Dec 28, 2011

Mwaka 2011 ndiyo mwisho wa mashambulizi ya al-Qaida?

Aliyekuwa kiongozi wa al-Qaida, Osama bin Laden

Wanachama wa al-Qaida

BISHOP HILUKA
Dar es salaam

TUKIWA tunaumaliza mwaka huu hapo kesho na kuuanza mwaka mwingine siku ya Jumapili, bado kuna kumbukumbu zilizotikisika dunia. Kumbukumbu hizo ni pamoja na nguvu za umma zilizowang’oa baadhi ya viongozi waliokita mizizi katika nchi za Kiarabu, na kifo cha kiongozi wa kundi la al-Qaida, Osama bin Laden.

Kifo cha bin Laden ndicho kilichotikisa zaidi dunia kwani baada ya kifo chake dunia ilitawaliwa na hofu. Kuna walioamini kuwa baada ya kifo hicho, kundi la al-Qaida litakuwa limesambaratika, lakini wengine wakihofu ghadhabu zaidi kutoka kwa wafuasi wa kundi hilo. Uingereza na nchi nyingine za Magharibi zinaendelea kuchukua tahadhari kutokana na hofu kwamba mauaji ya Osama yanaweza kuibua mashambulizi mapya ya ugaidi. Tanzania tulionja adha ya al-Qaeda pale Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam uliposhambuliwa kwa bomu na kusababisha vifo kadhaa. Lakini sijui kama kufuatia shambulizo hilo tumekuwa tunachukua tahadhari stahili baada ya kifo cha Osama ingawa kwa siku za karibuni tumekuwa macho dhidi ya ‘watoto’ wa al-Qaeda wanaotokea Somalia kwa jina la al-Shabab.

Kwa Uingereza, baada ya kifo cha Osama Wizara ya Mambo ya Nje, ilitoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi nje kufuatilia vyombo vya habari ndani ya nchi walimo kuangalia wanavyochukulia, kuuawa kwa Osama na wawe macho. Pamoja na hali hiyo Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza, William Hague, aliziamuru balozi zote za Uingereza kupitia upya mpangilio wao wa ulinzi na usalama. Hakuna uchunguzi wa kiintelijensia ulioonesha shambulio  lolote dhidi ya Uingereza hivyo kiwango cha ugaidi kikabakia kuwa 'kikali'.

Wataalamu wa masuala ya ulinzi waliamini kwamba katika muda mfupi tishio kubwa lingeweza kuwa kwa raia wa nchi za Magharibi na hata mali na maslahi yao nje ya nchi na hususani kwenye maeneo ya Mashariki ya Kati na Asia. Kufuatia hali hiyo Polisi wa Kimataifa (Interpol) walichukua hatua ya kuonya kuhusu kuongezeka kwa kiwango cha mashambulizi ya kigaidi na kuutaka umma kuwa macho.

Mashambulizi ya Osama na al-Qaeda  

Baadhi ya mashambulizi ya kigaidi ambayo yameshafanywa na mtandao wa al-Qaeda chini ya Osama bin Laden yalitokea kati ya 1993 na 2011 ni pamoja na kulipuliwa kwa gari kwenye Kituo cha Kimataifa cha Biashara Oktoba mwaka 1993, jijini New York ambapo watu sita waliuawa.

Juni 1996 kulipuliwa lori lililokuwa na mafuta kwenye eneo la Khobar, Saudi Arabia kwenye ubalozi wa Marekani ambalo lilisababisha vifo vya askari 19 wa Marekani na kujeruhi watu 400. Agost 1998 mabomu kwenye balozi za Marekani kwenye miji ya Dar es Salaam na Nairobi yalilipuka na kuua wa 224 wakiwemo Wamarekani 12. Oktoba 2000 shambulizi la mabomu dhidi ya meli ya kivita ya Marekani kwenye bandari ya Aden lilisababisha vifo vya mabaharia 17.  

Septemba 11, 2001, magaidi 19 waliziteka ndege nne za abiria na kuzielekeza kugonga minara pacha ya Kituo cha Biashara duniani (WTC) ambayo iliteketea na kuangamiza, saa mbili baadaye, ndege ya tatu  ilielekezwa kwenye  jengo la makao makuu ya jeshi la Marekani Pentagon jijini Washington. Ndege ya nne iliianguka kwenye  uwanda wa Pennsylvania. Katika shambulizi hilo kwenye minara pacha ya WTC takribani watu 3,000 na waliokuwa kwenye ndege  waliuawa. 

Oktoba 7, 2001, kwenye kanda ya video iliyooneshwa na Televisheni ya Al Jazeera, Osama alisikika akisema kuwa Marekani haitaishi kwa amani hadi hapo Palestina nao watakapoishi kwa amani. Mwanzoni mwa mwaka 2002, mwandishi wa habari wa gazeti la Wall Street Journal, Daniel Pearl, alitekwa nyara nchini Pakistan na baadaye aliuawa kwa kukatwa kichwa na video yake kurekodiwa na al-Qaeda.

Aprili 11, 2002; lori lililipuka karibu na sinagogi la El Ghriba kwenye kisiwa cha Djerba, Tunisia kusini na kuua Wajerumani 14, raia watano wa Tunisia na Mfaransa mmoja, ambapo al-Qaeda ilidai kuhusika na shambulizi hilo. Oktoba 12, 2002 bomu lililipuka kwenye klabu ya usiku kwenye ufukwe wa Kuta, Bali nchini Indonesia na kuua watu 202 tukio hilo lilifanywa na kundi la Jemaah Islamiyah, linalohusiana na al-Qaeda.

Novemba  28, 2002 shambulizi la kujitoa mhanga lililipua  hoteli inayotumiwa sana na Waisreali nchini Kenya mjini Mombasa na kuua watu 15. Siku hiyo hiyo mizinga miwili nusura ilipue ndege ya Boeing 757 ya Israeli ikiwa na abiria 261 wakati ikiondoka kwenye uwanja wa ndege wa Mombasa na al-Qaeda wakadai kuhusika.

Mei 12, 2003 watu 35 wakiwemo Wamarekani tisa waliuawa kwenye uwanja wa Riyadhi, Saudi Arabia na mlipuko mwingine ukatokea Casablanca, Morroco na kuua watu 45 wakiwemo walipuaji 13 na kujeruhi  watu 60. Agosti na Septemba 2003 ulipuaji wa Hoteli ya Canal ambayo ilikuwa inatumika kama makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini Baghdad na kuua watu 22 akiwemo balozi wa Umoja wa Mataifa, Sérgio Vieira de Mello.

Machi 11, 2004 milipuko mfululizo wa mabomu kwenye treni mjini Madrid ilisababisha vifo vya watu zaidi ya 200 na kujeruhi wengine 1,500. Julai 7, 2005 watu wanne walijitoa mhanga na kuua watu 52 katika shambulio lililofanyika kwenye treni ipitayo chini ya ardhi.

Aprili 11, 2007 mabomu ya kujitoa mhanga yalisababisha vifo vya watu 33 katikati ya Algiers na shambulizi jingine lilifanyika Desemba ambapo milipuko miwili ilisababisha vifo vya watu 41 wakiwemo maofisa 17 wa Umoja wa Mataifa kwenye ofisi ya Umoja wa Mataifa mjni Algiers. Aprili 28, 2011, mlipuko wa bomu ulisababisha vifo vya watu 15 wakiwemo wageni kumi mjini Marrakesh, Morroco.

No comments:

Post a Comment