Mar 16, 2011

Ni lini walemavu watapewa fursa sawa kwenye jamii yetu?

 Walemavu kama huyu wanahitaji kuwezeshwa

 Watoto wenye ulemavu wa ngozi wakifarijiwa

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HIVI karibuni nilishuhudia kupitia moja ya vituo vya televisheni habari iliyonisikitisha sana kumhusu binti mwenye ulemavu wa ngozi, Mariam Juma, aliyefungwa minyororo miguuni na baba yake kwa zaidi ya miaka mitatu huko wilayani Muheza, Tanga.

Mariam ambaye ni mtoto wa kwanza katika familia ya Juma Salim Ngatu ambaye kwa sasa ni marehemu, amezaliwa mwaka 1982 katika familia ya watoto sita.

Kwa habari hiyo naamini kuwa kuna matatizo kwa pande zote; jamii na serikali. Bahati mbaya walemavu wengi walioko katika familia au jamii duni, na wengi wao wanafichwa na familia zao ndani ya nyumba na hawatoki nje kukubali ukweli wa mambo.

Nimepata bahati ya kuwa mmoja wa waandishi wa kwanza waliobahatika kupata mafunzo maalum ya Uandishi wa Habari za Walemavu yaliyoandaliwa na Baraza la Habari Tanzania (MCT), ambapo tulidokezwa kuwepo jinsi mbili za jamii inavyouangalia ulemavu:
Medical model; Mtizamo unaoangalia ulemavu kama ugonjwa, walemavu wanaangaliwa kama watu wanaohitaji matibabu ili waweze kupona pamoja na kusaidiwa. 
Bio-psychosocial model; Mtizamo unaoonesha ulemavu ni muunganiko wa mambo mengi na mitizamo ya kibinadamu, mila desturi na kadhalika.

Bahati mbaya walio wengi (nikiwemo mimi kabla sijapata mafunzo) wapo kwenye mtizamo wa kwanza, wakidhani kuwa walemavu wanahitaji kuhurumiwa badala ya kuwezeshwa. Suala la watu wenye ulemavu ni suala linalohitaji msukumo mkubwa wa kisiasa.

Kama Jamii tunapaswa kukazia umuhimu wa kulinda na kutunza utu na heshima ya mwanadamu, lengo likiwa kuhakikisha kuwa Jamii inafanikiwa, utu wa mwanadamu unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika mikakati ya maendeleo endelevu.

Ili kulinda na kuheshimu zawadi ya maisha, changamoto inayokwenda sambamba na mapambano dhidi ya baa la umaskini, huduma bora za afya na fursa makini zitakazowawezesha watoto wote, hata walio na ulemavu kukuza karama na vipaji walivyokirimiwa na Mungu, katika mchakato wa makuzi ya mtu mzima.

Serikali pia inapaswa kuhakikisha kwamba, watu wanapata huduma bora za afya, bila kusahau kutoa msaada na huduma kwa walemavu ambao ni sehemu ya jamii, ili walau kila mtu aweze kuishi maisha yenye hadhi kama binadamu.

Ukirejea sera ya Taifa letu ya Ulemavu ya 2004 utaona tafsiri ifuatayo:Disability is the loss or limitation of opportunities to take part in the normal life of the community on an equal level with others due to temporary or permanent physical, mental or social barriers.

Watanzania tumekuwa tukiliangalia suala la walemavu kama fursa finyu ya kupata ajira pekee badala ya kuliangalia katika uwanja mzima wa maisha kwa ujumla kama ilivyo katika maana ya ulemavu.

Hivyo pamoja na suala la ajira pia tunapaswa kuangalia maeneo mengine ambayo mlemavu wa Tanzania hapewi haki sawa:
Mosi, elimu; hakuna mkazo wa kuongeza Shule za Sekondari na hata Vyuo Vikuu maalum kwa ajili ya walemavu wa aina fulani mfano viziwi, vipofu na kadhalika.
Pili, miundombinu; Ujenzi wa majengo na barabara zinazowajali walemavu.
Tatu, mawasiliano; Kuongeza Ukalimani katika vipindi vya televisheni kwa ajili ya viziwi, au majarida yenye maandishi maalum (braille) kwa ajili ya wasioona na kadhalika.
Nne, starehe na Michezo; Kubuniwa michezo na mashindano mbalimbali ambayo washiriki walemavu wasioona, wasiosikia, wasioongea na wale wenye ulemavu wa ngozi wangeshiriki na kupewa zawadi kama kujengewa nyumba na kupewa usafiri unaostahili.
Nawapongeza sana waandaaji wa michezo ya Olympic kwa kuliona hilo na kuanzisha mashindano maalum (
Paralympic) kwa ajili ya walemavu.

Naomba ieleweke kuwa sisi tunaodhani kuwa si walemavu twaweza kuwa si walemavu wa viungo, ubongo wala ngozi lakini tukawa Walemavu wa Kisiasa na Kifikra (
Politically and Mentally Disabled). Lakini pia tutambue kuwa kesho na keshokutwa tunaweza kujikuta tupo katika kundi hili.

Tusiwatenge au kuwanyanyasa walemavu kwa ulemavu wao. Badala yake tuwaoneshe upendo, tuwathamini na tuwatie moyo ili waweze kuendeleza vipaji vyao na hivyo kuboresha maisha yao. Tunapaswa tuondokane na ulemavu wetu wa kisiasa na kifikra ili kuwasaidia wenzetu wenye ulemavu wa viungo katika kujikwamua.

Pia kuna kosa kubwa sana ambalo tumekuwa tukilifanya bila kujua kwa kudhani aliye na ulemavu ni mtu asiyejiweza na anayestahili huruma (
charity), tukasahau kuwa wengi wa watu wenye ulemavu wakipewa fursa stahiki ni watu walio na uwezo mkubwa wa kuchangia maendeleo yao na maendeleo ya jamii kwa ujumla.

Walemavu wanaweza kuchangia kwa kiwango kikubwa kuliko hata watu wasio na ulemavu. Wenye ulemavu ni sehemu ya jamii yetu na wakiwezeshwa na kuthaminiwa wanaweza. Watu wenye ulemavu ni rasilimali watu ya taifa kama wale wasio na ulemavu.

Haya yote yanawezekana, pamoja na kumtambua mlemavu kuwa sehemu muhimu ya jumuiya tumruhusu atoe mchango wake inavyopaswa badala ya kudhani kuwa yeye ni mtu wa kuhurumiwa na kusaidiwa tu, huku tukifikiria kuwa haki yake ni kubeba kibakuli maeneo ya posta kuomba msaada au kusubiri Ijumaa. Kwa nini tunashindwa kuweka sheria zitakazompa haki sawa mlemavu kati yetu?

Katiba ya Tanzania inasema wazi kuwa ni wajibu wa serikali kuwahudumia watu wenye mahitaji maalumu kama walemavu na wazee. Huduma ni wajibu na siyo msaada. Walemavu mara nyingi hupata huduma toka mashirika ya dini na vyama vyao vya hiari vya kutetea haki zao. Hali hii inaonesha kuwa serikali na jamii kwa ujuma vimeyaachia mashirika ya dini jukumu hili muhimu.

Pengine sina taarifa sahihi, lakini naamini kuwa serikali inapaswa kuzidisha uboreshaji wa mifumo yetu ya elimu na mazingira yake ili kuwarahisishia watoto wenye ulemavu kupata fursa ya elimu. Pia serikali ina jukumu la kuwahamasisha wazazi wenye watoto wenye ulemavu kuwapeleka watoto wao shule.

Kutokana na baadhi ya imani potofu kuhusu wenye ulemavu, mara nyingi wamekuwa wanakumbana na vikwazo vingi kutoka katika ngazi za familia zao na jamii kwa ujumla katika kuendesha shughuli zao na kuendeleza maisha yao. Hata mauaji yaliyokuwa yakifanyika si walemavu wa ngozi tu waliokuwa wanauawa bali hata walemavu wengine. Baadhi ya jamii zilikuwa zikiwaua watoto wachanga waliozaliwa na ulemavu.

Ni wakati sasa tufikirie kuanzisha kitu kinachoitwa universal accessibility kwenye maeneo yetu ikiwemo vyoo kwa ajili ya walemavu na vyombo vya usafiri; mabasi yanayoshuka kumwezesha mlemavu apande bila bughudha. Kwenye majengo; milango mipana yenye kuruhusu walemavu kupita. Taa za barabarani (traffic light) pia ziboreshwe kwa kuziwekea sauti maalum itakayokuwa ikimruhusu mtu asiyeona kujua wakati gani anaweza kuvuka.

Nimekuwa nasita kuamini kuwa jamii yetu ina mapenzi kwa walemavu. Wengi katika jamii hii wanawaona walemavu kama mzigo na wasingependa kukumbushwa kuwepo kwao. Mtazamo huu vilevile upo katika tunavyowaona wenye kuishi na virusi vinavyosababisha ugonjwa wa Ukimwi (VVU). Ni aghalabu mtu kuutangazia umma kuwa ndugu yake ana VVU na anapofariki magonjwa mbadala yanatafutwa kuelezea kifo chake.

Kitu kingine tusichokijua ni kwamba watu wenye ulemavu hawahitaji “kuhurumiwa” kama tunavyowafanyia, wanachohitaji ni kutengenezewa sera bora na kuwezeshwa. Kunatakiwa kuwe na mfumo wa jamii utakaosimamia na kulinda haki zao, na kuwapa fursa zitakazowawezesha kuchangia katika maendeleo ya taifa.

Huruma haiwezi kujenga, sana sana itaendelea kuongeza watu wenye ulemavu wenye vibakuli wakiomba barabarani kama ilivyo pale Posta na Selander Bridge kwa jiji la Dar es Salaam na maeneo mengine mijini!

Kwa Tanzania Serikali huratibu huduma za walemavu kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Kabla ya hapo Walemavu walikuwa wanahudumiwa na Wizara ya Kazi, Vijana na Michezo. Kama mtakumbuka kutokana na mateso na shida, Walemavu walitaka kumpiga aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Marehemu Sebastian Kinyondo, miaka ya 1990.

Kwa mtizamo wangu tunahitaji utashi wa kisiasa katika hili. Suala la walemavu linapaswa kushughulikiwa na ofisi ya juu: Ofisi ya Rais, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu. Mojawapo kati ya ofisi hizi inapaswa iwe na shughuli ya kuratibu masuala yote ya walemavu toka sehemu mbalimbali.

Busara itumike kuanzisha Wizara itakayoshughulikia masuala ya watu wenye ulemavu na iwe chini ya Rais au Waziri Mkuu. Lakini kuiweka chini ya Wizara ya Afya ni kuendeleza ile dhana kwamba Walemavu ni watu wagonjwa wanaohitaji matibabu! Hii si kweli kwani walemavu wanahitaji fursa (opportunity) katika kutenda kazi zao.

Lakini pamoja na hayo, katika kila Wizara kuanzishwe dawati maalum la kushughulikia masuala ya walemavu (
Disability Desk). Kama imewezekana katika masuala ya jinsia (Gender) kwa nini isiwezekane kwa watu wenye ulemavu? Sidhani kama ni sahihi kuyaacha masuala ya walemavu kwa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kutaleta tija.

Nchi kama Afrika Kusini wamejitahidi katika hili kwa kuweka kurugenzi (
Directorate) ya watu wenye ulemavu chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais.
Nitwangie: 0755 666964
bjhiluka@yahoo.com

No comments:

Post a Comment