Dec 14, 2011

YAHYA JAMMEH: Ajigamba kuitawala Gambia hata kwa miaka bilioni

Rais wa Gambia, Yahya Jammeh

BANJUL
Gambia

WASWAHILI wanasema ukistaajabu ya Mussa, utaona ya Firauni. Rais wa Gambia, Yahya Jammeh, ameliambia Shirika la Habari la Uingereza (BBC) kwamba ataongoza kwa miaka "bilioni moja", kama Mungu akipenda. Anasema wale wanaomkosoa na kumshutumu kuwa alishinda uchaguzi wa mwezi uliopita kwa kutumia vitisho na ufisadi "wanapoteza muda wao".

Shirika la Afrika Magharibi Ecowas lilisema kuwa wapiga kura "walitishwa" na serikali ya Jammeh aliyekuwa akipania kurejea madarakani. Jammeh, aliyeingia madarakani kwa mapinduzi mwaka 1994, alichaguliwa tena kwa asilimia 72, kwa mujibu wa takwimu rasmi.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 46 anasema haogopi kile kilichomtokea Rais wa Misri aliyeondolewa madarakani kwa nguvu ya umma, Hosni Mubarak au Muammar Gaddafi wa Libya ambaye aliuawa.

"Hatima yangu iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu," Jammeh alimwambia mwandishi wa BBC.

"Nitawatimizia raia wa Gambia na kama nitatawala nchi hii kwa miaka bilioni moja, nitafanya hivyo, Mungu akipenda."

Uchaguzi wa mwezi Novemba ulikuwa wa nne tangu Jammeh alipompindua rais wa kwanza aliyeingia madarakani wakati nchi hiyo ilipopata uhuru, Dawda Jawara, akiwa na umri wa miaka 29.

Wagombea wa upinzani, Ousainou Darboe na Hamat Bah walipata asilimia 17 na 11. Darboe aliyataja matokeo hayo kama "yasiyo halali, ya kifisadi na ya kipuuzi".

Historia yake

Alhaji Dk. Yahya Abdul-Aziz Jemus Junkung Jammeh alizaliwa Mei 25, 1965. Amekuwa Rais wa Gambia tangu mwaka 1994. Kama afisa wa jeshi kijana, alichukua madaraka mwezi Julai 1994 katika mapinduzi ya kijeshi na alichaguliwa kuwa Rais mwaka 1996; alichaguliwa tena mwaka 2001, 2006, na mwaka huu wa 2011.

Rais Jammeh alipata elimu ya sekondari nchini Gambia kisha akajiunga na Jeshi la Taifa la Gambia mwaka 1986. Alipata cheo cha Luteni mwaka 1989, na mwaka 1992 akawa Kamanda wa Polisi Jeshi (Military Police) katika jeshi la Gambia. Alipata mafunzo ya kina ya kijeshi katika nchi jirani ya Senegal na katika Shule ya Jeshi la Marekani.

Julai 22, 1994, kundi la maafisa wadogo katika Jeshi la Taifa la Gambia lilichukua madaraka kutoka kwa Rais Dawda Jawara katika mapinduzi ya kijeshi na kuchukua udhibiti wa vifaa muhimu katika mji mkuu, Banjul. Mapinduzi yalifanyika bila ya umwagaji damu na kukutana na upinzani kidogo. Kundi lilijitambulisha kama Baraza la Utawala la Muda la Kijeshi (AFPRC). Jammeh, ambaye alikuwa na umri wa miaka 29 wakati huo, ndiye alikuwa mwenyekiti wa AFPRC. AFPRC iliahirisha katiba na kufunga mipaka, na kutekelezwa kwa amri ya kutotoka nje.

Wakati serikali mpya ya Jammeh ikihalalisha mapinduzi na kupiga vita rushwa na ukosefu wa demokrasia chini ya utawala wa Jawara, wanajeshi pia hawakuridhishwa na mishahara yao, hali ya maisha, na matarajio ya maendeleo yao.

Uchaguzi

Jammeh alianzisha chama cha kisiasa cha Alliance for Patriotic Reorientation and Construction.  Alichaguliwa kama rais mwezi Septemba 1996. Waangalizi wa nje walichukuliwa kuwa uchaguzi ulikuwa huru na wa haki. Alichaguliwa tena Oktoba 18, 2001 kwa asilimia 53 ya kura; uchaguzi huu kwa ujumla ulichukuliwa kuwa huru na wa haki na waangalizi, licha ya baadhi ya mapungufu makubwa ya waziwazi na vitisho vya serikali dhidi ya wapiga kura kwa kupotosha mchakato ili kumpendelea mtawala aliyepo madarakani.

Jaribio la mapinduzi dhidi ya Jammeh liliripotiwa kufanywa tarehe 21 Machi, 2006; Jammeh, ambaye alikuwa nchini Mauritania, alilazimika kurudi nyumbani haraka. Mkuu wa Jeshi, Kanali Ndure Cham, anayedaiwa kuongoza njama hizo, aliripotiwa kukimbilia nchi jirani ya Senegal, wakati wengine walikamatwa na walifunguliwa kesi ya uhaini. Aprili 2007, maofisa kumi wa zamani waliotuhumiwa kuhusika walipatikana na hatia na kuhukumiwa; wanne kati yao walihukumiwa kifungo cha maisha jela.

Jammeh aligombea kwa awamu ya tatu katika uchaguzi wa rais uliofanyika tarehe 22 Septemba, 2006; uchaguzi awali ulipangwa kufanyika Oktoba lakini ulisogezwa mbele kwa sababu ya mwezi mtukufu wa Ramadhani. Alichaguliwa tena kwa asilimia 67.3 ya kura na kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi; mgombea urais wa upinzani Ousainou Darboe alishika nafasi ya pili, kama ilivyokuwa mwaka 2001.

Novemba, 2011, Jammeh alichaguliwa tena kama rais kwa awamu ya nne, alipata asilimia 72 ya kura.

Mahusiano ya nje

Jammeh alisafiri kwenda Marekani kukutana na Prince George, Mtendaji Mkuu wa Kata ya Maryland, Jack Johnson mnamo Mei 2004.  Wakati katika Washington, eneo la DC metro, alitoa hotuba kwa Chuo cha mtakatifu Mary - Maryland wakati wa mahafali ya 2004. Katika hotuba hiyo alisisitiza dhamira ya kuinua elimu tangu alipochukua madaraka nchini Gambia.

Mwanzoni mwa Desemba 2006, Jammeh alifanya ziara ya siku tatu Iran, ambako alikutana na Rais wa Iran, Mahmoud Ahmadinejad na Kiongozi Mkuu Ali Khamenei; Ahmadinejad alisema kuwa Iran itatoa misaada ya kusaidia katika maendeleo ya Gambia, na walizungumza jinsi ya kuimarisha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Desemba 2007, alisafiri hadi Taiwan kwa lengo la kuendeleza mahusiano ya biashara kati ya nchi mbili.

Ushoga

Mei 15, 2008, Jammeh alitangaza kuwa serikali yake ingeanzisha sheria dhidi ya mashoga ambazo zitakuwa "kali zaidi kuliko zile za Iran", na kwamba "atakata kichwa" cha shoga au msagaji yeyote atakayegundulika katika nchi yake. Habari za magazeti zilionesha nia ya serikali yake kwa mashoga wote nchini humo kuuawa. Katika hotuba iliyotolewa Tallinding, Jammeh alitoa "mwisho wa mwisho" kwa mashoga au wasagaji nchini Gambia kuondoka nchini humo.

Madai ya kutibu

Januari 2007, Jammeh alidai anaweza kutibu VVU/UKIMWI na pumu kwa mimea ya asili. Alidai mpango wake ni pamoja na kuwasaidia wagonjwa kusitisha kuchukua dawa za kurefusha maisha (ARV). Madai yake yalikosolewa kwa kutangaza matibabu yasiyo ya kisayansi ambayo yanaweza kuwa na matokeo ya hatari, kutokana na imani kwamba walioruhusiwa kutoka mpango wake hawezi kuambukiza wengine. Desemba 2011, wakati wa mahojiano alirudia madai kwamba tiba ya VVU/UKIMWI "ilikwenda vizuri sana".

Gwaradzimba Fadzai, mwakilishi wa Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa (UNDP) nchini Gambia, aliamriwa kuondoka nchini humo baada ya yeye kuonesha wasiwasi kuhusu madai hayo na akasema tiba hiyo itahamasisha tabia hatarishi. Agosti 2007,

Jammeh alidai kutengeneza dripu ya mitishamba dozi moja ambayo inaweza kutibu shinikizo la damu. Jammeh pia alidai kuanzisha matibabu ya utasa kwa wanawake kama sehemu ya kile kinachoitwa Programu ya Tiba Mbadala wa Rais (PATP).

Dini

Rais Jammeh, kama walivyo Wagambia wengi, ni Muislamu. Mwezi Julai 2010, Jammeh alisisitiza kwamba watu wanapaswa kumwamini Mungu, akisema kuwa "Kama humwamini Mungu, huwezi kuwa na shukrani kwa ubinadamu na pia una hadhi ya chini kuliko ya nguruwe."

Vikwazo kwa uhuru wa habari

Jammeh amekuwa akituhumiwa kuzuia uhuru wa vyombo vya habari. Sheria mpya kali kwa waandishi wa habari zilifuatiwa na mauaji ya kutatanisha ya Deyda Hydara, mhariri wa gazeti la Point. Hydara, ambaye alikuwa mkosoaji wa utawala wa Jammeh, aliuawa kikatili Desemba 2004.  Alhagie Martin, mmoja wa wasaidizi wa karibu wa kijeshi wa Jammeh, amekuwa akitajwa kuhusiana na mauaji ya Hydara. Hata hivyo, bado haijathibitishwa kuhusu madai ya Martin na mauaji ya Hydara. Inaaminika kwamba Jammeh anawajibika na mauaji ya Hydara. Jammeh amekanusha vyombo vya usalama wala yeye mwenyewe kushiriki katika mauaji hayo.

Aprili 2004, alitoa wito kwa waandishi wa habari kutii serikali yake "au kwenda kuzimu". Juni 2005 alisema katika redio na televisheni kwamba ameruhusu "kujieleza sana" katika nchi.

Maisha ya binafsi

Ndoa ya kwanza ya Jammeh iliishia katika talaka. Jammeh alioa mke wa pili, Zeinab Suma Jammeh, mwaka 1999, na wana watoto wawili: Mariam Jammeh, na Muhammed Yahya Jammeh. Watoto wake wote wawili walizaliwa mjini Washington, DC, na uraia wa Marekani uliombwa kwa mtoto wa kwanza - lakini ombi lake lilikataliwa.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment