Feb 17, 2011

ABDELAZIZ BOUTEFLIKA: Akabiliwa na vurugu za wanaotaka makazi, ajira, na maisha mazuri Algeria

 Abdelaziz Bouteflika

KUINGIA kwa mwaka mpya wa 2011 kumeambatana na vurugu zilizosababishwa na maandamano ya vijana nchini Algeria, yaliyozuka tarehe 1 Januari 2011 na kupelekea hali ya wasiwasi nchini humo. 
 
Watu watatu wameuawa na mamia kujeruhiwa katika maandamano yanayoendelea nchini Algeria, na kupelekea serikali kukutana na kujadili njia ya kuondokana na vurugu hizo zilizosababishwa na kupanda kwa gharama za chakula na ukosefu wa ajira. 
 
Waziri wa Mambo ya Ndani na Serikali za Mitaa wa Algeria, Daho Ould Kablia, alisema kuwa kuanzia tarehe 1 Januari, vurugu kubwa zilizotokea katika sehemu nyingi nchini Algeria na kusasababisha vifo hivyo na wengine 400 hivi kujeruhiwa. 
 
Kablia alisema katika vurugu zilizotokea eneo la Ain Lahdjel, mkoani Msila, kilomita 300 kutoka mji mkuu, Algiers, kijana mmoja alijaribu kuingia katika idara ya polisi na kupigwa risasi na polisi akafa. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 18 anajulikana kwa jina la Azzedine Lebza. 
 
Mwandamanaji wa pili aliuawa Ijumaa katika eneo la Bou Smail, mji mdogo ulio kilomita 50 magharibi ya Algiers. Mwandamanaji huyo aliuawa alipojaribu kupambana na jeshi la usalama na kufariki kutokana na kujeruhiwa vibaya. Daktari alisema kwamba mtu huyo, alitambuliwa kupitia vyombo vya habari kama Akriche Abdelfattah mwenye umri wa miaka 32. Mwili wa tatu ulikutwa katika hoteli ukiwa umeunguzwa kwa moto. 
 
Mbali na hayo vurugu hizo zilisababisha takriban watu 400 kujeruhiwa, wakiwemo wananchi na watekelezaji wa sheria.

Polisi walitumia mabomu ya machozi na maji yanayowasha dhidi ya vijana waandamanaji waliokuwa wakiwatupia mawe. Maandamano hayo yanaohusishwa na kupanda kwa bei ya chakula, uhaba wa makazi, na malalamiko ya kisiasa na kijamii. Mawaziri wa serikali wametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu, huku shirikisho la soka la nchi hiyo likifuta mechi zote za mwishoni mwa wiki hii. 
 
Takriban watu 300 kati ya watu 400 waliojeruhiwa katika maandamano hayo walikuwa ni maafisa wa polisi, Kablia alibainisha. Algeria imeshuhudia siku tatu za machafuko yaliyotokana na kupanda kwa gharama za maisha na ukosefu wa ajira, ambapo takwimu za serikali zinaonesha kuwa asilimia ni 10, lakini mashirika ya kujitegemea yanaonesha kuwa ni karibu asilimia 25.

Algiers, ambayo imeshuhudia maandamano katika siku za karibuni, ilikuwa katika hali ya utulivu siku ya Jumamosi, lakini mashuhuda wametaarifu kuwepo kwa maandamano ya kawaida eneo la Kabylie. 
 
"Serikali imekuwa ikiwapuuzwa watu wake tangu ilipochaguliwa kuongoza nchi na kimsingi sasa (watu) wameamua kutoka katika mitaa ili kuitaka mamlaka iwawape ajira na kugawana utajiri wa taifa," mtu mmoja aliiambia televisheni ya Al Jazeera, akiwa London.

Nina hofu kuwa upo uwezekano wa mamlaka kuzidisha ufa kwa wanaopinga badala ya kuwapatia wanachohitaji. Waziri aliwaita kuwa ni 'wahalifu'.”

Maandamano hayo yanaonesha picha halisi ya wananchi waliokatishwa tamaa na watawala na ukosefu wa uhuru wa kisiasa, pamoja na wasiwasi zaidi juu ya kupanda kwa gharama za maisha, makazi, na ukosefu wa ajira. Bei ya unga, mafuta ya kupikia na sukari zimepanda mara dufu katika kipindi cha miezi michache iliyopita. Maandamano nchini Algeria yanafuatia kipindi adimu cha utulivu katika nchi jirani ya Tunisia.
Pengine ni mapinduzi
 
Mohamed Zitout, mwanadiplomasia wa zamani wa Algeria, aliiambia televisheni ya Al Jazeera: "Ni uasi, na pengine ni mapinduzi, ya watu wanaohisi kuonewa, kwa muda wa miaka 50, wamekuwa wakisubiri kupatiwa makazi, ajira, na maisha mazuri na heshima katika nchi hiyo tajiri. 
 
Lakini bahati mbaya nchi inatawaliwa na wasomi matajiri sana wasiojali kuhusu kile kinachoendelea katika nchi - kwa sababu hawakuwapa watu wanachokihitaji, hata kama serikali ina uwezo wa kufanya hivyo, watu wameamua kuasi.” 
 
Vijana walipambana na polisi mjini Algiers na miji mingine kadhaa nchini kote siku ya Ijumaa pamoja na kutakiwa kuwa watulivu na maimamu. Eneo la Annaba, kilomita 600 magharibi ya mji mkuu, maandamano yalizuka baada ya sala ya Ijumaa katika kitongoji maskini cha mji na kuendelea hadi usiku. Ofisi ya serikali ya mtaa ilivunjwa na kuporwa, kwa mujibu wa mashuhuda.

Waandamanaji pia walikata nguzo za umeme wakati wa usiku, kukata umeme unaokwenda kwenye kitongoji cha Auzas. 
 
Mapigano pia yamezuka kwa mara ya kwanza mjini Annaba, kama kilomita 550 (maili 350) Mashariki ya mji mkuu, ambapo mamia ya watu walikuwa wakiwarushia mawe polisi waliopelekwa nje ya ofisi za serikali, habari hii ni kwa mujibu wa AFP.

Taarifa zimeongeza kuwa vurugu zilifanyika katika mji wa Tizi Ouzou, mji ambao ni makao makuu ya mkoa wa Kabylia, kama kilomita 90 mashariki ya Algiers. Wakazi walisema kuwa maandamano yalienea kutokea katikati ya mji na kuelekea nje ya mji, na waandamanaji walichoma matairi wakiziba barabara kuu ya kuelekea Algiers. 
 
Pia kulikuwa na vurugu zilizoripotiwa katika jiji la pili kwa ukubwa wa Oran.
Abdelaziz Bouteflika, Rais wa Algeria, anayetumikia kipindi cha tatu, hajasema chochote kuhusiana na maandamano hayo ya umma.
Historia yake 
 
Abdelaziz Bouteflika amezaliwa tarehe 2 Machi 1937 katika eneo la Oujda, Morocco. Ni rais wa kumi wa Algeria ambaye ameitumikia nchi hiyo tangu mwaka 1999. 
 
Ni mtoto wa kwanza wa mama yake, na wa pili wa baba. Bouteflika ana dada-wa kambo (half-sisters) watatu: Fatima, Yamina, na Aicha, ndugu wanne: Abdelghani, Mustapha, Abderahim na Said, na dada mmoja (Latifa). Said amekuwa akitumikia kama daktari binafsi wa Abdelaziz Bouteflika, na inasemwa kuwa amekuwa mtu muhimu kati ya washauri wa Bouteflika.

Miaka ya mwanzo ya Vita na Uhuru

Bouteflika aliishi na kusoma nchini Algeria hadi alipojiunga na Front de Liberation Nationale (FLN) mwaka 1956, akiwa na umri wa miaka 19. Alianza kazi kama mdhibiti, akikusanya taarifa kuhusu hali mpaka wa Morocco na magharibi mwa Algeria, baadaye akawa katibu wa utawala wa Houari Boumedienne.
Aliibuka kama mmoja wa washirika wa karibu wenye ushawishi mkubwa kwa Boumédienne, na mwanachama wa kundi la Oujda. Mwaka 1962, wakati wa uhuru, aliambatana na Boumédienne na Majeshi ya mpakani kwa msaada wa Ahmed Ben Bella dhidi ya Serikali ya muda ya Jamhuri ya Algeria.

Baada ya uhuru na kazi ya kisiasa

Baada ya uhuru wa Algeria mwaka 1962, Bouteflika akawa msaidizi wa Tlemcen katika Bunge na Waziri wa Vijana na Michezo katika Serikali iliyoongozwa na Ahmed Ben Bella. Mwaka uliofuata, aliteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, na kubakia katika nafasi hiyo hadi kifo cha Rais Houari Boumédienne mwaka 1978.

Mfululizo wa mapambano na kuishi uhamishoni

Baada ya kifo kisichotarajiwa cha Boumédienne mwaka 1978, Bouteflika alionekana kama mmoja kati ya wagombea wawili wakuu wanaofaa kuchaguliwa kuwa rais. Bouteflika alidhaniwa kuwakilisha “mrengo wa kulia” wa chama uliokuwa wazi zaidi kuhusu mageuzi ya kiuchumi ili kurejesha mahusiano na nchi za Magharibi. Kanali Mohamed Salah Yahiaoui yeye aliwakilisha mrengo wa kushoto wa Kiboumediennist. Mwisho, jeshi liliingia makubaliano maalum na mgombea, Kanali mwandamizi wa jeshi Chadli Bendjedid.
 
Bouteflika aliteuliwa tena kushika nafasi ya Waziri wa Nchi, lakini alipoteza nguvu kutokana na sera za Bendjedid. 
 
Baada ya miaka sita akiishi nje ya nchi, jeshi likamrejesha kwenye Kamati Kuu ya FLN mwaka 1989, baada ya nchi kuingia katika machafuko na kukosekana kwa utulivu kutokana naa mpango wa majaribio katika mageuzi.

Mwaka 1992, mchakato wa mageuzi ulimalizika ghafula wakati jeshi lilipochukua madaraka na kutupilia mbali uchaguzi uliowapa ushindi chama cha Islam Salvation Front.

Hii hii ilisababisha vita ya wenyewe kwa wenyewe ambayo iliyodumu katika miaka ya 1990. Katika kipindi hiki, Bouteflika alikaa pembeni, na alisikika kidogo sana kwenye vyombo vya habari na hakuwa na nafasi ya kisiasa.
Januari 1994, Bouteflika alikataa pendekezo la Jeshi la kutakiwa kurithi madaraka ya rais aliyeuawa, Mohamed Boudiaf; alidai baadaye kwamba ilikuwa ni kwa sababu jeshi halikuwa limempa udhibiti kamili juu ya vikosi vya jeshi. Badala yake, Jenerali Liamine Zeroual akawa Rais.

Uchaguzi kama Rais katika 1999

Mwaka 1999, bila kutarajia Zeroual aliachia ngazi na kutangaza uchaguzi wa mapema. Sababu ya uamuzi wake haikuwa wazi. 
 
Bouteflika akajitosa kugombea Urais kama mgombea binafsi, akiungwa mkono na jeshi. Alichaguliwa kwa asilimia 74 ya kura, kwa mujibu wa hesabu za serikali. Wagombea wengine wote walijiondoa kwenye uchaguzi mara moja kabla ya kupiga kura, wakidai kuwepo udanganyifu.
 
Aprili 8, 2004, alichaguliwa tena kwa asilimia 85 ya kura katika uchaguzi uliokubaliwa na waangalizi kama uchaguzi huru na wa haki, licha ya makosa madogo madogo

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa mashirika mbalimbali ya habari.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment