Nov 28, 2011

Mnigeria aongoza kwa utajiri Afrika, Tanzania haina kati ya 40

*Afrika Kusini ina matajiri wengi zaidi

Aliko Dangote akiwa ndani ya boti ya kifahari

JARIDA la Forbes ambalo huwa linachapisha orodha ya watu matajiri duniani, wiki iliyopita lilichapisha orodha ya kwanza ya watu matajiri Barani Afrika. Wa kwanza katika matajiri hao ni mfanyabiashara kutoka Nigeria, Aliko Dangote, ambaye anamiliki kampuni za saruji na utajiri wake unazidi dola za Kimarekani bilioni 10.Orodha hiyo iliyotolewa na jarida hilo la Forbes ina majina ya watu 40 tajiri zaidi barani Afrika ambapo utajiri wa hao wote kwa pamoja unafikia zaidi ya dola bilioni 65. katika orodha hiyo Nicky Oppenheimer (Dola 6.5 bilioni), mwenyekiti wa kampuni ya madini ya almasi nchini Afrika Kusini, De Beers, anashika nafasi ya pili.


Wengine walio katika nafasi 10 za kwanza ni Naseef Sawiris wa Misri (dola 4.75 bilioni), Johann Lupert wa Afrika Kusini (dola 4.7 bilioni), Mike Adenuga wa Nigeria (dola 4.3 bilioni), Miloud Chaabi wa Morocco (dola 3 bilioni), Naguib Sawiris wa Misri (dola 2.9 bilioni), Christoffel Wiese wa Afrika Kusini (dola 2.7 bilioni), Onsi sawiris wa Misri (dola 2.6 bilioni), na anayeshika namba kumi ni Patrice Motsepe wa Afrika Kusini (dola 2.5 bilioni).


Idadi ya matajiri 40 na nchi wanazotoka, ni kama ifuatavyo; Afrika Kusini (16), Misri (9), Nigeria (8), Morocco (5), Kenya (2) na Zimbabwe mmoja. Tanzania haina tajiri hata mmoja katika orodha ya matajiri 40 wa Bara la Afrika wakati Kenya ina wawili ambao ni pamoja na Uhuru Kenyatta anayeshika nafasi ya 26 kwa utajiri barani Afrika na Chris Kirubi wa 31.


Dangote ni nani?


Aliko Dangote alizaliwa 10 Aprili, 1957, ni mfanyabiashara wa nchini Nigeria ambaye anamiliki muungano wa makampuni yanayojulikana kama Dangote Group, ambayo yana shughuli katika nchi ya Nigeria na nchi nyingine kadhaa za Afrika Magharibi. Msaidizi huyo tajiri wa Rais wa zamani, Olusegun Obasanjo, na chama tawala cha People's Democratic Party (PDP), Dangote, huendesha biashara ya bidhaa nchini Nigeria kupitia kampuni yake na anafahamiana na wanasiasa wengi.


Akiwa na wastani wa thamani wa karibu dola bilioni 2.5, alihesabiwa na Forbes kama mmoja wa watu wenye asili ya Kiafrika walio matajiri zaidi, nyuma ya Mohammed Al Amoudi (dola bilioni 9.0) na Oprah Winfrey (dola bilioni 2.7). 


Dangote ni mwanzilishi na rais wa Dangote Group. Kwa kutajwa kwake katika orodha ya watu tajiri duniani anasema "Nadhani kuwa nilipaswa kupimwa na jarida la Forbes kwanza kabla sijaweza kuwa (kuitwa) mtu tajiri zaidi katika Afrika,” anasema Dangote. "Lakini, unajua, nina starehe." 


Aliwekwa katika nafasi ya kwanza nchini Nigeria katika orodha ya Forbes ya mwaka 2008 ya watu tajiri zaidi duniani akikadiriwa kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 3.3.


Mwanzo


Alizaliwa katika mji wa Kano, babu yake, marehemu Alhaji Sanusi Dantata alimpa mtaji mdogo wa kuanza biashara yake, na ilikuwa desturi wakati huo. Kwa hiyo, akaanza biashara katika mji wa Kano mwaka 1977 akiuza bidhaa na vifaa vya ujenzi. Alhaji Aliko Dangote alihamia Lagos mwezi Juni 1977 na kuendelea na biashara ya saruji na bidhaa nyingine. Akitiwa moyo na mafanikio makubwa na kuongezeka kwa shughuli za biashara, alianzisha kampuni mbili mwaka 1981.  kampuni hizi na nyingine zilizofuata sasa zikaunda muungano unaojulikana kama Dangote Group.


Wasifu wa Biashara


Dangote Group, ina thamani ya Naira (pesa ya Nigeria) trilioni nyingi na iliyosambaa katika nchi za Benin, Ghana, Nigeria na Togo. 


Biashara za Dangote ni pamoja na usindikaji wa chakula, utengenezaji saruji na kusafirisha mizigo. Dangote Group inatawala soko la sukari nchini Nigeria, kwani yeye ndiye msambazaji mkubwa zaidi wa sukari nchini humo katika makampuni ya vinywaji laini, watengenezaji pombe na watengenezaji peremende. 


Dangote Group imekua kutoka katika kampuni ya biashara hadi kuwa kundi kubwa zaidi la Viwanda nchini Nigeria, pamoja na kiwanda cha kusafishia sukari cha Dangote (kampuni iliyo na pesa zaidi katika Soko la Hisa la Nigeria, yenye thamani ya zaidi ya dola bilioni 3 na usawa wa Aliko Dangote umefika dola bilioni 2), kiwanda kikubwa zaidi barani Afrika cha kutengeneza simenti: Obajana Cement, na Kiwanda cha Unga cha Dangote miongoni mwa viwanda vingi.


Dangote aliwahi kujihusisha kwa sehemu kubwa katika kufadhili kampeni za Olusegun Obasanjo wakati wa awamu ya pili katika uchaguzi wa mwaka 2003, ambapo alichangia zaidi ya Naira milioni 200 (dola milioni 2). 


Alichangia Naira 50 milioni (dola milioni 0.5) akitumia kikundi cha “Marafiki wa Obasanjo na Atiku” (Friends of Obasanjo and Atiku), na akachangia Naira 200 milioni (dola milioni 2) kwa hifadhi ya vitabu ya Rais. Zawadi hizi zenye utata kwa wanachama wa chama tawala cha People's Democratic Party zimechangia wasiwasi juu ya ufisadi licha kampeni za kupambana na rushwa zilizoongozwa na Obasanjo katika kipindi chake cha pili cha uongozi.


Kama mfanyabiashara asiye mfuasi mwenye ari wa chama na aliyevunja ukabila, amekuwa mwema kwa vyama mbalimbali vya kisiasa, mashirika ya kidini na taasisi za utamaduni. Mbali ya kutoa ajira kwa wahitimu wasomi wa matabaka na makabila tofauti, amepunguza kiwango cha uhalifu kwa kushirikisha vijana wanaohitimu shule katika maeneo ya usafiri, ufungashaji vitu na usalama miongoni mwa mengi.


Inaweza kuwa ni wazo sahihi kusema kwamba kila Mnigeria ameshasikia jina lake kwa sababu ya matokeo ya biashara yake. Bidhaa zake zinatumika katika familia nyingi nchini kote. Hata wale wasiotumia bidhaa zake watakuwa wamekosa tu kwa bahati mbaya. Dangote anapatikana katika bidhaa mbalimbali zinazouzwa nje ya nchi, zinazoagizwa toka nje, mali za viwandani, mashambani na uhisani. Haya yote yameunganishwa pamoja katika kile kinachojulikana kama Dangote Group. 


Kwa masuala yake kama Rais na Mtendaji Mkuu, Aliko Dangote ni mtu mnyenyekevu. Mtazamo wa uwekezaji wake umeegemea zaidi kwenye chakula, mavazi na makazi. 


Dangote Group inaagiza tani 400,000 za sukari kwa mwaka ambazo zinachangia asilimia 70 ya mahitaji ya jumla ya nchi na ni muuzaji mkubwa wa bidhaa kwa wazalishaji wa Coca Cola, Pepsi Cola na Seven-Up nchini Nigeria. Inaagiza tani 200,000 za mchele kila mwaka, na kuagiza nje tani nyingi za saruji na mbolea na vifaa vya ujenzi.


Dangote Group pia inaagiza samaki na inamiliki meli tatu kubwa za uvuvi zilizoidhinishwa kwa ajili ya uvuvi na uwezo wa 5,000 MT. Dangote Group inauza nje pamba, kakao, korosho, mbegu za ufuta, tangawizi na ubani wa Kiarabu katika nchi kadhaa.


Shughuli


Dangote Group leo inashiriki katika aina mbalimbali ya viwanda na ina mauzo ya juu. Viwanda vya nguo vya Dangote na Nigeria Plc, ambavyo vinazalisha zaidi ya mita 120,000 za nguo zilizokamilika kila siku. Dangote inamiliki jineri katika eneo la Kankawa, Jimbo la Katsina yenye uwezo wa kuzalisha 30,000 MT za mbegu za pamba kwa mwaka.


Kiwanda cha kusafishia sukari katika bandari ya Apapa, Lagos ambacho ni kikubwa zaidi katika Afrika na cha tatu kwa ukubwa duniani chenye uwezo wa kuzalisha tani 700,000 za sukari iliyosafishwa kwa mwaka. Pia ina uwezo wa kuzalisha tani 100,000 nyingine za sukari katika kiwanda cha Hadeja katika Jimbo la Jigawa. 


Mbali na kuwekeza katika Kampuni ya Taifa ya Chumvi ya Nigeria katika eneo la Ota, Jimbo la Ogun Nchi, pia Dangote ana viwanda vya chumvi katika eneo la Apapa na Calabar, kiwanda cha mifuko ya plastiki ambacho kinazalisha mifuko inayohitajika kwa ajili ya bidhaa zake, zaidi ya matera 600 kwa ajili ya mtandao wa usambazaji na bidhaa zilizokusudiwa kuuzwa nje pia husafirishwa kwa kutumia kifuko hiyo kwenda bandarini. 


Dangote Group ina wafanyakazi 12,000. Mafanikio ya biashara za Alhaji Aliko Dangote yanaweza kuwa yamechangiwa na sababu mbalimbali. Anaonekana kuwa na upeo mkubwa. Tofauti na baadhi ya watu, msaidizi wake binafsi ni wa kutoka kabila la Yoruba wakati Mkuu wake wa Mambo ya mashirikiano ni Mkristo kutoka Jimbo la Delta. 


Kama mjasiriamali, mwenye elimu ya kawaida, amethibitisha kuwa mafanikio ya biashara yanaweza kuchangiwa na dhamira, uaminifu na uvumilivu, na si lazima uwe umepata shahada kutoka Harvard au Oxford au umefuzu daraja la kwanza la taaluma. Badala ya kuficha fedha zake katika mabenki ya nje, jambo ambalo ni la kawaida la ulaghai na uporaji wa mali za umma, Dangote amewekeza katika sekta ya uzalishaji wa uchumi wa Nigeria.


Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment