Feb 17, 2011

HOSNI MUBARAK: Asita kuachia madaraka kwa kuhofia machafuko zaidi, na asema hatarajii kuikimbia nchi yake.

 Hosni Mubarak

CAIRO
Misri

PAMOJA na rais wa Misri, Hosni Mubarak kutangaza nia ya kutowania tena madaraka, wapinzani wake bado wanasisitiza kuwa ang'oke haraka iwezekanavyo! 
 
Huku maandamano ya kuupinga utawala wa Misri yakiendelea, kile kinachoonekana kama upepo wa mageuzi uliloanzia na mapinduzi yaliyomng'oa Zein El-Abidine Ben Ali wa Tunisia, kimeanza kusambaa nchi nyingine za Kiarabu.

Serikali inayoongozwa na rais Hosni Mubarak imefanya kikao chake cha kwanza cha Baraza jipya la Mawaziri Jumatatu ya wiki hii, tarehe 7 Februari, 2011, tangu kuzuka kwa maandamano dhidi ya utawala wake huku kukiwa hakuna ishara ya hatua zilizopigwa katika mazungumzo na upande wa upinzani ambao unataka aondoke madarakani.

Baraza hilo jipya la Mawaziri nchini Misri limetangaza nyogeza ya mshahara kwa wafanyakazi wa serikali kwa asilimia 15, kwa mara ya kwanza tangu kuanza vuguvugu la maandamano wiki mbili zilizopita.
 
Kuna wafayakazi millioni sita katika sekta ya umma nchini Misri. Mnamo siku za nyuma wengi wao walikuwa wafuasi wakubwa wa serikali lakini katika miaka ya hivi karibuni mishahara ya chini na bei ghali za vitu vimesababisha manun'guniko mengi. 
 
Na sasa baada ya takriban wiki mbili za machafuko, juhudi zinaendelea kujaribu kuwavutia kuiunga mkono serikali kwa kuwapa nyongeza ya asilimia 15 kwa mshahara na malipo ya uzeeni, kuanzia mwezi wa Aprili. 
 
Hapo awali Baraza la Mawaziri pia lilitoa ahadi mpya za kuchunguza vitendo vya rushwa serikalini na wizi wa kura. Na likatangaza kuwa mmojawapo wa vijana waliotayarisha maandamano hayo ambaye ni meneja wa huduma ya tovuti ya Google ataachiliwa. 
 
Lakini hatua zote hizi hazijazuia ari ya waandamanaji kuendelea na maandamano yao katika uwanja wa Tahrir Square - na kuendelea kudai Rais Mubarak aondoke. 
 
Mazungumzo hayo baina ya serikali ya Misri na makundi ya upinzani yaliyolenga kutatua mzozo wa kisiasa nchini humo yameshindwa kumaliza maandamano katikati ya mji wa Cairo. Waandamanaji ambao wamekuwapo katika eneo la Tahrir kwa wiki mbili zilizopita wanasema kuwa wataondoka katika eneo hilo iwapo rais Mubarak atajiuzulu. 
 
Lakini Mubarak mwenye umri wa miaka 82 anasisitiza kuwa ataendelea kubaki madarakani hadi Septemba mwaka huu huku Serikali yake ikiridhia mambo kadhaa katika mazungumzo ya jana, lakini upinzani umesema hayatoshi.

Kuanzia Jumanne, 1 Februari, 2011, mamillioni ya wananchi wa Misri walifurika kwenye Uwanja wa Tahrir, maarufu kama Uwanja wa Mapinduzi, ili kumshinikiza Rais Hosni Mubarak kung'oka toka madarakani, kazi ambayo ameifanya kwa takriban miaka thelathini, ili kuanza mchakato wa kuandika Katiba mpya nchini Misri, itakayowashirikisha wadau wengi zaidi, kama kielelezo cha matunda ya mshikamano miongoni mwa wananchi wa Misri; uchaguzi mkuu ambao utazingatia misingi ya uhuru, haki na demokrasia ya kweli, kufanyika katika kipindi cha miezi sita kuanzia sasa pamoja na kuendeleza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; ili kuhakikisha kwamba, utawala sheria unashika mkondo wake.

Rais Hosni Mubarak akizungumza kwenye Televisheni ya Taifa, pamoja na kutangaza rasmi kwamba, hatawania tena nafasi ya uongozi katika uchaguzi mkuu nchini Misri, uliopangwa kufanyika mwezi Septemba, 2011, alisema atajitahidi kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na mabadiliko ya kisiasa katika hali ya utulivu na amani na kwamba, anatambua na kuthamini mchango wa vyama vyote vya upinzani katika harakati za kidemokrasia nchini Misri.

Rais Mubarak alisema, anajivunia kuiongoza Misri na kamwe, hatarajii kuikimbia nchi yake, bali atahakikisha kwamba, anabaki humo hadi dakika ya mwisho wa maisha yake na kwamba, historia itaweza kumhukumu kwa haki. Mubarak alisema siku ya Alhamisi wiki iliyopita kuwa anahofia kutakuwa na machafuko iwapo ataondoka madarakani sasa.

Rais Barack Obama wa Marekani kwa upande wake baada ya hotuba ya Rais Mubarak, anaendelea kuhimiza umuhimu wa mabadiliko ya kisiasa kufanyika nchini Misri; mabadiliko ambayo yatakuwa na maana kwa wananchi wa Misri, yakizingatia misingi ya haki na amani na kwamba, kuna haja ya mabadiliko haya kujumuisha pia vyama vya upinzani.

Marekani imesema inafanya mashauriano na serikali ya Misri kuhusu utaratibu wa rais Hosni Mubarak kukabidhi madaraka. Taarifa zinasema kuwa mojawapo wa masuala yanayozingatiwa ni Mubarak kujiuzulu na kukabidhi mamlaka kwa Baraza la Kikatiba.

Serikali ya Marekani hata hivyo imesisitiza kuwa uamuzi kamili utatoka kwa watu wa Misri.

Historia ya Mubarak
Muhammad Hosni Sayyid Mubarak alizaliwa Mei 4, 1928, katika eneo la Kafr-El-Meselha, Misri, ni rais wa nne wa Jamhuri ya Kiarabu ya Misri. 
 
Baada ya kumaliza masomo yake ya sekondari ya juu, alijiunga na Chuo cha Mafunzo ya Jeshi, ambako alipata shahada ya Sayansi katika Jeshi mwaka 1949. Tarehe 2 Februari, 1949, Mubarak wa alipoondoka katika Chuo cha Jeshi na alijiunga na Chuo cha Jeshi la Anga, na kufuzu mafunzo ya urubani Machi 13, 1950, na hatimaye kupata Shahada ya Sayansi ya Usafiri wa Anga. Hosni Mubarak amemuoa Suzanne Mubarak, na wana watoto wawili: Alaa na Gamal.
Kabla ya kuingia kwenye siasa, Mubarak alikuwa afisa katika Jeshi la Anga la Misri , akiwa kama kamanda wake kuanzia mwaka 1972 hadi 1975.

Akiwa afisa wa Jeshi la Anga la Misri, Mubarak alitumikia katika vitengo mbalimbali, ikiwa ni pamoja na miaka miwili aliyotumikia katika kitengo cha Spitfire fighter. Kuna wakati katika miaka ya 1950, aliwahi kurudi Chuo cha Jeshi la Anga, wakati huu kama mwalimu, na kubakia huko hadi mwaka 1959.

Kuanzia Februari 1959 hadi Juni 1961, Mubarak ilichukua mafunzo zaidi katika Umoja wa Kisoviet, katika chuo cha mafunzo ya urubani cha Umoja wa Kisoviet jijini Moscow na mengine katika Chuo cha Kant (Kant Air Base), karibu na Bishkek nchini Kyrgyzstan (zamani Jamhuri ya Urusi). 
 
Mubarak ilichukua mafunzo ya ushambuliaji ndege ya Ilyushin Il-28 na Tupolev Tu-16, na kisha alijiunga na Chuo cha Kijeshi cha Frunze mwaka 1964. Aliporudi Misri, alifanya kazi katika tawi na baadaye kama kamanda mteule wa kikosi, akichukua wadhifa wa Kamanda wa Kikosi cha Cairo West Air Base Oktoba 1966.

Novemba 1967, Mubarak akawa kamanda wa Chuo cha Jeshi la Anga na miaka miwili baadaye akawa Mkuu wa Watumishi wa Jeshi la Anga la Misri.
Kazi yake ya kijeshi ilifikia kilele chake mwaka 1972 alipokuwa Kamanda wa Kikosi cha Anga cha Misri na Naibu Waziri wa Ulinzi, na mwaka uliofuata alipandishwa cheo.

Makadirio ya mali ya Mubarak na familia yake yanafikia dola za Marekani kati ya bilioni 40 hadi bilioni 70. Shirika la Utangazaji la ABC linaripoti kuwa mali hii imepatikana wakati wa mikataba ya kijeshi enzi hizo Mubarak alipokuwa afisa wa Jeshi la Anga.

Makamu wa Rais wa Misri
Mwezi Aprili 1975, Mubarak aliteuliwa na Sadat kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Misri. Katika nafasi hii, alitumikia kwa uaminifu sera za Sadat. Alishiriki katika mashauriano ya serikali ambayo yalishughulikia mustakabali wa mkataba na vikosi vya Israel. 
 
Kama sehemu ya usaidizi wake kwa sera za Sadat, mwezi Septemba 1975 alikwenda Riyadh na Damascus, ili kuzishawishi serikali za Saudi na Syria kukubali mkataba na Israel serikali ("Sinai II"), lakini alikuwa amekataa mkutano na Rais wa Syria.

Rais wa Misri
Baada ya kuuawa kwa Rais Anwar El Sadat Oktoba 14, 1981, na maafisa wa jeshi lake kufuatia kutia saini mkataba wa Misri – Israel kitu kilichoonekana ni kinyume, Mubarak alishika madaraka ya Urais.

Mubarak pia Mwenyekiti wa Taifa wa chama cha Kidemokrasia (NDP) ambacho hivi sasa viongozi wake wote wamejiuzuru nyazifa zao serikalini. Mubaraka ndiye mkuu wa nchi aliyetumikia kwa muda mrefu nchini Misri tangu Muhammad Ali Pasha.

Makala hii imeandaliwa na Bishop J. Hiluka kwa msaada wa vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment