Mar 7, 2011

Kwa gharama hizi, maisha bora kwa kila Mtanzania ni ndoto

 Nembo ya Shirika la Ugavi wa Umeme (Tanesco)

Makao Makuu ya Tanesco yaliyopo Ubungo, Dar es Salaam

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MAMLAKA ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) imetangaza kupanda kwa gharama za umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari 2011. Kupanda kwa bei ya umeme hakika kutazidisha ugumu wa maisha ambao upo hasa kwa wananchi walio wengi ambao ni wenye kipato cha chini.

Pamoja na Tanesco kupandisha gharama ya umeme, lakini shirika hilo bado linatakiwa kufanya maboresho zaidi ya mitambo kwa kuwa umeme umekuwa ukikatika mara kwa mara na kuleta madhara makubwa ikiwemo kuunguza vitu majumbani na maofisini.

Hatua ya kupandisha gharama hizi itazidi kuwaongezea umaskini Watanzania kwa sababu hata bei ya awali wengi walikuwa hawaimudu. Pia kupandisha bei bado hakuwezi kuwa suluhisho au kuifanya Tanesco ijiendeshe kwa ufanisi kwani kinachotakiwa ni mbinu za kiutendaji na ubunifu katika kuliendesha shirika. Mbona mapato Tanesco yako mengi, isipokuwa imekosa mbinu na mikakati ya kuzuia wizi wa umeme unaofanywa na watumiaji wengi wa umeme.

Mfano eneo ninaloishi na hata maeneo mengi ninayotembelea, wezi wanaotumia umeme wa wizi bila malipo ni wengi, tena wanashirikiana na wafanyakazi wa Tanesco na wala hakuna jitihada za makusudi kuwazuia vishoka.

Kitu kingine ambacho hakikubaliki ni ukweli kwamba wafanyakazi wa Tanesco, tofauti na watumishi wengine wa mashirika ya umma wao hawalipi ankara za umeme, kwa maana kwamba wanatumia umeme bure.

Lingine kubwa linalodaiwa kupandisha gharama za umeme ni mikataba ya kihayawani ya makampuni yanayoiuzia umeme Tanesco ambayo inasemekana zaidi ya nusu ya mapato yake yote inayalipa makampuni haya ya kinyonyaji ikiwemo Songas.

Kupandisha gharama hizi kunaambatana na tetesi kuwa Tanesco wanatafuta fedha za kufidia deni la Sh. bilioni 185 wanalodaiwa na Dowans, kama ni kweli kwa nini wasitafute njia nyingine badala ya kuwaongezea wananchi bei ya umeme? Kupandisha bei ya umeme wakati hata huduma zenyewe hazijaboreshwa!

Kupanda kwa bei hakika kutapunguza watumiaji wa umeme na kuwarudisha watu katika utumiaji wa vibatari na mishumaa kwa sababu ya kuogopa gharama ya umeme. Aidha kutowaongezea ‘ulaji’ vishoka kwani wengi wataangukia katika kuiba umeme ili maisha ‘yaende’.

Hali hii imefika hapo ilipo kutokana na mfumo wa nchi hii kuegemea zaidi kwenye siasa kuliko kujali utaalamu. Siyo siri kuwa wananchi wa Tanzania kwa sasa wanaishi kwenye kiza kinene baada ya kujitokeza jinai ya kugawiwa umeme wakati huu.

Inawezekanaje nchi yenye vyanzo vyake yenyewe vya umeme, kuwa na mgawo wa umeme ilhali nchi kama Kenya inayotegemea umeme toka nchi jirani ya Uganda haina mgawo?

Uchumi wa Tanzania unaporomoka kwa kasi kubwa kutokana na ukosefu wa nguvu ya umeme wa uhakika pamoja na kuwa madini ya Uranium yanayotengeneza nishati ya nyuklia yanapatikana kwa wingi Tanzania. Madini ambayo kwa nchi kama Iran na Korea yanatumika kwenye uzalishaji nguvu za umeme kwa njia ya nyuklia.

Hebu fikiria ni biashara ngapi zinaathirika kutokana na mgao huu wa umeme. Hata kama ni biashara ya mwananchi wa kawaida ya kuuza barafu, ice cream au juisi bado ina mchango katika ujenzi wa taifa changa kama Tanzania. Kukosekana umeme wa uhakika katika mgao wa siku ni pigo kubwa kwa taifa kwani shughuli nyingi za uzalishaji zinasimama.
Mgao huu wa umeme licha ya kudhoofisha uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja unasababisha uharibifu na uchafuzi wa mazingira. Majenereta yanayofanya kazi mchana kutwa mijini yamekuwa yanachafua mazingira kwa moshi na hata kelele.

Kama alivyowahi kuandika mwandishi mmoja, mgao wa umeme mbali na kusababisha kuparaganyika kwa uchumi pia ni chanzo cha rushwa. Mara nyingi sehemu za wenye pesa na vigogo serikalini huwa haziathiriki na kadhia kama hizi.

Hii ni kwa vile ama wenye nazo wanahonga watendaji wa Tanesco, au wenye madaraka wanapendelewa kwa vile wameshikilia kila kitu katika nchi hii.

Moja ya tatizo ambalo tumekuwa nalo kipindi kirefu sasa, Watanzania wengi tunategemea nishati hii kutoka kwenye vyanzo vya mabwawa ya maji. Miundombinu bado haijaboreshwa, halafu linakuja suala la kuongeza bei ambalo ni kumwongezea mwananchi mzigo mkubwa usiobebeka na hiyo ni hatari kwa taifa, kwani itashusha hata uzalishaji na uchumi wa taifa utashuka.

Kwa nini tusiachane na vyanzo hivi na kuangalia vyanzo mbadala, kwani siku zote ambazo mabwawa hayo hupungua kina cha maji au kukauka, tumekuwa tukishuhudia mgao mkali, jambo ambalo tunaamini sasa umefika wakati wa serikali kutafuta njia mbadala ya kukabiliana na hali hii.

Kingine ni kuangalia upya mikataba hii ambayo inaigharimu Tanesco pesa nyingi na kukimbilia kuwakamua wananchi huku ikijuliakana kwamba kuna watu wachache wanafaidika sana kupitia mikataba ya makampuni haya binafsi.

Ni wakati sasa wa kuweka utaratibu wa makampuni haya kuuza umeme wao moja kwa moja kwa wananchi kwani itasaidia kuongeza ushindani kama ilivyo kwenye makampuni ya simu.

No comments:

Post a Comment