Feb 17, 2011

Tumekataa kona tukakubali penati!

Jengo la Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
 
Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja
 
Mitambo ya Richmond/ Dowans
 
BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema hivi karibuni alikaririwa akisema kwamba serikali inatakiwa kuilipa kampuni ya kufua umeme ya Dowans Tanzania Ltd fidia ya bilioni 185/-; kwamba mjadala kuhusu Dowans umefungwa rasmi na kwamba hakuna mpango wa serikali kukata rufaa.

Kwa wengi wetu, kauli hiyo imekuwa tata na yenye kutiliwa shaka kidogo. Uamuzi wa kulipa Dowans mabilioni hayo ambayo umewaacha midomo wazi Watanzania ulitolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC), eti kwa kukiuka masharti ya mkataba.

Mwanasheria Mkuu aliyasema hayo alipofanya mahojiano na gazeti moja litolewalo kila siku katika viwanja vya Ikulu jijini Dar es Salaam mara baada ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman.

Kwa hukumu hii siwezi kusema tutalivalia njuga suala la Dowans maana kwa hukumu hii hata ukiivalia hiyo njuga itafikia mahala njuga hizo zitakatika tu,” alinukuliwa Jaji Werema akisema. 

Hukumu ya ICC ilitolewa Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti wake, Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali na Jonathan Parker. 

Baadhi ya wasomaji walinipigia simu na wengine kuniandikia ujumbe mfupi wakitaka kujua mawazo yangu kuhusu kauli ya Mwanasheria Mkuu kusema kuwa mjadala wa Dowans umefungwa na kilichobaki ni kulipa deni ana maslahi gani na kampuni hiyo? Wengine walihoji anamuogopa nani? Wapo pia waliotaka kujua katumwa nani? 

Watanzania kwa sasa wanahitaji kujua nani mmiliki wa kampuni ya Dowans Tanzania Ltd na ikiwezekana serikali ikate rufaa.

Kitendo cha serikali kukubali kuilipa kampuni ya Dowans ‘kikondoo’ namna hii kinaacha maswali mengi kuliko majibu, na kinakera kweli kwani kinamaanisha kuwa serikali itatumia fedha za Watanzania kuilipa kampuni hiyo, fedha ambazo zingesaidia kuboresha maisha yao.  

Kuufunga mjadala huu na kuamua kulipa bilioni 185/- bila kuwaeleza Watanzania (ambao ndiyo wenye pesa zao zinazotumika kuilipa Dowans) uhalali wa kulipa deni hilo si haki hata kidogo na historia lazima iwahukumu. 

Ikumbukwe kwamba Watanzania walishaelezwa kwamba mkataba huo ulikuwa batili kwa hiyo wanahitaji maelezo ya kina, wanataka kujua mwenendo wa kesi ulivyokuwa, ofisi ya mwanasheria ilipeleka vielelezo gani na wamjue mchawi aliyesababisha tukashindwa kesi hiyo.

Haiingii akilini kuwaambia wananchi hatuna mpango wa kukata rufaa bila kuwaambia ugumu uko wapi. 

Kampuni ya Dowans ilipata kazi hiyo baada ya kurithi mkataba wa kufua umeme kutoka kwa dada yake – Richmond Development Company (LLC), ambayo ilibainika baadaye kuwa haikuwa na hadhi, sifa wala uwezo wa kupewa kazi iliyoomba. Mbaya zaidi mkataba huo uliingiwa kinyemela wakati nchi ikiwa haina haja tena na umeme wa dharura. 

Hivi Serikali inapata kigugumizi gani kumtaja mmiliki wa Dowans ni nani, kwa vyovyote inamjua kwa sababu kama ni kulipa inataka kumlipa nani? 

Je, serikali inaposhikwa kigugumizi kumtaja mmiliki, ikashindwa kesi hii bila shaka kwa njama na kukataa kukata rufaa, hivi sisi wananchi wanataka tueleweje? Kwa akili ya kawaida tu unapata jibu kwamba wakubwa wana mkono wao na ndio wanaojilipa hizo pesa! 

Na je, hao walioingia mkataba huo ambao kwa akili ya kawaida ulikuwa feki wao wamechukuliwa hatua gani? Tungesikia nchi inaingia hasara lakini imewashikisha adabu walioifikisha hapo pengine maumivu yangepungua.

Niliwahi kuandika makala moja huko nyuma kuwa nchi yetu imekuwa haithamini kabisa taaluma kwa kuwa kumekuwepo na madai ya maamuzi mengi kufanywa kisiasa zaidi kuliko utaalamu wala bila kujali athari zake za baadaye. Mfano ni wanasiasa kusaini mikataba ambayo imekuwa ikituingiza kwenye matatizo makubwa bila kuwashirikisha wanasheria wa wizara husika.

Wanasiasa lazima wawajibike katika hili la mjadala wa Kampuni ya Dowans kwa kuwa siasa ziliingia kuanzia kutolewa kwa zabuni hadi kuvunjwa kwa mkataba. Sakata la Dowans lilijaa siasa “mwanzo-mwisho” na ndiyo lililotufikisha hapa. 

Inasemekana kuwa taarifa zinazotolewa kuhusu Dowans ni za kichochezi kwani zinakuza mjadala wa Dowans kuishinda serikali na kuficha ukweli wa serikali kuishinda kampuni ya Richmond. 

Na kwamba ushindi wa Dowans hauna uhusiano na kuvunjwa kwa mkataba, kwani wao ndio waliuvunja kwa kisingizio kwamba mazingira ya kazi Tanzania si mazuri kwao, lakini walikuwa na makubaliano fulani na Tanesco ambayo walitaka yatimizwe.

Hukumu ya Dowans dhidi ya Tanesco ni kielelezo cha wazi kwamba, masuala yanayohusu mikataba ya kimataifa kama hayo yanapaswa kushughulikiwa kwa umakini mkubwa ili kuepuka gharama za namna hiyo.

Hivi tunasema nini kama wawakilishi wa umma, yaani wabunge wangeshirikishwa katika mkataba huo? Kwa kifupi mambo kama haya ndio yanaongeza ile nia ya sasa ya Watanzania ya kudai katiba mpya ili mikataba inayohusu mustakabali wa maisha yao na rasilimali zao ipitiwe na wawakilishi wao, wabunge. Mikataba kama hii isiendelee kuwa siri ya watu wachache huku wahusika wakiwa hawawajibishwi ipasavyo pale wanapoharibu mambo.

Mwaka 2006, serikali kupitia Tanesco iliingia mkataba uliodaiwa kuwa na harufu ya rushwa kwa ajili ya kuzalisha megawati 100 za umeme na kampuni ya Richmond Development LLC ili kuiokoa nchi na giza kwa kukosa umeme kulikotokana na ukame.

Mjadala wa mitambo ya Dowans, uliwahi kuligawa taifa kwa kipindi kirefu mwaka 2008 baada ya Kamati teule ya Bunge chini ya Uenyekiti wa Dk. Harrison Mwakyembe, kutoa taarifa ya kuchunguza uhalali wa kampuni ya Richmond na mkataba baina yake na serikali.

Kutokana na taarifa iliyowasilishwa bungeni mwezi Februari mwaka 2008, aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alijiuzulu ikiwa ni ishara ya kuwajibika kama kiongozi mkuu wa ofisi yake iliyodaiwa kushiriki katika kuiwezesha Richmond kushinda zabuni ya kuzalisha umeme wa dharura. 

Wakati wa mjadala huo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Tanesco, Dk. Idris Rashid, aliishauri serikali kuinunua mitambo hiyo jambo lililoungwa mkono na Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni wa sasa, Zitto Kabwe, ingawa alipingwa vikali na wabunge wenzake wa Chadema na watu wengine ndani na nje ya chama chake.

Hata hivyo, Bunge lilikataa kupitisha pendekezo la ununuzi wa mitambo ya Dowans likisema kufanya hivyo ni kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma ya mwaka 2004 inayokataza serikali au taasisi zake kununua mitumba.

Ukiangalia sakata zima, wengi wana wasiwasi kwamba bado Watanzania wanachezwa sherehe. Hata mgao huu wa umeme unaoendelea, upo wasiwasi kwamba unatengenezwa na hao hao mafisadi.

Lakini ninachotaka kumalizia hapa ni kwamba, hakuna siri ya watu wawili duniani. Ipo siku siri hizi zitakuwa hadharani kwa sababu ushindi wa Dowans katika kesi hii unatia shaka na UMEKATAA KABISA KUINGIA KWENYE VICHWA VYA WATU.

SOURCE: KULIKONI 

No comments:

Post a Comment