Mar 2, 2011

Serikali inawaandaaje vijana na Shirikisho la Afrika Mashariki?

 Wanafunzi wa shule moja ya msingi hapa nchini

Eneo la Afrika Mashariki, kabla Rwanda na Burundi hawajajiunga

Bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam
HIVI karibuni nilisoma habari kwenye magazeti kuwa wafanyabiashara wa nchi tano wanachama wa Jumuia ya Afrika Mashariki, sasa wako huru kuvuka mipaka na kuuza bidhaa zao bila kulipa ushuru wa forodha katika eneo la Afrika Mashariki linalokadiriwa kuwa na zaidi ya watu milioni 120.

Hatua hiyo inalenga katika kuleta ustawi wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo, hasa baada ya kuondolewa vikwazo vilivyokuwa vinasababisha kero katika ama kuzalisha au kuagiza mali ghafi na kusambaza bidhaa katika nchi hizo.

Taarifa zilizotangazwa kwenye vyombo vya habari zilisema kuwa Itifaki ya Umoja wa Forodha, sasa imepewa nguvu ya kisheria na kwamba tayari jumuiya imeanzisha utaratibu wa kutambua vikwazo visivyo vya kiforodha, ili hatimaye, viondolewe.
Shirikisho la Afrika Mashariki linahusisha nchi za Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi na Rwanda na tayari nchi hizo zilishapiga hatua kubwa kuelekea kuwa kitu kimoja, huku mabilioni ya fedha yakiwa yametumika katika mchakato ikiwemo kutafuta maoni kwa wananchi.

Binafsi naipongeza sana hatua hii itakayoleta ufanisi na ustawi kwa vijana wa jumuia hii, lakini bado nina wasiwasi kuhusu nafasi ya vijana wa Tanzania katika kufaidika na soko la Afrika Mashariki, hasa kwa kuwa serikali yetu haioneshi kuwaandaa vijana wake kwa ajili ya kuingia kwenye soko la ushindani.
Kwa mtazamo wangu naona serikali haina nia kabisa ya kumsaidia mwananchi wa kawaida kuingia kwenye ushindani, kwani Tanzania ndio imejaa kila bidhaa bandia (fake), hakuna hata kukagua kama sheria zinafuatwa katika kuagiza.
Tanzania ukilinganisha na nchi nyingine wanachama wa Jumuiya, imejaaliwa kuwa na ardhi kubwa inayofaa kwa kilimo na kuweza kuwa mzalishaji na mlishaji wa Jumuiya.
Serikali ingeweza kuitumia hii kama fursa kwa kumuandaa kijana wa Tanzania kufaidika. Kiukweli Tanzania tuna mambo mengi ambayo tumewazidi wenzetu lakini mfumo mbovu wa elimu na jinsi kijana wa Tanzania asivyoandaliwa limekuwa ni tatizo kubwa.
Huwa sioni sababu ya kupinga kuingia kwenye shirikisho wala kutafuta muda mwingi zaidi wa kujiandaa, bali mbinu kabambe zinahitajika kwa nchi hii katika kukabiliana na changamoto za soko la Afrika Mashariki.

Ili kuweza kwenda sambamba na dira ya Jumuiya ya Afrika Mashariki katika kukuza kipato, kuinua hali ya maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki, kukuza uchumi, na kujenga ushindani wa kanda katika ngazi ya kimataifa, tunapaswa kuwa makini katika kuangalia upya mfumo wetu wa elimu.
Kama alivyowahi kunukuliwa Maalim Seif Sharif Hamad (Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar) siku za nyuma kuwa hali ilivyo sasa katika nchi zinazounda Jumuiya ni kuwepo uwiano mdogo baina ya nchi hizo. Na moja katika vigezo muhimu vya kuunda shirikisho la kisiasa, ni kuwa nchi husika ziwe na uwiano katika mambo kadhaa kama ifuatavyo:
-Sarafu za nchi zetu haziwiani kithamani kwa kuzilinganisha na thamani za fedha za kigeni.
-Kiswahili kinachotajwa kuwa lugha rasmi kinakwamishwa kwa kuwa Kenya na Uganda wameweka umuhimu na uzito katika matumizi ya Kiingereza.
-Kenya na Uganda tayari raia wao wana vitambulisho vya uraia wakati Tanzania raia wake bado hawana vitambulisho.
-Maendeleo ya kiuchumi, hasa katika sekta za uchumi na biashara katika nchi hizi pia ni tofauti.
-Viwango vya elimu ya wananchi wa nchi hizi havilingani.

Unapozungumzia elimu ya msingi hapa kwetu unalenga elimu inayotolewa kuanzia darasa la kwanza hadi darasa la saba. Kwa ujumla elimu hii inatolewa chini ya mazingira magumu sana hasa upande wa vijijini ambapo kuna upungufu wa walimu, madarasa, madawati na vifaa vya elimu.
Mfumo mbovu wa elimu yetu umewafanya vijana wengi kuwa na hofu ya shirikisho hilo ambalo wamekuwa wakilikosoa kwa nguvu zao zote. Wamekuwa na hofu juu ya ushindani mkubwa wa ajira na bidhaa wanazozalisha.

Hofu hii ya vijana wengi imetokana na mfumo wa elimu yetu, mfumo unaowafanya wengi kusubiri kuletewa taarifa na fursa zilizopo katika Jumuiya hiyo badala ya wao kutafuta taarifa na fursa zaidi walizo nazo.
Mbaya zaidi hata waajiri wengi wanaonekana kupendelea mtu anayeongea Kingereza hata kama uwezo wake kitaaluma ni mdogo ama kazi anayokenda kuifanya haihitaji utaalamu wa lugha hiyo.

Kama nilivyowahi kuandika
huko nyuma katika gazeti hili kuwa wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi na hata sekondari bila kupata fursa yoyote ya kwenda chuo kupata mafunzo huwa ni mzigo kwa taifa, wengi wanaishia mitaani wakiwa wanatembeza bidhaa chache mikononi kuanzia alfajiri hadi jioni huku wakiambulia kipato duni kisicho na tija katika maisha yao ya kila siku na kuishia kulala mzungu wa nne kwenye makazi duni pembezoni mwa miji ya Tanzania.

Ni jambo ambalo kwa hakika halina upinzani kuwa mfumo wa elimu unahitaji mabadiliko makubwa ili kila mwanafunzi anayehitimu asiwe tegemezi na badala yake awe mbunifu kwa maendeleo ya Taifa. Suala hili linapaswa kusimamiwa vyema na serikali.

Kwa kweli hili ni janga la taifa, kubwa kuliko El Nino, Tsunami au hata tetemeko la ardhi na lina madhara makubwa kwa taifa kuliko hata vita.

Alamsiki

No comments:

Post a Comment