Feb 17, 2011

UHURU KENYATTA: Mtuhumiwa wa machafuko nchini Kenya mwenye nia ya kugombea urais mwakani.

Uhuru Kenyatta

Nairobi
KENYA
MACHAFUKO baada ya Uchaguzi nchini Kenya bado yanaacha hali ya sintofahamu miongoni mwa vigogo wa nchi hiyo waliotajwa na kiongozi wa mashtaka katika mahakama ya ICC, Luis Moreno Ocampo. Vigogo wawili kati ya wanasiasa waliotajwa kuhusika na machafuko hayo; Naibu Waziri Mkuu, Uhuru Kenyatta na mbunge wa Eldoret Magharibi William Ruto tayari wameonekana kuwa na nia ya kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2012.

Iwapo majaji wa mahakama ya kimataifa wataidhinisha mashtaka dhidi yao, basi huenda mipango yao ikawa imesambaratika. Wiki iliyopita nilielezea kuhusu William Ruto na madai yake kuwa tuhuma dhidi yake zinasababishwa na wabaya wake kisiasa.

Ghasia zilizuka mara tu baada ya kutangazwa Mwai Kibaki kuwa mshindi wa uchaguzi, zilisababisha mapigano makubwa kati ya makabila makubwa nchini humo ya Wakalenjin, Wakikuyu na Wajaluo.

Mapigano hayo yalipeleka mauaji ya watu takribani 1500 na wengine zaidi ya nusu milioni kuachwa bila makazi.

Raila Odinga aliyekuwa mpinzani wa Kibaki alipinga matokeo hayo akisema kuwa serikali ilifanya udanganyifu mkubwa kwa maslahi ya Kibaki.

Hatimaye nchi hiyo ilirejea katika utulivu kufuatia upatanishi wa kimataifa uliopelekea kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa. 

Japo Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga hawakutajwa, orodha iliyotolewa na Ocampo inawagusa kwa karibu viongozi hao wakuu. Uhuru Kenyatta ambaye pia ni waziri wa fedha ni mtu wa karibu wa Rais Kibaki ambaye baadhi ya wakazi wa mkoa wa kati anakotoka Kibaki, wamekuwa wakimwona kama ndiye mrithi wa wadhifa wa urais.

Hivi karibuni taarifa za siri za ubalozi wa Marekani zilizotolewa na tovuti ya wikileaks zilimnukuu balozi wa Kenya, Michael Ranneberger akiwataja Rais Mwai Kibaki na Waziri Mkuu Raila Odinga kama baadhi ya viongozi wanaopinga mabadiliko nchini Kenya na jamiii ya kimataifa sasa itakuwa ikitazama kwa makini jinsi viongozi hawa watakavyojiendesha baada ya watu wao wa karibu kutajwa na Ocampo. 
 
Ocampo, Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ICC alitangaza majina ya watuhumiwa sita wa machafuko yaliyozuka nchini Kenya mara tu baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi mwishoni mwa mwaka 2007.

Katika mkataba wa amani uliofuatiwa, ilikubaliwa wale waliopanga au kufadhili machafuko hayo watakabiliwa na mkono wa sheria nchini Kenya au katika mahakama ya ICC mjini Hague.

Baada ya Kenya kushindwa kubuni mahakama maalum ya kuwahukumu washukiwa hao mahakama ya ICC ilichukua jukumu hilo.

Ocampo analenga kesi mbili katika machafuko hayo ya baada ya uchaguzi.
Washukiwa sita waliotajwa kila mmoja atapewa ilani ya kumtaka afike mbele ya mahakama hiyo, lakini iwapo watakataa au kuvuruga uchunguzi dhidi yao, Ocampo ataomba kutolewa kwa hati ya kukamatwa kwao.

Wengi wa Wakenya wanahisi mashtaka haya ni muhimu ili kukomesha kasumba ya kutoheshimu sheria.

Kenya imekumbwa na msururu wa uchaguzi uliokumbwa na ghasia, lakini uchaguzi wa mwaka 2007 uliokumbwa na utata, nusura ulitumbukize taifa hilo katika vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Baada ya mgawanyiko wa kikabila, jamii ziligeukiana kwa kupigana huku baadhi ya watu wakitiwa hamasa au hata kulipwa pesa na wanasiasa walafi kutekeleza mauaji.

Maafisa wa polisi walitumia nguvu kupita kiasi na kuua watu holela. Silaha ziliwekwa chini wakati aliyekuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Kofi Annan, alipopatanisha pande mbili hasimu kati ya Kibaki na Odinga.

Kama sehemu ya mkataba huo wa amani, walikubaliana kuhakikisha wale waliohusika katika machafuko hayo, wanashtakiwa nchini Kenya au mjini Hague. Wanasiasa walihujumu juhudi zote za kubuniwa kwa mahakama maalum nchini Kenya na hivyo Mahakama ya ICC ikaingilia kati.

Lakini pia inasemwa kuwa mashahidi kadhaa walitishwa, na ICC imewaondoa baadhi ya mashahidi hao nchini humo.

Hata hivyo wabunge wa Kenya wamepiga kura ya kutaka kujitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya uhalifu ya The Hague (ICC), nchini Uholanzi.
Wawakilishi hao wa wananchi wa Kenya, wamefikia hatua hiyo, wiki moja tu baada ya Ocampo kutaja majina hayo sita ya watu anaowatuhumu kuhusika na ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya.

Kama ilivyo kwa William Ruto, Uhuru Kenyatta naye amekanusha vikali kuhusika na ghasia hizo na kusema kuwa yuko tayari kushirikiana na mahakama ya Hague kwa lengo la kusafisha jina lake kutokana na tuhuma hizo. 

Baada ya majina hayo kutajwa, rais Kibaki alitangaza kuwa serikali yake itaendesha uchunguzi kuhusu suala hilo, hatua ambayo wapinzani wake wameiona kuwa ni sawa na jaribio la kuzuia watuhumiwa kupelekwa The Hague.

Kibaki amesema serikali yake itaimarisha mahakama zake ili ikiwezekana watu hao wasomewe mashtaka na kuhukumiwa katika mahakama zao na si ICC.
Wapinzani wake wanasema lengo la Kibaki ni kuzuia uwezekano wa viongozi wengine kutajwa zaidi katika mahakama ya ICC.

Hata kama kufikishwa watuhumiwa wa ghasia hizo mbele ya mahakama ya The Hague ni jambo ambalo lilibainishwa wazi katika mapatano ya kubuniwa serikali ya umoja wa kitaifa lakini mwendo wa kinyonga wa kushughulikiwa jambo hilo na serikali ni jambo ambalo liliwakatisha tamaa Wakenya na hivyo kutoa udharura wa mahakama ya Hague kuingilia kati. 
 
Uzembe wa serikali katika kushughulikia watuhumiwa wa mauji hayo uliwafanya Wakenya wengi kuamini kuwa viongozi wa kisiasa wa nchi hiyo walikuwa wakijishughulisha zaidi na masuala yao ya kibinafsi yakiwemo kujitafutia nafasi bora serikalini na kuimarisha kampeni za uchaguzi mkuu wa 2012 badala ya kushughulikia maslahi ya kitaifa.

Ni nani huyu Uhuru Kenyatta?
Uhuru Muigai Kenyatta amezaliwa tarehe 26 Oktoba, 1961. Ni mtoto wa Jomo Kenyatta aliyekuwa rais wa Kenya na mke wake Ngina Muhoho maaruf kama Mama Ngina.

Kuingia katika siasa
Baada ya kumaliza masomo alishughulika na biashara za familia alizorithi kutoka kwa baba yake mzee Jomo Kenyatta. Mwaka 1997 aliingia kwa mara ya kwanza katika siasa lakini alishindwa katika uchaguzi wa bunge.
Mwaka 1999, rais Daniel Arap Moi alimpa cheo cha mwenyekiti wa bodi ya utalii. Moi aliendelea kumpandisha ngazi kwa kumpa nafasi ya mbunge wa kitaifa na waziri msaidizi. Mwaka 2002 akawa makamu wa mwenyekiti wa Kanu.

Mgombea wa urais 2002
Tangu Julai 2002 ilionekana wazi kwamba Moi alimtaka Uhuru awe mgombea urais kupitia Kanu. Mkutano mkuu wa Kanu wa mwezi Oktoba 2002 uliitikia mapenzi ya Moi ukamtangaza Uhuru kama mgombea urais.

Kitendo hiki kiliwasikitisha wanasiasa wengi wasio Wakikuyu. Waliondoka Kanu na kuunda ushirikiano wa upinzani wa Narc. Uhuru ulishindwa kwenye uchaguzi wa 2002 kwa kupata asilimia 31 ya kura.

Katika bunge jipya alikuwa kiongozi wa upinzani lakini pia alikabiliwa na upinzani ndani ya chama chake hasa kutoka kwa Nicholas Biwott pamoja na wanasiasa wa Bonde la Ufa. Kwenye mkutano wa Kanu Januari 2005, Uhuru alithibitishwa kwa kura nyingi kitendo kilichopelekea Biwott aunde chama cha New Kanu.

Katika kura maalum ya wananchi kuhusu katiba, Uhuru alishirikiana na viongozi wa LDP kuunda kambi ya chungwa (Orange Democratic Movement “ODM”). Mpango wake wa kushirikiana na ODM ulipingwa vikali ndani ya Kanu kwa sababu wanachama pamoja rais mstaafu, Moi waliogopa kupotea kwa chama chao ambacho ni cha kwanza katika historia ya Kenya.

Novemba 2006, Biwott alirudia jaribio la kumpindua Uhuru kwa kuita mkutano wa Kanu mjini Mombasa bila idhini ya mwenyekiti wala kamati ya chama. Alichaguliwa kuwa mweyekiti mpya. 
 
Kwa msaada wa serikali, Biwott alifaulu kuandikisha kamati yake kama uongozi rasmi hivyo kumwondoa Uhuru katika nafasi ya kiongozi wa upinzani bungeni. Uhuru alipinga na mahakama kuu ikabatilisha maamuzi ya Mombasa tarehe 29 Desemba 2006.

Juni 2007, Uhuru alionesha wazi kwamba alitaka kuachana na ushirikiano wa ODM kwa kutopeleka jina lake kati ya wagombea urais wa ODM. Badala yake alieleza kuwa atampigania rais Kibaki achaguliwe tena.
Katika uchaguzi wa 2007, Uhuru alichaguliwa tena kama mbunge wa Garundu Kusini kwa tiketi ya Kanu.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment