Feb 17, 2011

Mfumo wa elimu na mporomoko wa maadili ya taifa

 Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, 
Dk. Shukuru Kawambwa

Nembo ya Baraza la Mitihani la Taifa (Necta)

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

WIKI iliyopita matokeo ya mtihani kwa wanafunzi waliomaliza sekondari yalitoka huku baadhi ya wanafunzi kushangilia na wengine kuhuzunika. Niliandika kuhusu mfumo wa elimu yetu wiki mbili zilizopita, leo najaribu kuutazama tena mfumo huu katika 'Angle' nyingine.

Matokeo hayo ya mtihani yameleta huzuni kwa walio wengi (hasa wa sekondari za Kata) ambao hawakupata matokeo mazuri.

Matokeo hayo yametumika kuwakejeli watoto wa mafukara na wazazi wao kwa kuwa wamewekwa kando na mfumo wa kijamii – kiuchumi unaowapendelea, kuwajenga na kuwaendeleza wachache huku ukiwapuuza, kuwachuja na kuwatupa walio wengi.

Wakati wanaharakati na wasomi wakijadili kuhusu Katiba mpya, ni wakati muafaka pia kujaribu kuangalia na kushauri namna nzuri ya kurudisha maadili ya taifa yaliyomong'onyoka.

Ukitafakari kwa kina kuhusu kupotea kwa maadili ya taifa utagundua kuwa mfumo wetu wa elimu umechangia kwa asilimia kubwa.

Katika machapisho mbalimbali inaelezwa kuwa elimu hapa nchini na Afrika ilianza kama chombo cha kuandaa vijana wake kuchukua nafasi yao katika jamii ya Afrika. Uzoefu wa elimu ya Kiafrika ilianzishwa hasa kuandaa vijana kwa jamii katika jumuiya ya Kiafrika na siyo kwa maisha nje ya Afrika.

Elimu katika jamii ya awali ilijumuisha mambo kama sanaa, sherehe, michezo, matamasha, dansi, kuimba, na kuchora. Wavulana na wasichana walifunzwa wakiwa wametenganishwa kusaidia kuandaa kila kikundi kwa majukumu yao kama watu wazima.

Wakati ukoloni
na ubeberu wa Ulaya ulipoingia ulianza kubadili mfumo wa elimu wa Kiafrika. Shule ikawa haihusu tena mila, shule sasa ikamaanisha kupata elimu ambayo ingeweza kuwaruhusu Waafrika kushindana na nchi kama vile Marekani na zile zilizoko Ulaya. Afrika ikaanza kuzalisha wanafunzi wao wenyewe walioelimishwa kama vile wa nchi zingine.

Hata hivyo, viwango vya ushiriki katika nchi nyingi za Afrika ni vya chini. Mara nyingi shule zetu hukosa vifaa vingi vya msingi, na vyuo vikuu vya Afrika vinakabiliwa na msongamano na wakufunzi wanaovutiwa kwenda nchi za Magharibi kwa malipo na mazingira bora zaidi.

Lakini baadhi ya nchi za Kiafrika wamejitahidi kuboresha mifumo ya elimu yao iendane na mazingira yao, ndiyo maana zimepiga hatua kubwa katika maendeleo.

Hapa Tanzania, ukiangalia matatizo mengi yanayochangia kuporomoka kwa uchumi wa Tanzania utagundua kuwa yamejikita zaidi katika mfumo wetu wa elimu.

Na ukichunguza kwa makini zaidi utaona kuwa matatizo yetu yapo kwenye kila ngazi ya jamii: kuanzia Taifa hadi kitongoji na ufisadi upo kila idara ya jamii si serikalini tu bali hadi kwenye vyama binafsi.

Kuna changamoto nyingi zinazoukabili mfumo wetu wa elimu, ikiwemo kuvurugika kwa mfumo wa elimu na mafunzo ya ufundi ambao hivi sasa unasimamiwa na wizara mbili tofauti.

Elimu ya ufundi inasimamiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, huku elimu ya sayansi ikisimamiwa na Wizara ya Sayansi, Mawasiliano na Teknolojia. Pia kuwapo kwa taasisi nyingi zinazosimamia na kudhibiti kitu kimoja kunachangia kuwepo migogoro ya kiutendaji baina ya taasisi husika na hivyo kupelekea kudorora kwa elimu.

Kwa mfano; Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), limeachwa kufanya tathmini ya elimu ya msingi, sekondari na elimu ya mafunzo ya ualimu huku Mamlaka ya Elimu ya Ufundi Stadi (Veta) ikisimamia usajili na udhibiti wa taasisi zote za mafunzo ya ufundi stadi nchini.

Pia kuna taasisi zingine zinasimamia elimu ya juu: Baraza la Taifa la Elimu ya Ufundi (Nacte), linadhibiti taasisi za elimu ya mafunzo ya ufundi na Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), inadhibiti vyuo vikuu vyote nchini.

Hivi sasa elimu ya msingi si ya msingi tena kama ilivyokuwa miaka michache baada ya uhuru kwani msingi unapaswa uwe imara siku zote. Sioni juhudi zinazofanywa kuifanya elimu ya msingi kuwa msingi kama ilivyo kwa nchi jirani ya Kenya ambao wamefaulu sana katika kuimarisha elimu ya msingi.

Nakubaliana na mchambuzi aliyewahi kuandika kuwa miaka inavyozidi kwenda ndivyo ubora wa elimu Tanzania unavyozidi kushuka; ukichunguza kati ya wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi kati ya miaka ya 1980, miaka ya 1990 na miaka ya 2000 utagundua kuwa wote hao wana uelewa tofauti tena mkubwa tu.

Pia inashangaza kwa nini hakuna masomo maalum kwa maeneo maalum yanayoendana na mazingira?

Kuhusu matokeo ya hivi karibuni, imenisikitisha kusikia shule za Kata zimekuwa za mwisho kwenye matokeo ya mtihani, hasa kwa sababu ya mfumo mbovu uliopo wa kutotambua uwezo tofauti, mazingira tofauti na changamoto tofauti na matatizo tofauti waliyonayo wanafunzi wa shule moja na nyingine.

Serikali ilipaswa kuwa na watu wabunifu wa kubuni mitaala inayoendana na mahitaji ya ulimwengu wa sasa badala ya kuifanya elimu yetu iendeshwe kisiasa. Kufundisha kiholela bila malengo ya ukuaji wa nchi hakutusaidii kabisa. Malengo haya lazima yaendane na uwekezaji katika elimu.
Elimu yetu kuanzia shule ya msingi hadi Chuo Kikuu mfumo wake hauendani na matakwa husika, umekuwa ukiendeshwa kwa mtindo wa chukua notisi nenda kajisomee (kakalili) harafu yote uliyojifunza mhula mzima njoo uyajibu ndani ya saa mbili na hizo saa mbili ndiyo mustakabali wako mzima!

Jambo jingine katika mfumo wetu wa elimu; mwanafunzi wa Kitanzania anakabiliana na kikwazo kikubwa cha lugha katika mafunzo yake. Kwenye mtihani, akiulizwa swali kwa Kiingereza itambidi alitafsiri kwanza kwa Kiswahili (wakati mwingine hulitafsiri tena kwa lugha ya kwao), kabla ya kutoa jibu ambalo bila shaka itabidi lifuate mtiririko huohuo kwa kuugeuza.
Kwa nini tusipunguze lugha moja kati ya Kiswahili na Kiingereza ili kuleta ufanisi zaidi?

Binafsi sina ugomvi wa lugha ipi itumike, lakini serikali inapaswa kuwa na sera madhubuti ya lugha, wakati umefika tukubaliane kutumia lugha moja ya kufundishia. Hii haina maana kuwa tukitumia moja tutakuwa hatutumii nyingine, kwani kwa mtazamo wangu Kiingereza bado ni muhimu sana kwenye mawasiliano ya kimataifa.

Hii sera ya sasa ya wanafunzi kuanza na Kiswahili wakiwa shule ya msingi, na kufundishwa kwa Kiingereza wanapoanza sekondari ni kuwadumaza kifikra. Matokeo yake wanafunzi wa Kitanzania wanajikuta wakiwa hawajui Kiswahili wala Kiingereza.

Staili hii ya ufundishaji imekuwa ikizima vipaji vingi na kuvilazimisha kukalili na mwisho kuviandaa vipaji hivyo kuwa mafisadi, ufisadi unaoanzia kwenye wizi wa mitihani.

Kipindi cha nyuma mtu akiteuliwa kwenye nafasi yoyote ya uongozi ilionekana kama kutwishwa mzigo kwani ile dhana ya cheo ni dhamana ilikuwepo, lakini siku hizi mtu akiteuliwa kuwa kiongozi utasikia wakisema kuwa 'ameula' ikimaanisha amepata nafasi ya kufanya biashara au shughuli ya kuingiza pesa chapchap.

Hii imepelekea watu kutoheshimu tena amri za Serikali: maeneo ya wazi yanavamiwa ovyo, ongezeko la wafanyakazi hewa Serikalini, wanasiasa kutoheshimu taaluma, sheria za nchi kutoheshimiwa, wizi mkubwa mkubwa wa mali ya umma, uingizaji na uuzwaji wa bidhaa feki bila woga, kuporomoka kwa elimu, kukwepa kodi, kuongezeka kwa uhalifu na kadhalika.

Tatizo la tofauti ya kipato kuwa kubwa miongoni mwa makundi katika jamii pia linaidumaza jamii yetu. Madhara ya ongezeko hilo yanapelekea hatari ya matajiri wachache kuyaendesha maisha ya maskini walio wengi kwa njia ambayo itazidi kuwaongezea utajiri huku ikiwadidimiza zaidi maskini.

Kama alivyowahi kunukuliwa kiongozi mmoja wa serikali yetu kuwa matajiri hao wachache ndio wanaoendesha vyama vya siasa, Serikali, Mahakama, Bunge, Makanisa, Misikiti na kadhalika. Hii ni hatari sana.

Tukiwa tunaelekea miaka 50 tangu nchi yetu ipate uhuru, ndoto za wananchi wengi kuwa yangetokea marekebisho muhimu ya kisera yatakayoleta uwiano mzuri katika kupata elimu na hatimaye kugawana madaraka kwa uwiano muafaka zimetoweka kabisa.

Alamsiki 

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment