Feb 23, 2011

Saif al-Islam: Mtoto wa nyoka aliyeandaliwa kuwa mrithi wa urais

 Mtoto wa Gaddafi, Saif al-Islamu

Tripoli
LIBYA

UTAWALA wa Kanali Muammar Gaddafi uko katika hali tete, kufuatia maandamano makubwa katika mji mkuu wa Libya yenye lengo la kumshinikiza kuachia madaraka. Kadhalika kujiengua kwa baadhi ya mabalozi kunazidisha shinikizo kwa Gaddafi ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo kwa mkono wa chuma. 
 
Maofisa wa usalama walifyatua risasi na mabomu ya machozi kwa waandamanaji katika mitaa ya Tripoli Jumapili iliyopita, na hata mji wa pili kwa ukubwa, Benghazi, sasa unaonekana uko chini ya udhibiti wa waandamanaji hao.

Hofu ya wimbi hilo imemlazimisha mwana wa Gaddafi, Saif al-Islamu kujitokeza kwa mara ya kwanza tangu harakati hiyo ianze na kutoa ahadi ya kutayarisha katiba mpya itakayojali misingi ya demokrasia. Hatua hiyo pia haikufua dafu kwani imekuja ikiwa imechelewa. 
 
Ili kujaribu kutuliza harakati ya wananchi, Kiongozi wa Libya ametumia hata mbinu ya kuwaajiri mamluki wa Kiafrika ambao wamekuwa wakishiriki katika kukandamiza harakati hiyo. Jinai hiyo imezidisha hasira za wananchi na kuchochea zaidi maandamano. 
 
Kwa kuzingatia hayo yote, wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa jinai na mauaji ya mamia ya watu yaliyofanywa na jeshi la Kanali Gaddafi katika siku chache zilizopita, zimegonga kengele ya kuanza kuporomoka kwa utawala ulioongoza Libya kibabe kwa kipindi cha miaka 42. 
 
Mtoto huyo wa Gaddafi, ameonya kuwa vita vya wenyewe kwa wenyewe huenda vikazuka kama maandamano hayo hayatasitishwa. Katika hotuba ndefu kupitia televisheni, motto huyo wa Gaddafi ametoa mapendekezo ya mabadiliko ya kisiasa, lakini pia kuahidi kuwa utawala huo “utapigana mpaka mwisho” dhidi ya “wachochezi”.

Amesema makundi ya upinzania na wageni wanajaribu kuigawa Libya kuwa katika majimbo madogo madogo, na kwamba iwapo watafanikiwa amesema uwekezaji wa nje utasitishwa na viwango vya maisha vitashuka kwa kasi.

Saif Gaddafi pia amevikosoa vyombo vya habari vya nje kwa kile alichokiita kukisia kiwango cha vurugu zinazoendelea nchini Libya.

Hata hivyo, amekiri kuwa miji ya Mashariki ya Benghazi na al-Badya imechukuliwa na wapinzani na pia amekiri kwamba baadhi ya kambi za jeshi la nchi hiyo na vifaru vinadhibitiwa na wananchi. 
 
Waziri wa sheria, Mustapha Abdul Jalil, amekuwa afisa wa hivi karibuni kujiuzulu. Amesema alikuwa akiachia madaraka yake kwa sababu ya “matumizi makubwa ya nguvu”, amekaririwa na gazeti binafsi la Quryna, siku ya Jumatatu akisema.

Maandamano na machafuko makubwa yanayoendelea nchini Libya na kuongezeka idadi ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi vimezidisha wasiwasi mkubwa na kuteteresha nguzo za utawala wa kiongozi wa nchi hiyo, Kanali Muammar Gaddafi. Vyombo vya habari vimeripoti kuwa askari wa usalama waaminifu kwa utawala wa Gaddafi wanatekeleza mauaji dhidi ya wananchi kama wendawazimu katika mitaa ya miji mbalimbali ya nchi hiyo. 
 
Hospitali za Libya zimewekwa katika hali ya tahadhari na inaripotiwa kuwa idadi ya watu waliouawa hadi sasa inakaribia mia tano. Pamoja na hayo maandamano na harakati za wananchi za kutaka kung'oa madarakani utawala wa miaka 42 wa Kanali Gaddafi yanazidi kupamba moto. 
 
Baadhi ya ripoti zinasema kuwa familia ya kiongozi huyo wa Libya imekimbilia nje ya nchi. Kumekuwepo habari za kutatanisha pia kuhusu kukimbia nchi kwa kiiongozi huyo wa Libya, ingawa tetesi hizo zimekanushwa na Gaddafi mwenyewe pale alipojitokeza hadharani kwenye televisheni ya Taifa. Ni wazi kwamba harakati ya sasa ya wananchi wa Libya imesababisha mtetemeko mkubwa katika nguzo za utawala wa kipolisi na kidikteta wa karibu nusu karne wa Kanali Muammar Gaddafi. 
 
Hali ya machafuko imeenea nchini kote na wananchi hawaridhiki na chochote isipokuwa kuondolewa madarakani kwa utawala uliowadunisha na kuwaendesha kipolisi kwa kipindi cha zaidi ya miaka 40.

Jeshi la Libya ambalo ni moja ya nguzo kuu za utawala wa miongo kadhaa wa Gaddafi limegawanyika na inasemekana kuwa baadhi ya kambi za jeshi la nchi hiyo zimejiunga na harakati za mageuzi za wananchi zikilalamikia mauaji na ukandamizaji wa wiki moja sasa unaotekelezwa na vikosi vya usalama. Baadhi ya wanadiplomasia wa Libya katika nchi za kigeni, akiwemo mwakilishi wa nchi hiyo katika Jumuiya ya Nchi za Kiarabu pia wamejiuzulu kulalamikia mauaji yanayotekelezwa na serikali ya Tripoli dhidi ya wananchi wanaoandamana mitaani. 
 
Jambo lisilokuwa na shaka ni kuwa hali ya Libya imeingia katika kipindi nyeti mno na viongozi wa nchi hiyo wanaelewa vyema ukweli huo. Ni kwa sababu hiyo ndiyo maana Kanali Muammar Gaddafi akakusanya majeshi yake katika mji mkuu, Tripoli kutokana na hofu ya dikteta huyo ya kukumbwa na wimbi la hasira za wananchi. Hata hivyo, wimbi la mageuzi sasa limeingia Tripoli na kuenea kwa kasi kama moto unavyochoma nyasi katika majira ya kiangazi.

Historia ya mtoto wa Gaddafi
Saif al-Islam Muammar al-Gaddafi amezaliwa tarehe 25 Juni 1972. Ni mtoto wa pili wa Muammar Gaddafi, kutokana na mke wake wa pili, Safia Farkash.

Elimu na kazi
Mwaka 1994, Saif al-Islam alifuzu shahada ya BSc katika Sayansi ya Uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha Al Fateh cha Tripoli, alipata shahada ya Uzamili (MBA) kutoka Chuo Kikuu cha IMADEC cha Vienna mwaka 2000 na shahada ya Uzamivu (PhD) kutoka Shule ya Uchumi ya London mwaka 2008. Pia ni mtaalam wa majengo (architect) mwenye kumiliki kampuni yake ya uhandisi iliyopo jijini Tripoli inayoitwa “National Engineering Service and Supplies Company”. 
 
Saif pia ndiye Rais wa Chama cha Taifa la Libya cha Udhibiti wa Madawa ya Kulevya (DNAG). Mwaka 1997, alianzisha rasmi taasisi ya hisani, Gaddafi International Foundation for Charity Association, ambayo inahusisha uingiliaji kati mambo ya utekaji yanayohusiana na wanamgambo wa Kiislamu na maambukizi ya VVU nchini Libya.

Saif pia hufanya kazi za kimahusiano ya umma na majukumu ya kidiplomasia kwa niaba ya baba yake. Na amekuwa akitajwa kama mrithi wa urais, ingawa yeye amekanusha hili. Agosti 20, 2008, Saif alisema kwamba hakutaka tena kuhusishwa katika masuala ya serikali ya baba yake. Alibainisha kwamba hapo awali alikuwa “akiingilia kutokana na kukosekana kwa taasisi za kufanya hivyo”, lakini alisema ya kwamba hakuwa tena na sababu ya kufanya hivyo. 
 
Alipuuza maoni kwamba uamuzi huo ulitokana na kutokubaliana na baba yake, akifafanua kwamba yeye na baba yake walikuwa na maelewano mema. Alitoa wito kwa mageuzi ya kisiasa ndani ya mazingira ya mfumo wa Jamahiriya na kukataa wazo la kwamba angeweza kumrithi baba yake, akisema kuwa “Libya si shamba ya kurithi”. 
 
Kulingana na mwandishi Landon Thomas wa New York Times, Saif imeibuka kama rafiki wa nchi za Magharibi katika uso wa Libya na nembo ya matumaini yake kwa ajili ya mageuzi ya kweli na uwazi.

Diplomasia ya kimataifa
Tarehe 10 Desemba, 2004, muda mfupi kabla ya safari na Waziri Mkuu wa Canada, Paul Martin kuelekea Tripoli, Saif aliomba kufanya mahojiano na jalida la The Globe and Mail, kuiomba serikali ya Canada kuomba msamaha rasmi, kwa kujiunga katika kuongeza vikwazo dhidi ya Libya vinavyoongozwa na serikali ya Marekani baada ya mabomu ya Lockerbie, na kwa kummnyima visa ya kwenda kusoma nchini Canada mwaka 1997. 
 
Ombi lake lilionekana la kushangaza sana nchini Canada na serikali ya Canada ilitangaza kwamba hakuna msamaha wowote utakaoombwa. 
 
Saif ilianzisha pendekezo la kudumu la kutatua mgogoro wa Israel-Palestina kwa njia ya kidunia, kishirikisho, ufumbuzi wa Jamhuri ya nchi moja. Maoni ya kwanza kabisa kuhusu tafiti zilizozofanyika kutatua mzozo kati ya nchi mbili za Pakistan na India juu ya udhibiti wa Kashmir, uliofanywa na Chuo cha Mfalme, London, na Shirika la Ipsos-Mori, ilikuwa pia ni wazo la Saif, akiibuka kutoka nje ya majadiliano akiwa na mwanataaluma wa Uingereza, Robert Bradnock, mwandishi wa ripoti ya utafiti ya 2010, Chatham House.

Akihojiwa na gazeti la Kifaransa la 'Le Figaro', Desemba 7, 2007, Saif alisema kuwa Walibya saba waliotiwa hatiani kwa ulipuaji ndege za Pan Am 103 na UTA 772 “hawana hatia”.

Maandamano ya 2011
Tarehe 20 Februari 2011, saa 12:00 jioni kwa saa za Libya, Saif alitoa hotuba ya papo kwa papo kupitia Televisheni ya serikali ya Libya. Katika hotuba hiyo, alielekeza lawama ya kukosekana kwa utulivu nchini Libya kwa makundi ya kikabila na Waislam kutekeleza ajenda zao wenyewe, walevi na wabwia unga. 
 
Aliahidi mageuzi, na kusema mbadala wa haya itakuwa ni vita vya wenyewe kwa wenyewe na kusababisha kutokufanyika biashara, na kwamba hakutakuwa na pesa ya mafuta, na nchi kuchukuliwa na wageni. Alifunga kwa kusema, “Hatutakubali Al Jazeera, Al Arabiya na BBC kutuhadaa.” Wachambuzi wengi wameonesha kuhitalifiana na tathmini yake, ikiwa ni pamoja na Oliver Miles, aliyekuwa Balozi wa Uingereza nchini Libya.

Maisha ya binafsi
Mwaka 2006, Saif al-Islam aliingia katika mahusiano ya kimapenzi na mwigizaji wa Israel, Orly Weinerman. Mwaka 2009, aliandaa sherehe ya miaka 37 ya kuzaliwa kwake mjini Montenegro. Mabilionea Oleg Deripaska, Peter Munk na Prince Albert wa Monaco walihudhuria tukio hilo. 
 
Baadhi ya waalikwa walikwenda huko kwa ndege binafsi na kukaa katika klabu kubwa mbili za ufukweni wakipaki ndege zao jirani ya ufukwe “wa kifahari”, ambapo tukio lilikuwa likifanyika. Kabla ya hapo aliwahi kufanya sherehe ya aina hiyo katika miji ya St. Tropez na Monaco.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka, kwa msaada wa Mashirika mbalimbali ya Habari ya Kimataifa.

No comments:

Post a Comment