Feb 17, 2011

Nini hiki Upinzani ndani ya Upinzani!

 Freeman Mbowe, Mkuu wa Kambi ya Upinzani (Chadema)

 Hamad Rashid, aliyekuwa Mkuu wa Kambi ya Upinzani (CUF)

 David Kafulila, Mbunge (NCCR Mageuzi)

BISHOP J. HILUKA
Dar es salaam

KUNA kila dalili kwamba vyama vya upinzani ndani ya bunge vimemeguka baada ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuchukua nafasi zote za juu za uongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni bila kuvihusisha vyama vingine.

Vyama hivyo vya upinzani vimeunda kambi mbili za upinzani katika Bunge la Jamhuri la Muungano baada Chadema kuunda kambi yake ikijitegemea kutokana na kuwa na idadi kubwa ya wabunge huku Chama cha Wananchi (CUF) kikiungana na NCCR-Mageuzi, TLP na UDP kuunda kambi nyingine.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Mambo ya Bunge wa chadema, John Mrema, nafasi ya Kiongozi wa kambi ya upinzani bungeni ni Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe na makamu wake ni Naibu Katibu Mkuu wa chadema na Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe. Nafasi ya Mnadhimu wa Kambi hiyo ni Mbunge wa Singida Kusini, Tundu Lissu.

Kwa mujibu wa kanuni za Bunge, chama kinachofikisha asilimia 12 ya wabunge kina uwezo wa kuunda kambi ya upinzani bungeni. Chadema kimezidi asilimia hizo baada ya kupata wabunge 23 wa kuchaguliwa kwenye majimbo na 23 wa viti maalum. Hata hivyo, imezuka minong’ono kwa baadhi ya vyama vya upinzani vikidai kuwa Chadema kimehodhi kambi yote ya upinzani na kuviacha solemba vyama hivyo.

Awali ilielezwa kuwa CUF kilichokuwa kikishikilia uongozi wa kambi hiyo katika Bunge lililopita kingekiunga mkono Chadema katika kambi ya upinzani na katika nafasi ya mgombea wa nafasi ya Spika ambayo tayari inashikiliwa na Anne Makinda wa CCM.

Badala yake CUF waliamua kukaa kimya, ukimya wao ulitafsiriwa kuwa ulilenga kuiunga mkono CCM badala ya Chadema na ndivyo ilivyojidhihirisha baada Makinda kuzoa kura 265 huku mpinzani wake kutoka Chadema akiambulia kura 53 tu, wakati wabunge wa upinzani wapo kama 86 hivi.

Pamoja na Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid kukanusha madai hayo lakini imezidi kujidhihirisha hata wakati wa kugombea nafasi ya Unaibu spika, ambapo Job Ndugai wa CCM alipata kura 276 kati ya 328 zilizopigwa (asilimia 84,2) na kumwacha Mustafa Akunay wa Chadema akiambulia kura 46 tu (idadi ya wabunge wa Chadema), sawa na asilimia 14, huku kura sita zikiharibika.

Mbunge wa Kigoma Kaskazini ambaye pia ni naibu kiongozi wa upinzani bungeni, Zitto Kabwe alisema kuwa hoja ya kuhodhi kambi ya upinzani na kuifanya kuwa ya Chadema badala ya upinzani wote, siyo jambo la ajabu kwani ni utaratibu unaofanywa hata na nchi nyingine, chama chenye wabunge wengi ndicho kinachotoa waziri mkuu kwa hiyo hata Chadema kwa kuwa kina wabunge wengi kuliko vyama vingine vya upinzani kina haki ya kuunda kambi ya upinzani.

Inanitatiza kidogo, iweje suala la kambi ya upinzani bungeni kuhodhiwa na Chadema liwe 'issue' ya kuwafanya wapinzani wasishirikiane? Au kuna ajenda nyingine zaidi ya hiyo? Mbunge wa Wawi, Ahamed Rashid anaposema kuwa wameamua kuunda kambi yao kwa kushirikiana na NCCR-Mageuzi baada ya Chadema kushindwa kutimiza sharti la kushirikisha vyama vingine kwenye kambi ya upinzani ni jambo la kushangaza kwa kuwa hata wao hawakuvishirikisha vyama vya NCCR-Mageuzi na Chadema walipounda kambi ya upinzani bungeni mwaka 1995.

Inaposemwa kuwa uwepo wa Serikali kivuli ya Chadema bila ushirikiano na CUF ni kitu kibaya, wanasahau kuwa ni CUF hiyo hiyo iliyowahi kuvizunguka NCCR-Mageuzi na Chadema kikaungana na UDP na kuunda Serikali kivuli. Hatukusikia malalamiko kutoka Chadema wala NCCR-Mageuzi. Mimi nadhani kuna viongozi ambao wanataka kuhubiri na kuendeleza tofauti ambazo zinapaswa kupigwa vita, na kinachojitokeza sasa ni Upinzani ndani ya Upinzani!

Mbunge wa Vunjo ambaye pia ni mwenyekiti wa TLP, Augustine Mrema alisema haoni kama kuna tatizo kwa kambi yote ya upinzani kwenda Chadema, na kusisitiza kuwa Chadema wana vijana wengi wazuri ambao wataleta changamoto kubwa Bungeni. Pia sheria za Bunge zinawaruhusu, hivyo hakuna sababu ya kuwalalamikia kwani huwezi kumlazimisha mtu akupende.

kinyang’anyiro cha uspika kilichompa ushindi wa kishindo Anne Makinda wa CCM, kimeonesha kuwepo kwa dalili ya kutokujitosheleza kwa kambi nzima ya upinzani. Wapinzani wanahitaji kuungana ili kuwa na nguvu zaidi kama kweli wana nia ya kuleta changamoto kwa serikali.

Kwa hali hii inanifanya nidhani kuwa pengine baadhi ya wapinzani hawajajitambua na hawajui wanataka nini au wapo kwa makusudi fulani. Ukiangalia hata kwenye majimbo mengi kufuatia uchaguzi wa wabunge utagundua kuwa wapinzani wangeweza kupata wabunge wengi zaidi, pengine ni zaidi ya wabunge 100! Mfano katika mkoa wa Dar e Salaam ambapo wapinzani wameshinda majimbo mawili tu; Kawe na Ubungo, lakini kwa mujibu wa matokeo halisi ni kwamba wameshinda pia majimbo ya Segerea, Kinondoni na Temeke ambako kura za ubunge zilikuwa nyingi kwa wapinzani kuliko kwa CCM.

Hii inadhihirishwa na matokeo kutoka majimbo mbalimbali ambapo wapinzani waliongoza lakini ni CCM iliyoibuka kidedea.

Ni wakati sasa wa watu wanaojiita wapinzani kuamua kuwa wapinzani au kujiunga na CCM.

No comments:

Post a Comment