Feb 17, 2011

Zimeishia wapi enzi za uongozi ni dhamana?

 Rais Jakaya Kikwete

Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere

Mzee Rashid Kawawa
 
BISHOP J. HILUKA

NIMEKUWA nikifuatilia habari mbalimbali zinazoripotiwa na vyombo vya habari tangu michakato ya uchaguzi wa meya na wenyeviti wa halamshauri za miji na wilaya ilipoanza baada ya uchaguzi mkuu kumalizika.

Imekuwa ikiripotiwa kuwa kumekuwepo vitendo vya rushwa na kufitiniana miongoni mwa wagombea katika kutaka kuungwa mkono ili kuukwaa umeya au uenyekiti wa halmashauri kitendo kinachoashiria kupotea kwa maadili ya uongozi hapa Tanzania.

Ni kama ilivyokuwa wakati wa mchakato wa viongozi walipokuwa wakiwania kuteuliwa na vyama vyao kugombania nafasi za Ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.

Tulishuhudia wakati wa uchaguzi mkuu na sasa hivi sasa tunashuhudia tena aina ya watu waliojitokeza kuwania umeya na uenyekiti wa halmashauri za wilaya na miji ambao wameelezewa kuwania nafasi hizo kutokana na shinikizo ama wanatakiwa kupata uongozi huo kutoka makundi ya wafanyabiashara ambao wengi wao ama historia zao binafsi katika suala zima la uadilifu zinafahamika waziwazi ndani ya jamii na zimekuwa zinatiliwa shaka sana.

Wafanyabiashara wakubwa wenye kashfa mbalimbali za kuhujumu Taifa wamekuwa wakijitokeza kugombania nafasi mbalimbali za kisiasa, wanapokosa wanaamua kupandikiza watu wao katika uongozi ili kuhakikisha dili zao na biashara zao zinakaa sawa. Hiki ni kitu cha hatari sana ambacho kikiachwa hivi hivi tutaangamia kabisa siku moja.

Kuwepo kwa hisia za ukabila na udini katika baadhi ya maeneo na baadhi ya waliojitokeza kufikia hatua ya kuchafuana kwa kutengenezeana majungu ili kudhoofishana si jambo zuri hata kidogo. Hali hii imeripotiwa karibu mikoa yote ambako waliojitokeza kuwania nafasi hiyo ni wenye majina makubwa na uwezo kifedha.

Pia kuwepo wanaoutaka umeya na uenyeviti wa halmashauri ambao waliwahi kuhusishwa na tuhuma mbalimbali zikiwemo za ulaji rushwa na ukosefu wa maadili ya uongozi, au waliowahi kutuhumiwa katika kashfa za uuzaji maeneo ya wazi, kuingia mikataba feki ya tenda za manispaa na halmashauri ni jambo linaloashiria kuangamia kwa Taifa la Tanzania.

Huu mtindo wa kuchafuana na kutuhumiana kugawa rushwa ni jambo linalotisha sana kwani linaibua mpasuko mkubwa miongoni mwa jamii. Majungu, fitna, matumizi ya fedha na kutumia jina la Rais sasa imekuwa kansa itakayotushinda kuitibu.

Pia taarifa za kuwepo genge la watuhumiwa wa ufisadi ambalo linatuhumiwa kujilimbikizia mabilioni ya fedha chafu, linatajwa na duru mbalimbali za kisiasa ndani na nje ya CCM, kwamba limekuwa likifanya kampeni kubwa katika kiti cha umeya wa jiji la Dares Salaam, na tuhuma za kutoa fedha kwa kila diwani anayeingia katika vikao vya chama vya madiwani si habari njema kabisa.

Hata hatua ya baadhi ya wagombea wenye nguvu za mafisadi kutumia vyombo vya habari kuwapaka matope wenzao ili waonekane hawafai kushika nafasi hiyo inaashiria nini katika uongozi?

Jambo la namna hii ni udhalilishaji mkubwa wa maana ya uongozi, kwa lugha ya sasa hivi tunasema ni uchakachuaji wa uongozi uliopitiliza kipimo.
Taifa limechafuliwa na hawa wanaoutaka uongozi kwa gharama na mbinu yoyote mpaka kufikia kiwango cha kuiona rushwa kama rafiki wa haki na si adui tena, wagombea hawajali kununua wapiga kura ili mradi wapewe kura wanazohitaji.

Ni jambo lililo dhahiri kuwa mgombea wa namna hii hawezi na hatakuwa mtumishi wa watu maana hakuupata uongozi kwa ridhaa ya watu bali kwa ghiliba ya rushwa.

Kinyume na ilivyokuwa katika awamu mbili za kwanza za uongozi wa nchi hii, uongozi wa Tanzania kwa sasa si dhamana tena kama tulivyokuwa tukifundishwa shuleni kwamba 'cheo ni dhamana'. Uongozi sasa hivi umegeuka kuwa njia ya kumfanya mtu mambo yake yamnyookee, uongozi umekuwa biashara 'bab kubwa' isiyo na hasara.

Kwa nchi inayojivuna kutimiza miaka 49 tangu ijitawale kwa maana ya kuwa huru lakini yenye maendeleo duni, kunapotokea wimbi la wafanyabiashara wanaotaka kupandikiza watu wao kwenye uongozi, au unapoona wataalamu wa fani tofauti wanaacha fani zao na kukimbilia kwenye siasa si jambo la kujivunia hata kidogo. Hebu fikiria maprofesa, madaktari, wahandisi, na wataalamu wa fani mbalimbali wanaacha kazi zao walizosomea na kupigania kwenda kusinzia bungeni au kwenye mikutano ya halmashauri.

Lakini unaporudi na kuanza kujiuliza, hivi haya yote chanzo chake hasa ni nini? Kwa nini wagombea watumie mbinu chafu, hujuma, ghiliba na ujanjaujanja katika kupata uongozi? Kwa nini wapigane hadharani, wajidhalilishe, watoe rushwa, wavunjiane heshima na kupakana matope?

Watu wa namna hii wakipata uongozi hawawezi kuwa na uchungu na Watanzania masikini. Kwa hali hii masikini wategemee kusikilizia maumivu zaidi na kasi zaidi ya ugumu wa maisha.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment