Feb 17, 2011

Tujadili pia mfumo wa elimu ya Tanzania

 Wanafunzi wa sekondari

Mwl Julius Nyerere, aliamini ujinga ni adui mkubwa wa taifa letu

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

KILA mwaka matokeo ya mtihani kwa wanafunzi wanaomaliza elimu ya msingi au sekondari yanayoambatana na baadhi ya wanafunzi kushangilia na wengine kubaki wameduwaa hutangazwa.

Matokeo hayo huleta huzuni kwa walio wengi ambao hawakupata matokeo mazuri. Kuna ambao hufutiwa matokeo kwa sababu za udanganyifu katika mtihani.

Matokeo haya hutumika kuwakejeli watoto wa mafukara na wazazi wao kwa kuwa wamewekwa kando na mfumo wa kijamii – kiuchumi unaowapendelea, kuwajenga na kuwaendeleza wachache huku ukiwapuuza, kuwachuja na kuwatupa walio wengi.

Mfumo wa kijamii – kiuchumi nchini umejengwa kitabaka, hautumiki kuleta usawa katika jamii bali unatumika kuzidisha tabaka kati ya matajiri na masikini.

Enzi za Mwalimu Nyerere, matarajio na malengo ya mfumo wa elimu ilikuwa kwanza kupiga vita ujinga. Lengo lilikuwa kuhakikisha kila Mtanzania anajua kusoma na kuandika ili kuweza kujitegemea. 
 
Huo ndio ulikuwa msingi ambao ulijengwa na Serikali ya awamu ya kwanza. Baada ya Mwalimu, awamu zilizofuata zilipaswa kuendeleza mambo muhimu yanayohitajika katika mfumo wa elimu bora.

Tukiwa tunaelekea miaka 50 ya Uhuru, tunapaswa kuutazama upya mfumo wetu wa elimu unamsaidiaje Mtanzania wa karne hii ya sayansi na teknolojia.

Mfumo huu unamjengaje kijana wa Kitanzania kushindana na kijana wa Kikorea, Kihindi au Kimexico? Kwa nini tuendelee kutumia mfumo wa miaka 7 ya elimu ya msingi, miaka 4 ya sekondari na 2 ya sekondari ya juu kabla mwanafunzi hajakanyaga chuo chochote kupata mafunzo anayoweza kuyatumia? Hivi kwa miaka 13 kijana wa Tanzania anakuwa amepatiwa ujuzi wa aina gani? Ni kweli anakuwa ameandaliwa kushindana na vijana wenziwe kutoka nchi nyingine kama hatafanikiwa kuingia chuo chochote? 
 
Hivi mfumo huu wa mtoto kuanza elimu ya msingi akifundishwa masomo yote kwa Kiswahili isipokuwa somo la Kiingereza kwa miaka yote saba, kisha anapoanza sekondari masomo yote kufundishwa kwa Kiingereza isipokuwa somo la Kiswahili umewekwa kwa sababu gani? Hatuoni kuwa mwanafunzi huanza kujifunza mambo mageni kwa lugha ya kigeni?

Mfumo huu unazalisha vijana wenye uwezo wa juu wa kukariri na si vijana wenye uwezo wa kufikiri na kuchambua mambo. Kama matarajio yetu ni kuhakikisha wanafunzi wanafaulu mitihani, basi tumepiga hatua kurudi nyuma kwa kuwa miaka yote 13 kijana wa Kitanzania huandaliwa ili afanye mtihani wa kidato cha sita!

Ubora wa elimu Tanzania unapimwa kwa kushindanisha shule zipi zinatoa wanafunzi wengi wa daraja la kwanza, na si shule zipi zinatoa wanafunzi wenye uwezo wa juu wa kufikiri na kuchambua mambo.

Ukichunguza utagundua kuwa shule zinazosifiwa kufanya vizuri ni zilezile zenye vifaa bora na ambazo wenye uwezo huwapeleka watoto wao. 
 
Inavyoonekana ukiwa na pesa mtoto wako atapata elimu nzuri na fursa bora zaidi ya kuendelea mbele kimaisha. Usipokuwa na pesa shauri yako na wanao! Hatuwezi kujenga nchi yenye amani, usalama, demokrasia na maendeleo endelevu kwa kutumia mfumo wa elimu unaoendeleza utamaduni wa kuwaacha walio wengi nyuma.

Mfumo wetu wa elimu ni wa kibaguzi na haujengi maadili ya kiutu, kusaidiana na kuendelezana miongoni mwa wanafunzi ambao wanafanywa kushindana kimasomo badala ya kusaidiana. 
 
Badala ya kuwapa watoto elimu ya kuwafanya wajitambue na kuendeleza vipawa vyao tunatumia muda mwingi kuwafanya wafaulu mitihani kitendo kinachohamasisha wizi wa mitihani. Mfumo wa kutathmini vipawa vya watoto kwa mitihani ya siku chache katika kipindi kirefu cha masomo hautufai.

Mbaya zaidi hakuna usawa wa mazingira ya masomo huku mtihani ni mmoja. Kwa hali hiyo, tunapojadili Katiba mpya ni muhimu tukadai uwepo mfumo wa elimu wenye kuweka usawa na kumjenga kijana anayejitambua na mwenye ujuzi wa kuchangia maendeleo ya taifa unaotokana na kuendelezwa kwa vipawa alivyozaliwa navyo.

Hatuwezi kulikwepa Shirikisho la Afrika Mashariki, na sioni juhudi zozote za serikali kuuboresha mfumo wa elimu kabla hatujaingia kwenye ushindani. Tutaogopa hadi lini kuungana na Kenya au Uganda kwa sababu eti wanajua Kiingereza au wana wasomi wengi? 
 
Serikali inapaswa kuwekeza kwenye ubora wa elimu kwa kuachana na mtindo wa kuwachukua waliopata matokeo yasiyoridhisha kuwa walimu, badala yake itazame waliofanya vizuri, na walimu wa stashahada na wa shahada kufundisha katika shule za msingi huku mazingira yao yakiboreshwa.
Mazingira hayo ni pamoja na nyumba nzuri za kuishi, huduma kama umeme, maji, intaneti na kadhalika.

Kwa nini Wizara ya Elimu na Mafunzo inashindwa kufikia muafaka wa lugha ya ufundishaji toka ngazi ya chini hadi elimu ya juu? Malumbano ya lugha gani kati ya Kiswahili au Kiingereza itumike kufundishia hayatusaidii. Watanzania tunayumba kwa kuwa Kiingereza hatukijui na Kiswahili tumekitupa, tofauti na Wakenya ambao hatuwawezi kwenye Kiingereza wala kwenye Kiswahili.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment