Apr 20, 2011

Sherehe hizi bila kutatua kero za Muungano kazi bure

 Tanzania katika bara la Afrika

 Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, 
Jakaya Mrisho Kikwete

Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,
Dk. Ali Mohammed Shein

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MUUNGANO wa nchi mbili za Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa jipya la Tanzania ulizaliwa Aprili 24, 1964, na Jumanne ya wiki ijayo unatimiza miaka 47.

Hadi sasa Muungano huu umeshapitia misukosuko na dhoruba za kila aina, lakini bado unaendelea kuwepo na kunawiri hata kama kuna hali ya mashaka, huku nchi nyingi za Kiafrika, Kiarabu na hata Asia zilizokuwa zimeungana kama sisi miaka ya nyuma zilishindwa kuuendeleza.

Kumbukumbu zangu zinanieleza kuwa mojawapo ya waliokuwa nchi moja na kutengana ni Ethiopia iliyotengana na Eritrea, pia iliyokuwa Rwanda-Burundi ambayo sasa ni nchi mbili za Rwanda na Burundi, India iliyogawanyika na kuzaa Pakistan, na Pakistan ikazaa Bangladesh.

Hali ya mashaka ninayoizungumzia hapa inatokana na kile kinachodaiwa kuwa kuundwa kwa Muungano wetu kulikuwa siri na tangazo la kutiwa saini mkataba wa Muungano kati ya Rais wa Tanganyika, Mwalimu Julius K. Nyerere, na Rais wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, liliwashangaza watu kutoka pande zote za muungano; Bara na Visiwani.

Habari zinazidi kupasha kuwa hali hii ilitokana na habari za Muungano kuwa za siri na watu wa pande zote mbili za Muungano hawakushauriwa utadhani hawakuwa na haki yoyote ya mustakabali wa nchi yao.

Ndiyo maana nafikiri kuendelea kudhani kuwa kujadili jambo lolote linalohusu Muungano ni uhaini au kuendelea kuyafumbia macho masuala ya Muungano tutakuwa tunajidanganya, kwani kuficha au kudharau maradhi ni ugonjwa hatari, na ipo siku mauti itatuumbua.

Ukiuangalia Muungano wetu kijuujuu utaona kuwa ni mfano mzuri sana wa maelewano kwa watu wa Bara la Afrika, lakini chini kwa chini kunafuka moshi ambao ukiachwa hivi hivi bila kutafutiwa ufumbuzi utakuja kujitokeza moto mkubwa ambao tunaweza kushindwa kuuzima na hivyo matokeo yake hayatakuwa mazuri.

Kwa kuwa tupo katika kipindi cha kuelekea kwenye mchakato wa kupata Katiba mpya, nadhani ni wakati mwafaka kila Mtanzania aweke maslahi ya taifa mbele bila ushabiki, viongozi nao wawe mstari wa mbele kuonesha njia na siyo kuwa na sauti ya mwisho juu ya Muungano.

Japo sijabahatika kukutana na mtu yeyote aliyeeleza waziwazi kuwa hautaki Muungano, lakini karibu kila mtu ninayezungumza naye kuhusu Muungano amekuwa akiulalamikia kwa namna moja au nyingine. Nadhani Jumanne ijayo tutakapokuwa tukiadhimisha miaka 47 ya Muungano si vibaya Serikali ikakaribisha maoni, kwa dhati kabisa, namna ya kuuboresha muungano wetu na kuyafanyia kazi.

Kwa Watanzania wengi kutoka pande zote zinazohusika na Muungano, inaonekana wazi hawapingi kuungana, kwani muungano kwao ni baraka. Ila hiki kinachoitwa Kero za Muungano.

Kero hizi ni pamoja na mfumo wa Muungano, ikiwa ni pamoja na wanaotaka muundo wa serikali mbili uendelee, lakini wapo wanaosema uwe wa serikali moja na wapo wanaopendelea mfumo wa shirikisho wa serikali tatu. Nadhani wote wanapaswa kusikilizwa, ikiwa ni pamoja na sababu wanazotoa kama kweli tunataka kuuboresha Muungano. Muundo wa Muungano, hata kama chama tawala kimekuwa kikidai kuwa sera yake ni ya serikali mbili, linatakiwa liwe jambo litakaloamliwa na wananchi wenyewe kupitia kura ya maoni.

Ukiangalia kwa makini utagundua kuwa Muungano wetu uliundwa ukiwa zaidi na sura ya kisiasa na ulikuwa wa mambo 11 kama ambavyo imekuwa ikielezwa, lakini sasa wapo wanaosema yamefika 22 na wengine hudai ni zaidi ya 30. Kumekuwa na utata juu ya kuongezeka mambo ya Muungano na viongozi wengine wanasema mengi yameongezwa kinyemela.

Hata hili la ushirikiano wa kimataifa halikuwa limejumuishwa katika orodha asili ya mambo ya Muungano na ndiyo maana Zanzibar waliamua kujiunga na Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), kwa vile suala hili halikuwa la Muungano, hali iliyoutikisa Muungano na kusababisha mzozo mkubwa.

Kero nyingine ni kuhusu Rais wa Zanzibar aliyetakiwa moja kwa moja awe Makamu wa Rais wa serikali ya Muungano kama Rais atatoka Bara, na pale Rais atakapotoka upande wa pili, yaani Zanzibar mwenzake wa Bara awe Makamu wa Rais. Lakini hili limeondolewa bila ya kura ya maoni, kwa hofu tu zisizo na maana yoyote

miaka ya hivi karibuni zimekuwa zinasikika kelele kutoka Zanzibar kutaka masuala ya uchimbaji na biashara ya mafuta na bahari kuu yatolewe katika orodha ya Muungano, huku Mamlaka ya Kodi ya Mapato pia ikilalamikiwa.

Maadhimisho haya yaende sambamba na kuchukua hatua za uhakika na si propaganda ili kumaliza kero za Muungano ili watu wa upande mmoja wasihisi wenzao wa upande wa pili wanapendelewa kama ilivyo sasa.

Suala hili la Muungano limejitokeza hata wakati Watanzania walipokuwa wakitoa maoni yao kuhusu kuandikwa kwa Katiba mpya, Wazanzibari wameonesha kuwa na maoni tofauti na hata jinsi walivyoshiriki katika mchakato huo.

Wengi wameona kwamba kabla ya kuangalia mambo yanayoweza kuwemo kwenye Katiba mpya ni lazima tuanze na kura ya maoni kuamua juu ya suala la Muungano kati ya Zanzibar na Tanzania Bara, huku wakisisitiza kuwa Zanzibar lazima ijadili kwa uhuru Katiba hiyo mpya na lazima wahakikishe kero zilizopo juu ya Muungano zinaondolewa kabisa.

Ndiyo maana nasema sherehe za muungano hazina maana kama hatutatatua kero za Muungano.

No comments:

Post a Comment