Mar 30, 2011

Kulikoni tuzo za muziki za Kili?

 Mratibu wa Tuzo za Kili Music 2011, kutoka BASATA, Angelo Luhala

Msanii Abbas Kinzasa maaruf kama 20%


BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KOMBINENGA, Man Walter, Man Maji...” kibwagizo hiki kimetokea kuwa maarufu sana miongoni mwa wadau wa muziki wa kizazi kipya na sasa kinatamba kwenye vituo mbalimbali vya redio na televisheni kila unapopigwa wimbo wowote wa msanii Abbas Kinzasa, maaruf kwa jina la 20 percent.

Naomba nikiri kuwa mimi binafsi ni mpenzi mkubwa wa nyimbo za msanii huyu kutokana na ujumbe wake kuigusa jamii moja kwa moja na wala sikushangaa kuona akizoa tuzo tano na kuweka rekodi ya aina yake tangu tuzo zianze kufanyika miaka 12 iliyopita zilipoasisiwa. Sina shaka kuwa rekodi iliyowekwa na msanii huyu haitavunjwa na msanii yeyote katika miaka mingi ijayo. Ama kweli Wabongo sasa wanaelewa asili na vionjo vya muziki wa nyumbani.

Kama ambavyo wadau wengi wa muziki wamebainisha, kwa kweli usiku wa Jumamosi iliyopita ulikuwa ni ‘Usiku mwaka' wa msanii 20 percent (20%), katika tamasha liliooneshwa moja kwa moja na kituo cha televisheni cha ITV, kutokea ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam. Hongera sana 20 percent.

Umahiri wa 20 percent katika tungo zenye kuigusa jamii ulidhihirishwa na mashabiki wengi walioonekana kumshangilia kila jina au wimbo wake ulipokuwa ukitajwa, taswira iliyoonesha kwamba anakubalika vilivyo katika jamii kwa ujumla na alistahili kutwaa tuzo hizo.

Tuzo alizonyakua msanii huyo ni; Msanii Bora wa Kiume, Wimbo Bora wa mwaka, Mwimbaji Bora wa Kiume, Mtunzi Bora wa nyimbo na Wimbo Bora wa Afro Pop.

Katika tamasha la mwaka huu kulikuwa na tuzo 23 zilizotolewa. Binafsi sikuona sababu ya kuwa na tuzo nyingi kiasi chicho kulikopelekea baadhi ya tuzo kukanganya kwa kuonekana zinafanana sana. Sijui waratibu wa tuzo hizo, Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA), na wadhamini wake, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia Bia ya Kilimanjaro Premium Lager waliziweka kwa maslahi ya nani?

Mfano sikuona sababu ya kutenganisha tuzo ya Msanii bora wa kiume na Mwimbaji Bora wa Kiume. Halikadhalika Msanii Bora wa Kike na Mwimbaji Bora wa Kike.

Hata hivyo, kama kawaida, tuzo za mwaka huu hazikukosa kulalamikiwa na wadau kuwa kulikuwa na uchakachuaji wa makusudi ili kuwabeba baadhi ya wasanii wasiostahili ili kukidhi matakwa ya watu fulani wenye nguvu katika kamati inayoratibu tuzo hizo.

Kwa mfano, inawezekanaje msanii 20 percent ang'are katika sehemu tano halafu mtayarishaji wa nyimbo zake, Man Walter ambaye naye alikuwa akiwania nafasi ya Mtayarishaji Bora akose tuzo kwa kushindwa na Lamar? Kwa wadau walio makini huu ni ubababishaji wa wazi.

Halikadhalika chombo kimoja cha habari kilimnukuu mwimbaji gwiji wa mipasho, Hadija Kopa akipinga kukosa tuzo huku akisema kuwa baadhi ya washindi waliandaliwa na wahusika. Chazo hicho cha habari kilimnukuu Kopa kushangazwa kwake katika tuzo ya Mwimbaji Bora wa Kike kuchukuliwa na msanii chipukizi, Linah Sanga na kuwabwaga wakongwe akiwemo Kopa mwenyewe.

Malalamiko hayakuishia hapo, kuna mdau mmoja mfuatiliajia mkubwa wa masuala ya muziki aliniuliza inawezekana vipi Msanii Bora wa Hip hop asiwe na wimbo bora ya Hip hop? Aliniuliza akichukulia kuwa Joh Makini kapata tuzo ya Msanii Bora wa Hip hop lakini ameshindwa kwenye wimbo bora ya Hip hop na JCB, akienda mbali zaidi kwa kusema kuwa JCB ndiye aliyestahili kupewa tuzo ya Msanii bora wa mwaka.

Sikuwa nimelifikiria hilo kwa sababu binafsi nikiri kuwa sizifahamu nyimbo za wasanii hao wawili na wala mimi si mpenzi wa aina ya nyimbo wanazoziimba, hivyo nilijaribu kufanya utafiti mdogo na kuulizia uhusiano wa mambo hayo mawili. Wapo baadhi ya wadau walionieleza ya kwamba kuwa na wimbo bora ya Hip hop hakumaanishi kuwa Msanii Bora wa Hip hop, kwani Msanii Bora wa Hip hop ni mshindi wa moja kwa moja (overall winner) katika Hip hop.

Lakini kuna waliopinga kwa kusema utakuwaje overall winner wa kipengele ambacho hujashinda hata wimbo mmoja? Je, inawezekana kuwa hiki ni kituko cha mwaka? Au ndo kama tulivyojionea kituko kingine cha wimbo wa Mpoki 'Shangazi' kuushinda 'Adela' wa Mrisho Mpoto!

Kwa nini waandaaji wasitafute namna nzuri ya kuzishindanisha nyimbo ili kuondoa malalamiko yanayojitokeza kila mwaka? Mbona tuzo kama Grammy Music Awards zinaendeshwa kwa uwazi na vigezo vyake vinajionesha dhahiri kiasi cha kupelekea kutokuwepo manung'uniko, na hata kama kunatokea lawama basi huwa ni za kawaida sana.

Tuzo za Kili ni mfano wa tuzo maarufu za Grammy ambazo huratibiwa na National Academy of Recording Arts and Science ya Marekani na hutolewa ili kutambua mafanikio bora katika sekta ya muziki. Tofauti na tuzo za Kili, Grammy Awards huwa na Vipengele vichache, hasa wakikazia kwenye Albamu ya Mwaka, Rekodi ya Mwaka, Wimbo wa Mwaka, Msanii bora Anayechipukia na kadhalika.

Jambo jingine lisilopendeza machoni mwa wadau wa muziki ni kusahauliwa kwa muasisi wa tuzo hizo, marehemu James Dandu kana kwamba hakuwahi kuwepo wala kuzianzisha tuzo hizo! Jambo hili linakwenda sambamba na kutoa tuzo (trophy) zisizo na ubora wowote kabisa.

Inasikitisha kwa msanii aliyefanya kazi mwaka mzima akirekodi nyimbo zake kwa gharama kubwa anapokuja kuzawadiwa kipande cha mbao kilichopakwa rangi ya chuma na shilingi laki tano tu! Basata na TBL mnatupeleka wapi?

Washindi wa tuzo za muziki za Kili 201 ni kama ifuatavyo: Wimbo Bora wa Asili (Shangazi – Mpoki Ft. Kassim), Wimbo Bora wa Bendi (Shika Ushikapo – Mapacha Watatu Ft. Mzee Yusuph), Wimbo Bora wa Taarab (My Valentine – Jahazi), Wimbo Bora wa R&B (Nikikupata – Ben Paul), Wimbo Bora wa Hip-Hop (Ukisikia Pah! – JCB Ft. Fid Q, Jay Mo na Chidi Benz), Wimbo Bora wa Afro-Pop (Tamaa Mbaya – 20 percent), Wimbo Bora wa Zouk/Rhumba (Nabembelezwa – Barnaba) na Wimbo Bora wa Reggae (Ujio Mpya – Hard Mad Ft. Enika & BNV).

Tuzo zingine ni Wimbo Bora wa Ragga Dancehall (Action – Cpwaa Ft. Ms. Triniti, Dully Sykes na Ngwear), Wimbo Bora wa Kushirikiana (Ukisikia Pah! – JCB Ft. Fid Q, Jay Mo na Chidi Benz), Wimbo Bora wa Afrika Mashariki (Nitafanya – Kidum Ft. Lady Jay Dee), Video Bora ya Mwaka ya Muziki (Action – Cpwaa Ft. Ms. Triniti, Dully Sykes na Ngwear), Mtunzi Bora wa Nyimbo (20 percent), Mtayarishaji Bora wa Nyimbo (Lamar) na Rapa Bora wa Mwaka kwa Bendi (Khalid Chokoraa).

Nyingine ni pamoja na Msanii Bora wa Hip-Hop (Joh Makini), Msanii Bora Anayechipukia (Linah), Hall of Fame;
Taasisi – (TBC), Binafsi – Said Mabela. Mwimbaji Bora wa Kike (Linah), Mwimbaji Bora wa Kiume (20 percent), Wimbo Bora wa Mwaka (Tamaa Mbaya – 20 percent), Msanii Bora wa Muziki wa Kike (Lady Jay Dee) na Msanii Bora wa Muziki wa Kiume (20 percent).

Tuzo ya mwimbaji bora wa kike ilikwenda kwa Lina Sanga aliyekuwa akichuana na Judith Wambura ‘Lady Jay Dee’, Mwasiti Almasi, Khadija Kopa na Sara Kaisi ‘Shaa’.

No comments:

Post a Comment