Feb 17, 2011

Alassane Ouattara: Mwathirika mwingine wa mfumo mbovu wa tawala za Kiafrika

 Alassane Ouattara

Abidjan
IVORY COAST

WIKI hii hali ya kisiasa nchini Ivory Coast imezidi kuwa tete baada ya wagombea wote wa urais kujitangaza kushinda na kuapishwa kwa nyakati tofauti, hali inayoondoa matumaini ya kurejea kwa amani kwenye taifa hilo.

Rais aliyekuwa anayetetea kiti chake, Laurent Gbagbo alikula kiapo cha kuongoza muhula mpya katika sherehe iliyofanyika Ikulu na kutangazwa moja kwa moja na televisheni, lakini saa kadhaa baadaye mpinzani wake mkuu, Alassane Ouattara akaapishwa na kuhakikishia umma kuwa yeye ndiye rais wa nchi hiyo.

Hali hiyo ikamlazimu Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki kwenda Ivory Coast kujaribu kupatanisha pande hizo mbili ingawa Umoja wa Mataifa (UN), Umoja wa Ulaya (EU) pamoja na Marekani wanashikilia msimamo kuwa watamtambua Ouatarra kuwa mshindi halali na si Gbagbo kama alivyojitangaza.

Ouattara ndiye aliyetangazwa mshindi na Tume ya Uchaguzi, lakini matokeo hayo yalibadilishwa na Baraza la Uchaguzi ambalo linaongozwa na mshirika wa rais Gbagbo.

Tume huru ya uchaguzi ya Ivory Coast ilitangaza kuwa Ouattara ameshinda kwa kupata asilimia 54.1 ya kura. Lakini siku iliyofuata kamati ya katiba ya nchi hiyo ilitangaza upya matokeo ya uchaguzi wa rais ikisema Laurent Gbagbo ameshinda kwa asilimia 51.45 ya kura.

Katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baadaye, mwakilishi wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa anayeshughulikia mambo ya Ivory Coast, Choi Young-jin alisema kamati ya katiba kutangaza ushindi wa Gbagbo ni hatua isiyolingana na hali halisi, kwa sababu kura za majimbo 7 yaliyoko kaskazini mwa nchi hiyo hazikujumuishwa kwenye matokeo hayo.

Hali inaonesha kuwa huenda machafuko makubwa zaidi yanaweza kutokea endapo juhudi za makusudi hazitachukuliwa kuepusha machafuko hayo hasa kufuatia kitendo cha wagombea hao kila mmoja kuungwa mkono na upande fulani, Gbagbo anaungwa mkono na jeshi la serikali na taasisi nyingi, ikiwemo ya Baraza la Katiba, huku Ouatarra akiungwa mkono na Jeshi Jipya la Uasi na Jumuiya ya Kimataifa.

Kumekuwepo taarifa za watu kadhaa kufa jijini Abidjan katika ghasia zinazotokana na uchaguzi huo. Mitaani, wafuasi wa upinzani wanaendelea kuandamana pamoja na kuchoma matairi ovyo, wakionesha kupinga kitendo cha Gbagbo kujitangaza mshindi, huku wakisema kuwa hayo ni mapinduzi.

Alassane Ouattara Dramane (tamka Alasan Watara), alizaliwa 1 Januari 1942. Alikuwa Waziri Mkuu wa Ivory Coast kuanzia Novemba 1990 hadi Desemba 1993. Ni Rais wa chama cha Rally of the Republican (RDR), chama ambacho kina wafuasi eneo la kaskazini ya nchi.

Mbali ya kuwa mwanasiasa pia ni mtaalamu wa teknokrasia, mchumi na amewahi kufanya kazi Shirika la Fedha Duniani (IMF) na Benki Kuu ya Afrika Magharibi (BCEAO).

Alassane D. Ouattara alikuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Kimataifa la Fedha tarehe 1 Julai, 1994.
Ouattara alihitimu shahada yake ya kwanza ya B.Sc. (Business Administration) huko Drexel Institute of Technology, Philadelphia (1965), na shahada ya pili katika uchumi, MA (Economics) mwaka 1967, pia alipata shahada ya uzamivu katika uchumi, Ph. D. in economics mwaka 1972 aliyoipata kwenye Chuo Kikuu cha Pennsylvania.

Aliteuliwa kuwa Mchumi katika Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kuanzia mwaka 1968 hadi mwishoni mwa 1973, baada ya hapo alitumikia Benki Kuu ya Afrika Magharibi (BCEAO) mjini Paris mwishoni mwa 1973 hadi mwanzoni mwa 1975, alipoteuliwa kuwa Mshauri Maalum wa Gavana na Mkurugenzi wa Utafiti. Alishikilia nafasi hii hadi alipoteuliwa kuwa Makamu wa Gavana wa BCEAO mwaka 1983. Mwishoni mwa mwaka 1984, alirudi tena IMF na kuwa Mkurugenzi wa Idara ya Afrika, na wakati huohuo kuanzia 1987, alikuwa Mshauri wa Mkurugenzi Mtendaji.

Oktoba 1988, Ouattara aliteuliwa kuwa Gavana wa BCEAO. Alitumikia nafasi hiyo mwaka 1990 pia kama Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uratibu wa Mpango wa Udhibiti na Ufufuaji Uchumi Ivory Coast, Abidjan.

Ouattara amewahi kutunukiwa nishani kadhaa, ikiwa ni pamoja na: “Commander of the Ordre du Lion, Senegal”, “Commander of the Ordre du Mono, Togo”, “Commander of the National Order of Niger”, “Grand Officier of the National Order of Côte d'Ivoire”, na Gavana wa heshima, BCEAO.

WAZIRI MKUU
Mwezi Aprili mwaka 1990, Rais wa Ivory Coast Felix Houphouet-Boigny alimteua Ouattara kuwa Mwenyekiti wa Kamati Maalum ya Uratibu wa Mpango wa Udhibiti na Ufufuaji Uchumi Ivory Coast, wakati huohuo akiendelea na nafasi yake kama Gavana BCEAO. Baadaye alikuwa Waziri Mkuu wa Ivory Coast Novemba 7, 1990, huku Charles Konan Banny akichukua nafasi ya Gavana wa BCEAO badala yake.

Wakati akiwa Waziri Mkuu, Ouattara pia alibeba majukumu ya urais kwa miezi 18, ikiwa ni pamoja na kipindi cha kuanzia Machi 1993 hadi Desemba 1993, wakati Houphouet-Boigny alipokuwa mgonjwa. Houphouet-Boigny alikufa Desemba 7, 1993, na Ouattara alilitangazia taifa kuhusu kifo chake, akisema kuwa “Ivory Coast imeachwa yatima”. Ndipo ukafuata msuguano mkubwa baina ya Ouattara na Rais wa Bunge, Henri Konan Bedie, kuhusu mrithi wa urais; Bédié alifanikiwa kushika madaraka ya Urais na Ouattara akaamua kujiuzulu nafasi yake ya Waziri Mkuu Desemba 9. Akarudi IMF kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, akishika nafasi hiyo tangu Julai 1, 1994 hadi Julai 31, 1999.

UCHAGUZI WA MWAKA 1995
Kabla ya uchaguzi wa urais wa Oktoba 1995, katika hali iliyoonekana kuwa inachukuliwa kwa nia ya kumzuia Ouattara asigombee urais, Bunge la Taifa la Ivory Coast lilipitisha kanuni ya uchaguzi ambayo ilimzuia mgombea ambaye aidha wazazi wake wana asili ya nje ya Ivory Coast au kama ameishi nje ya Ivory Coast kwa miaka mitano.

Chama cha upinzani cha Rally of the Republican (RDR) kiliundwa kufuatia mgawanyiko ndani ya chama tawala cha Democratic Party of Ivory Coast (PDCI) mwaka 1994, wakitaka Ouattara awe mgombea urais pamoja na kuwepo kanuni hizo za uchaguzi. Mwishoni mwa Juni 1995, Katibu Mkuu wa RDR, Djeni Kobina alikutana na Ouattara, katika wakati ambao, kulingana na Kobina, Ouattara alisema “Niko tayari kujiunga nanyi”. Chama kilimpitisha Ouattara kuwa mgombea wake wa urais Julai 3, 1995 katika mkutano wake wa kwanza wa kawaida. Serikali hata hivyo haikuweza kubadili kanuni za uchaguzi, na Ouattara aliupinga uteuzi. RDR kiliamua kugomea uchaguzi, pamoja na chama cha Ivorian Pupolar Front (FPI) cha Laurent Gbagbo, na kumuacha mgombea wa PDCI, Rais aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo Henri Konan Bedie kushinda ukirahisi.

RAIS WA RDR
Wakati akiwa Naibu Mkurugenzi IMF, Machi 1998 Ouattara alionesha nia yake ya kurudi Ivory Coast kushiriki tena siasa. Baada ya kuondoka IMF Julai 1999, alichaguliwa kuwa Rais wa RDR tarehe 1 Agosti 1999 katika mkutano wa chama hicho, ikiwa ni pamoja na kuchaguliwa kuwa mgombea kwa ajili ya uchaguzi ujao wa rais. Alisema kwamba alikuwa na haki ya kugombea katika uchaguzi, akionesha nyaraka zilizomtambulisha yeye na wazazi wake kuwa walikuwa wazaliwa wa Ivory Coast.

Alituhumiwa kugushi nyaraka hizo, hata hivyo, uchunguzi ulianza. Rais Bedie alimwelezea Ouattara kuwa mtu wa kutoka Burkina Faso na kusema kuwa Houphouet-Boigny "alimhitaji Alassane Ouattara ili kufufua uchumi tu”. Vyeti vya utaifa wa Ouattara vilitolewa mwishoni mwa Septemba 1999, lakini vikabatilishwa na mahakama Oktoba 27. Kibali cha kukamatwa kwa Ouattara kilitolewa Novemba 29, ingawa kwa wakati huo alikuwa nje ya nchi; hata hivyo alisema kuwa angerudi mwisho wa Desemba.

Desemba 24, jeshi likachukua madaraka, na kumfanya Bedie kukimbilia nje. Ouattara alirejea Ivory Coast Desemba 29 baada ya miezi mitatu ya kuishi Ufaransa, akimtumia salamu Bedie kuwa “hayakuwa mapinduzi ya kijeshi”, bali ni “mapinduzi ya wananchi wote wa Ivory Coast”.

Katiba mpya iliidhinishwa kwa kura ya maoni mwezi Julai 2000, ikiweka kipengele chenye utata wa kuzuiliwa kwa mgombea urais labda tu wazazi wake wote wawili wawe na asili ya Ivory Coast, na kumfanya Ouattara kukosa uhalali wa kugombea kwenye uchaguzi wa rais 2000. Hali hii ilipelekea mvita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Ivory Coast, mwaka 2002.

Alipoulizwa kuhusu uraia wa Ouattara, Rais wa Burkina Faso, Kapteni Blaise Compaore alijibu, “Kwetu jambo hili ni rahisi: yeye hatoki Burkina Faso, si kwa kuzaliwa, kwa ndoa, au uraia. Mtu huyu amekuwa Waziri Mkuu wa Ivory Coast.”

Rais Gbagbo alithibitisha tarehe 6 Agosti 2007 kuwa Ouattara anaweza kugombea katika uchaguzi wa rais wa Ivory Coast ujao. Ouattara aliteuliwa na RDR kuwa mgombea urais Februari 1-3, 2008, apia alichaguliwa tena kuwa Rais wa RDR kwa miaka mingine mitano.

UCHAGUZI WA RAIS 2010
Desemba 2, 2010, baada ya mfululizo wa ucheleweshaji wa matokeo, Tume Huru ya Uchaguzi ya Ivory Coast (CEI) ilimtangaza Alassane Ouattara kuwa mshindi wa raundi ya pili ya uchaguzi wa urais nchini humo huku matokeo hayo yakibadilishwa na Baraza la Uchaguzi.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa vyanzo mbalimbali vya habari.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment