Apr 27, 2011

Kupuuza migogoro hii ya ardhi nchini ni kama kuatamia bomu

 Mgogoro wa ardhi uliozuka baina ya wanakijiji wa Horohoro Border na uongozi wa kijiji hicho unaodaiwa kupora sehemu ya eneo la kijiji kwa lengo la kuligawa kwa wawekezaji umefanya Rais Jakaya Kikwete aombwe kuingilia kati.

 Maeneo ya migodi kama haya yameshuhudia migogoro mikubwa kati ya wananchi na wawekezaji

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MIGOGORO ya ardhi hapa nchini hivi sasa imekithiri na imefikia hatua ya umwagaji damu. Migogoro hii imegawanyika katika makundi mawili, baina ya wakulima na wafugaji na wananchi na wawekezaji.

Migogoro hasa ya wananchi na wawekezaji ambayo imechukua sura mpya hivi sasa inaitafsiri serikali yetu kuwa siyo ile ya 'mgeni njoo mwenyeji apone', bali mgeni njoo mwenyeji asulubike.

Katika maeneo mengi hapa nchini, tayari kumeshatokea uvunjifu wa amani uliosababisha damu kumwagika na hata kutokea vifo. Vurugu hizi zimetokea hata kwenye maeneo ambayo udugu na kuvumiliana vilitawala na hakuna mtu aliyedhani zingeweza kutokea. Hata hivyo, bado sizioni jitihada za haraka za kumaliza migogoro hii ambazo zimeshachukuliwa na serikali yetu.

Badala yake najionea hatua za kujaribu kuahirisha matatizo haya jambo linaloweza kutuletea maafa makubwa baadaye. Kwa mfano Serikali mkoani Manyara ilipoamua kupiga marufuku baadhi ya mashirika yasiyo ya kiserikali kutoa elimu ya masuala ya ardhi wilayani Hanang kwa madai kuwa yanawachochea wananchi, kwa mtazamo wangu sikuona kama ni dawa ya kutibu tatizo.

Jambo muhimu katika kutatua tatizo la migogoro hii ya ardhi ni kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa kutunga sera nzuri ya ardhi itakayowashirikisha wananchi moja kwa moja, kwani kuahirisha ufumbuzi wake kunaweza kusababisha madhara makubwa zaidi ikiwepo kuendelea kumwagika kwa damu ya wananchi wanaotetea ardhi yao.

Katika upekuzi wangu hivi karibuni nilibahatika kuisoma ripoti ya Taasisi ya Utafiti na Utetezi wa Haki za ardhi – HAKIARDHI ya January 30, 2009, iliyojaribu kuonesha hali halisi ya migogoro ya ardhi jinsi ilivyokithiri hapa nchini, ambapo inaonekana kuwa migogoro ya ardhi kati ya makundi mbalimbali ya watumiaji imekuwa ikiongezeka kila kukicha.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo; migogoro hiyo ni baina ya wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji na wanavijiji na serikali zao za vijiji ama serikali kuu, migogoro imeendelea kuripotiwa katika maeneo mbalimbali nchini. Migogoro hii imefikia hatua ya kusababisha uvunjifu wa amani, upotevu wa maisha na mali na kuongezeka kwa chuki miongoni mwa raia.

Kwenye vyombo mbalimbali vya habari, kuanzia magazeti, redio na hata televisheni ni migogoro ya ardhi 'kwa kwenda mbele' inayoripotiwa, vurugu zimekuwa zikijitokeza kwenye maeneo mbalimbali nchini hivi sasa, si Tarime, Kilosa, Kiteto wala Kilindi tu, bali sehemu nyingi za nchi ikiwemo Dar es Salaam na Zanzibar.

Mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji, wanavijiji na wawekezaji yamekuwa yakiripotiwa kila kukicha na kuyafanya masikio yetu kusikia vurugu hizi mara kwa mara kiasi cha akili kudhani kuwa ni jambo la kawaida tu. Hivi sasa kuna taarifa za fukuto la migogoro kama hiyo karibu katika maeneo yote yenye wafugaji nchini.

Huko Zanzibar, ingawa Serikali imeonesha kulivalia njuga suala la uporaji wa viwanja na ardhi za wananchi lakini bado kumekuwepo na malalamiko mengi kwa baadhi ya wananchi wanaofanyiwa dhuluma katika maeneo na ardhi ambazo wamemiliki kutoka kwa wazazi wao.

Chanzo cha migogoro hiyo kinadaiwa kuwa ni familia ya wakubwa fulani wakiongozwa na kiongozi mstaafu kuhodhi sehemu kubwa ya ardhi na kuwaacha wananchi wengine wakiambulia patupu huku sheria zikionekana kupindishwa makusudi ili kumlinda mkubwa huyo.

Ukiacha kando migogoro ya asili kama vile baina ya wakulima na wafugaji, au kijiji na kijiji kuhusu mipaka na kadhalika, siku za hivi karibuni hili wimbi la kuibuka migogoro inayohusiana na uwekezaji katika maeneo ya vijiji kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa, uchimbaji madini na vito na shughuli mbalimbali zinazohusiana na utalii limekuwa kubwa na linatishia amani ya nchi.

Migogoro hii inanifanya nione kuwa sera za uwekezaji mkubwa katika ardhi zimepitwa na wakati na ni muhimu sasa ziangaliwe upya na maslahi ya wazalishaji wadogo yapewe kipaumbele hasa katika kipindi hiki ambacho vijana wengi wamekosa shughuli muhimu za kuwawezesha kujikimu.

Kwa ardhi yetu hii kubwa na nzuri, vijana wengi kama watawezeshwa wanaweza kujishughulisha badala ya kukaa bila kazi huku ardhi nayo ikibaki mikononi mwa wachache, ugumu wa maisha kwa vijana utaendelea kuwepo na kuwafaanya wengi wao kujiingiza kwenye vitendo vya uhalifu.

Kwa upande wa wafugaji mabadiliko ni suala ama mchakato ambao huchukua muda mrefu, hivyo ni vyema kuhakikisha kwamba rasilimali muhimu kama maeneo ya kuchungia mifugo na maji vinapatikana sanjari na huduma kama malambo, majosho, dawa na masoko ili kuongeza tija ya mfumo wa ufugaji kwa kundi lao na kwa pato la taifa pia.

Huwa napata 'kigagaziko' kila ninapoiangalia sheria inayouruhusu mkutano wa kijiji kutoa ardhi hekari 50 bila kuingiliwa kwa kile kinachosemwa kuwa taratibu zinafuatwa, sidhani kama sheria hii ina lengo zuri kwa wananchi na isipoangaliwa upya itasababisha umwagaji mkubwa wa damu hasa pale wananchi watakapohisi kunyang'anywa ardhi yao kifisadi au vinginevyo.

Serikali kuamua kuwa na sera ya uwekezaji siyo jambo baya lakini nadhani itakuwa inafanya kosa kubwa kukaribisha wawekezaji katika ardhi bila kuwashirikisha wananchi wa eneo husika ambao wanapaswa kuridhia ardhi yao kugawiwa mgeni, serikali inapaswa kuangalia kwa upana uwekezaji huu inaoufagilia maana hao wanaoitwa wawekezaji wengi wao wanapora ardhi na kuwaacha wananchi masikini kutokana na sheria kutokuwa wazi.

Mimi si mtabiri lakini jambo hili lisipoangaliwa kwa undani zaidi kuna hatari ya kutokea maafa makubwa sana kutokana na wananchi walio wengi kukosa ardhi, ndiyo maana migogoro hii naifananisha na kuatamia bomu ambalo wakati wowote linaweza kulipuka.

No comments:

Post a Comment