Dec 28, 2011

KIM JONG-UN: Mrithi wa utawala Korea Kaskazini aliyewapiku kaka zake wakubwa

Kim Jong-un

PYONGYANG
Korea

KIM Jong-un, mtoto wa kiongozi wa Korea Kaskazini aliyefariki, Kim Jong-il, ametajwa kuwa ndiye kamanda mkuu kabisa wa jeshi lenye nguvu la taifa hilo la kikomunisti.

Gazeti la chama tawala nchini humo limetoa wito kwa Kim Jong-un kuiongoza Korea Kaskazini kufikia ushindi wa daima. Hii ni mara ya kwanza kwa shirika la habari la taifa kumtaja kiongozi huyo kuwa kamanda mkubwa kabisa.

Kabla ya hapo aliitwa mrithi mkubwa kabisa, baada ya baba yake kufariki. Gazeti hilo limeahidi kuunga mkono sera iitwayo "songun", yaani jeshi ndio muhimu kabisa, sera inayoyapa kipaumbele matumizi juu ya jeshi la Korea Kaskazini.

Historia yake

Kim Jong-un ambaye pia anajulikana kama Kim Jong-Eun, zamani aliitwa Kim Jong-Woon, alizaliwa tarehe 8 Januari 1983 au 1984, ni mtoto wa tatu wa marehemu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-il na mke wake Ko Young-hee. Tangu mwishoni mwa 2010, Kim Jong-un alionekana dhahiri kuwa ndiye mrithi wa uongozi wa taifa, na hivyo kufuatia kifo cha baba yake, alitangazwa kama "mrithi mkuu" na kituo cha televisheni cha taifa. Tarehe 24 Desemba 2011, alitangazwa kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Watu wa Korea Kaskazini.

Ni Daejang katika Jeshi la Watu wa Korea, kijeshi cheo hicho ni sawa na Jenerali. Inasemwa kuwa Kim alisomea sayansi ya kompyuta kibinafsi nchini Korea ya Kaskazini. Alipata shahada mbili, moja katika fizikia kutoka katika Chuo Kikuu cha Kim Il Sung na nyingine katika Chuo cha Kijeshi cha Kim Il Sung.

Maisha ya awali

Kim anadhaniwa kuwa alizaliwa mwaka 1983 au 1984. Vyanzo vya Usalama vinasema tarehe ya kuzaliwa kwake ni tarehe 8 Januari 1984.

Alihudhuria mafunzo ya lugha ya Kiingereza katika Shule ya Kimataifa ya Bern, Uswisi, hadi 1998 kwa kutumia jina bandia. Wanafunzi wenzake wa zamani wameelezea kuwa alisoma katika Shule ya Kimataifa ya Gümligen au shule ya umma ya Liebefeld. Jina alilotumia akiwa Gümligen lilikuwa "Pak Chol" na alidai kuwa yeye ni mtoto wa dereva, ingawa hapo Liebefeld, mwalimu wa darasa aliwaambia wanafunzi kuwa anatoka Korea ya Kaskazini.

Kim anaelezewa kuwa alikuwa mtoto mwenye aibu aliyeepuka kujichanganya na watu asiowafahamu na alikuwa anajulikana kwa tabia yake ya ushindani, hasa katika michezo, na alivutiwa sana na liga ya mpira wa kikapu ya Marekani (NBA) huku akimhusu sana mchezani wa kimataifa wa nchi hiyo wa mpira wa kikapu, Michael Jordan. Moja wa marafiki zake alidai kuwa alikutana na hata kupiga picha na Kobe Bryant na Toni Kukoč, lakini hana uhakika alipiga picha wapi na wakali hao katikaNBA. Aliripotiwa kukaa Uswisi – akiwa hafungamani na upande wowote katika mgogoro kati ya Korea Kaskazini na Kusini, hadi mwishoni mwa mwaka 1999 au mapema 2000 wakati mwanafunzi mmoja alipodai "kutoweka" kwake shuleni hapo.

Balozi wa Korea Kaskazini nchini Uswisi, Ri Tcheul, alikuwa na uhusiano wa karibu na Kim na alikuwa mshauri wake. Familia ya Kim inasemekana iliandaa mikutano ya kifamilia katika Ziwa Geneva na Interlaken.

Kwa miaka mingi, ni mmoja tu aliyethibitisha picha ya Kim kwamba alikuwa anajulikana pia nje ya Korea Kaskazini, na inaonekana kupigwa katika miaka ya 1990, alipokuwa na miaka kumi na moja. Ni Juni 2010 tu, muda mfupi kabla ya kupewa rasmi nafasi ya kutambulishwa hadharani kwa watu Korea Kaskazini, picha zaidi za Kim zilinyeshwa, na hasa zilichukuliwa wakati alipokuwa akisoma nchini Uswisi. Picha yake rasmi ya kwanza katika utu uzima ilikuwa ni picha ya kikundi iliyotolewa tarehe 30 Septemba, 2010 mwishoni mwa mkutano wa chama ikielezea ufanisi wake, ambayo yeye ameketi katika mstari wa mbele, nafasi mbili kutoka kwa baba yake. Hii ilifuatiwa na picha zake za kuhudhuria mkutano huo.

Kaka yake mkubwa, Kim Jong-nam, ndiye mwanzoni alirakuwa kuwa mrithi, lakini imeripotiwa alipoteza sifa baada ya mwaka 2001, alipokamatwa akijaribu kuingia Japan kwa kutumia hati bandia ya kusafiria ili kutembelea Tokyo Disneyland.

Mpishi binafsi wa zamani wa Kim Jong-il, Kenji Fujimoto, amemebainisha maelezo kuhusu Kim Jong-un, ambaye alikuwa na uhusiano naye mzuri, na kusema kwamba aliandaliwa kuwa mrithi wa baba yake. Fujimoto pia alidai kuwa Jong-un alipendekezwa na baba yake kati ya ndugu yake, Kim Jong-chul, na sababu kubwa Jong-chul ana tabia za kupenda sana wanawake, wakati Jong-un ni "kama baba yake hasa".

Fujimoto alisema zaidi kuwa "Kama madaraka yatakabidhiwa basi ni Jong-un anayefaa. Amejengeka kimwili, ni mnywaji mkubwa na kamwe hakubali kushindwa."  Wakati Jong-un alipokuwa na miaka 18, Fujimoto alielezea tukio ambapo Jong-un alihoji kuhusu maisha yake ya kifahari, akamwuliza, "Tupo hapa, tunacheza mpira wa kikapu, tunaendesha farasi, tunaendesha Skis Jet, tuna furaha. Lakini vipi kuhusu maisha ya watu wasio na uwezo na wasiopata fursa kama hizi zetu?"

Januari 15, 2009 shirika la habari la, Yonhap la Korea Kusini, lilitoa taarifa kwamba Kim Jong-il amemteua Kim Jong-un kuwa mrithi wake.

Machi 8, mwaka 2009, BBC ilitangaza kuwepo uvumi kuwa Kim Jong-un alionekana kwenye kura kwa ajili ya uchaguzi wa Bunge Kuu la Watu, bunge la Korea Kaskazini. Baadaye taarifa zilionesha kuwa jina lake halikuwa katika orodha ya watunga sheria. Hata hivyo, baadaye alipandishwa katika nafasi ya kati katika Tume ya Taifa ya Ulinzi, ambayo ni tawi la kijeshi la Korea Kaskazini.

Kuhusu afya yake licha ya kujengeka kimwili, ripoti pia zimefichua kuwa Jong-un ni mgonjwa wa kisukari na anakabiliwa na shinikizo la damu.

Kuanzia mwaka 2009, ilieleweka kwa diplomasia za nje kwamba Kim alikuwa mrithi wa baba yake Kim Jong-il kama mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Korea na kiongozi wa Korea ya Kaskazini. Baba yake pia aliwataka wafanyakazi wa balozi nje ya nchi kuwa waaminifu kwa mtoto wake. Pia kulikuwepo taarifa kuwa wananchi wa Korea ya Kaskazini walihimizwa kuimba "wimbo wa sifa" kwa Kim Jong-un, kwa mtindo sawa na ule wa nyimbo za sifa zinazohusiana na Kim Jong-il na Kim Il-sung.

Baadaye mwezi Juni, Kim aliripotiwa kutembelea China kwa siri na "kujitambulisha mwenyewe" kwa uongozi wa China, ambao baadaye walionya dhidi ya Korea ya Kaskazini kufanya jaribio lingine la kinyuklia. Wizara ya Nje ya China ilikanusha vikali kuwepo ziara hii.

Baada ya kifo Kim Jong-il

Desemba 17, 2011, Kim Jong-il alifariki.  Pamoja na mipango ya Kim mkubwa, haikufahamika mara moja baada ya kifo hicho kama Jong-un atachukua madaraka kamili, na nini nafasi yake kamili katika serikali mpya. Baadhi ya wachambuzi waliamini kwamba baada ya kifo cha Kim Jong-il, Chang Sung-taek angechukua hatua kama mtawala wa muda, kwa kuwa Jong-un hana uzoefu wa kuongoza nchi na bado ni ‘mtoto’.

Lakini kwa sasa ametangazwa hadharani kuwa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Watu wa Korea, Jumamosi ya tarehe 24 Desemba 2011, hatua inayoonesha kuwa atatwa madaraka ya nchi punde.

Makala haya yameandaliwa na Bishop Hiluka kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

No comments:

Post a Comment