May 4, 2011

MARTHA KARUA: Mwanamke jasiri aliyejitosa kutangaza rasmi nia ya kugombea urais wa Kenya

 Martha Karua

NAIROBI
Kenya

MWENYEKITI wa chama cha Narc, Martha Wangari Karua, ametangaza kugombea urais wa Kenya unaotarajiwakuifanyika mwakani.
Mbali na urais, mwanamke huyo pia amepania kutetea nafasi yake ya ubunge kupitia Jimbo la Guchugu. Karua alitangaza uamuzi huo Jumapili iliyopita alipokuwa kwenye ibada katika kanisa la Anglikana la Ngariama jimboni kwake.
Mnakumbuka kesi ya Spika Kenneth Marende, alipochaguliwa nafasi hiyo ilimlazimu kuachia ubunge na kufanyika uchaguzi mdogo na hiyo itatokea kwangu,” alisema.
Kaka zangu waliotangaza nia katika Jimbo la Gichugu wawe tayari kushindana mwaka 2012, tusubiri kuona sanduku la kura litakavyoonesha juu yangu na Uhuru Kenyatta na uamuzi wowote watakaoufanya Wakenya nitauheshimu.” Martha Karua pia aliahidi kufanya kazi kwa ajili ya kuboresha afya na maisha ya Wakenya.

Historia yake:
Martha Karua alizaliwa mnamo 22 Septemba, 1957, ni mwanasiasa wa Kenya, akiwa Mbunge kupitia Jimbo la Gichugu na Mtetezi wa Mahakama Kuu ya Kenya. Alikuwa Waziri wa Sheria hadi alipojiuzulu kutoka nafasi hiyo mwezi Aprili 2009.
Miaka ya Mwanzo:
Karua alizaliwa katika Wilaya ya Kirinyaga, Mkoa wa Kati wa Kenya; akiwa ni mzaliwa wa pili katika familia yao ya watoto wanane, wasichana wanne na wavulana wanne. Alisomea sheria katika Chuo Kikuu cha Nairobi kuanzia mwaka 1977 hadi mwaka 1980.

Kati ya mwaka 1980 na 1981 alijiunga na Kenya School of Law kwa kozi ya sheria ya waliohitimu ambayo ni kozi inayofanywa kabla ya kujiunga na Shirika la Wanasheria la Kenya na kupewa leseni ya kufanya mazoezi ya sheria nchini humo. Kisha aliingia katika huduma ya umma, na kufanya kazi kama Hakimu kuanzia mwaka 1981 hadi 1987. Toka mwaka 1987 hadi 2002 alikuwa anafanya kazi kibinafsi kama mtetezi.

Mtaalamu wa kazi, 1981 – 2002:
Alifanya kazi katika mahakama kama Hakimu wa Wilaya na alipanda cheo kuwa Hakimu Mkuu Mkazi wakati akiondoka mwaka wa 1987. Katika kipindi hicho, alikuwa anasimamia Mahakama ya Sheria ya Makadara kuanzia mwaka 1984 hadi 1985 na Mahakama ya Sheria ya Kibera kuanzia mwaka 1986 hadi mwaka 1987 wakati alipojiondoa ili kuanza kampuni yake ya binafsi.
Mnamo mwaka 1987 Martha Karua alianzisha kampuni yake iliyoitwa Martha Karua & Co Advocates ambayo aliiendesha hadi mwaka 2002. Wakati alipokuwa katika shughuli hizo, Karua alionesha kesi nyingi za pro bono, mashuhuri kati ya kesi hizi ilikuwa kesi ya uhaini ya Koigi Wamwere na wakati akimwakilisha marehemu Mirugi Kariuki.

Alichangia kwa kiasi kubwa katika maendeleo ya familia kupitia sheria na hasa mgawanyo wa mali ya kuozwa na vilevile sheria ya kikatiba na utawala.

Wasifu wa kisiasa, 1990 – 2002:
Karua alikuwa mwanachama wa harakati za kisiasa za upinzani zilizofanikiwa kuanzisha tena demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya mapema miaka ya 1990. Kenya wakati huo ilikuwa chini ya utawala wa kimabavu wa Kenya African National Union (Kanu), chama pekee kilichotambuliwa kisheria nchini Kenya na ambacho kilikuwa kinaongozwa na aliyekuwa rais wakati huo, Daniel arap Moi.
Martha Karua alijiunga na chama cha Kenneth Matiba cha Ford-Asili lakini alipoteza nafasi ya uteuzi kwa kushindwa na tajiri na mshawishi Mkuu wa zamani wa Utumishi wa Umma Geoffrey Kareithi. Kisha alipewa nafasi na aliungwa mkono na wazee wa Democratic Party of Kenya (DP) ambao walitaka kuvunjwa kwa upinzani wa Kareithi - Nahashon Njuno.
Karua alishinda uchaguzi mkuu wa mwaka 1992 na akawa Mbunge wa Gichugu na mwanamke wa kwanza mwanasheria kuchaguliwa kuwa Mbunge. Pia aliteuliwa kama katibu wa chama wa masuala ya kisheria kati ya mwaka 1992 na 1997.
Mwaka 1998, Karua alikataa nafasi ya Waziri Kivuli wa Utamaduni na Huduma za Jamii ambayo ilikuwa na mgogoro na nafasi yake ya Katibu wa Taifa wa mambo ya Katiba (ofisi aliyochaguliwa) iliyomfanya kuwa msemaji rasmi wa masuala ya kisheria wa chama. Aliamua kujiuzulu kutoka nafasi yake kama Katibu Mkuu wa Taifa.
Mwaka 2001, wakati wa kupitia tena Mswada ya Katiba uliopelekwa bungeni, upinzani mzima isipokuwa Karua uliondoka Bungeni. Mswada ulikuwa umekataliwa na upinzani na vilevile Mashirika ya Kiraia (Civil Society) lakini Karua alikuwa na mtazamo tofauti kwamba kama wawakilishi waliochaguliwa, badala ya kuondoka, itakuwa busara zaidi kubaki Bungeni na kuweka kupinga kwao katika rekodi. Basi alichagua kubaki Bungeni na kupinga kwake Mswada kulirekodiwa kihalali katika Hansard.
Baadaye alikuwa miongoni mwa wale ambao walianzisha muungano wa kisiasa, Narc, ambayo ilishinda Uchaguzi Mkuu wa 2003 nchini Kenya na kumaliza utawala wa Kanu wa karibu miongo minne katika siasa za Kenya.

2003 hadi Machi 2009:
Karua bado ni mwanasiasa mashuhuri wa kitaifa. Hadi Aprili 6, 2009 alikuwa Waziri wa Sheria na Katiba. Hapo awali aliwahi kuwa Waziri wa Usimamizi wa rasilimali za Maji na Maendeleo, na alikuwa chachu ya utekelezaji wa Sheria ya Maji ya mwaka 2002, ambayo imeharakisha kasi ya mageuzi ya maji na utoaji wa huduma nchini Kenya.
Karua alibakia katika nafasi ya Waziri wa Katiba na Sheria katika Baraza la Mawaziri lililoteuliwa na Kibaki mnamo Januari 8, 2008, kufuatia utata wa uchaguzi wa Disemba mwaka 2007. Katika mahojiano na BBC HARDtalk mnamo Januari 2008, Karua alisema, kuhusu mgogoro na vurugu zilizotokea baada ya matokeo ya uchaguzi, kwamba ingawa serikali ilitarajia kuwa chama cha upinzani, Orange Democratic Movement (ODM) cha Raila Odinga kinaweza kuwa "kinapanga mgogoro iwapo kitapoteza ", lakini alishangazwa na “ukubwa” wa ghasia na aliuita “utakaso wa kikabila”.
Alipoambiwa kufafanua, Karua alisema kwamba alikuwa anasema "kinamna" kwamba ODM ilipanga utakaso huo wa kikabila. Odinga hatimaye aliyaita mashtaka ya Karua "outrageous". Karua aliiongoza timu ya serikali katika mazungumzo na upinzani kuhusu mgogoro wa kisiasa ulioibuka baada ya uchaguzi.
Mgogoro wa kisiasa hatimaye ulisababisha kutiwa saini kwa mkataba wa kugawana madaraka kati ya Kibaki na Odinga. Katika Baraza la Mawaziri la muungano unaotawala lililotangazwa mnamo April 13, 2008, Karua alibaki katika nafasi yake kama Waziri wa Haki na Mambo ya Katiba.
Alipewa cheo kama mwenyekiti wa kitaifa wa chama cha kisiasa cha Narc-Kenya tarehe 15 Novemba, 2008. Hakukuwa na ushindani wowote wakati wa uchaguzi wa wajumbe wa kitaifa wa chama hicho uliofanyika Bomas of Kenya, jijini Nairobi kwani viongozi wote pamoja na Bibi Karua walibaki katika nyazifa zao. Baada ya kupata nafasi ya mwenyekiti alitangaza kuwa atagombea kiti cha urais katika uchaguzi mkuu wa 2012 nchini Kenya.
Martha Karua alijiuzulu nafasi ya Waziri wa Katiba na Sheria Aprili 6, 2009, akidai kusumbuliwa katika kutoa majukumu yake. Mfano wazi wa kusumbuliwa kwake ulikuwa wakati Rais Mwai Kibaki alipowateua Majaji bila ushauri wake siku chache kabla hajajiuzulu. Alikuwa Waziri wa kwanza kujiuzulu kwa hiari tangu mwaka wa 2003.

Mwanamke Shuja:
Wakati mmoja katika Wilaya yake ya Kirinyaga, Karua aliondoka wakati Rais Moi alipokuwa anahutubia umati katika uwanja wa wilaya ya Kirinyaga. Amekuwa kinara anayeongoza katika upanuzi wa nafasi ya demokrasia na masuala ya kijinsia nchini Kenya. Amekuwa akipigania haki za wanawake kupitia maslahi ya umma, ushawishi na utetezi kwa kuboresha sheria na kulinda haki za wanawake kupitia kazi yake pamoja na mashirika mbalimbali ya wanawake, hasa Shirikisho la Kimataifa la Wanasheria Wanawake (Fida-Kenya) na Ligi ya wapiga kura Wanawake wa Kenya.
Mnamo Februari 2009 wakati wa muda wake kama Waziri wa Sheria, wakati mmoja alikuwa na ugomvi mkali na Waziri wa Kilimo, William Ruto katika mkutano wa Baraza la Mawaziri huku Rais Kibaki akiwa amekaa kimya, mawaziri wakitazama vinywa wazi, chanzo katika mkutano kilisema. "Rais hakusema au kufanya lolote. Aliketi kimya akitazama mawaziri hawa wakizozana. Hali ilikuwa imechemka na moto. Mawaziri hawa wawili walikuwa wakigombana mbele ya umma kwa muda zaidi ya wiki tatu, huku Bibi Karua akidai kuwa Ruto ajiuzulu kufuatia kashfa ya mahindi. Alijulikana kama "mwanamme pekee" katika baraza la mawaziri la PNU.

Maisha binafsi:
Martha Karua alipata misukosuko wakati yeye na padri wa Kikatoliki, Dominic Wamugunda, walipotekwa nyara na kuibiwa tarehe 6 Desemba, 2003. Aliliambia Bunge kwamba hakuwa na wajibu wowote wa kutoa maelezo yoyote kwa nini alikuwa katika gari la Wamugundai au nini alichokuwa anafanya wakati wakitekwa nyara. Walinzi wake wa Usalama hawakuwepo wakati wa uhalifu huo; Karua alisema kuwa wakati ambao anaona hahitaji ulinzi wa askari yeye hawatumii. Martha Karua alipewa talaka na mumewe.

Matumaini:
Martha Karua ametangaza kuwa atagombea urais mwaka wa 2012 na ana matumaini ya kuibuka mshindi.

Kutambuliwa:
Mwaka wa 1991, Karua alitambuliwa na Shirika la Haki za Binadamu (Human Rights Watch) kama mchunguzaji wa haki za binadamu. Desemba mwaka wa 1995 alituzwa na Shirikisho la Wanasheria Wanawake Kenya (Fida) kwa ajili ya kuendeleza mwendo wa wanawake. Mwaka wa 1999 Kenya Section of the International Commission of Jurists ilimtuza tuzo ya mwaka 1999 ya mwanasheria bora na katika mwaka huohuo mwezi huohuo, Law Society of Kenya (LSK) ilimtuza tuzo la Legal Practitioners Due Diligence.

No comments:

Post a Comment