Apr 27, 2011

JENERALI MUHAMMADU BUHARI: Asababisha vurugu kubwa Kaskazini mwa Nigeria baada ya kupinga matokeo

 Jenerali Muhammadu Buhari

ABUJA
Nigeria

BAADA ya Tume ya uchaguzi ya Nigeria (INEC) kumtangaza rasmi mgombea wa chama kinachotawala nchini humo, Goodluck Jonathan, kuwa rais baada ya uchaguzi mkuu kumalizikika nchini humo kwa kupata kura milioni 22.5, zilizuka ghasia kubwa Kaskazini mwa Nigeria zilizopelekea vifo vya mamia ya watu.

Awali ghasia ziliripotiwa kuzuka Kaskazini mwa Nigeria wakati matokeo ya awali ya urais yalipokuwa yakionesha kuwa Goodluck Jonathan anaelekea kushinda. Nyumba za wafuasi wa Jonathan, mgombea aliyekuwa anatetea kiti cha urais, zilishambuliwa katika miji ya Kano na Kaduna.

Wafuasi vijana wa mgombea urais mwenziye, Muhammadu Buhari, ambaye ana umaarufu upande wa Kaskazini mwa nchi, walikuwa wakipambana na polisi na wanajeshi. Wafuasi hao walifanya vurugu hizo wakiwa wanahisi kuwa uchaguzi ulikuwa umevurugwa katika baadhi ya maeneo upande wa Kusini.

Baada ya kutangazwa mshindi, Rais Jonathan alitoa wito wa kuwepo kwa hali ya utulivu, akisema "Hakuna mwanasiasa mwenye thamani ya kumwaga damu ya Wanigeria".

Kwa sasa hali ya ghasia nchini humo imeanza kuwa shwari huku mji wa Kaskazini mwa Nigeria wa Kaduna ukiwa umeanza kutulia baada ya kuzuka machafuko makubwa ya kupinga matokeo hayo ya Uchaguzi Mkuu.

Duru za habari zinasema watu 400 wamekamatwa kuhusiana na machafuko hayo yaliyoambatana na uchomaji wa makanisa, vituo vya polisi na nyumba za watu katika siku mbili za ghasia. Shirika la msalaba mwekundu lilikaririwa likisema kuwa watu wengi wameuawa na wengine 48,000 kuzikimbia nyumba zao.

Chanzo cha machafuko hayo ni baada ya mgombea urais kupitia upinzani, Jenerali Muhammadu Buhari kupinga matokeo akidai kuwa kulikuwa na udanganyifu. Kadhalika ilikuwa kufuatia hali ya baadhi ya wafuasi wake sehemu za kusini mwa nchi hiyo kushindwa kupiga kura.

Ingawa waangalizi wa kiamataifa wanasema kuwa uchaguzi huo ulikuwa huru na Goodluck Jonathan kutangazwa mshindi, lakini Jenerali Buhari anayetoka Kaskazini mwa nchi amesema chama chake kitapinga kisheria matokeo hayo na ametoa wito wa kuwepo utulivu baada ya ghasia.

Historia ya Buhari

Muhammadu Buhari alizaliwa Desemba 17, 1942, aliwahi kuwa kiongozi wa kijeshi wa Nigeria kuanzia Desemba 31, mwaka 1983 hadi 27 Agosti 1985, na mgombea urais katika chaguzi za mwaka 2003, 2007 na uchaguzi wa mwaka huu 2011. Buhari anatokea katika kabila la Fulani, na ni mwenye imani ya Uislamu, huku familia yake ikitoka Jimbo la Katsina.

Waziri wa Petroli

Buhari alifamahika kwa mara ya kwanza kwenye umma mwaka 1976 wakati alipokuwa Waziri (au "Kamishna wa Shirikisho") wa Petroli na Maliasili chini ya aliyekuwa Mkuu wa Nchi wakati huo, Olusegun Obasanjo. Kabla ya hapo aliwahi kuwa Gavana wa Jimbo jipya la Kaskazini-Mashariki wakati wa utawala wa Murtala Mohammed. Baadaye akawa mkuu wa Shirika jipya la Petroli la Nigeria mwaka 1977.

Serikali ya Buhari

Meja Jenerali Buhari alichaguliwa kuongoza nchi ya Nigeria baada ya mapinduzi ya kijeshi yaliyofanikiwa kuuondoa madarakani utawala wa kiraia wa Rais Shehu Shaghari tarehe 31 Desemba, 1983. Wakati huo, Buhari alikuwa mkuu wa Idara ya Tatu ya Jeshi iliyopo Jos. Buhari aliteuliwa kuwa Mkuu wa Nchi na Amiri Jeshi Mkuu wa vikosi vya jeshi, na Tunde Idiagbon aliteuliwa kuwa Kiongozi Mkuu wa Wafanyakazi.

Buhari aliyaelezea mapinduzi hayo ya kijeshi kama nguvu ya kuiondoa madarakani serikali ya kiraia iliyokuwa imekithiri kwa rushwa, na utawala wake hatimaye ulianzisha kampeni ya umma dhidi ya ukosefu wa maadili iliyojulikana kama "Vita dhidi ya ukosefu wa maadili". Masuala ya kampeni hii ilikuwa ni pamoja na udhalilishaji wa umma wa watumishi wa umma ambao waliwasili kazini wakiwa wamechelewa, walinzi waliokuwa na silaha na mijeledi waliwekwa kuhakikisha kunakuwepo utaratibu mzuri wa foleni katika vituo basi.

Pia alifanya kazi ya kuwanyamazisha wakosoaji wa utawala wake, akapitisha amri kupambana na uhuru wa vyombo vya habari na kuruhusu wapinzani wake watiwe kizuizini hadi miezi mitatu bila mashtaka rasmi. Pia alipiga marufuku migomo na wafanyakazi kuwafungia mabosi, na kuanzisha jeshi la kwanza la polisi wa siri nchini Nigeria, Shirika la Usalama wa Taifa. Serikali yake ilimhukumu mwanamuziki maarufu na mkosoaji wa siasa za nchi hiyo, Fela Kuti kwa miaka kumi gerezani. Kuti baadaye alipata msamaha na aliyekuwa mrithi wa Buhari.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Uingereza (BBC), “Buhari alijaribu kuweka uwiano wa fedha za umma kwa kupambana na bidhaa zilizopelekea wengi kupoteza kazi na hasara nyingi zilizopelekea kufungwa kwa biashara.” Hasara hizo ziliambatana na kupanda kwa bei na kushuka kwa hali ya maisha.

Mapinduzi ya 1985 na kuwekwa kizuizini

Kufuatia kuwepo hali mbaya ya kiuchumi, na kuendelea kuenea kwa rushwa, Buhari aliangushwa katika mapinduzi yaliyoongozwa na Jenerali Ibrahim Babangida na wanachama wengine wa Halmashauri Kuu ya Jeshi (SMC) Agosti 27, 1985.

Babangida aliwachukuwa watu wengi zaidi walioonekana kama wakosoaji wa serikali ya Buhari na kuwaingiza katika utawala wake, ikiwa ni pamoja na ndugu wa Fela Kuti, Benko Ransome-Kuti, daktari ambaye alikuwa ameongoza mgomo dhidi ya Buhari kupinga kupungua huduma za afya. Kisha Buhari aliwekwa kizuizini Katika jiji la Benin hadi mwaka 1988.
Miaka iliyofuata

Buhari alifanya kazi kama Mwenyekiti wa Mfuko wa Petroli, chombo kilichoanzishwa na serikali ya Jenerali Sani Abacha, na kufadhiliwa na mapato yanayotokana na kuongezeka kwa bei ya mafuta ya petroli, ili kutekeleza miradi ya maendeleo nchini kote.

Mwaka 2003, Buhari aligombea katika uchaguzi wa rais kama mgombea wa All Nigeria People's Party (ANPP). Alishindwa na mgombea wa People's Democratic Party, Rais Olusegun Obasanjo, kwa kiasi cha zaidi ya kura milioni kumi na moja. Hata hivyo, ilidaiwa na wafuasi wa Buhari na wanachama wengine wa chama cha upinzani kwamba katika baadhi ya majimbo, kama Ebonyi, kulikuwa na kura nyingi zaidi ya wapiga kura.

Pamoja na madai ya kuwepo udanganyifu yaliyothibitishwa katika mahakama na mwenendo wa uchaguzi ulikosolewa mno na Kundi la Waangalizi kutoka Jumuia ya Madola, makubaliano kati ya Wanigeria yalikuwa kwamba Buhari asipoteza muda wake katika mahakama kwa kuwa hakuwa na rasilimali za kumsaidia "kujinunulia" haki.

Hatimaye, mahakama hiyo pia iliamua kwamba madai ya udanganyifu yaliyothibitishwa hayakutosha kuathiri matokeo ya uchaguzi na uthibitisho wa kufuta uchaguzi mzima wa Rais.

Tarehe 18 Desemba 2006, Jen. Buhari aliteuliwa tena kuwa mgombea wa All Nigeria People's Party. Mpinzani wake mkuu safari hii katika uchaguzi wa Aprili 2007 alikuwa mgombea wa chama tawala cha PDP, Umaru Yar'Adua, waliyetoka sehemu moja ya Katsina.

Katika uchaguzi, Buhari alipata asilimia 18 ya kura dhidi ya asilimia 70 ya Yar'Adua, lakini Buhari aliyakataa tena matokeo haya. Baada ya Yar'Adua kuingia madarakani, chama cha ANPP kilikubali kujiunga na serikali yake, lakini Buhari alikataa.

Machi 2010, Buhari alijiondoa katika chama cha ANPP na kujiunga na Congress for Progressive Change (CPC). Buhari aligombea tena urais katika uchaguzi mkuu wa 16 Aprili 2011, dhidi ya rais wa sasa, Goodluck Jonathan wa People's Democratic Party (PDP), na wengineo. Alikuwa anagombea akiwa na sera kubwa ya kupambana na rushwa na kuahidi kuondoa ulinzi na kinga kutoka kwa maafisa wa serikali.

Pia aliunga mkono utekelezaji wa sheria za Kiislamu (Sharia), katika Majimbo ya Kaskazini mwa Nigeria, sera ambayo hapo awali ilimsababishia matatizo makubwa ya kisiasa miongoni mwa wapiga kura Wakristo katika maeneo ya Kusini.

Hata hivyo, matokeo ya mwaka huu yaamemwacha Buhari akishika nafasi ya pili kwa kupata kura 12,214,853, nyuma ya rais rais Goodluck Jonathan, aliyepata kura 22,495,187 na kutangazwa mshindi.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari

Kupuuza migogoro hii ya ardhi nchini ni kama kuatamia bomu

 Mgogoro wa ardhi uliozuka baina ya wanakijiji wa Horohoro Border na uongozi wa kijiji hicho unaodaiwa kupora sehemu ya eneo la kijiji kwa lengo la kuligawa kwa wawekezaji umefanya Rais Jakaya Kikwete aombwe kuingilia kati.

 Maeneo ya migodi kama haya yameshuhudia migogoro mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MIGOGORO ya ardhi hapa nchini hivi sasa imekithiri na imefikia hatua ya umwagaji damu. Migogoro hii imegawanyika katika makundi mawili, baina ya wakulima na wafugaji na wananchi na wawekezaji.

Migogoro hasa ya wananchi na wawekezaji ambayo imechukua sura mpya hivi sasa inaitafsiri serikali yetu kuwa siyo ile ya 'mgeni njoo mwenyeji apone', bali mgeni njoo mwenyeji asulubike.

Katika maeneo mengi hapa nchini, tayari kumeshatokea uvunjifu wa amani uliosababisha damu kumwagika na hata kutokea vifo. Vurugu hizi zimetokea hata kwenye maeneo ambayo udugu na kuvumiliana vilitawala na hakuna mtu aliyedhani zingeweza kutokea. Hata hivyo, bado sizioni jitihada za haraka za kumaliza migogoro hii ambazo zimeshachukuliwa na serikali yetu.

Badala yake najionea hatua za kujaribu kuahirisha matatizo haya jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa baadaye. Kwa mfano Serikali mkoani Manyara ilipoamua kupiga marufuku baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu ya masuala ya ardhi wilayani Hanang kwa madai kuwa yanawachochea wananchi, kwa mtazamo wangu sikuona kama ni dawa ya kutibu tatizo.

Jambo muhimu katika kutatua tatizo la migogoro hii ya ardhi ni kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kutunga sera nzuri ya ardhi itakayowashirikisha wananchi moja kwa moja, kwani kuahirisha ufumbuzi wake kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwepo kuendelea kumwagika kwa damu ya wananchi wanaotetea ardhi yao.

Katika upekuzi wangu hivi karibuni nilibahatika kuisoma ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za ardhi – HAKIARDHI ya January 30, 2009, iliyojaribu kuonesha hali halisi ya migogoro ya ardhi jinsi ilivyokithiri hapa nchini, ambapo inaonekana kuwa migogoro ya ardhi kati ya makundi mbalimbali ya watumiaji imekuwa ikiongezeka kila kukicha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo; migogoro hiyo ni baina ya wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji na wanavijiji na serikali zao za vijiji ama serikali kuu, migogoro imeendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini. Migogoro hii imefikia hatua ya kusababisha uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na mali na kuongezeka kwa chuki miongoni mwa raia.

Kwenye vyombo mbalimbali vya habari, kuanzia magazeti, redio na hata televisheni ni migogoro ya ardhi 'kwa kwenda mbele' inayoripotiwa, vurugu zimekuwa zikijitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini hivi sasa, si Tarime, Kilosa, Kiteto wala Kilindi tu, bali sehemu nyingi za nchi ikiwemo Dar es Salaam na Zanzibar.

Mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji yamekuwa yakiripotiwa kila kukicha na kuyafanya masikio yetu kusikia vurugu hizi mara kwa mara kiasi cha akili kudhani kuwa ni jambo la kawaida tu. Hivi sasa kuna taarifa za fukuto la migogoro kama hiyo karibu katika maeneo yote yenye wafugaji nchini.

Huko Zanzibar, ingawa Serikali imeonesha kulivalia njuga suala la uporaji wa viwanja na ardhi za wananchi lakini bado kumekuwepo na malalamiko mengi kwa baadhi ya wananchi wanaofanyiwa dhuluma katika maeneo na ardhi ambazo wamemiliki kutoka kwa wazazi wao.

Chanzo cha migogoro hiyo kinadaiwa kuwa ni familia ya wakubwa fulani wakiongozwa na kiongozi mstaafu kuhodhi sehemu kubwa ya ardhi na kuwaacha wananchi wengine wakiambulia patupu huku sheria zikionekana kupindishwa makusudi ili kumlinda mkubwa huyo.

Ukiacha kando migogoro ya asili kama vile baina ya wakulima na wafugaji, au kijiji na kijiji kuhusu mipaka na kadhalika, siku za hivi karibuni hili wimbi la kuibuka migogoro inayohusiana na uwekezaji katika maeneo ya vijiji kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa, uchimbaji madini na vito na shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii limekuwa kubwa na linatishia amani ya nchi.

Migogoro hii inanifanya nione kuwa sera za uwekezaji mkubwa katika ardhi zimepitwa na wakati na ni muhimu sasa ziangaliwe upya na maslahi ya wazalishaji wadogo yapewe kipaumbele hasa katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wamekosa shughuli muhimu za kuwawezesha kujikimu.

Kwa ardhi yetu hii kubwa na nzuri, vijana wengi kama watawezeshwa wanaweza kujishughulisha badala ya kukaa bila kazi huku ardhi nayo ikibaki mikononi mwa wachache, ugumu wa maisha kwa vijana utaendelea kuwepo na kuwafaanya wengi wao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Kwa upande wa wafugaji mabadiliko ni suala ama mchakato ambao huchukua muda mrefu, hivyo ni vyema kuhakikisha kwamba rasilimali muhimu kama maeneo ya kuchungia mifugo na maji vinapatikana sanjari na huduma kama malambo, majosho, dawa na masoko ili kuongeza tija ya mfumo wa ufugaji kwa kundi lao na kwa pato la taifa pia.

Huwa napata 'kigagaziko' kila ninapoiangalia sheria inayouruhusu mkutano wa kijiji kutoa ardhi hekari 50 bila kuingiliwa kwa kile kinachosemwa kuwa taratibu zinafuatwa, sidhani kama sheria hii ina lengo zuri kwa wananchi na isipoangaliwa upya itasababisha umwagaji mkubwa wa damu hasa pale wananchi watakapohisi kunyang'anywa ardhi yao kifisadi au vinginevyo.

Serikali kuamua kuwa na sera ya uwekezaji siyo jambo baya lakini nadhani itakuwa inafanya kosa kubwa kukaribisha wawekezaji katika ardhi bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika ambao wanapaswa kuridhia ardhi yao kugawiwa mgeni, serikali inapaswa kuangalia kwa upana uwekezaji huu inaoufagilia maana hao wanaoitwa wawekezaji wengi wao wanapora ardhi na kuwaacha wananchi masikini kutokana na sheria kutokuwa wazi.

Mimi si mtabiri lakini jambo hili lisipoangaliwa kwa undani zaidi kuna hatari ya kutokea maafa makubwa sana kutokana na wananchi walio wengi kukosa ardhi, ndiyo maana migogoro hii naifananisha na kuatamia bomu ambalo wakati wowote linaweza kulipuka.

Tunapojadili Katiba tujadili pia hili la asilimia moja tu kumiliki uchumi wote!

 Mwananchi mjasiriamali kama huyu ana safari ndefu katika kumiliki uchumi

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI iliyopita niliona kipindi kimoja kilichoonesha vijana wawili ambao sikumbuki ni viongozi wa asasi gani, lakini walikuwa wakielezea mikakati yao kuhusu Mkukuta awamu ya pili na jinsi walivyopania kutoa elimu kwa vijana ili kujikwamua na umasikini.

Mkukuta ni neno maarufu katika jamii ya Tanzania toka ulipozinduliwa mwaka 2005. Kirefu chake ni Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, ukiwa umeboreshwa kutoka katika Mkakati wa kwanza wa kupunguza umaskini uliozinduliwa Oktoba mwaka 2000 na ulitekelezwa kuanzia 2005 hadi ulipoisha mwezi Juni 2010 kabla ya kuzinduliwa kwa awamu ya pili ya mpango huo.
Mojawapo ya eneo ambalo Mkukuta ulipaswa kujikita ni ukuaji wa uchumi na kupunguza umaskini wa kipato, ikisemwa kuwa eneo hili lina malengo sita likiwemo la kupunguza umaskini wa kipato kwa wanawake na wanaume wa maeneo ya vijijini. Ilidhamiriwa kuwa ifikapo mwaka 2010 wanaoishi chini ya mstari wa umaskini wangepungua toka asilimia 38.6 hadi asilimia 14.

Lakini taarifa iliyotolewa mwaka jana ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi, iliyowasilishwa katika kikao cha Kamati ya Bunge ya Fedha na Uchumi, kuwa ni asilimia moja tu ya watu, tena wenye asili ya mabara ya nje ndiyo wanaomiliki uchumi wa Tanzania!

Ilielezwa kuwa zaidi ya asilimia 90 ya uchumi wa Tanzania unaendelea kumilikiwa na watu hao wenye asili ya Asia na Ulaya, huku kukiwa na kilio kikubwa cha Watanzania wazawa, kutaka wajengewe mazingira mazuri ya uwezeshaji ili kumiliki uchumi wa nchi yao kupitia migodi mikubwa ya madini na maeneo nyeti ya kiuchumi.

Taarifa imeeleza kuwa tangu uhuru Watanzania wengi hawajawahi kushiriki kikamilifu katika kumiliki uchumi wa nchi yao. Uchumi wa nchi umeendelea kutawaliwa na wageni wakishirikiana na Watanzania wachache.
Huwa ninashangaa sana pale ninaposikia hoja ya uchumi wa nchi unakuwa kwa kigezo cha wingi wa magari, na wengine kusifu uchumi wetu kwa sababu ya kuongezeka kwa ‘masupamaketi’ makubwa tena yenye bidhaa nzuri (japo nyingi ni za nje pia), ilihali wananchi wengi hawana uwezo wa kuingia na kununua kilichopo.

Tujaribu kutofautisha maendeleo yaliyopo Oysterbay na Masaki na yale unayoweza kuyaona Manzese au Vingunguti, maendeleo yatakuwa ni barabara za kupitisha mchanga wa kujenga nyumba za mapumziko ya wikiendi. Tutataendelea kupita huku watoto wadogo wenye kamasi vifua wazi wakiendelea kupungia magari yetu makubwa kama nyumba. Hatutasikia kelele zao kwani vioo vitakuwa vimefungwa ili hewa iliyochujwa isichanganyike

Kwa taarifa ya Utendaji ya Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi inanifanya nishindwe kuelewa tofauti ya ukoloni na sasa katika umilikaji wa uchumi. Hivi ina maana 'fact' ya maendeleo ni kumilikiwa na Wazungu na wale wenye asili ya kutoka Asia?

Ile dhana kwamba kipimo cha mafanikio ya Mkukuta ni wananchi kila mahali kuanzisha vyama vya kukopa na kuweka (SACCOS). Vyama hivi vinawasaidia wananchi wenye kipato cha chini kupata mikopo inayowasaidia kuendeleza kilimo au biashara zao ndogo ndogo lakini sidhani kama vitawawezesha kumiliki uchumi.

Inashangaza kuona kuwa tuna ardhi nzuri, tuna madini na rasilimali kibao lakini tunaendelea kuwa masikini wa kutupwa, tukitegemea misaada ya wahisani ili kuendesha maisha yetu.

Kwa sasa huduma za jamii hususan elimu na afya zimedorora mno, mashule ya serikali yamebaki majengo tu, walimu hawatoshi, vitendea kazi kwa walimu havitoshi na zana za kujifunzia kwa wanafunzi havikidhi mahitaji halisi, madawati hayatoshi na hivyo watoto wengi wanakaa chini wakati wakisoma, na michango na ada sasa ni kero na vikwazo kwa watoto wengi kupata elimu.

Kwa sasa shule za serikali zimekuwa kama biashara, ada na michango inaanzia shule za msingi mpaka Chuo Kikuu. Pia ubaguzi katika elimu kwa sasa umekuwa rasmi, kwani kuna shule za matajiri na zile za watoto wa masikini, shule za matajiri zina huduma zote muhimu na ni za kisasa, wakati zile za walalahoi ziko hoi bin taaban.

Watoto wengi wa masikini sasa hawaendi shule na hivyo kusababisha kuongezeka kwa idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika, jambo linaloongeza umasikini miongoni mwa Watanzania, ambapo sasa inakadiriwa kuwa wananchi karibu asilimia 30 hawajui kusoma wala kuandika.

Mahospitali na zahanati za serikali sasa si mahali pa kuokoa maisha ya watu bali ni mahali pa kufia ndiyo maana watu wameona tegemeo pekee la kupata tiba ni Loliondo kwa Babu, kwani mahospitalini hakuna dawa na huduma zingine muhimu za matibabu, watumishi wa afya hawana ari ya kufanya kazi kwa kuwa hawalipwi vizuri, imefikia hatua wagonjwa wanakufa mikononi mwa manesi na madaktari kwa kukosa huduma huku uchumi wetu tukiwa tumeukabidhi mikononi mwa wageni.

Serikali imekuwa tegemezi, bajeti ya serikali inategemea misaada na mikopo kutoka kwa wageni kwa asilimia 35, na hili limesababisha manyanyaso na kuingiliwa kwa uhuru wetu kwa kupangiwa mambo ya kufanya na hawa wanaojiita wawekezaji.
Ingawa Katiba yetu inatamka kuwa nchi ya kijamaa lakini ukweli ni kwamba Tanzania siyo nchi ya Kijamaa na wala siyo nchi ya Kibepari bali iko tu katika hatua za kusahau nasaha za ujamaa na kuuelekea ubepari.

Kilichofanyika hapa ni kuacha kuvaa kaunda suti na kuanza kuvaa suti za Kimagharibi. Kutokuwa na msimamo kamili ndo’ kunaleta utata juu ya faida na hasara za mifumo hii katika kuleta maendeleo yetu.

Mimi naamini kuwa mfumo tunaoufuata hivi sasa ni mfumo wa Ubepari ingawa serikali ya CCM haitaki kukubali, ambao utaweza kuleta maendeleo kwa watu wachache tu wanaojua kucheza katika anga za ubepari, walio wengi hawajui na hawatajua nini kinaendelea na wanaweza kuuzwa kwa bei ya jumla.

Kinachofanyika sasa hivi katika mfumo huu wa kibepari ni kwa wachache kulimbikiza mali na si rahisi kujenga uwiano – hapa ni rahisi kujenga jamii mbili za wazalishaji na walaji na mara nyingi masikini ambao ni asilimia 99 ya Watanzania ndiyo wazalishaji.


Hatuwezi kufanikiwa katika Mkukuta kwa mfumo huu, vinginevyo tutakuwa tunadanganyana. Kwa mtazamo wangu ubepari si njia bora ya kuwafanya wananchi kujikwamua kwenye lindi la umasikini.


Mungu ibariki Tanzania

Apr 20, 2011

Sherehe hizi bila kutatua kero za Muungano kazi bure

 Tanzania katika bara la Afrika

 Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 
Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania ulizaliwa Aprili 24, 1964, na Jumanne ya wiki ijayo unatimiza miaka 47.

Hadi sasa Muungano huu umeshapitia misukosuko na dhoruba za kila aina, lakini bado unaendelea kuwepo na kunawiri hata kama kuna hali ya mashaka, huku nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na hata Asia zilizokuwa zimeungana kama sisi miaka ya nyuma zilishindwa kuuendeleza.

Kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa mojawapo ya waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia iliyotengana na Eritrea, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo sasa ni nchi mbili za Rwanda na Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.

Hali ya mashaka ninayoizungumzia hapa inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.

Habari zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya mustakabali wa nchi yao.

Ndiyo maana nafikiri kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.

Ukiuangalia Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima na hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.

Kwa kuwa tupo katika kipindi cha kuelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.

Japo sijabahatika kukutana na mtu yeyote aliyeeleza waziwazi kuwa hautaki Muungano, lakini karibu kila mtu ninayezungumza naye kuhusu Muungano amekuwa akiulalamikia kwa namna moja au nyingine. Nadhani Jumanne ijayo tutakapokuwa tukiadhimisha miaka 47 ya Muungano si vibaya Serikali ikakaribisha maoni, kwa dhati kabisa, namna ya kuuboresha muungano wetu na kuyafanyia kazi.

Kwa Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na Muungano, inaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.

Kero hizi ni pamoja na mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka kuuboresha Muungano. Muundo wa Muungano, hata kama chama tawala kimekuwa kikidai kuwa sera yake ni ya serikali mbili, linatakiwa liwe jambo litakaloamliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa wa mambo 11 kama ambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa kinyemela.

Hata hili la ushirikiano wa kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na ndiyo maana Zanzibar waliamua kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.

Kero nyingine ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili limeondolewa bila ya kura ya maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote

miaka ya hivi karibuni zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibar kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia ikilalamikiwa.

Maadhimisho haya yaende sambamba na kuchukua hatua za uhakika na si propaganda ili kumaliza kero za Muungano ili watu wa upande mmoja wasihisi wenzao wa upande wa pili wanapendelewa kama ilivyo sasa.

Suala hili la Muungano limejitokeza hata wakati Watanzania walipokuwa wakitoa maoni yao kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya, Wazanzibari wameonesha kuwa na maoni tofauti na hata jinsi walivyoshiriki katika mchakato huo.

Wengi wameona kwamba kabla ya kuangalia mambo yanayoweza kuwemo kwenye Katiba mpya ni lazima tuanze na kura ya maoni kuamua juu ya suala la Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, huku wakisisitiza kuwa Zanzibar lazima ijadili kwa uhuru Katiba hiyo mpya na lazima wahakikishe kero zilizopo juu ya Muungano zinaondolewa kabisa.

Ndiyo maana nasema sherehe za muungano hazina maana kama hatutatatua kero za Muungano.

GOODLUCK JONATHAN ACHAGULIWA RAIS: Alipewa jina la Goodluck na baba yake akimtabiria kuwa na bahati

 Rais Goodluck Jonathan

ABUJA
Nigeria

UCHAGUZI wa rais nchini Nigeria umemalizika huku Rais aliyefanikiwa kutetea kiti chake, Jonathan Goodluck akitoa wito wa kusitisha kile alichokisema “mambo yasiyo ya lazima yanayoweza kuepukwa” yanayosababisha ghasia za baada ya uchaguzi katika eneo la Kaskazini ya nchi. Rais Jonathan ametangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais, ambapo tume ya uchaguzi imesema kuwa amepata asilimia 57 ya kura.

Maandamano yameenea katika eneo linalokaliwa na Waislamu la Kaskazini – ngome ya upinzani – baada ya matokeo kubainika. Hii ni mara ya kwanza katika historia ya Nigeria ya hivi karibuni kwa matokeo ya uchaguzi kuleta mgawanyiko mkubwa kati ya Waislamu walio Kaskazini na Wakristo walio Kusini mwa nchi.

Goodluck Jonathan ameshinda katika karibu eneo lote la Kusini, ambalo ni eneo linalokaliwa na Wakristo isipokuwa kwenye Jimbo moja, wakati mpinzani wake mkuu, Muhammadu Buhari ameshinda katika eneo la Kaskazini-Mashariki na Kaskazini-Magharibi linalokaliwa na Waislamu. Wagombea wote wawili wamepata kura katika eneo la Kaskazini ya Kati ambalo linakaliwa kwa pamoja na Waislamu na Wakristo.

Kiongozi wa kundi la waangalizi kutoka Muungano wa Afrika, rais wa zamani wa Ghana, John Kufuor, aliliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC), kuwa alikuwa ameridhishwa na jinsi uchaguzi huo ulivyoendeshwa.

Uchaguzi muhimu wa Rais nchini humo umefanyika mwishoni wa wiki iliyopita katika hali ambayo wagombea watatu wa upinzani ndiyo walionekana wangetoa ushindani mkubwa kwa Rais wa sasa wa nchi hiyo, Goodluck Jonathan, kati ya wagombea ishirini walijitokeza kuwania kiti cha Urais katika uchaguzi huo. Hata hivyo, ni wagombea wanne tu akiwemo Rais Goodluck Jonathan ndio waliotajwa kuwa na nafasi ya kuibuka na ushindi katika uchaguzi huo.

Kwa mujibu wa Katiba ya Nigeria mgombea yeyote anayejinyakulia theluthi mbili ya kura katika majimbo 36 ya nchi hiyo atatangazwa mshindi na hakutakuwa na haja ya uchaguzi huo kuingia katika duru ya pili. Wachambuzi wa mambo walikuwa wanaamini kuwa, Goodluck Jonathan ambaye ni Mkiristo hatopata kura za wakazi wa majimbo ya Kaskazini mwa nchi hiyo ambayo ni ya wakazi wengi wa Kiislamu. Pamoja na hayo, weledi wa siasa za Nigeria walitabiri kwamba, Jonathan ataibuka na ushindi hasa kutokana na kutokuweko nguvu moja na mgombea mmoja katika kambi ya upinzani.

Viongozi wa vyama vya upinzani hawakuweza kufikia mwafaka wa kusimamisha mgombea mmoja katika uchaguzi huo; hali ambayo bila shaka imeonekana kumpa ahueni mgombea huyo wa chama tawala nchini Nigeria cha PDP, yaani Rais Goodluck Jonathan. Hata hivyo hatua ya wapiga kura wa Kiislamu wa maeneo ya Kaskazini mwa Nigeria ya kuwaunga mkono wagombea watatu ilikuwa inatathminiwa na wajuzi wa mambo kuwa ni sawa na kuunda kambi moja ya wapiga kura dhidi ya Rais Jonathan.

Jenerali wa zamani, Muhammadu Buhari wa Chama cha CPC ndiye aliyekuwa anahesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Jonathan. Buhari anapendwa mno na wakazi wa maeneo ambayo kawaida ni majimbo ya Waislamu na inatabiriwa kuwa hiyo ndio nguvu ya mgombea huyo. Muhammadu Buhari amewahi pia kuwa mgombea wa kiti cha Urais wa nchi hiyo katika miaka ya 2003 na 2007.

Historia ya Goodluck Jonathan:

Goodluck Ebele Jonathan Azikiwe, amezaliwa 20 Novemba 1957, ni Rais wa 14 na wa sasa wa Nigeria. Alikuwa Gavana wa Jimbo la Bayelsa tangu Desemba 9, 2005 hadi Mei 28, 2007, na aliapishwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Shirikisho la Nigeria tarehe 29 Mei 2007.

Jonathan ni mwanachama wa chama tawala cha People's Democratic Party (PDP). Tarehe 13 Januari 2010, mahakama ya shirikisho ilimkabidhi Jonathan mamlaka ya kuendesha mambo ya serikali wakati Rais Umaru Yar'Adua alipokuwa akipata matibabu katika hospitali nchini Saudi Arabia. Aliyekuwa Waziri wa Habari wa Nigeria, Prof. Dora Akunyili alikuwa wa kwanza kulaani uongozi kwa kutokuwa na hakika.

Hoja ya Baraza la Seneti la Nigeria ya tarehe 9 Februari 2010, ilithibitisha mamlaka hayo ya Jonathan kama Kaimu Rais, huku wakiyatambua maoni ya Prof. Akunyili. Tarehe 24 Februari 2010, Yar'Adua alirejea Nigeria, lakini Jonathan aliendelea kukaimu Urais. Baada ya kifo cha Yar'Adua tarehe 5 Mei 2010, Jonathan alichukuwa madaraka ya Urais, na kula kiapo tarehe 6 Mei 2010.

Maisha ya awali, elimu na maisha ya binafsi:

Jonathan alizaliwa katika eneo la Otueke, katika halmashauri ya Ogbia iliyopo eneo la Jimbo la Mashariki, ambalo baadaye lilijulikana kama Jimbo la River, na sasa linajulikana kama Jimbo la Bayelsa, kutoka kwenye familia ya watengeneza mitumbwi. Makundi mengi ya kikabila ndani ya Nigeria yana utamaduni wa kutoa majina kwa watoto ambapo jina la mtoto linaelezea matarajio fulani ya wazazi kuhusu mtoto au mazingira yake ya kuzaliwa. Baba mzazi wa Jonathan, Ebele Jonathan (Mkristo wa kabila la Ijaw kutoka sehemu ya Kusini mwa Nigeria) alisema kuwa jina la mwanaye, Goodluck lilimjia baada ya mtoto wake kuzaliwa, alimpa jina hilo alipogundua kwamba mtoto huyo alionekana kuwa na chembe chembe za bahati.

Jonathan amefuzu shahada ya kwanza (B.Sc.) ya Zoology. Pia ana shahada ya uzamili (M.Sc.) katika biolojia ya Uvuvi na Hydrobiology, na shahada ya uzamivu (Ph.D.) ya Wanyama kutoka Chuo Kikuu cha Port Harcourt. Baada ya kupata shahada yake, alifanya kazi mbalimbali kama mkaguzi wa elimu, mhadhiri, na afisa mazingira, mpaka alipoamua kuingia katika siasa 1998.

Miaka ya mwanzo katika kisiasa

Ugavana wa Jimbo la Bayelsa: Jonathan alianza siasa mwaka 1998, alipojiunga na People's Democratic Party (PDP) mwaka 1998. Jonathan, ambaye mwanzo alikuwa Naibu Gavana wa Jimbo la Bayelsa, alichukuwa nafasi ya Gavana Diepreye Alamieyeseigha, ambaye alituhumiwa na Bunge la Jimbo la Bayelsa baada ya kushtakiwa kwa kujihusisha na biashara ya fedha haramu nchini Uingereza.

Mbio za Urais:
Desemba 2006, Jonathan alichaguliwa kuwa mgombea mwenza wa aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Umaru Yar'Adua kwa tiketi ya chama tawala cha PDP katika uchaguzi wa rais wa Aprili 2007. Tarehe 20 Aprili 2007, muda mfupi kabla ya uchaguzi wa rais, mashambulizi ya kijeshi ambayo ilikuja kuelezwa na polisi kuwa lilikuwa ni jaribio la mauaji dhidi ya Jonathan yalitokea katika Jimbo la Bayelsa.
Makamu wa Rais:
Kufuatia mgogoro baada ya ushindi wa PDP, wanamgambo waliishambulia nyumba ya Jonathan iliyoko eneo la shamba katika eneo la Otu-Eke, Jimbo la Bayelsa, tarehe 16 Mei; polisi wawili waliuawa katika shambulio hilo. Jonathan hakuwepo wakati wa tukio hilo. Baada ya kuchukua madaraka, Yar'Adua alitangaza mali zake, na tarehe 8 Agosti 2007, Jonathan pia alifanya hivyo.

Kaimu Rais:
Rais Umaru Yar'Adua aliondoka Nigeria tarehe 23 Novemba 2009 kwa ajili ya matibabu. Hakutoa idhini kwa mtu yeyote kuchukua nafasi yake kwa kipindi ambacho yeye hakuwepo. Tarehe 13 Januari 2010, mahakama ya shirikisho ilitoa idhini kwa Makamu wa Rais, Jonathan kufanya kazi za rais katika kipindi cha kutokuwepo rais.

Tarehe 22 Januari 2010, Mahakama Kuu ya Nigeria ilifanya maamuzi kuwa Baraza Kuu la Shirikisho (FEC) lilikuwa na siku 14 kuamua juu ya azimio kama Rais Yar'Adua “hawezi kutekeleza majukumu yake ya kiofisi.” Katika hotuba ya kitaifa mwezi Februari 2010, Jonathan alitoa wito kwa Wanigeria wote kuweka kando tofauti zao za kidini na kikabila na kufanya kazi pamoja kwa faida ya wote.

Tarehe 9 Februari 2010, Seneti iliamua kuwa madaraka ya rais lazima yahamishiwe kwa Makamu wa Rais. Aliteuliwa kutumikia nafasi ya Kaimu Rais, akipewa mamlaka yote ya maamuzi, mpaka pale Yar'Adua atakapopata afya kamili.

Kuhamisha madaraka kwa Makamu wa Rais iliitwa “mapinduzi bila ya neno” na wanasheria wa upinzani na wabunge. Katiba ya Nigeria inatamka uwepo wa barua iliyoandikwa na Rais mwenyewe kuthibitisha kashindwa kuongoza au Baraza la Mawaziri lipeleke timu ya madaktari kumchunguza, lakini takwa hili halikutimizwa kabla ya kukabidhiwa madaraka Jonathan na kuacha wasiwasi wa kikatiba.

Urais:
Umaru Yar'Adua alifariki tarehe 5 Mei 2010. Goodluck Jonathan aliapishwa kumrithi Yar'Adua tarehe 6 Mei 2010, na kuwa Rais wa 14 wa Nigeria na ameitumikia nafasi hiyo hadi uchaguzi wa mwaka huu ambapo amefanikiwa kushinda.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

Apr 13, 2011

CCM KUJIVUA GAMBA: Suala lisiwe kujisafisha tu bali kuleta maendeleo kwa wananchi

 Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM) na Mjumbe wa NEC, 
Andrew Chenge anahusishwa kwenye kashfa ya rada.

 Mbunge wa Igunga (CCM) na Mjumbe wa NEC, 
Rostam Aziz anahusishwa kwenye kashfa ya Dowans.

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI hii imetawaliwa na habari kuhusu Chama Cha Mapunduzi (CCM) kwenye vyombo mbalimbali vya habari na kila mtu ameonekana kuguswa kwa kile kilichokuwa kikiendelea huko Dodoma, hasa kufuatia chama hicho kuamua kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu yake ya uongozi ndani ya Kamati Kuu kwa nia ya kujisafisha.

Mabadiliko hayo ya kiuongozi yamekuja katikati ya tuhuma mbalimbali na za muda mrefu za ufisadi wa viongozi wakuu ndani ya chama zilizokuwa zikiharibu sifa ya chama hicho kikongwe katika siasa za Tanzania, kulikopelekea mkakati wa kujisafisha kuanza na sekretarieti ya chama hicho iliyokuwa ikiongozwa na Yusuf Makamba ijiuzuru.

Sikuwepo kwenye kikao cha CCM lakini kutokana na taarifa zilizonifikia nikiwa mdau wa habari, inasemekana kuwa mwenyekiti alikuwa na mtihani mkubwa sana kuwatosa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwa kuwa bado wameonekana kukita mizizi yao ndani ya Halmashauri Kuu na chama kwa ujumla.

Mabadiliko hayo ya kiuongozi ndani ya Kamati Kuu yamepelekea chama kupata Katibu Mkuu mpya aliyechukua nafasi ya mzee Yusuf Makamba ambaye ni Wilson Mukama, akiwa na manaibu, John Chiligati, Naibu Katibu Mkuu upande wa Bara na Vuai Ali Vuai, Naibu Katibu Mkuu upande wa Zanzibar.

Nadhani kwa hatua hii Chama Cha Mapinduzi kinastahili pongezi japo kwa mtazamo wangu naona kuwa bado hakijakidhi matarajio ya wengi kwani mafisadi wanaolalamikiwa bado wanaonekana kuwa na nguvu na wamo kwenye NEC. Si hivyo tu, inaonekana imeshindikana kuwatosa kabisa, hali inayoashiria kuwa kama gamba walilojivua ni gamba la kichwani tu, bado gamba la mwilini.

Sitaki kusema kuwa kujivua gamba kwa maana ya kubadilisha uongozi ndani ya sekretarieti ya chama na kuwatosa mafisadi inatosha, nadhani bado haitoshi kuishia kwenye kuwastaafisha mafisadi tu bali iwe ni pamoja na kuwashitaki na kuwafilisi mali zote walizopata kwa njia ya kifisadi.

Hata hivyo, isionekane kufanya kazi na maamuzi yake kama wanavyotaka tuelewe kuwa ni kwa faida ya Tanzania na vizazi vijavyo, bali ionekane inafanya hivyo na wananchi waone, kwa kuanzia iwe ni kuwaongoza Watanzania kujipatia Katiba mpya bila ya kuangalia maslahi ya chama peke yake.

Na kama ni kweli kauli ya mwenyekiti wa CCM kuhusu kujivua gamba ilimaanisha CCM ni kama nyoka, ujumbe huo utakuwa na maana kubwa kwani tumeshang'atwa sana na mwenyekiti atakuwa ametambua kile kinacholalamikiwa muda mrefu na wananchi kuhusu IPTL, Deep Green, Meremeta, Richmond/Dowans, EPA na mengine kibao. Hivyo gamba jipya litusaidie kumwona nyoka huyo hata kama atajificha gizani.

Kama kweli Chama Cha Mapinduzi kina nia ya dhati kujivua gamba na kuwatumikia wananchi, kinapaswa kianze sasa kuwekeza katika kuhakikisha kunakuwepo uwiano sawa kwenye mgawanyo wa rasilimali ili kwenda sawa na kaulimbiu ya mwenyekiti wake ya “Maisha bora kwa kila Mtanzania”.

Watawala waelewe kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania wanaishi vijijini kwa kutegemea jembe la mkono, kipato wanachopata kutokana na kilimo cha aina hiyo sote tunatambua kwamba hakiwasaidii kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku. Ile kauli ya mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe ingekuwa na ukweli, basi wananchi wengi wa Tanzania wangekuwa matajiri.

CCM sasa kiangalie namna ya kuinyima ajenda Chadema kwa kuboresha maisha ya Watanzania, wasikalie kulalamika tu pindi Chadema inapotumia nguvu ya umma na wananchi wanapoamua kuandamana kwa kuwa hawana ajira. Sijui watawala wanataka wananchi wakafanye kazi gani, wakati wakulima huko vijijini hawapati kile kinachostahili kwa kutumia jembe la mkono?

Wananchi wanalalamika kwa kuwa wakija mijini hali bado ni ngumu wakati watawala waliopewa dhamana ya kuweka mazingira hayo wakiwa wamelala usingizi na kufikiria jinsi ya kutengeneza mikataba feki ili wachote fungu wanaloliona lipo 'idle'.

Ni wakati sasa watawala wetu waelewe kuwa Watanzania siyo wavivu kama wanavyofikiria, uchumi siyo kutoa takwimu tu bali kuwawezesha Watanzania kuwa na matumaini ya kuuza mazao yao kwa wakati kutoka mashambani. Kwa hiyo kujivua gamba kwa chama hicho kikongwe kusiishie kwenye kubadilisha uongozi tu, wanapaswa wayaone haya na kuyatekeleza kivitendo.

Hili jambo la kila uchaguzi mmoja ukiisha wanaanza kufikiria kupata pesa ya uchaguzi mwingine linapaswa liachwe sasa kama kweli mabadiliko hayo yana lengo la kumnufaisha mwananchi wa kawaida. Ninavyoamini mimi, adui namba moja wa maendeleo ya nchi hii ni viongozi mafisadi hasa walio ndani ya CCM ambao wengi wanakosa maadili.

Chama kinatakiwa kuwaondoa viongozi wengi ambao wanafikiria kujilimbikizia mali ili Mungu siku akiwaita, watoto wao na jamaa zao waendelee kutumia walichoiba na si kutafuta vyao kwa kuwa wamewaachia mazingira mazuri ya wao kufanikiwa kwenye nchi yao bila kufanya kazi.

Kwa hiyo nadhani bado kazi ya kujivua gamba ni ngumu sana na chama hicho kikaze buti zaidi maana inaeleweka wazi kuwa kiongozi mtendaji mkuu aliyekuwepo alikuwa mwanamipasho, lakini si yeye aliyetumia pesa za Kagoda. Yupo anayewalinda wahalifu na kufanya kuwepo uzito hata kuwakemea watumishi wengine wa serikali wanaofanya ufisadi wa kufuru.

Chama hiki kwa kuwa ndicho chama tawala hakina budi kiangalie pia mfumo wa elimu uliopo ili kuwasaidia wananchi kuondokana na ujinga, maana hiyo imekuwa ikitumiwa kama njia (loop-hole) ya kuwakandamiza wananchi wasiozijua haki zao. Wanachama wake pia wapewe nafasi ya kukikosoa chama, kukaa pamoja na kuzungumza chochote juu ya mustakbali wa nchi.

Suala la elimu ni nyeti maana imeonekana kuwa hata pale elimu nzuri inapotolewa huwa ni kwa kundi la watu maalumu ambao wanaaminika kwamba watakuwa tayari kuendeleza mfumo uleule wa kudumaza fikra za wananchi kwa propaganda kinyume na hali halisi ilivyo.

Nakubaliana na wanaosema kuwa serikali ya CCM imeshatengeneza bomu la kwanza kupitia sekondari za kata, na sasa inatengeneza bomu jingine kubwa iwapo itatekeleza mpango wake wa kuwaita wawekezaji wakubwa kupora ardhi ya wananchi kupitia sera yake ya kilimo kwanza.

Siku hizi kila kukicha ni migogoro ya ardhi tu inayorindima na imepelekea kumwagika damu za watu wasio na hatia, hivi hali hii itaisha lini? Viongozi wetu wataendelea kulifumbia macho suala hili hadi lini?

Nilishangazwa siku moja kusikia kauli za wawaziri wakiwasihi wananchi wasiokuwa na ardhi wasiharibu mali (mashamba, matrekta) za wawekezaji wala wasiwatumie meseji za kuwatisha. Lakini cha ajabu hakuna waziri hata mmoja aliyekuwa tayari kukiri kwamba serikali itawatafutia ardhi sehemu nyingine au ardhi kubwa iliyogawiwa wawekezaji itapunguzwa ili wananchi wagaiwe.

Mungu ibariki Tanzania

KATIBA MPYA: Tusiwafanye Watanzania mbumbumbu

 Rais Jakaya Mrisho Kikwete, amepewa madaraka makubwa sana katika mchakato wa kutafuta katiba mpya

 Tambwe Hiza, kada wa CCM anayedai wananchi hawahitaji katiba mpya

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MNAJADILI Katiba kwa kuwa nyie mmeshiba, kuna matatizo mengi ya msingi, vyakula vinapanda bei kila kukicha, wanafunzi wanakosa mikopo, wazazi wetu vijijini wana maisha magumu, mbona hayo hamjadili?...”
Maneno ninayoyakumbuka yaliyosemwa na kijana mmoja mwenye jazba (bahati mbaya silijui jina lake) wakati akichangia mjadala wa rasimu ya muswada wa kuanzisha mchakato wa kuandika katiba kwenye ukumbi wa Nkrumah, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, hivi karibuni.

Nimekuwa nikifuatilia kwa ukaribu sana mchakato unaoendelea wa kutafuta maoni ya wananchi kuhusu rasimu ya muswada wa kuanzisha mchakato wa kuandika katiba mpya na kugundua jambo moja kubwa, mijadala hii imejikita katika pande mbili kubwa.

Wanaodai katiba mpya wamekuwa na sababu zao ikiwemo ile ya kukosekana uhalali wa kisiasa kwa katiba iliyopo ambayo haikuwashirikisha wananchi, kuonekana kama ni ya chama kimoja, kumpa madaraka makubwa rais, kuhisi kwamba haihamasishi uwajibikaji, kujaa viraka vingi mno na kadhalika. Upande wa wanaopinga katiba mpya pia wana madai kuwa hakuna haja ya kuwa na Katiba mpya kwa kuwa wananchi walio wengi bado hawana elimu ya kutosha kuhusu uraia na hawahitaji katiba mpya kwa sasa.

Mara kwa mara nimekuwa nikisikia lugha ya dharau ya aina fulani kutoka kwa watu wasiolitakia mema taifa letu kuwa “Watanzania hawaijui katiba iliyopo” na kuwa hakuna umuhimu wa kujadili katiba mpya wakati iliyopo hawaijui ndiyo maana wanaishia kushabikia katiba mpya bila kuelewa.

Kama hiyo haitoshi, wiki hii nimesikia taarifa za baadhi ya viongozi wa asasi fulani kuishauri serikali isitishe mchakato wa katiba mpya kwa kuwa wananchi hawana elimu ya kutosha ya uraia, isitishwe hadi pale watakapopata elimu hiyo na kuielewa katiba ya zamani kwanza kabla ya kutaka mpya!

Nadhani tunakosea sana kutaka kuwasemea wananchi bila kujua nini mtazamo wao, kama wanaona haja ya kuwa na katiba mpya au la.

Nimewahi kuandika katika makala zangu zilizopita kuwa ipo haja ya kuiangalia upya katiba tuliyonayo ili kurekebisha mambo yaliyopitwa na wakati na naamini kabisa kuwa viongozi wetu wanajua umuhimu wa Katiba ya nchi na mahitaji ya wananchi kuhusu Katiba. Ile hoja ya kwamba wananchi hawaijui Katiba iliyopo haimaanishi kuwa hawahitaji Katiba nzuri itakayowahakikishia kupata haki zao za msingi.

Kama ilivyojitokeza kwa kijana mwenye jazba pale Nkrumah Hall, Chuo Kikuu wakati wa mdahalo, wananchi wengi pia wanaponung'unikia vitendo vya matumizi ya nguvu vinavyofanywa na polisi, kuongezeka kwa rushwa, ukosefu wa miundo ya usawa ndani ya jamii, ubadhirifu wa mali ya umma pamoja na kukosekana maadili mema yanayozingatia tunu za msingi za maisha ya kifamilia inaonesha udhaifu wa katiba iliyopo na kuhimiza uwepo wa katiba mpya.

Kwa kutaja tu mambo haya ambayo yule kijana mwenye jazba na hata wananchi wanataka yarekebishwe ili kuwapa maisha bora inaonesha dhahiri kuwa wananchi wanayagusa mahitaji halisi ya kuwepo Katiba mpya.

Wananchi wanapolalamika kukosa viongozi waadilifu, wakweli na wenye kuelewa maana ya Uongozi na umuhimu wa kuhamasisha na kutetea haki za jamii zao na si kujifikiria wao kwanza, wanaonesha kuifahamu Katiba vizuri sana kuliko hata sisi tunaojifanya tumeisoma kwa kuwa naamini tumeishia kukariri vifungu tu lakini hatuielewi kwa kuwa haitugusi moja kwa moja.

Mara nyingi watu wanashtushwa wakisikia wanakijiji fulani wamembana waziri huko vijijini, hii inaonesha dhahiri kuwa Watanzania wana uelewa mkubwa. Uelewa kwamba uongozi mbaya haufai. Ndio maana utaona hata leo hii ni vijijini ndiko kuna mwamko mzuri zaidi wa kupokea demokrasia na sera mbadala kuliko mijini.

Haihitaji shahada au diploma kujua uongozi mbovu, siku zote wananchi wamewaelewa viongozi wabovu na kuwatimua. Tatizo liko kwa hawa wanaojidai wana uelewa na kuwasemea wananchi ambao kwa kweli wamezoea kuishi katika mfumo wa kitawala wa ufisadi, wamevuna matunda yake na wanayafurahia.

Kabla hatujarukia kusema kuwa wananchi hawaijui katiba iliyopo hivyo hakuna haja ya kutaka katiba mpya inabidi sisi wenyewe kukubali hoja kwa mtazamo wake kisha kupambanua ukweli.

Inashangaza kuona baadhi ya wasomi kudai eti hakuna haja ya katiba mpya, hali hii inaonesha kuwa bado wana fikra za kutawaliwa kiasi kwamba leo hii hata ukiwauliza wakupe tofauti baina ya kutawaliwa na mkoloni sidhani kama wengi wanafahamu.

Ingawa sioni sababu ya kusitisha mchakato wa kutafuta katiba mpya lakini bado sikubaliani na aina ya mchakato tunaoutumia katika kupata katiba mpya kwa kuwa aina hii hujulika kama Power-centred constitution (katiba kuandaliwa na viongozi), badala ya people-centred consitution (katiba kuandaliwa na wananchi).

Tusisahau kuwa ni vigumu kwa Power-centred constitution kutusaidia kupata katiba nzuri kwa kuwa miongoni mwa waandaaji wa katiba yupo mwenye nguvu kuliko wengine wote ya kukataa jambo bila kuhojiwa; rais.
Vilevile, ni vigumu kupatikana katiba nzuri iwapo mmoja wapo ana uwezo wa kulazimisha jambo fulani likubaliwe kinyume cha matakwa ya wengine. Na ni vigumu mno kupata katiba nzuri kama mmoja kati ya waandaaji ana uwezo peke yake wa kuteua wajumbe wa kuandaa katiba hiyo.

Katiba nzuri haiandaliwi na wajumbe walioteuliwa na mamlaka moja, bali makundi yanayoshiriki yakishatambuliwa na kujulikana, huteua wawakilishi kwenye kongamano la kuandaa katiba.

RAIS RUPIAH BANDA: Akina mama wa Zambia waapa kumnyima usingizi uchaguzi ujao

 Rais wa Zambia, Rupiah Banda

LUSAKA
Zambia

ELIZABETH Phiri aliwahi kukasirishwa mno alipopuuzwa kama mgombea wa ubunge wa chama cha Patriotic Front katika uchaguzi mdogo mwaka 2008 kutokana na jinsia yake na hivyo kujiondoa katika chama hicho. Miaka mitatu baadaye, amejiunga tena na chama hicho lakini bado ana wasiwasi – lakini wanawake wengine wanasiasa wanaona kuna sababu ya matumaini katika uchaguzi wa mwaka huu 2011.

Edith Nakawi ni kiongozi katika chama cha Forum for Democracy and Development (FDD), anakubali kuwa kuna tabia ya kawaida kwa wanaume “kuwadharau wagombea wanawake”. Nakawi, ambaye ameongoza chama chake tangu mwaka 2005, ameweka historia kwa kuwa rais wa chama cha siasa mwanamke wa kwanza katika taifa la Zambia. Kabla ya hapo, alivunja rekodi nyingine ya kuwa waziri wa fedha wa kwanza mwanamke nchini Zambia na Kusini mwa Afrika mwaka 1998. Pia aliwahi kushika nafasi ya uwaziri katika wizara mbalimbali kati ya mwaka 1992 na 2001.

Siku za karibuni imekuwa ikisemwa kuwa siku za wanaume pekee kugombea urais zimeisha nchini Zambia. Wakati tarehe za uchaguzi wa mwaka huu zitakapotangazwa, Nakawi ataingiza jina lake, pamoja na wengine ambao wanataka kuongoza nchi ya Zambia kwa miaka mitano ijayo.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 2006, kulikuwa na kilio hasa kutoka kwa mashirika ya kiraia juu ya uwakilishi mdogo wa wanawake. “Lakini siyo wakati huu,” anasema Nakawi. Ana imani kuwa mwaka huu wanawake wengi zaidi watashinda uchaguzi.

Kwa sasa kuna wabunge 24 tu kati ya wabunge 150. Katika Baraza la Mawaziri kuna wanawake watano mawaziri kati ya 21. Kuna manaibu waziri wanawake 6 kati ya 20.

Pia kumekuwepo habari ambazo ni nzuri kwa rais Banda kuhusu kuvunjika kwa Muungano kati ya vyama viwili vikubwa vya upinzani nchini Zambia baada ya kutokea sintofahamu miongoni mwa viongozi wa vyama hivyo. Muungano huo uliobuniwa mwaka 2009 uliviunganisha pamoja vyama vya Patriotic Front (PFP) na United Party for National Development (UPND).

Muungano huo ulikuwa ukimkosesha usingizi Rais Rupia Banda pamoja na chama tawala. Habari zilisema kuwa ndoa hiyo ya kisiasa kati ya PFP na UPND ilivunjika baada ya pande mbili hizo kushindwa kufikia makubaliano juu ya nani hasa anafaa kuwania urais kwa tiketi ya muungano huo.

Weledi wa siasa za Zambia wamelitaja tukio hilo kuwa pigo kwa demokrasia ya nchi hiyo kwani hakuna chama chochote cha upinzani kinachoweza kushinda uchaguzi kikiwa peke yake.

Historia ya Rupiah Banda

Rupiah Bwezani Banda alizaliwa Februari 13, 1937, ni rais wa nne wa Zambia tangu ijipatie uhuru wake kutoka kwa wakoloni. Ameshika wadhifa huo tangu 2008.

Wakati wa Urais wa Kenneth Kaunda, Banda alishika nyadhifa muhimu za kidiplomasia na alikuwepo katika ulingo wa siasa kama mwanachama wa United National Independent Party (UNIP). Miaka iliyofuata, aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais na Rais Levy Mwanawasa Oktoba mwaka 2006, baada ya uchaguzi wa marudio. Alishika madaraka ya urais baada ya Mwanawasa kuugua kiharusi mwezi Juni 2008, na kufuatia kifo cha Mwanawasa mwezi Agosti 2008, alikuwa Kaimu Rais.

Kama mgombea wa chama kilicho madaralani cha Movement for Multiparty Democracy (MMD), alishinda uchaguzi wa urais Oktoba 2008 kwa kupata ushindi mwembamba, kwa mujibu wa matokeo rasmi.

Maisha ya awali na diplomasia

Banda alizaliwa katika mji wa Miko, Gwanda, Rhodesia ya Kusini (sasa Zimbabwe); wakati wazazi wake walipokwenda huko wakitokea Rhodesia ya Kaskazini (Zambia), walikwenda kutafuta ajira kabla ya kuzaliwa kwake, na alifadhiliwa na mhubiri Kiholanzi aliyemsaidia kuendelea elimu yake. Aliweza kushiriki siasa wakati alipojiunga na tawi la vijana wa UNIP mwaka 1960.

Banda kamuoa Hope Mwansa Makulu, mwaka 1966 na wana watoto watatu. Banda pia ana watoto wawili kutoka katika mahusiano yake ya awali.

Alikuwa mwakilishi wa UNIP katika nchi za Ulaya ya Kaskazini miaka ya 1960, na 1965 aliteuliwa kuwa Balozi wa Zambia nchini Misri. Wakati huo, akawa na urafiki na kiongozi wa UNITA, Jonas Savimbi, na uamuzi wa kuruhusu UNITA ifungue ofisi mjini Lusaka wakati huo ulitokana na ushawishi wa Banda.

Banda aliteuliwa kuwa Balozi nchini Marekani Aprili 7, 1967. alifanya kazi kwa miaka miwili, kisha akarudi Zambia na kuwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Vijijini kwa miaka miwili na baadaye akawa Meneja Mkuu wa Bodi ya Masoko ya Kilimo ya Taifa kwa miaka miwili.

Kisha aliteuliwa kuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Umoja wa Mataifa, na wakati akiwa katika nafasi hii aliongoza Baraza la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya Namibia. Baada ya mwaka mmoja katika Umoja wa Mataifa, aliteuliwa katika Baraza la Mawaziri kama Waziri wa Mambo ya Nje. Katika kipindi kifupi cha Uwaziri wa Mambo ya Nje (1975-1976), Banda alikuwa na kazi ya ngumu kujaribu kusitisha vita vilivyopamba moto Angola.

Siasa

Banda alichaguliwa kuwa Mbunge wa jimbo la Munali mwaka 1978 na kuchaguliwa tena mwaka 1983. Ingawa alishindwa katika uchaguzi wa mwaka 1988, alifungua kesi mahakamani. Pia, wakati huo alifanya kazi kama Waziri wa Nchi anayeshugulikia Madini. Mwaka 1991, alishindwa katika uchaguzi wa ubunge wa jimbo la Munali na mgombea wa Movement for Multiparty Democracy (MMD), Ronald Penza. Ingawa awali alikuwa na nia ya kuwania tena katika uchaguzi wa mwaka 1996, aliunga mkono mgomo ulioitishwa na UNIP kugomea ya uchaguzi.

Baada ya Rais Mwanawasa kuchaguliwa tena Septemba 2006, alimteuwa Banda kuwa Makamu wa Rais Oktoba 9, 2006 pamoja na baraza jipya la mawaziri. Baadaye alijiunga na MMD baada ya uteuzi wake. Uteuzi wa Banda ulichukuliwa kama zawadi ya Wazambia wa Mashariki kwa kuikiunga mkono MMD katika uchaguzi, hii ilikuwa ni mara ya kwanza kwa watu wa Mashariki kufanya hivyo.

Kabla ya mkutano uliopangwa wa Jumuia ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) Agosti 2007, Banda alitumwa na Mwanawasa kuboresha mahusiano na nchi jirani ya Zimbabwe kufuatia Mwanawasa kuukosoa utawala wa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe.

Kaimu Rais

Baada ya Mwanawasa kuugua kiharusi wakati akihudhuria mkutano wa Umoja wa Afrika nchini Misri 29 Juni, 2008, Banda alikaimu nafasi ya Rais.

Kama Makamu wa Rais, Banda pia alifanya kazi kama kiongozi wa shughuli za serikali katika Bunge la Taifa, hata hivyo, wakati Bunge lilipokutana Agosti 5, 2008, kufuatia ugonjwa wa kiharusi wa Mwanawasa, Banda alimteua Waziri wa Ulinzi, George Mpombo, kuongoza serikali katika biashara ndani ya ubunge.

Mwanawasa hakupona kiharusi, alikufa wakati akiwa bado yupo hospitali mjini Paris Agosti 19, 2008. Akielezea “huzuni kubwa na masikitiko makubwa”, Banda alitangaza kifo chake kwa taifa na kutangazwa kipindi cha siku saba za maombolezo ya kitaifa, kuwataka Wazambia “kubaki watulivu na kumuomboleza Rais wetu kwa heshima.” Banda alichukua rasmi nafasi ya kaimu rais kabla ya uchaguzi mpya wa rais, ambao kwa mujibu wa Katiba unafanyika ndani ya siku 90 baada ya kifo cha Mwanawasa.

Banda aliomba ateuliwe kuwa mgombea wa MMD Agosti 26, 2008. Siku hiyohiyo, chama cha MMD katika jimbo la Mashariki kilitoa taarifa kuunga mkono ugombea wa Banda. Halmashauri Kuu ya Taifa ya MMD ilimchagua Banda kuwa mgombea urais kwa kura ya siri Septemba 5. Alipata kura 47 dhidi ya 11 za Ngandu Magande, Waziri wa Fedha. Katika tukio hili, Banda aliahidi “kuunganisha chama na taifa zima” na “kuendelea kutekeleza mipango ya Mwanawasa”.

Uchaguzi wa rais ulifanyika Oktoba 30. Matokeo ya awali yalimuonesha mpinzani mkuu wa Banda, Michael Sata wa Patriotic Front (PF), kuongoza, lakini kura kutoka maeneo ya vijijini zilipohesabiwa, Banda alipunguza pengo na hatimaye kumshinda Sata. Matokeo ya mwisho ya Novemba 2 yalionesha Banda kupata asilimia 40 ya kura dhidi ya asilimia 38 za Sata.

Banda aliapishwa katika Ikulu siku hiyohiyo, alitumia hotuba yake kutoa wito wa umoja. Chama cha PF kilitoa madai ya kuwepo udanganyifu na kilikataa kuutambua ushindi wa Banda, wakati wafuasi wa Sata walipofanya vurugu katika miji ya Lusaka na Kitwe.

Urais

Kama Rais, Banda alilenga kwenye maendeleo ya kiuchumi, alisafiri nje ya nchi kutangaza biashara ya Zambia kwa viongozi wengine wa dunia. Mwezi Disemba 2010, alisafiri hadi Misri kukutana na Rais Hosni Mubarak.

Katikati ya 2009 ilitangazwa kwamba Halmashauri Kuu ya Taifa ya MMD imemteua Banda kuwa mgombea wa chama hicho kwa uchaguzi wa rais 2011. Baadhi ya watu wamekosoa, wakisema kuwa mchakato wa uteuzi unapaswa kuwa wazi kwa wagombea wengine; Mpombo, Waziri wa Ulinzi, alijiuzulu wadhifa wake mwezi Julai 2009 wakati akikosoa mchakato huo kuwa haukuwa wa kidemokrasia.

Makala hii imeandalaiwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari