Dec 14, 2011

Inashangaza pale mwakilishi wa watu anapokosa busara kwa sababu ya posho

Peter Selukamba, mbunge wa Kigoma Mjini (CCM)

Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MIAKA hamsini ya uhuru wa nchi yetu inashuhudia kutamalaki kwa ufisadi nchini mwetu, ufisadi ambao umekua na kustawishwa na mfumo uliohalalishwa na watawala, ingawa ni watawala haohao wanaojivuna kupambana na ufisadi, huku wakija na kaulimbiu ya “Tumethubutu, Tumeweza na Tunasonga mbele”.

Kwa utamaduni huu waliojiwekea watawala wetu wa posho za vikao hata kwa mikutano ya kikazi ya idara katika mfumo mzima wa serikali, taasisi na mashirika yake, hakuna tofauti kabisa na ufisadi tunaoupigia kelele. Na sasa kuna viongozi wanaojitokeza kutetea ongezeko la posho za vikao kwa kiwango hiki cha kutisha kutoka sh 70,000/ kwa siku hadi sh 200,000/ kwa siku. Watafiti wanasema kwamba kwa ongezeko hilo, Bunge likiketi mbunge atakuwa anaingiza jumla ya 330,000/- kwa siku!

Inashangaza sana kuona mbunge aliyechaguliwa na wananchi masikini na anayewakilisha jimbo masikini zaidi kujisifu kwa uadilifu kwamba ametumwa na watu wa jimbo lake kuwatetea, lakini anainuka na kutetea/kuhalalisha ufisadi huu kwa kisingizio cha ugumu wa maisha mjini Dodoma ambako Bunge hufanya mikutano yake! Je, mbunge huyo anategemea pesa zitoke wapi za kuwapa barabara, shule, maji, umeme na kadhalika wananchi wake wakati anataka akiwa Dodoma afanye matanuzi?

Hivi anasahau kwamba Watanzania wa leo si wa jana na wameshavuka kiwango cha kudanganywa kwa hoja dhaifu kama hizo anazozitoa kuwatetea na si kuhalalisha ufisadi?

Kwa kweli leo sikufikiria kabisa kuandika makala kuhusu suala hili la ongezeko la posho kwa kuwa niliamini kabisa yote yaliyoandikwa na waandishi wengine kuhusu ongezeko hili yalitosha kufikisha ujumbe, na sikuona kama kuna jambo jipya hasa baada ya chama tawala (CCM) kuvunja ukimya na kupinga ongezeko hili.

Lakini kitendo kilichofanywa na Mbunge mmoja wa jimbo moja lililopo Magharibi kabisa mwa nchi yetu, ambaye licha ya chama chake kupinga ongezeko hili yeye amejitosa kutetea wabunge kuongezewa posho kwa nguvu zote kupitia akaunti yake ya twitter. Tena akichangia katika hali inayojionesha waziwazi kuwa ni ya jazba!

Mbunge huyo, ambaye hata hivyo anafahamika kwa kuwa kigeugeu katika masuala muhimu, amediriki kwenda mbali kidogo kwa kusema eti kama tunaona tatizo la wafanyakazi wa umma kulipwa kidogo ni sababu ya posho za wabunge basi ubunge ufutwe kabisa ili wafanyakazi wa umma wapate mishahara minono! Haya ni mawazo ya ajabu kabisa na hayakupaswa kutolewa na mtu mwenye hadhi ya ubunge kama yeye.

Hapa chini nanukuu baadhi ya hoja zake kupitia twitter.com (kama kuna makosa yoyote ya kiuandishi ieleweke kuwa sijahariri chochote kwenye maandishi yake):

“Msiwe na monopoly ya akili jamani na kudhani wengine hawafikili, you are wrong dam wrong!... Mshahara wangu ni 2,560,000 kabla ya kodi! Upotoshaji tuache!... Tujifunze na tuvumilie wanaofikilia tofauti tujadili hoja matusi sio uungwana!...”

“Anayesema alipoteza kura yake! Kwanza naamini hakunichagua! Na hatuwezi
watu wote kuna msimamo sawa! Let us think msikwepe hoja yangu! Mnaonaje tukifuta bunge! Ili tupate pesa nyingi tulipe watumishi vizuri… This is the radica thinking tujadili! Tufute bunge ili watumishi walipwe vizuri!...”

Hizi ni baadhi ya kauli za mwakilishi ambaye nimekuwa nina wasiwasi na uelewa wake, huku jimbo lake likiongoza kwa umasikini ingawa lina rasilimali nyingi mno.

Baada ya kubanwa sana na wasomaji wa mtandao, mbunge huyo alionesha kukerwa zaidi na watu wasiotaka posho ziongezwe kwa kuandika yafuatayo:

“Hakuna kuzira! Kama nyie mnaishi bila kuwa wabunge na sisi tunaweza kuishi bila ubunge! Tufute bunge kuondoa maneno!... Hakuna panic we can live without ubunge! Tufute tu! Tumesoma tutafuta kazi kwingine!...

“Nataka tufikilie jambo hili kwa mapana yake! Serikalini na mashirika yake kuna watu wanalipwa 20 mil kwa mwezi! Tujadili mfumo wote...”  
    
Huyu ndiye mwakilishi wa watu! Kwa kweli inashangaza kuona akikosa busara kwa sababu ya kutaka kuhalalisha alipwe mishahara miwili kwa kazi moja - kwa maana ya mshahara halisi na “mshahara posho nono”, jambo ambalo ni sawa na kushiriki katika kujenga misingi ya ufisadi ambayo bunge linapaswa kupambana nayo. Bahati mbaya tumefika mahali ambapo wahusika wanakosa kabisa busara na hawawezi kuona soni kuhalalisha ufisadi kwa kuwa wanaamini kuwa wanachofanya ni halali.

Anachokisema mbunge huyu kuwa kuna wafanyakazi katika mashirika hulipwa milioni 20 kwa mwezi, binafsi siwezi kukizungumzia sana kwa kuwa sina uhakika na hilo, lakini bado hakumfanyi yeye kama mbunge kung’ang’ania alipwe hizo sh 330,000/- kwa siku kama posho tu, achilia mbali mshahara. Kimsingi hakuna anayepinga mtu kulipwa vizuri lakini kwa uchumi na kipato gani cha serikali? Wabunge wakitaka kulipwa hilo, na inawezekana, wajitahidi kuisaidia na kuibana serikali katika matumizi sahihi ya rasilimali ili kipato cha nchi kipanuke. Tunaambiwa wakati tunapata uhuru mwaka 1961, nchi kama Singapore, Thailand, Malaysia na zingine kadhaa tulikuwa sawa kimaendeleo lakini leo wametuzidi maradufu. Kwa vile tumejaaliwa rasilimali kibao basi wabunge watusaidie kuifikisha nchi yetu zilikofika hizo Singapore ili wapate uhalali wa malipo zaidi

Wajue kwamba kama ni suala ni ugumu wa maisha mjini Dodoma ambako Bunge hufanya mikutano yake, ina maana maisha yamepanda mjini Dodoma tu, tena kwa wabunge peke yao? Hawajui wakati wa Bunge kuna maofisa mbalimbali ambao pia huenda huko wakiwemo waandishi wa habari? Hao hawaoni ugumu wa maisha? Au ndo ule msemo wa mwenye kisu kikali ndiye anayekula nyama!

Nakumbuka wakati ule Bunge likijadili bajeti, kiongozi wa kambi ya upinzani aliwahi kubainisha kuwa yapo maeneo ambayo viongozi wa serikali wamekuwa wanalipana hadi kati ya Shilingi milioni 1.5 na Shilingi milioni mbili kama posho za kuhudhuria vikao, hatua ambayo imewalemaza viongozi wengi wa serikali na wakati mwingine kususa kushiriki vikao wanavyoona havina posho, jambo analoona mbunge huyu (mpenda posho) kuwa ni halali kwa kisingizio cha ugumu wa maisha mjini Dodoma.

Tangu awali suala la posho lilikuwa likilalamikiwa, kwa kuwa limetumiwa vibaya kwa maslahi ya wachache wenye hulka ya ubinafsi. Ni ufisadi ambao wanaonufaika nao hawataki kukiri au kuuona kuwa ni ufisadi bali wanatumia maneno haya na yale kuuhalalisha uendelee kuwepo. Ikumbuke posho hizi zinazolalamikiwa ni zile za vikao. Yaani mbunge kwa kukaa tu Bungeni analipwa wakati ni kazi yake na analipwa mshahara.

Ndio maana nimekuwa na mashaka na hiki kinachoitwa 'Utawala Bora' kwa kuwa kwa walio wengi kimegeuka kuwa wimbo mtamu unaoimbwa na kufanyiwa semina elekezi ilimradi wateule kama huyu walipane posho zao, na kushibisha matumbo yao basi!

Naomba kuwasilisha...

No comments:

Post a Comment