Nov 30, 2011

KATIBA MPYA Wakati muafaka kuliangalia suala la walemavu kwa mapana zaidi

 walemavu hawahitaji hisani bali wanahitaji fursa

BISHOP HILUKA
Dar es Salaam

TAKWIMU za Shirika la Afya la Dunia (WHO) zinaonesha kuwa angalau asilimia 10 ya watu wote duniani wana ulemavu wa aina fulani. Kuna aina nyingi za ulemavu, ikiwa ni pamoja na ule wa Kimwili (Physical Disability), Kiakili (Mental Disability), Ulemavu wa ngozi (Albino), Uziwi, Wasioona na kadhalika.

Ulemavu unaweza kumpata mtu kwa kuzaliwa au katika maisha kwa ajali au ugonjwa. Leo hii mtu yoyote mzima anaweza kupata ulemavu wakati wowote kwa ajali au ugonjwa! Kuwa mzima ni bahati tu – hakuna anayeweza kukwepa jambo hili!

Ingawa Katiba tuliyonayo inasema wazi kuwa ni wajibu wa Serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na wazee - kwa maana kwamba huduma kwao ni wajibu na siyo msaada - lakini hali imekuwa tofauti kabisa, kwani mara nyingi walemavu huwa wanapata huduma toka Mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao, huku serikali ikionekana kuyaachia mashirika hayo ya dini jukumu hili muhimu.

Hata ukitaka kuangalia kwa undani kuhusu tafsiri sahihi ya Mlemavu, utagundua kuwa tayari imeshapindishwa na kupunguzwa (sijui kwa maslahi ya nani) kuwa zaidi suala la fursa finyu ya kupata ajira pekee, badala ya kuliangalia suala hili katika uwanja mzima wa maisha kwa ujumla kama ilivyo katika maana halisi ya ulemavu.

Kwa kuwa tafsiri halisi ya Mlemavu imepindishwa, basi hata sera, mikakati na hata utekelezaji wake navyo vimekuwa hivyo hivyo, jambo ambalo si haki na hatuwasaidii watu wenye ulemavu japo kwenye katiba yetu inatamkwa hivyo.

Kwa mujibu wa 'tafsiri halisi' ya neno ulemavu, hata tunaojidhani si walemavu bado twaweza walemavu, japo si walemavu wa viungo, ubongo wala wa ngozi, lakini tutakuwa walemavu katika namna nyingine: Walemavu wa Kisiasa (Political Disability). Wakati tukifikiria kuanza mchakato wa kujadili katiba mpya tunapaswa kwanza kujivua ulemavu huu wa kisiasa ‘Political Disability’ ndipo tuweze kuchangia maoni yetu katika katiba mpya ili kuwasaidia wenzetu wenye mahitaji maalum.

Huu ni muda muafaka wa kuachana na dhana potofu kwamba ulemavu ni ugonjwa; hii inatokana na Serikali ya Tanzania kuratibu huduma za walemavu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Nimekuwa najiuliza swali hili bila majibu; kwa nini Wizara ya Afya?

Kwa nini masuala ya walemavu tumeamua kuyaweka Wizara ya Afya, hii ni sawa na kuchukulia kuwa Walemavu ni watu wagonjwa wanaohitaji matibabu! Uratibu wa huduma za walemavu kabla ya kupelekwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, walihudumiwa na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo.

Nadhani mtizamo wetu katika suala hili unaangukia kwenye ile jinsi ya “Medical model” katika kuuangalia ulemavu. Mtizamo huu unaoangalia ulemavu kama ugonjwa, na walemavu kama watu wanaohitaji matibabu ili waweze kupona pamoja na kusaidiwa, ni mtizamo uliopotoshwa sana. Tunasahau kuwa walemavu hawahitaji hisani bali wanahitaji fursa (opportunity) ili waweze kujikwamua, na ieleweke kuwa wengine wao ni wazuri katika kazi kuliko hata sisi watu wazima.

Nadhani si vibaya wakati tukijadili Katiba mpya tukaangalia mifano ya Afrika Kusini ambao wameweka Kurugenzi (Directorate) ya watu wenye ulemavu chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, na Malawi ambao wana Waziri anayeshughulikia masuala ya Walemavu. Kwetu sisi si vibaya kama masuala ya walemavu tutaamua kuyaweka chini ya ofisi ya Raisi, Makamu wa Rais au Ofisi ya Waziri Mkuu.

Katika katiba mpya tuwe na sera zitakazoweka mikakati madhubuti ya kuwajali walemavu kwani suala la ulemavu ni suala mtambuka linalohusisha kila Wizara. Hapa panahitaji zaidi utashi wa kisiasa. Tujaribu kufikiria kuingiza katika Katiba sheria itakayozitaka Wizara zote kuwa na 'Disability desk'. Kama imewezekana kwenye suala la 'Jenda' kwa nini isiwezekane kwa watu wenye ulemavu?
Naomba kutoa hoja...

No comments:

Post a Comment