Dec 13, 2011

CCM wangeyatumia maadhimisho ya miaka 50 ya Uhuru kujisafisha

 
Operesheni vua magamba imebaki kama hadithi licha ya uongozi huu mpya wa sekreterieti ya CCM kupita mikoani ukielezea falsafa ya uvuaji magamba

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KAMA kuna jambo lililowahi kunigusa sana ni kile ambacho kiongozi mkuu wa Chama Cha Mapunduzi, Rais Jakaya Kikwete, alichoita kujivua gamba, yaani kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu ya uongozi ndani ya Kamati Kuu ya chama hicho kwa nia ya kujisafisha. Binafsi nilianza kuona tukipaa na kuelekea kwenye nchi mpya yenye neema, na kama kweli wangejivua gamba kwa dhati leo hii tungekuwa tunasherehekea uhuru wetu kwa furaha zaidi.

Kufuatia tuhuma mbalimbali za muda mrefu za ufisadi wa viongozi wakuu ndani ya CCM zilizokuwa zikiharibu sifa ya chama hicho kikongwe katika siasa za Tanzania, kulisababisha sekretarieti ya chama hicho iliyokuwa ikiongozwa na Yusuf Makamba ijiuzulu. Wafuatiliaji wa masuala ya siasa tulidhani kuwa huo ulikuwa mwanzo mzuri wa chama hicho kutupeleka kwenye nchi ya sali ya maziwa, kumbe...

Baada ya mabadiliko ya kiuongozi, kumtoa Makamba na timu yake na kumuingiza Wilson Mukama na timu yake, hakuna kingine kipya kilichofanyika hadi sasa zaidi ya kusikia tu kuwa mwenyekiti na chama chake wana mtihani mkubwa sana kuwatosa wanaotuhumiwa kwa ufisadi kwa kuwa bado wanaonekana kukita mizizi ndani ya Halmashauri Kuu na chama kwa ujumla.

Kwa mtazamo wangu, kama kweli viongozi wa CCM na chama wana nia ya dhati kujivua gamba kwa maana ya kujisafisha na kuwatumikia wananchi, wanapaswa wayatumie maadhimisho haya kuweka mikakati madhubuti na kuhakikisha kunakuwepo uwiano sawa kwenye mgawanyo wa rasilimali ili kwenda sawa na kaulimbiu ya mwenyekiti wao “Maisha bora kwa kila Mtanzania”.

Waelewe kuwa asilimia kubwa ya wananchi wa Tanzania (ambao wanasherehekea siku hii) wanaishi vijijini kwa kutegemea jembe la mkono, kipato wanachopata kutokana na kilimo cha aina hiyo sote tunatambua kwamba hakiwasaidii kukidhi mahitaji yao muhimu ya kila siku. Ile kauli ya mtaji wa masikini ni nguvu zake mwenyewe ingekuwa na ukweli, basi wananchi wengi wa Tanzania wangekuwa matajiri.

Maadhimisho haya CCM wanapaswa wayatumie kujivua gamba kiukweli na kuuvaa Uzalendo wa nchi yetu – kwa maana ya kuipenda nchi na kuwatumikia watu wake kikamilifu. Uzalendo ni tabia njema na inapaswa iwe pambo la kila kiongozi. Tabia hii ina athari kubwa sana katika kuchochea maendeleo ya mtu binafsi na nchi yake kwa ujumla. Uzalendo humsukuma kiongozi kuithamini na kuionea fahari nchi yake, vitu ambavyo ni chachu na hamira ya maendeleo. Uzalendo humfanya kiongozi kuitakia mema nchi yake.

Kiongozi yeyote mzalendo husukumwa na mapenzi kwa nchi yake, hawezi kulazimisha kununua ndege ya rais ya mabilioni eti hata wananchi wakila nyasi. Kiongozi mzalendo hawezi kujilimbikiza mali haramu ambazo upatikanaji wake una utata. Je, viongozi matajiri wamefanya biashara gani madarakani hadi wakaupata utajiri walio nao sasa kama si ukosefu wa uzalendo kwa nchi yao? Hivi utajiri wa viongozi wetu umelipiwa kodi ya mapato?

Kiongozi mzalendo hawezi kuchukua “ten parcent” ili kupitisha mikataba ya kinyonyaji ambayo italeta maafa kwa wananchi na kumfaidisha mgeni ambaye akishapata akitakacho ataondoka zake. Kwa kukosa viongozi wazalendo leo hii pesa za kodi ya wananchi zinaishia kujenga mahekalu na kununua magari ya kifahari ya viongozi huku wananchi wanaendelea 'kusaga rhumba' kwa kuishi chini ya dola moja ya Marekani kwa siku.

Kukosekana kwa uzalendo kumewafanya viongozi kujivua majukumu yao ya kuhakikisha wananchi wanapata fursa sawa katika kushiriki masuala ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Maadhimisho haya CCM ingeyatumia kuwaondoa viongozi wanaoshirikiana na wafanyabiashara wasio waaminifu kufanya udanganyifu na kuifisidi nchi yetu, ambayo leo tunajivuna kutimiza miaka 50 ya kuwa huru (?).

Kiongozi au mwananchi mzalendo ni yule afikaye kazini mapema kwa muda utakiwao na kufanya kazi kikamilifu kwa mujibu wa taratibu za kazi, atokaye kazini kwenda nyumbani kwa muda uliopangwa. Hili ndilo jambo CCM walipaswa kuliangalia kwa makini wakati tukisherehekea miaka hii 50. kwani ukosefu wa uzalendo (chini ya CCM) ndiyo umefanya viwanda vingi kufa, mashirika ya umma kufa na kuongeza idadi ya wazururaji na wakaa vijiweni ambao walikuwa wameajiriwa kwenye mashirika hayo.

Ukosefu wa uzalendo umesababisha umasikini nchini ambao ni wa kujitakia. Umaskini wa aina zote mbili: umaskini wa nchi na umaskini wa watu walio wengi katika ujumla wao. Yaani tunashindwa hata kujinasua kwenye hili moja la kuwa na umaskini wa watu tu huku nchi ikiondoka kwenye utegemezi wa wahisani, kama sasa ambapo bajeti yetu haikamiliki bila kutegemea wahisani.

Inapotokea serikali imekuwa maskini hadi kuendeshwa kwa misaada toka nje ya nchi huku ikiendeshwa na viongozi matajiri kuliko serikali yao, ndipo kunapokuwa na maswali, halafu mbaya zaidi na wananchi nao wakawa maskini hadi kufikia kiwango cha kushindwa kufanya lolote. Hili nalo CCM wanapaswa kuliangalia.

Ni wakati sasa watawala wetu (CCM) waelewe kuwa Watanzania siyo wavivu kama wanavyofikiria, uchumi siyo kutoa takwimu tu bali kuwawezesha Watanzania kuwa na matumaini ya kuuza mazao yao kwa wakati kutoka mashambani. Kwa hiyo sherehe hizi ziendane na kujivua gamba kivitendo.

Hadi sasa serikali ya CCM imeshatengeneza mabomu makubwa mawili; sekondari za kata, na mpango wake wa kuwaita wawekezaji wakubwa kupora ardhi ya wananchi kupitia sera yake ya kilimo kwanza.

Siku hizi kila kukicha ni migogoro ya ardhi tu inayolindima na imesababisha kumwagika damu za watu wasio na hatia, hivi hali hii itaisha lini? Viongozi wetu wataendelea kulifumbia macho suala hili hadi lini? Hili pia CCM walitazame wakati wakisherehekea miaka hii ya uhuru wa Tanganyika ambayo hata sijui imepotelea wapi!

Naomba kuwasilisha...

No comments:

Post a Comment