Feb 17, 2011

Wasomi wanaposhindwa kusimamia chombo chao!

 Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo 
ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu, 
George Nyatega akizungumza na 
waandishi wa habari (hawapo pichani) 
jijini Dar es Salaam.

 Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), 
Padri Dk. Charles Kitima

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kutangaza kwamba ataunda Tume Maalum ya kuchunguza mfumo mzima wa utoaji mikopo kwa wanafunzi na kuangalia utendaji wa Bodi ya Mikopo ya wanafunzi kwa nia ya kuboresha mfumo uliopo, na kauli ya Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustino (Saut), Padri Dk. Charles Kitima, aliyoitoa alipohojiwa na kituo kimoja cha televisheni hivi karibuni, kuhusu changamoto ya mikopo elimu ya juu ndivyo vitu vilivyonisukuma kuandika makala hii.

Rais aliyasema hayo alipofungua rasmi Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), ambacho ni kikubwa kuliko kingine chochote nchini na ambacho kimejengwa kwa miaka minne ya kipindi cha kwanza cha uongozi wa wake.

Katika kuonesha dhamira yake ambayo bila shaka ni ya dhati, Rais alisema Tume hiyo ifikapo Januari mwakani, itakuwa imeundwa na ataiagiza ikusanye mawazo kwa wamiliki wa vyuo vikuu, wahadhiri na wanafunzi.

Naye Dk. Kitima alisema ili nchi iweze kushindana katika dunia ya sasa, haina budi kuwekeza kwenye elimu ya juu. Na Serikali ina wajibu wa kuwasaidia watoto wa maskini kufikia elimu hiyo, lakini udhaifu uliopo ndani ya wizara na bodi husika ni dhahiri kuwa malengo hayawezi kutimia.

Mimi pia kwa muda mrefu nimekuwa nikijiuliza inakuwaje wasomi wameshindwa kusimamia chombo chao cha elimu ya juu?

Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu imekuwa chanzo cha malalamiko na migomo isiyokwisha kati ya wanafunzi na serikali. Yamekuwepo malalamiko kuwa Bodi haina uwezo wa kutambua hali ya kiuchumi ya Watanzania, na haifanyi tathmini ya kutambua kila Mtanzania mahali alipo.

Kama alivyosema Dk. Kitima, watendaji wabovu wizarani na kwenye bodi ya mikopo ambao wamekuwa wabinafsi wasiojali na kuthamini kuwatumikia Watanzania maskini ndiyo wanaoikwamisha. Matumizi katika mawizara yetu yamekuwa makubwa kuliko tunavyowekeza kwenye elimu. Watu wanaidhinisha mamilioni ya fedha kwa ajili ya chai na vitafunwa maofisini mwao wakati watoto wa maskini katika shule za msingi wanakosa chakula, na madawati.

Kuhusu utaratibu wa Serikali kukusanya madeni ya mikopo, Dk. Kitima alisema urejeshaji unakuwa mdogo kutokana na mazingira ya holela yaliyowekwa.

Madai ya siku nyingi ya wanafunzi kwamba bodi ya mikopo haina uwezo wa kutambua nani ana uwezo na nani hana ulidhihirishwa na barua ya Mkurungezi wa Bodi ya tarehe 5 Januari 2009 yenye Kumb. Na. CB/89/92, kwenda kwa marais wa vyuo vya elimu ya juu Tanzania, ikiomba msaada wa serikali za wanafunzi.

Mkurugenzi alitaka serikali za wanafunzi kuisaidia bodi kujua kama kweli wanafunzi wanaolipiwa asilimia 100, wanastahili kupewa kiwango hicho.

Inasemekana kwamba vigezo vinavyotumika kutoa mikopo havijafanyiwa tafiti kulingana na hali halisi ya maisha ya wananchi. Kuna mkanganyiko kuanzia uanzishwaji, jina lake na matokeo ya kazi yake, na kwamba taasisi hii haijaleta tija. Badala ya kushughulikia mikopo, imekuwa ikisababisha migogoro kati ya wanafunzi na serikali.

Watendaji wa bodi badala ya kushughulikia kero, wamekuwa wabinafsi wakitanguliza maslahi yao kwanza. Bodi hii inatekeleza sera ya ukopeshaji katika elimu ya juu, lakini wakati huohuo inashughulikia sera ya uchangiaji! 
 
Sera ya uchangiaji iliazishwa bila ridhaa ya Watanzania kwani wananchi hawakushirikishwa katika maandalizi ya awali ya kuazisha sera hii. Uchangiaji ni kupeana michango. Kwa kuwa Serikali inakusanya kodi ya wananchi hivyo haina budi kutumia kodi hiyo kuwapa elimu iliyo bora Watanzania na isiyo ya kibaguzi. 
 
Kasoro nyingine ni kwenye utendaji na uwezo wa bodi yenyewe ni kufanya kazi ya kutambua hali ya kiuchumi ya waombaji mikopo. Inaelezwa kwamba Bodi haina uwezo wa kuwatambua wenye uwezo. Inafanya kazi ya kubahatisha katika kutoa viwango vya kuwakopesha wanafunzi visivyojali uwezo wa mwombaji.

Pia inasemwa kuwa Bodi inatumia mifumo miwili; mmoja wa Afrika Kusini ambao haukufanya kazi inavyotakiwa, ndipo ikakimbilia kuagiza mwingine toka Kenya ambao nao haufanyi kazi vizuri.

Mbona wenzetu wa Kenya bodi ya mikopo ya vyuo vikuu inafanya kazi vizuri sana? Hapa kwetu waliuparamia mpango huu bila ya maandalizi ya misingi ili kuwaridhisha Benki ya Dunia (WB) na Mfuko wa fedha duniani (IMF) ‘walipotulazimisha’ kufanyia kazi sera zao za uchumi ambazo ndizo zilizaa uchangiaji (Structural Adjustment Programs).

Pia hivi karibuni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Shukuru Kawambwa, alikaririwa akiiagiza Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu kubadilisha mfumo wa utoaji mikopo, kwani mfumo uliopo hivi sasa unawanufaisha watoto wa vigogo na matajiri kuliko walengwa ambao wanashindwa kupata elimu kutokana na umaskini wa wazazi wao.

Hii ilifuatia malalamiko ya muda mrefu ya wanafunzi wa elimu ya juu. Ukweli ni kwamba wadau wa masuala ya elimu wana dhana kwamba suluhisho la tatizo haliwezi kupatikana pengine kwa sababu hakuna utashi wa kisiasa ama uwezo mdogo wa wahusika waliokabidhiwa kuendesha taasisi hiyo nyeti. 
 
Malalamiko yanatoka kwa wanafunzi wanaotoka katika familia maskini wanaodai kwamba bodi ya mikopo haiwatendei haki kwa vile watoto wa vigogo na matajiri ndio hasa wanapewa mikopo ya asilimia 100.

Naafiki kabisa agizo la Waziri Kawambwa la kuitaka bodi hiyo ya mikopo kubadili mfumo wa utoaji mikopo na linapaswa litekelezwe haraka kwani ndio suluhisho la tatizo la mikopo kwa watoto wanaotoka katika familia masikini.

Pengine ni wakati mwafaka sasa kuanza kufikiria mawazo ya wale wanaopendekeza suala la mikopo kushughulikiwa na taasisi zilizobobea katika masuala ya mikopo kama mabenki ama mifuko mingine ya fedha ambayo, siyo tu inaweza kukopesha, bali pia ina utalaamu wa kusimamia urejeshwahi wa mikopo.

Alamsiki

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment