Feb 17, 2011

MORGAN TSVANGIRAI: Mfano wa viongozi waathirika wa mfumo mbovu wa tawala za Kiafrika

 Waziri Mkuu wa Zimbabwe, Morgan Tsvangirai

Harare
ZIMBAMBWE

WIKI iliyopita Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma alikwenda Zimbabwe alikokutana na viongozi wakuu watatu; Rais Robert Mugabe, Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai na Naibu Waziri Mkuu Arthur Mutambara, kushinikiza pande hizo kuingia kwenye makubaliano baada ya kutoafikiana kwenye masuala ya msingi.

Mugabe amekuwa anakataa kutekeleza makubaliano ya kisiasa kwa ukamilifu akidai kuwa anataka vikwazo dhidi ya nchi hiyo viondolewe kwanza na hivi karibuni aliibua chuki dhidi ya Tsvangirai baada ya kuwateua kwa siri magavana wa Zanu-PF kinyume na makubaliano ya kisiasa yanayoainisha kuwa pande zote tatu lazima zishirikiane kwenye uteuzi.

Tsvangirai, aliyekuwa mpinzani mkuu wa Mugabe kabla ya kuapishwa kuwa Waziri Mkuu wa Zimbabwe Februari 11, 2009. Hii ni baada ya maisha yaliyojaa vitisho na baadaye majeraha aliyoyapata katika ajali ya gari tarehe 6 Machi 2009 alipokuwa akielekea kijijini kwake Buhera. Mke wake, Susan Tsvangirai, aliuawa katika ajali hiyo baada ya kupata majeraha kichwani.

Tsvangirai aliyekuwa mgombea wa MDC katika uchaguzi wa rais uliozua utata mwaka 2002, na kushindwa na Mugabe. Baadaye aligombea tena mwaka 2008 kama mgombea wa MDC-T na kupata asilimia 47.8 ya kura kulingana na matokeo rasmi, akiwa mbele ya Mugabe, aliyeambulia asilimia 43.2. Tsvangirai alidai kuwa alishinda kwa kura nyingi na kusema kuwa matokeo yalichakachuliwa katika taarifa ya matokeo rasmi.

Baada ya mvutano hatimaye Tsvangirai alikubali kuingia kwenye raundi ya pili ya uchaguzi dhidi ya Mugabe, lakini alijitoa muda mfupi kabla ya uchaguzi kufanyika, akisema kuwa uchaguzi haukuwa huru na wa haki kutokana na vurugu na vitisho toka kwa wafuasi wa serikali dhidi ya wafuasi wake.

MAISHA YA AWALI
Morgan Tsvangirai Richard alizaliwa Machi 10, 1952, eneo la Gutu, Southern Rhodesia (sasa Zimbabwe), akiwa mtoto mkubwa kati ya watoto tisa wa fundi seremala. Baada ya kuondoka shule mwaka 1974, alianza kufanya kazi kwenye migodi ya Trojan Nickel, Mashonaland ya Kati.

Alifanya kazi kwenye migodi kwa miaka kumi, akipanda ngazi kutoka mfanyakazi wa kawaida na kuwa msimamizi. Kijijini kwake kwa sasa ni Buhera, kilomita 220 kusini mashariki ya Harare. Tsvangirai alimuoa Susan mwaka 1978 na walibahatika kupata watoto sita.

Aprili 4, 2009 Tsvangirai alimpoteza mjukuu wake, Sean Tsvangirai, aliyekuwa mtoto wa mwanaye wa pili Garikai, aliyezama katika bwawa. Familia ilichukulia kifo chake kama ajali ya kawaida na kusema hakukuwa na mchezo wowote mchafu.

HARAKATI ZA KISIASA
Wakati wa uhuru mwaka 1980 Morgan Tsvangirai, ambaye alikuwa na miaka 28, alijiunga na chama cha Zanu-PF kilichoongozwa na mtu aliyekuja kuwa mpinzani wake mkubwa kisiasa, Robert Mugabe.

Pia alijulikana kwa majukumu yake katika harakati za vyama vya wafanyakazi Zimbabwe, ambapo alikuwa na nafasi ya mwenyekiti wa tawi la wafanyakazi wa mgodini, na baadaye kuchaguliwa mtendaji mkuu wa wafanyakazi wa migodini ngazi ya Taifa. Mwaka 1989 akawa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini Zimbabwe.

Tsvangirai aliliongoza shirikisho hilo, huku uwezo wake kiutendaji na harakati zake zikikua, na kupelekea uhusiano wake na Serikali kudhoofika. Amewahi kunusurika kuuawa katika majaribio matatu, ikiwa ni pamoja na mwaka 1997 ambapo washambuliaji wasiojulikana walivamia ofisi yake na kujaribu kumtupa nje kupitia dirishani.

UKOSOAJI WA OPERESHENI GUKURAHUNDI
Miaka mitatu baada ya kuingia madarakani, Robert Mugabe aliiamuru Brigedi ya tano, kitengo maalum kilichopata mafunzo ya kijeshi nchini Korea ya Kaskazini, katika mauaji ya Matebeleland kwa kushirikiana na Waziri wa Ulinzi Enos Nkala, wakiongozwa na Perence Shiri kwa sababu ya tuhuma za madai ya kutaka kufanya mapinduzi yaliyopangwa na Joshua Nkomo. Operesheni hiyo iliitwa Gukurahundi.

Tsvangirai amekuwa akizuru mara kwa mara makaburi ya waathirika katika mauaji hayo maeneo ya Tsholotsho, Kezi, Lupane, Nkayi na maeneo mengine ya vijiji vya Matebeleland.

Akiwahutubia wanakijiji wa Maphisa mwaka 2001 alisema:
Hii ilikuwa ni operesheni ya Zanu-PF. Haikupaswa kutokea. Ni jambo la kusikitisha katika historia yetu na MDC itataka kuona haki ikitendeka siku ikiingia madarakani. Ukiukwaji huu wa haki za binadamu lazima uangaliwe kwa mapana na waliohusika wanapaswa kushughulikiwa kwa mauaji hayo.”

TUZO YA SOLIDAR SILVER ROSE
Mwaka 2001 Morgan Tsvangirai alitunukiwa Tuzo ya Solidar Silver Rose. Tuzo hiyo hutolewa kutambua mafanikio bora ya mtu binafsi au shirika katika shughuli za vyama vya kiraia katika kuifanya jamii iwe yenye haki zaidi.

MDC (KABLA YA 2005)
Mwaka 1999 Tsvangirai alianzisha chama cha MDC (Movement for Democratic Change), chama cha upinzani dhidi ya Rais Robert Mugabe na chama tawala cha Zanu-PF. Alisaidia kushindwa kwa kura ya maoni ya katiba Februari 2000, mafanikio ya kampeni yake dhidi ya Katiba ya Taifa.

Tsvangirai alishindwa katika uchaguzi wa rais wa Machi 2002 na Mugabe. Uchaguzi huo ulioambatana na madai kwamba Mugabe aliiba kura kwa njia ya matumizi ya nguvu, upendeleo wa vyombo vya habari, na ghiliba ya wapigakura katika baadhi ya maeneo ambayo Mugabe alikuwa anaungwa mkono.

KUKAMATWA NA VITISHO VYA KISIASA
Tsvangirai alikamatwa baada ya uchaguzi wa 2002 na kushtakiwa kwa uhaini, madai haya baadaye yalifutwa. Mwaka 2004, Tsvangirai aliachiliwa huru kufuatia mashitaka ya uhaini wa njama za kutaka kumuua Mugabe wakati wa mbio za uchaguzi wa rais 2002. George Bizos, mwanasheria wa haki za binadamu wa Afrika Kusini aliyewahi kuwa sehemu ya timu ya kuwatetea Nelson Mandela na Walter Sisulu katika kesi maarufu ya Afrika Kusini mwaka 1964, aliongoza timu ya utetezi wa Morgan Tsvangirai.

Tsvangirai alikamatwa baada ya serikali kudai kuwa alimtishia Rais Robert Mugabe. Wakati kiongozi huyo wa MDC alipowaeleza wafuasi 40,000 katika maandamano mjini Harare kwamba kama Mugabe hataachia ngazi kabla ya uchaguzi uliopangwa kufanyika mwaka 2002 basi wangemuondoa kwa nguvu.

Hata hivyo, Tsvangirai alisema kuwa alikuwa akimuonya Rais Mugabe kwa kuzingatia historia. "Kuna msururu wa madikteta ambao wamekataa kuachia ngazi kwa amani - na watu wameamua kuwaondoa kwa nguvu," alisema. Mahakama iliyafuta mashtaka.

KUKAMATWA, JUNI 2003
Mwezi Juni, 2003 Tsvangirai alikamatwa muda mfupi baada ya kuongea na waandishi wa habari, kwa madai ya kuchochea vurugu. Katika mkutano na waandishi wa habari alisema:
Kutoka Jumatatu Juni 2, hadi leo, Juni 6, Mugabe hakuwa mkuu wa nchi hii. Alikuwa akiandaa majeshi yake ya ukandamizaji dhidi ya uhuru wa watu wa Zimbabwe. Hata hivyo, katika mazingira hayo ya kihayawani, mioyo ya watu haikukata tamaa. Sauti ya milio ya risasi haitonyamazisha madai yao kwa ajili ya mabadiliko na uhuru.”

KUKAMATWA NA KUPIGWA, MACHI 2007
Machi 11, 2007 siku moja baada ya kutimiza miaka 55 ya kuzaliwa kwake, Tsvangirai alikamatwa akiwa njiani kuelekea kwenye maombi Highfield mjini Harare. Mke wake aliruhusiwa kumwona alipokuwa gerezani, na alitoa taarifa kuwa mumewe aliteswa sana na polisi, na kusababishiwa jeraha kubwa kichwani kwake na macho yake kuvimba vibaya.

Aliteswa na kitengo cha Vikosi Maalum vya Zimbabwe vya jeshi, kambi ya Cranborne tarehe 12 Machi 2007 baada ya kukamatwa na kushikiliwa kituo cha polisi Machipisa katika kitongoji cha Highfield Harare.

UVAMIZI MAKAO MAKUU YA MDC
Tsvangirai aliachiwa, lakini tarehe 28 Machi 2007, polisi wa Zimbabwe waliivamia ofisi ya makao makuu ya kitaifa MDC iliyopo Mavuno House 44, na mara nyingine tena walimkamata, saa chache kabla ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu vurugu za kisiasa zilizokuwa zimetokea nchini humo.

MLINZI WA TSVANGIRAI AUAWA
Tarehe 25 Oktoba 2007 iliripotiwa kwamba Nhamo Musekiwa, aliyekuwa mlinzi wa Morgan Tsvangirai tangu kuundwa kwa MDC mwaka 1999, alikufa kutokana na majeraha ya Machi, 2007, wakati wa ukandamizaji na serikali. Msemaji wa MDC Nelson Chamisa alisema kuwa Musekiwa alikuwa akitapika damu tangu Machi 11, 2007, ilipodaiwa kuwa alipigwa sana, pamoja na viongozi wengine wa upinzani na wanachama (ikiwa ni pamoja na Tsvangirai mwenyewe).

MAJADILIANO YA KIMATAIFA
Agosti 2007, Tsvangirai alikutana na Waziri Mkuu wa Australia, John Howard mjini Melbourne, baada ya mazungumzo yao aliviambia vyombo vya habari kwamba Australia ina nafasi muhimu sana kusaidia mapambano dhidi ya serikali ya Rais Robert Mugabe.

Septemba 2007, Tsvangirai alikutana na Thabo Mbeki, Rais wa zamani wa Afrika kusini kwa ajili ya mazungumzo muhimu, na Mei 2008, Tsvangirai alikutana na Raila Odinga, Waziri Mkuu wa Kenya, aliyetoa wito uchaguzi dhidi ya Mugabe urudiwe.

UCHAGUZI WA 2008
uchaguzi wa rais na wabunge uliofanyika tarehe 29 Machi 2008. wagombea wakuu walikuwa watatu; Mugabe, Tsvangirai na Simba Makoni. Uchaguzi huo uligubikwa na utata, vitisho na wizi wa kura na kupelekea machafuko nchini Zimbabwe.

MAZUNGUMZO YA KISIASA 2008-2009
Tarehe 22 Julai 2008, Tsvangirai na Mutambara walikutana na Mugabe uso kwa uso na kupeana naye mikono kwa mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka kumi wakati wa mazungumzo mjini Harare, mazungumzo yaliyoongozwa na Thabo Mbeki, kwa lengo la kutatua migogoro iliyotokana na uchaguzi ili kupelekea ugawanaji wa madaraka kati ya MDC na Zanu-PF katika ngazi ya utendaji.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment