpango wa Haiti ulihudumia watu zaidi ya 100,000. Ni mafanikio ya ajabu kutibu magonjwa ya kuambukiza kwa gharama nafuu, wakitumia dola 150 na 200 kutibu wagonjwa wa kifua kikuu majumbani mwao, matibabu ambayo yangegharimu dola 15,000 hadi 20,000 katika hospitali nchini Marekani. Kim alikuwa mtu muhimu katika kubuni itifaki ya matibabu na kukata mikataba kwa bei nafuu, na ufanisi zaidi.

Mwaka 2003 Kim alijiunga na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama mshauri wa mkurugenzi mkuu. Mwezi Machi 2004, aliteuliwa kuwa mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani wa idara ya VVU/UKIMWI, baada ya kuonesha mafanikio katika mipango ya kupambana na ugonjwa huo kupitia taasisi ya PIH. Dk. Kim alisimamia kazi zote za Shirika la Afya Duniani kuhusiana na VVU/UKIMWI, akilenga mpango wa kusaidia nchi zinazoendelea kuongeza matibabu yao, kuzuia, na mipango ya huduma.

Kuanzia mwaka 1993, Dk. Kim alikuwa mhadhiri katika Shule ya Tiba ya Harvard, hatimaye akawa profesa katika tiba, tiba ya jamii na haki za binadamu. Alipoondoka mwaka 2009, Kim alishikilia cheo cha mwenyekiti wa Idara ya Afya na Tiba ya Jamii, Mkuu wa Idara ya Global Health Equity katika Hospitali ya Brigham na Wanawake, na Mkurugenzi wa Kituo cha François Xavier Bagnoud wa Afya na Haki za Binadamu katika Shule ya Afya ya Umma ya Harvard.

Katika miongo yake miwili ya kazi aliboresha afya katika nchi zinazoendelea, Kim amekuwa akishiriki katika jitihada kadhaa ya utafiti na kitaaluma. Katika miaka ya karibuni, Kim ameongoza maendeleo mapya akilenga katika kuboresha utekelezaji na utoaji wa shughuli za afya katika jamii maskini duniani kote.

Akiwa Harvard, Kim alichapisha makala mbalimbali kwa ajili ya majarida ya kitaaluma na kisayansi, ikiwa ni pamoja na New England Journal of Medicine, Lancet, Science, na mengineyo, na kuchangia katika vitabu kadhaa. Mtaalam wa kifua kikuu, Kim pia alikuwa mwenyekiti au mjumbe katika kamati kadhaa katika sera ya kimataifa ya TB.

Machi 2009, Kim alikuwa Rais wa 17 wa Chuo cha Dartmouth, akiwa Mmarekani wa kwanza mwenye asili ya Asia kushika madaraka ya urais katika taasisi ya Ivy League. Kim amesimamia maendeleo ya programu kadhaa ya kiubunifu katika Chuo cha Dartmouth, akitumia uzoefu wake wa zamani katika huduma za afya na masuala ya kimataifa. Januari 2010, Kim alisaidia wanafunzi wenzake wa Dartmouth na kitivo kupitia taasisi aliyoianzisha, Taasisi ya Washirika Katika Afya, na mashirika mengine, kukabiliana na tetemeko kubwa la ardhi nchini Haiti, na kuanzisha taasisi ya Dartmouth Haiti Response. Mpango huo ulisababisha upatikanaji wa zaidi ya dola milioni 1 katika michango, utoaji wa tani 18 ya vifaa tiba na wataalamu wa afya 25 wa kujitolea nchini Haiti, pamoja na mamia ya wanafunzi wa kujitolea.

Aprili 2010, Kim alizindua Mradi wa Kitaifa wa Chuo katika Uboreshaji wa Afya (NCHIP), ambao huzileta pamoja taasisi za kitaalam kuendeleza mbinu za kushughulikia masuala ya afya ya mwanafunzi. Mradi ulizindua programu yake, jitihada za kukabiliana na ulevi, mwezi Aprili 2011. Mei 2010, Kim alisaidia upatikanaji dola milioni 35 kuanzisha Kituo cha Dartmouth kwa ajili ya Huduma ya Afya na Sayansi. Kituo kilianzisha uwanja mpya wa mafunzo ya utafiti, kukuza ushirikiano wa kimataifa kati ya watafiti na madaktari, kutekeleza, na kuweka mipango mipya ya ubora wa huduma kwa gharama nafuu. Mwaka 2012, kufuatia wasiwasi mkubwa na juhudi za Kim kushughulikia unyanyasaji wa kijinsia chuoni, Dartmouth ilirithi hatua mpya ya chuo ya kuwaelimisha wanafunzi juu ya umuhimu wa kuingilia uangalizi katika kesi za kushambuliwa kingono kama sehemu ya Mpango wa Uelewa wa Unyanyasaji wa Kingono.

Mwaka 2011, Kim alikosolewa kutokana na kukataa kutoa bajeti ya chuo, na hivyo kusababisha sehemu ya azimio kwa kitivo kudai maelezo zaidi. Kim akajibu kwa kutoa ripoti kubwa ya ziada juu ya bajeti na kufanya mkutano wa hadhara na kitivo ambao baadaye walionesha kuridhika na majibu. Hata hivyo, Kim hakushughulikia ombi la Mkutano wa Wanafunzi walioomba kupata taarifa juu ya bajeti yote inayozidi dola 10,000. Mwaka 2011, wahariri wachache walionekana katika gazeti la wanafunzi la Dartmouth wakionesha kutoridhika na urais wa Kim, na mmoja akamuelezea Kim kama "asiye na umaarufu miongoni mwa wanafunzi wengi siku hizi." Uongozi wake pia umekosolewa kutokana na kashfa ya udhalilishaji, ambayo ilisababisha mashitaka dhidi ya udugu na kuundwa kwa kikosi kazi cha kushughulikia kashfa; na kukiwa na maoni kutoka kwa baadhi ya kuwa Kim hakutumia muda wa kutosha chuoni.

Machi 23, 2012, Rais wa Marekani, Barack Obama alitangaza uteuzi wake wa Jim Yong Kim kuwa rais wa Benki ya Dunia. Siku hiyohiyo Jim Yong Kim alituma barua akihutubia Jumuiya ya Dartmouth akisema kuwa nafasi ilikuwa ni "moja ya taasisi muhimu zaidi ya kupambana na umaskini na kutoa msaada kwa nchi zinazoendelea katika dunia ya leo. Baada ya kutafakari sana, nimekubali uteuzi huu kwa huduma ya kitaifa na kimataifa "na kwamba" kama nitachaguliwa, Bodi yetu itachukua hatua zinazofaa ili kuhakikisha mwendelezo wa uongozi na utafiti. Kwa sasa, nabakia kuwa rais wa Dartmouth".  Aprili 16, 2012, Benki ya Dunia ilimchagua rasmi Kim kuwa rais wake ajaye.

Maisha binafsi

Kim, amemuoa Younsook Lim, daktari wa watoto katika Hospitali ya Watoto ya Boston, wana watoto wawili, Thomas, ambaye alizaliwa mwaka 2000, na wa pili aliyezaliwa Februari 27, 2009, siku chache kabla ya kutangazwa kwa urais wa Kim katika Chuo cha Dartmouth. Anashiriki kikamilifu katika aina mbalimbali za michezo, ikiwa ni pamoja na mpira wa kikapu, volleyball, tennis, na golf.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment