Feb 17, 2011

OMAR AL-BASHIR: Kuwa kikwazo au kuruhusu uundwaji wa nchi mpya?

 Omar Hassan al-Bashir

Khartoum
SUDAN

BARAZA la Usalama la Umoja wa Mataifa limeongeza shinikizo kwa Sudan Kaskazini na Kusini kuhakikisha kuwa kura ya maoni inayotarajiwa na wengi kwamba itapelekea kugawanywa kwa taifa hilo ambalo ni kubwa zaidi barani Afrika inafanyika kwa njia ya amani mwezi ujao.

Baraza hilo la usalama limetaka pande zote mbili za Kaskazini na Kusini kutuliza hali ya wasiwasi inayozidi kuongezeka na kuafiki mkataba uliowekwa kuhusu kura tofauti ya maamuzi juu ya mustakabali wa jimbo lenye utajiri mkubwa wa mafuta la Abyei.

Pande zote mbili za Kaskazini na Kusini zinadai umiliki wa jimbo hilo. Umoja wa Mataifa pia umeelezea wasiwasi wake kuhusiana na matukio kadhaa ya kijeshi katika siku za hivi karibuni ambayo yamezidisha hali ya wasiwasi. Kura hiyo itakayofanyika Januari 9 inakuja baada ya mkataba wa amani wa mwaka 2005 ambao ulimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miongo miwili kati ya Kaskazini na Kusini.

Rais wa Sudan Omar Hasan al-Bashir amesema kuwa nchi yake haitarudi tena vitani licha ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Kaskazini na Kusini wakati kura ya maoni kuhusu uhuru wa Kusini ikikaribia.

Vyombo vya habari vya serikali ya Sudan vilimkariri al-Bashir akisema kwamba serikali yake inafanya kazi kuweka utulivu kote nchini humo. Kusini na kaskazini wamekuwa wakilaumiana kwa kuweka vikosi kwenye mpaka wao kabla ya kura ya maoni.

Urais wa al-Bashir?

Omar Hassan al-Bashir aliyezaliwa Januari 1944 ni Rais wa Sudan baada ya kushinda urais katika uchaguzi wa kitaifa mwaka 2010 ambao ni uchaguzi wa kwanza wa vyama vingi baada ya miaka 10.

Amekuwa rais tangu mwaka 1993. Historia inaonesha kuwa al-Bashir aliingia madarakani mwaka 1989 akiwa na cheo cha Brigedia katika jeshi la Sudan, aliongoza kundi la maafisa katika mapinduzi ya kijeshi yasiyokuwa ya umwagaji damu yaliyoiondoa madarakani serikali ya Waziri Mkuu Sadiq al-Mahdi mwaka 1989. Bashir aliongoza nchi kama mwenyekiti wa kamati ya wanajeshi na baadaye waziri mkuu hadi alipojipa cheo cha rais mwaka 1993.

Baada ya kushika uongozi alishirikiana na mwanasiasa na kiongozi wa Kiislamu, Hassan al-Turabi akatangaza sheria zilizoiweka nchi chini ya muundo wa shari'a ya Kiislamu. Aliwakandamiza vikali wapinzani, mwishowe hata mshauri wake al-Turabi alionja joto ya jiwe.

Mwaka 2004 al-Bashir alikubali mkataba wa amani uliomaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe na kupelekea kuipa Sudan Kusini haki ya kujitawala. Lakini vita vingine vya ndani vilianza katika eneo la Darfur (Sudan Magharibi). Kutokana na mauaji mengi na matendo ya kinyama dhidi ya raia, al-Bashir anakabiliwa na mashtaka mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai kama mkosaji wa jinai dhidi ya binadamu.

Tangu al-Bashir aingie madarakani, hata hivyo, kumekuwa na vurugu na mgogoro wa Darfur ambao umesababisha idadi ya vifo kati ya 200,000 na 400,000. Wakati wa urais wake, kumekuwa na vurugu kadhaa na mapambano baina ya wanamgambo wa Janjaweed na vikundi vya waasi vya Sudan Liberation Army (SLA) na Justice and Equality Movement (JEM) katika vita vya msituni kwenye eneo la Darfur.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilisababisha zaidi ya watu milioni 2.5 kupoteza makazi yao, na hata mahusiano ya kidiplomasia kati ya Sudan na nchi jirani ya Chad kuwa katika mgogoro. Al-Bashir ni mtu aliyezua utata sio nchini Sudan tu bali duniani kote.

Kushitakiwa

Mwezi Julai 2008, mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC), Luis Moreno Ocampo, alimtuhumu al-Bashir kuhusu mauaji ya kimbari, ukatili dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita katika eneo la Darfur.

Mahakama ilitoa hati ya kukamatwa kwa al-Bashir tarehe 4 Machi 2009 kwa makosa ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu, lakini ikasemwa kuwa hakukuwa na ushahidi wa kutosha kumhusisha na mashitaka ya mauaji ya kimbari. Hata hivyo tarehe 12 Julai 2010, baada ya muda mrefu wa rufaa ya mwendesha mashtaka, Mahakama ikasema kwamba kuna ushahidi wa kutosha kwa ajili ya mashtaka ya mauaji ya kimbari na kutoa hati ya pili yenye makosa matatu tofauti.

Al-Bashir ni mkuu wa nchi wa kwanza aliyepo madarakani kukabiliwa na mashitaka katika mahakama ya ICC na rais wa kwanza kushtakiwa kwa mauaji ya kimbari. Uamuzi huo wa mahakama umepingwa na Umoja wa Afrika, Umoja wa Mataifa ya Kiarabu, na serikali ya Urusi na Jamhuri ya Watu wa China. Mtaalam mmoja ametoa wito kwa mahakama hiyo kuahirisha kibali cha kukamatwa kwa Al-Bashir.

Historia yake

Al-Bashir alizaliwa katika kijiji cha Hosh Bannaga, Kaskazini ya mji mkuu, Khartoum. Anatokea katika ukoo wa Al-Bedairya Al-Dahmashya, wa kabila kubwa la ja'alin lililopo Kaskazini ya Sudan, sehemu ya Ufalme wa Misri na Sudan. Alipata elimu yake ya msingi huko, familia yake baadaye ilihamia Khartoum ambako alimalizia elimu ya sekondari.

Al-Bashir kamuoa binamu yake, Fatima Khalid. Pia ana mke wa pili aitwaye Widad Babiker Omer, ambaye ana watoto kadhaa kutoka kwa mume wake wa kwanza, Ibrahim Shamsaddin, aliyekuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi (Revolutionary Command Council for National Salvation) aliyefariki katika ajali ya helikopta.

Al-Bashir hajabahatika kupata watoto wa kwake mwenyewe. Alijiunga na Jeshi la Sudan mwaka 1960. Al-Bashir alisoma Chuo cha Kijeshi Misri kilichopo Cairo na pia alifuzu kutoka Chuo cha Kijeshi cha Sudan mjini Khartoum mwaka 1966. Baadaye, al-Bashir alilitumikia Jeshi la Misri wakati wa Vita ya Oktoba (ya 1973) dhidi ya Israel.

Mapema miaka ya 1990, utawala wa al-Bashir uliamua kuelea kwenye sarafu mpya iitwayo Sudan Dinar kuchukua nafasi ya Sudan Pound iliyokuwa imepoteza karibu asilimia 90 ya thamani yake katika miaka ya 1980.

Baadaye alichaguliwa kuwa rais (kwa muda wa miaka mitano) mwaka 1996 katika uchaguzi wa kitaifa, ambapo alikuwa mgombea pekee kufuatia sheria zinazoendesha uchaguzi, na Hassan al-Turabi alichaguliwa katika Bunge la Taifa ambako alikuwa spika wa Bunge “miaka ya 1990.”

Mwaka 1998, al-Bashir na Kamati ya Rais waliwekeza nguvu katika katiba mpya, isiyoruhusu wanasiasa kupingana na chama cha National Congress Party cha al-Bashir na wafuasi wake, ingawa makundi haya yalishindwa kupata huduma yoyote muhimu ya nguvu ya kiserikali mpaka pale ulipozuka mgogoro wa Darfur.

Desemba 12, 1999, al-Bashir alituma askari na mizinga dhidi ya bunge na kumuondosha madarakani Hassan al-Turabi, spika wa bunge. Hata hivyo, licha ya kupata upinzani wa kimataifa kuhusu migogoro ya ndani, Omar al-Bashir imeweza kufikia ukuaji wa uchumi nchini Sudan. Hii ni kwa sababu ya uchimbaji na biashara ya mafuta kutoka Sudan Kusini, pamoja na ushiriki wa makampuni ya Urusi na China.

Mvutano na al-Turabi

Katikati ya miaka ya 1990, uhasama kati ya al-Bashir na al-Turabi ulianza, hasa kutokana na al-Turabi kuwa na mahusiano na kikundi cha Islam fundamentalist, pamoja na kukiruhusu kufanya kazi nje ya Sudan, hata wakati mwingine binafsi alimkaribisha Osama Bin Laden nchini humo.

Marekani imeiweka Sudan kwenye kundi la nchi zinazofadhili ugaidi tangu mwaka 1993, hasa kutokana na al-Bashir na Hassan al-Turabi kunyakua mamlaka kamili mapema miaka ya 1990. Makampuni ya Marekani yalizuiliwa kufanya biashara nchini Sudan tangu mwaka 1997. Mwaka 1998, kiwanda cha dawa cha Al-shifa mjini Khartoum kiliharibiwa na ya Marekani kwa madai ya uzalishaji wake wa silaha za kemikali na uhusiano wake na al-Qaeda.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vilizuka kati ya Kaskazini na Kusini mwa nchi kwa zaidi ya miaka 19 kati ya Waarabu wa Kaskazini na makabila na asili yaliyopo Kusini, vita hiyo ikapelekea mapambano kati ya Jeshi la Ukombozi wa Watu Sudan Kusini (SPLA) na serikali ya al-Bashir.

Vita ilisababisha mamilioni ya watu wa Kusini kupoteza makazi yao, njaa, na kunyimwa elimu na huduma za afya, pamoja na majeruhi karibu milioni mbili. Kwa sababu ya hatua hizi, vikwazo mbalimbali vya kimataifa viliwekwa dhidi ya Sudan.

Shinikizo la kimataifa lilizidi mwaka 2001, hata hivyo, na viongozi viongozi wa Umoja wa Mataifa walitoa wito kwa al-Bashir kufanya jitihada za kumaliza mgogoro na kuruhusu misaada ya kibinadamu na wafanyakazi wa kimataifa kutoa msaada kusini mwa Sudan.

Amani ilipatikana baada ya kusainiwa rasmi kwa Mkataba wa Amani wa Nairobi kwa pande zote mbili, Januari 9, 2005, kuipa Sudan Kusini uhuru wa miaka sita, na kufuatiwa na kura ya maoni juu ya uhuru.

Makala hii imeandaliwa na BISHOP J. HILUKA kwa msaada wa mashirika ya habari ya kimataifa.

SOURCE: KULIKONI

No comments:

Post a Comment