Feb 17, 2011

Ben Ali: Nguvu ya umma yamkimbiza nchini Tunisia

 Zine El Abidine Ben Ali
 
 Waandamanaji waliokuwa wakipinga utawala wa Ben Ali
 
Tunis
TUNISIA

SAUDI Arabia imetangaza rasmi kuwa imempokea Rais wa Tunisia aliyepinduliwa, Zine El Abidine Ben Ali na familia yake, baada ya kushinikizwa kuondoka madarakani.

Taarifa ya jumba la kifalme iliyotangazwa na shirika la habari la nchi hiyo SPA imethibitisha kuwa Ben Ali aliwasili nchini humo mapema tarehe 15 Januari, baada ya kuondoka Tunisia tarehe 14 Januari na hivyo kumalizika kwa utawala wake wa miaka 23, kufuatia maandamano makubwa yaliyosababisha umwagaji damu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kutokana na wasiwasi wa mazingira ya kipekee yanayowakabili ndugu zao wa Tunisia na katika kuunga mkono usalama na utulivu nchini mwao, serikali ya Saudi Arabia imempokea Rais Ben Ali na familia yake.

Kabla ya kuondoka nchini humo alimkabidhi madaraka ya muda Waziri Mkuu wa Tunisia, Mohammed Ghannouchi.

Akizungumza na wananchi wa Tunisia Ghannouchi alisema ataiongoza kwa muda nchi hiyo hadi hapo uchaguzi wa mapema utakapofanyika na kwamba anachukua madaraka kutokana na rais kutoweza kutekeleza majukumu yake. 
 
Mitaa ya mji mkuu wa Tunis ilikuwa shwari, huku kukiwa na usalama wa hali ya juu, ingawa wachambuzi walihoji iwapo mabadiliko hayo ya uongozi wa juu, yangewaridhisha waandamanaji.

Hata hivyo, Baraza la Katiba la Tunisia limemtangaza spika wa ubunge, Fuad Mbazaa kuwa rais wa mpito wa nchi hiyo hadi uchaguzi utakapofanyika na tayari ameshaapishwa kushika nafasi hiyo ya juu.

Serikali ya Ben Ali ambaye amekuwa madarakani tangu mwaka 1987, ilitangaza hali ya hatari tarehe 14 Januari na ilitoa amri ya kutotoka nje kuanzia usiku hadi alfajiri. Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya siku kadhaa za vurugu zilizoanzia miji mingine na kusambaa hadi Tunis na kusababisha watu kuuawa wakati vikosi vya usalama vilipojaribu kuwadhibiti waandamanaji hao wenye hasira.

Kiongozi wa chama cha upinzani nchini Tunisia cha Democratic Progressive, Mohammed Nejib Chebbi, amekielezea kitendo hicho kama mabadiliko ya serikali. Akizungumza na kituo kimoja cha televisheni cha Ufaransa, Bwana Chebbi alisema hiki ni kipindi muhimu kwani kuna mabadiliko ya utawala.

Rais Barack Obama wa Marekani ametoa wito wa kufanyika uchaguzi ulio huru na wa haki nchini Tunisia. Rais Obama pia amepongeza ujasiri na utu wa Watunisia. Alisema analaani matumizi ya nguvu dhidi ya raia ambao wanaelezea maoni yao kwa njia ya amani nchini humo. Aidha, amevisihi vyama vyote kubakia shwari na kuepuka ghasia na ameitaka serikali ya Tunisia kuheshimu haki za binaadamu na kuandaa uchaguzi huru na wa haki hivi karibuni.

Kwa upande wake, Umoja wa Ulaya umetaka kupatikana kwa ufumbuzi wa amani nchini Tunisia wakati ambapo kiongozi wake ameondoka nchini humo. Mkuu wa sera za kigeni wa umoja huo, Catherine Ashton amevitaka vyama vyote kuonesha uvumilivu na kubakia shwari ili kuepusha ghasia na vifo zaidi. Ashton amesema mazungumzo ni muhimu na Umoja wa Ulaya upo tayari kuisaidia Tunisia na umma wake kupata suluhisho la kudumu la demokrasia katika mzozo unaoendelea.

Ghasia hizo zimefuatia machafuko yaliyoanza Desemba 16 eneo la Sidi Bouzid nchini Tunisia na kuutikisa mji mkuu Tunis.

Vikosi vya usalama vilifyatua risasi hewani na kuvurumisha maguruneti ili kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wakivunja vunja katika kitongoji cha Ettadamen karibu na mji mkuu, Tunis.

Mamia ya vijana waliwavurumishia mawe polisi kabla ya kuanza kuvunja maduka na kuitia moto benki moja katika eneo hilo. 
 
Ghasia hizo zimetokana na kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26, mwenye shahada ya chuo kikuu na ambaye hana kazi, Mohammed Buazizi, ambaye alijichoma moto katika mji wa kati wa Sidi Buzeid akipinga kukamatwa kwa mkokoteni wake wa matunda na mboga.

Jaribio la Buazizi la kujiua lilifuatiliwa na jaribio jingine kama hilo lililofanywa na karibu vijana wawili ambao wamemaliza elimu ya chuo kikuu wakipinga dhidi ya hali mbaya ya kiuchumi katika taifa hilo.

Ndipo raia wa Tunisia hasa vijana wakaanzisha maandamano kulalamika kuhusu ukosefu mkubwa wa ajira, rushwa na jinsi utajiri wa nchi hiyo unavyonufaisha wachache nchini humo. Pia walipinga hali ngumu ya maisha na kuzidi kuwa vuguvugu la umma dhidi ya serikali kupinga ukandamizaji wa kisiasa nchini humo.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani, Hillary Clinton aliitolea mwito serikali ya Tunisia “isake ufumbuzi wa amani” kwa mgogoro wa kijamii ulioitikisa nchi hiyo. Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Al Arabiya mjini Dubai, Clinton aliitaka serikali ya Tunisia ijitahidi kubuni nafasi za kazi kwa ajili ya vijana.

Waandamanaji walikuwa wanawasiliana kwa simu za mkono na mtandao, lakini hawakuwa na mwongozo maalum wala shirika lolote la kuwaongoza. 
 
Vyombo vya habari vya nchi za magharibi vimeonekana kutoyapa kipaumbele maandamano ya Tunisia. Matukio hayo ya Tunisia ambayo hayakutarajiwa yalipuuziwa kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari vya mataifa ya Magharibi. Waandishi wa blog katika mtandao wa intaneti pamoja na tovuti ya twita ndio waliokuwa vyanzo muhimu kwa ajili ya kupata taarifa za maendeleo ya kila siku za machafuko hayo.

Kama ilivyo kwa machafuko yanayotokea katika nchi kadhaa za Kiarabu zinazoungwa mkono na mataifa ya Magharibi, polisi walijibu ghasia hizo kwa matumizi makubwa ya nguvu. Kuna ripoti za matumizi ya risasi za moto, msako wa nyumba kwa nyumba kuwakamata wanaharakati, watu kadha kutiwa mbaroni pamoja na mateso dhidi ya watu waliokamatwa.

Polisi kimsingi walivunja maandamano katika mji wa Sidi Buzeid baada ya kukata mawasiliano yote pamoja na barabara katika mji huo, lakini walikabiliana na maandamano zaidi katika miji kadhaa ya jirani.

Utawala wa Ben Ali ulishutumu watu wenye msimamo mkali, na wanaochochea ghasia, pamoja na kundi dogo la mamluki, kwamba ndio wanaochochea ghasia hizo, ikiwa ni shutuma maalum ambazo hutolewa na watalawa wa Kiarabu kila kunapokuwa na ishara za hali isiyo ya utulivu miongoni mwa wananchi wao wanaokandamizwa.

Kabla hajakimbia nchi, muungano wa wafanyakazi wa Tunisia ulikuwa umemtaka Bin Ali kufanya uchunguzi juu ya watu waliouawa katika ghasia nchini humo. Muungano huo uliitaka serikali kuwaachia huru watu waliotiwa mbaroni wakati wa maandamano na kueleza kuwa utafanya mgomo mkubwa katika baadhi ya miji ya kusini mwa nchi hiyo katika kujibu kile ulichokitaja kuwa ni ukandamizaji wa polisi. 
 
Ili kujitakasa, Rais Zine el Abidine Ben Ali alimfuta kazi Waziri wa Mambo ya Ndani Rafik Belhaj Kacem na kusema serikali itachunguza hatua ya polisi kutumia nguvu za ziada kukabiliana na waandamanaji. Kacem alifanya idadi ya mawaziri watatu kufutwa kazi kufuatia machafuko ya ndani ya Tunisia kufuatia kulalamikia hali mbaya ya maisha, umaskini na ufisadi ndani ya taasisi za serikali. Wengine ni mawaziri wa biashara na masuala ya dini walitimuliwa kazi. Lakini hiyo haikusaidia kuwafanya wananchi kuacha maandamano na hatimaye kumng'oa Ben Ali madarakani.

Ben Ali ni nani hasa?
Zine El Abidine Ben Ali alizaliwa katika eneo la Hammam-Sousse tarehe 3 Septemba 1936. Alishika madaraka ya urais tangu Novemba 7, 1987. Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu Oktoba 1987, na mwezi Novemba 1987 akawa rais wa nchi kufuatia mapinduzi ya kijeshi yasiyo ya umwagaji damu yaliyomtoa madarakani Rais Habib Bourguiba. Ben Ali amekuwa akichaguliwa kwa kura nyingi katika kila uchaguzi, mara ya mwisho ilikuwa Oktoba 25, 2009.

Elimu na kazi ya kijeshi
Wakati akiwa mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Sousse, Ben Ali alijiunga na upinzani wa Taifa wakati wa utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Kwa sababu hiyo, alifukuzwa shule na kufungwa. Baadaye alimaliza sekondari, na kisha akapata digrii kutoka Special Inter-service School, Saint-Cyr, Ufaransa, Artillery School iliyopo Chalons-sur-Marne, Ufaransa, Senior Intelligence School (Maryland, USA) na Shule ya Anti-Aircraft Field Artiller (Texas, USA). 
 
Alianza kazi ya kijeshi mwaka 1964 kama afisa wa jeshi. Katika kazi yake ya kijeshi, alianzisha Idara ya Usalama ya Kijeshi na kuongoza shughuli zake kwa miaka 10. Pia alitumikia nafasi za kijeshi nchini Morocco na Hispania kabla ya kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Usalama wa Taifa mwaka 1977.
Mwaka 1980 aliteuliwa kuwa Balozi huko Warsaw, Poland, na kutumikia nafasi hiyo kwa miaka minne.

Familia
Ben Ali na familia yake wanajulikana kwa sababu ya uharibifu wao unaosababishwa na rushwa. Hii ndiyo imepelekea kuwepo maandamano. Wengi ya wanafamilia ya Ben Ali wameondoka nchini Tunisia kwa sababu ya usalama binafsi.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment