Dec 21, 2011

KIM JONG-IL: Kifo chake chazua simanzi kubwa, masoko ya hisa ya Asia yashuka

Kim Jong-il

PYONGYANG
Korea

KIONGOZI wa Korea Kaskazini, Kim Jong-il, aliyefariki dunia kwa mshtuko wa moyo katika umri wa miaka 69 au 70, amesababisha mamia  ya raia wa Korea Kaskazini kugubikwa na huzuni isiyoelezeka, na wameonekana wakimlilia kiongozi wao huyo waliyempachika jina la ‘Kiongozi Mpendwa’ katika mji mkuu Pyongyang.

Mwanaye wa tatu, Kim Jong-un anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 28, ameelezewa na Shirika la habari la Korea Kaskazini (KCNA) kuwa atakuwa "mrithi mkuu" ambaye Wakorea Kaskazini hawana budi kumuunga mkono na kuwa nyuma yake. Raia jirani wa Pyongyang wako katika hali ya tahadhari, ambapo taarifa zisizothibitishwa kutoka Korea Kusini zinasema kuwa Korea Kaskazini imefanya majaribio ya nyuklia Jumatatu wiki hii.

Shirika la habari la Yonhap mjini Seoul, lillisema kuwa kombora la nyuklia la masafa mafupi lilitupwa pwani ya mashariki ya nchi hiyo maskini iliyojitenga na yenye kumiliki nyuklia lakini haikujulikana haraka iwapo jaribio hilo linahusiana na tangazo la kifo cha Kim Jong-il.

Korea Kusini imeweka silaha zake kwa tahadhari baada ya tangazo hilo, ikisema nchi hiyo ilikuwa kwenye mgogoro unaofukuta. Serikali ya Japan imefanya mkutano wa dharura. Uhusiano wa China na Korea Kaskazini na wabia katika biashara walionesha kushtushwa na habari za kifo hicho na kuahidi kuendeleza na kuimarisha "mchango wa amani na utulivu katika rasi ya ukanda huo."

Tangazo la kifo cha Kim Jong-il lilitolewa kwa kusomwa kupitia televisheni ya Taifa huku mtangazaji, akiwa na mavazi meusi, alijitahidi kuzuia machozi wakati akisema kuwa Kim Jong-il alikufa kutokana na kufanya kazi za nguvu na kiakili kupita kiasi.

Baadaye shirika la habari la KCNA likaripoti kuwa alikufa kutokana na "maumivu makali ya kifua yaliyoambatana na mshtuko wa moyo (myocardial infarction)" saa mbili na nusu siku ya Jumamosi kwa saa za Korea. Wakati huo alikuwa kwenye treni katika moja ya ‘safari zake elekezi vijijini’, KCNA lilisema.

Historia yake

Kim Jong-il alizaliwa 16 Februari 1941. Alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea, chama tawala tangu 1948, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Ulinzi ya Korea ya Kaskazini, na kamanda mkuu wa Jeshi la Watu wa Korea, jeshi la nne kwa ukubwa duniani.

Aprili 2009, katiba ya Korea Kaskazini ilifanyiwa marekebisho ili kumuunga mkono kama "kiongozi mkuu". Pia alijulikana kama "Kiongozi Mpendwa", "Baba yetu", na "Mkuu". Mtoto wake, Kim Jong-un, alipandishwa cheo na kuwa katika nafasi za juu katika Chama cha Wafanyakazi na mrithi wake. Mwaka 2010, alikuwa katika nafasi ya 31 katika Orodha ya Watu wenye nguvu zaidi duniani kwa mujibu wa jarida la Forbes.

Kuzaliwa

Maelezo ya kuzaliwa kwa Kim Jong-il yanatofautiana kulingana na vyanzo tofauti. Kumbukumbu za Urusi zinaonesha kwamba alizaliwa katika kijiji cha Vyatskoye, karibu na Khabarovsk, mwaka 1941, ambako baba yake, Kim Il-sung, aliongoza Battalion ya 1 katika Brigade ya 88 ya Kisoviet. Mama wa Kim Jong-il, Kim Jong-suk, alikuwa mke wa kwanza wa Kim Il-sung.

Wasifu rasmi wa Kim Jong-il unasema kwamba alizaliwa katika kambi ya jeshi la siri katika milima ya Baekdu mpakani mwa Japan na Korea tarehe 16 Februari 1942. Waandika wasifu walidai kwamba kuzaliwa kwake katika milima ya Baekdu kulitabiriwa, na kuonekana kwa upinde wa mvua mara mbili juu ya mlima na nyota mpya katika mbingu.

Mwaka 1945, Kim alikuwa na miaka mitatu au minne wakati Vita Kuu ya Pili ikiishia na Korea ikipata uhuru kutoka Japan. Baba yake alirejea Pyongyang mnamo Septemba, na mwishoni mwa Novemba Kim akarudi Korea kwa meli ya Urusi, akifikia Sonbong. Familia ilihamia katika nyumba ya afisa wa zamani wa Kijapani mjini Pyongyang, yenye bustani na bwawa la kuogelea. Ndugu wa Kim Jong-il, "Shura" Kim (Kim Pyong-il wa kwanza), alikufa maji kwenye bwawa hilo mwaka 1948. Taarifa ambazo hazijathibitishwa zinaonesha kwamba Kim Jong-il  aliyekuwa na miaka mitano huenda alisababisha kifo hicho. Mwaka 1949, mama yake alikufa katika uzazi. Taarifa zisizothibitishwa zinaonesha kwamba mama yake huenda alipigwa risasi na kutokwa na damu nyingi kulikosababisha kifo.

Elimu

Kwa mujibu wa wasifu wake rasmi, Kim alipata elimu yake kati ya Septemba 1950 na Agosti 1960. Alihudhuria Shule ya Msingi na Shule ya Kati mjini Pyongyang. Lakini wasomi wa kigeni wanaamini uwezekano wa kuwa alipata elimu yake ya awali nchini China kama tahadhari ili kuhakikisha usalama wake wakati wa vita vya Korea.

Wakati akisoma, Kim alishirikishwa katika siasa. Alishiriki kikamilifu katika Umoja wa Watoto na Jumuia ya Vijana, akishiriki katika makundi ya masomo ya nadharia za kisiasa na maandiko mengine ya ki-Marxist. Septemba 1957 akawa makamu mwenyekiti wa Jumuia ya vijana wa tawi la shule.

Kim pia alipata elimu ya lugha ya Kiingereza katika Chuo Kikuu cha Malta katika miaka ya 1970, katika siku za sikukuu katika Malta akiwa mgeni wa Waziri Mkuu, Dom Mintoff.

Kim mkubwa wakati huohuo alioa tena na kupata mtoto mwingine, Kim Pyong-il (alimpa jina la ndugu wa Kim Jong-il aliyekufa maji). Tangu 1988, Kim Jong-il alifanya kazi katika balozi za Korea Kaskazini katika Ulaya na ubalozi wa Korea Kaskazini nchini Poland. Wachambuzi wa kigeni wanahisi kuwa Kim Jong-il alipelekwa kutumikia nafasi hizi mbali na nchi yake na baba yake ili kuepuka kugombea madaraka kati ya watoto wake wawili.

Baadhi ya vyanzo vya Korea Kaskazini vinasema Kim Jong-il aliteuliwa kuwa mrithi mnamo Februari 1974. Kim Pyong-il aliingia madarakani kufuatia kifo cha baba yake, Kim Il Sung mnamo Julai 8, 1994.

Mahusiano ya Nje

Mwaka 1998, Rais wa Korea Kusini, Kim Dae-jung, alitekeleza Sera ya "kuboresha mahusiano” ya Kaskazini na Kusini na kuruhusu makampuni ya Korea Kusini kuanza miradi Kaskazini. Kim Jong-il alitangaza mipango ya kuagiza na kuendeleza teknolojia mpya ili kuendeleza programu ya teknolojia nchini Korea Kaskazini. Matokeo ya sera mpya, eneo la viwanda la Kaesong Park lilijengwa mwaka 2003 kaskazini ya eneo la de-jeshi, pamoja na mpango wa ushiriki wa makampuni 250 ya Korea Kusini, na kuajiri Wakorea Kaskazini 100,000, mwaka 2007. Hata hivyo, Machi 2007, eneo hilo lilikuwa na makampuni 21 tu – na kuajiri wafanyakazi Wakorea Kaskazini 12,000. Mei 2010 zilipatikana ajira kwa wafanyakazi zaidi ya 40,000 wa Korea Kaskazini.

Mwaka 1994, Korea ya Kaskazini na Marekani zilisaini makubaliano ya kufunga mpango wa silaha za nyuklia kwa Korea Kaskazini ili kupatiwa misaada katika kuzalisha nishati ya nyuklia. Mwaka 2002, serikali ya Kim Jong-il ilikiri kuzalisha silaha za nyuklia tangu makubaliano ya 1994. Utawala wa Kim ulisema uzalishaji wa siri ulikuwa muhimu kwa ajili ya usalama - akionesha Marekani inavyomiliki silaha za nyuklia nchini Korea ya Kusini na mvutano mpya na Marekani chini ya Rais George W. Bush. 9 Oktoba 2006, Shirika la Habari la Korea Kaskazini lilitangaza kwamba kulikuwa na mafanikio ya majaribio ya nyuklia.

Ziara za kigeni 2010 na 2011

Kim aliripotiwa kutembelea Jamhuri ya Watu wa China Mei 2010. Aliingia katika nchi hiyo akiwa kwenye treni binafsi tarehe 3 Mei, na kukaa katika hoteli mjini Dalian. Mei 2010, Naibu Waziri wa Marekani wa Mambo ya Mashariki ya Asia na Pacific, Kurt Campbell, aliwaambia maafisa wa Korea Kusini kwamba Kim alikuwa na miaka mitatu tu ya kuishi. Kim alisafiri hadi China tena Agosti 2010, wakati huu akiwa na mwanaye, uvumi ulienea kwamba alikuwa tayari kukabidhi madaraka kwa mwanaye, Kim Jong-un. Alirejea China tena Mei 2011, kwenye sherehe ya miaka 50 ya kutiliana saini mkataba wa urafiki, Ushirikiano na Usaidizi baina ya China na Jamhuri ya Korea Kaskazini. Mwishoni mwa Agosti 2011, alisafiri kwa treni kwenda Urusi kukutana na Rais Dmitri Medvedev kwa ajili ya mazungumzo yasiyojulikana.

Maisha binafsi

Hakuna taarifa rasmi zilizopatikana kuhusu maisha ya ndoa ya Kim Jong-il, lakini anaaminika kuoa mara moja na amewahi kuwa na wanawake kadhaa. Ana watoto wanne, wakiume watatu: Kim Jong-nam, Kim Jong-chul na Kim Jong-un, na mtoto wa kike, Kim Sul-song.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment