May 4, 2011

CCM kujivua gamba sawa, lakini...

 Mwenyekiti wa CCM taifa, Jakaya Mrisho Kikwete

 Katibu Mkuu wa CCM, Wilson Mukama

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

UPEPO wa mabadiliko makubwa ya uongozi ndani ya Chama Cha Mapinduzi yaliyotokana na msukumo wa ndani na nje ya chama hicho, ulianza kuvuma na kuonekana wakati wa sherehe za miaka 34 ya CCM, pale Rais Jakaya Kikwete aliposema chama hicho kikongwe kinalazimika kuachana na wanachama na viongozi ambao ni mzigo. Mwenyekiti huyo alifananisha hatua ya kufanya mabadiliko ya kiuongozi sawa na nyoka ambaye huwa anajivua gamba linapochakaa.

Kwa upande wa nje, upepo mbaya wa kisiasa dhidi ya chama uliovuma na unaoendelea kuvuma umechochewa na kambi ya upinzani, hususan Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) huku kwa upande wa ndani, kwa muda mrefu wapo wana-CCM ambao wamekuwa hawaridhiki na mambo yanavyoenda ndani ya chama hicho, hususan kuonekana kinawakumbatia matajiri na wote wanaolalamikiwa kwa ufisadi unaoitafuna nchi.
Taarifa za CCM kujivua gamba zimeendelea kutawala vyombo vya habari hapa nchini hata sasa, na Jumatatu wiki hii Katibu Mkuu wa chama hicho, Wilson Mukama, katika mkutano wake na watendaji na wahariri wa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam (ambapo gazeti hili halikualikwa kwa sababu ambazo hazifahamiki), alisema kuwa kinachofanyika sasa katika chama hicho ni mageuzi makubwa ya kukisafisha na kwamba si ajali.
Mukama pia alisisitiza kwamba, CCM itaendelea kupambana na ufisadi huku akibeza kauli za baadhi ya wanasiasa hasa wa upinzani kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaelekea kufa.
“Kilichofanyika ni kwa utashi, siyo ajali. Ulifanyika uchambuzi uliojengwa katika misingi ya kukifanya chama kiendelee kuongoza,” alisema Mukama katika mkutano wake huo wa kwanza mkubwa na vyombo vya habari tangu ashike wadhifa wa Katibu Mkuu wa CCM mapema Aprili.
Mukama aliongeza kuwa vikao vya chama hicho havikukurupuka kufanya maamuzi ikiwemo kujiuzulu kwa Kamati Kuu na Sekretarieti, bali vilifanya hivyo kwa nia ya kuruhusu mageuzi hayo ambayo alisema maamuzi magumu zaidi yatarajiwe kuelekea mageuzi hayo.
Baadhi ya wasomaji walionipigia simu wamedai kuwa mabadiliko hayo ndani ya Kamati Kuu na Sekretarieti, inachofanya CCM ni 'cosmetic' tu, yaani wanajaribu kuvuta muda yasiwakute yaliyomkuta Rais Hosni Mubarak wa Misri na timu yake...
Msomaji mmoja alisema kuwa kila anapofikiria suala la CCM kujivua gamba kwa maana ya kupambana na ufisadi ndani ya chama hicho haimuingii akilini, hasa kujichanganya kwa CCM kuwaambia wezi waondoke bila kuwachukulia hatua za kisheria katika nchi inayoamini katika utawala wa sheria.
Msomaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Dk. Fikiri wa Singida alisema kuwa tatizo kubwa lililopo ni kuwa wanaotakiwa kuwawajibisha wenzao wao vilevile si wasafi. Akaongeza kuwa siku akisikia wale wote waliofanya ubadhilifu kupitia EPA, Meremeta, Kagoda, Richmond/Dowans, IPTL, Rites, ATCL, Uuzwaji wa mali za umma n.k, wameshitakiwa ndipo ataamini kwamba CCM ilidhamiri kufanya mabadiliko kwa manufaa ya chama na nchi lakini kwa sasa anahisi ni usanii mtupu.
Binafsi naelewa kabisa kuwa magamba si viongozi hao watatu tu wanaotajwa, ni wengi mno na majina yao yanatisha. Sidhani kama kuna ubishi kuwa imefikia mahali taratibu za kugombea kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (Nec) zinagubikwa na kila aina ya rushwa na ufisadi, kiasi kwamba watu masikini wameshajitenga na nafasi hizo kwa kuona haziwahusu, bila kujali kama wana sifa ama la. Kama alivyowahi kusema Mwalimu Julius Nyerere, zama za utawala wake utajiri wa mtu ulikuwa sababu ya kwanza ya kumkosesha fursa ya uongozi lakini hatua iliyofikiwa katika CCM ni kwamba umasikini ni kigezo cha kutochaguliwa. Elimu, uchapakazi na uadilifu si kitu tena. Swali ni hili: Je, ni ukarabati wa aina gani utakaoipendezesha nyumba hiyo (CCM) bila kuvunja nyumba nzima?
Hoja yangu kubwa ya leo inajikita katika jambo moja tu, kwamba kama kweli CCM wameng'amua kuwa chama hicho kiligubikwa na ufisadi kwa baadhi ya watendaji wake, tena waliokuwa katika nafasi nyeti kiuongozi hawakupaswa kuishia kujisifia kujivua gamba tu, walipaswa waende mbali zaidi.
Naamini kabisa kuwa mabadiliko hayo ya kiuongozi ndani ya CCM ni baada ya tuhuma nzito za ubadhirifu wa Meremeta, Kagoda, matumizi holela ya mali za umma na mikataba mibovu inayoendelea kuwatesa Watanzania hadi sasa.
Kujivua gamba kwa kujifananisha na nyoka, ni sawa na kuwaambia Watanzania kuwa kumbe wameshang'atwa sana na mikataba mibovu ya IPTL, Deep Green, Meremeta, Richmond/Dowans, EPA na mingine kibao, hivyo kuishia kujisifia kuwatosa mafisadi pekee hakutoshi. Kinachotakiwa ni CCM kuwashukia kama mwewe anavyoshukia kifaranga cha kuku watuhumiwa wote wa ufisadi, kuwafilisi mali zote walizopata kwa njia ya kifisadi na kuwaomba radhi Watanzania.
Kuwaomba radhi Watanzania hakumaanishi kuwa ni CCM ndiyo fisadi, la hasha bali watendaji wake walioaminiwa sana na chama na kupewa nafasi nyeti ndani ya chama na hata serikalini ambao chama kimekiri kuwa wamekipaka matope. Nawashauri wafuate mfano wa aliyekuwa Mkuu wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Yohane Paulo II aliyeomba msamaha mwaka 2000 kwa niaba ya Kanisa Katoliki kwa makosa yaliyofanywa miaka mingi sana iliyopita na watendaji wa kanisa hilo.
Kufuatia hali hiyo ya Papa kuomba msamaha, utakatifu wa Kanisa ulizidi kung'aa... Ilikuwa ishara rahisi na wakati huohuo Yohane Paulo II alitaka kutoa maono katika ulimwengu na kurejerea historia, lakini bila kuelekeza nguvu katika maelezo nje ya heshima ya historia. Alisema kuwa Kanisa silo lililotenda dhambi, waliotenda dhambi ni Wakristo na walifanya hivyo dhidi ya Kanisa alilolifananisha na Bibi Harusi wa Kristo.
Kitendo hicho kilitafsiriwa kama kitu cha ajabu na cha kukumbukwa kwa kanisa lililojichukulia kuwa takatifu, na kuwaamini mapapa wake kuwa wanaongozwa na mkono wa Mungu, lingeweza kukiri na kuomba msamaha kwa makosa ya zamani yaliyofanywa na mapapa hao.
Ili CCM nao watakasike na waaminike tena kwenye jamii wanapaswa kufuata mfano wa Papa Yohane Paulo wa Pili na kuacha propaganda.

No comments:

Post a Comment