May 11, 2011

Kama semina elekezi isipozaa matunda mawaziri hawa kwanini wasirudi shule?

 Rais Jakaya Kikwete

Chati inayoonesha Baraza la Mawaziri la Tanzania

BISHOP J. HILUKA
Dar es Salaam

MWEZI uliopita nchi yetu ilishuhudia mkutano mkubwa uliopewa jina la Jukwaa la Uwekezaji. Nikiwa mmoja wa wafuatiliaji nilisoma gazeti la Mwananchi la 19/04/2011 na kukumbana na kichwa cha habari kilichonishtua sana: “Wakili ataka mawaziri warudi darasani”. Habari iliyoambatana na maelezo haya, nanukuu:
Wakili wa Kampuni ya FB Attorneys, Fayaz Bhojani jana alitoa mpya katika Jukwaa la Uwekezaji Afrika, lililoanza jijini Dar es Salaam, baada ya kueleza kuwa Mawaziri wa Serikali za Afrika Mashariki ikiwamo Tanzania, hawana uelewa wa kutosha hivyo wanatakiwa kusoma.

Akichangia hoja katika mkutano huo uliohudhuriwa pia na marais wa nchi hizo, Bhojani alisema mawaziri hao wameshindwa kutekeleza ahadi zao kwa wananchi.

Mawaziri wetu wanatakiwa kurudi shuleni wakasome kwa sababu wanayoyaahidi hawayatekelezi na wakirudi siku nyingine, wanarudia tena kuahidi. Nadhani wanahitaji kwenda shule. Serikali ziwapeleke shule,” alisisitiza Bhojani.

Rais Nkurunzinza ambaye ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa hilo alikuwa wa kwanza kuwajibia mawaziri wake tuhuma hizo kwa kusema: “Mawaziri hawawezi kupelekwa tena shuleni kwa sababu walishamaliza masomo yao.” Kauli hiyo ya Rais Nkurunzinza iliungwa mkono na Rais Kikwete aliyesisitiza kuwa mawaziri hawawezi kurudishwa shuleni.

Habari hiyo ikanikumbusha jinsi wawekezaji katika nchi hii wanavyopewa miaka kumi bure ya kuchimba vito vya thamani kwa mikataba wanayoingia wakati nchi ina matatizo lukuki.

Lakini wiki hii kwa hiki kilichofanyika huko Dodoma katika Semina Elekezi kwa Viongozi na Watendaji Wakuu wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, semina iliyolizika jana Alhamisi imenifanya niyatafakari tena maneno na wakili Bhojan japo yalionekana kupingwa na Rais Kikwete ambaye hata hivyo wiki hii ameyaunga mkono kwa kuwarudisha darasani mawaziri wake.

Pamoja na mengi lakini Rais Kikwete alionekana kukazia zaidi mambo haya:

-Marufuku Mawaziri kutoelewana;
-Mawaziri wakishakubaliana katika Baraza la Mawaziri ni uamuzi wa wote;
-Ukiona ni vigumu kuafiki ni bora kutoka;
-Lazima kutekeleza uwajibikaji wa pamoja;
-Hata miswada ya sheria bungeni ni ya mawaziri wote;
-Ni kinyume cha maadili Waziri kupinga muswada wa Waziri mwenzake;
-Lazima wawe '
team players';
-Kuhudhuria vikao vya Bunge kwa Mawaziri ni lazima;
-Marufuku kutembelea jimbo wakati wa vikao;
-Katika kikao cha Bunge hatutegemei Waziri kuwa na safari zitakazomuondoa bungeni;
-Kuna udhaifu mkubwa katika kusema mafanikio yaliyopatikana;
-Wakifanya kitu bila kukieleza ni sawa na kwamba hawakukifanya;
-Wananchi wanalaumu serikali kutokana na kuelezwa uongo dhidi yake;
-Wawe wepesi kusahihisha uongo dhidi ya serikali, raslimali zipo, vyombo vya habari vipo, hawavipi habari;
-Kila Wizara kuna wasemaji, hawasemi, wasemaji wengine wanazuiwa kusema;
-Maafisa Habari wapewe fursa waitumie taaluma yao, wao wanajua; wasilaumu kwamba vyombo haviwataki;
-Lazima serikali iwasiliane na watu wake kupitia vyombo vya habari;
-Kama ulikubali kuwa Waziri ni lazima uitumikie, tafuta muda muafaka wa kuhudumia jimbo;
-Mawaziri wengine wanaongozana na kundi la waandishi wa habari majimboni;
-Uadilifu ni muhimu sana: Waziri, Naibu, Katibu Mkuu wanatakiwa kuwa mfano mwema. Mawaziri, Naibu wasinyooshewe vidole. Wasifike saa 5 na kuondoka saa 7 mchana, waache uzembe, wizi, 'michongo', kutumia ofisi kujinufaisha, ulevi, uzinzi wala ubabe;
-Haiwezekani kunywa kwenye baa mpaka wanataka msaada wa kubebwa;
-Ukiwa waziri ni kuwa kuna baadhi utavikosa. Unakatisha wananchi tamaa, waache ubabe, wanadhulumu watu;
-Utelezaji wa ilani kwa miaka mitano nyuma. Mipango ya baadaye na kadhalika katika kuwatumikia wananchi. Kilimo, afya, miundombinu kuboreshwa katika kutekeleza
vision ya 2025;
-Itafika wakati umeme utakuwa haukatiki;
-Bado kuna makosa mengi, kuna upotevu wa fedha za umma
-Kuna maendeleo fulani lakini hayatoshi;
-Watapate kusikiliza kutoka kwa watendaji wa vyombo vya dola kuhusu jitihada zinazofanywa na idara zao;
-Hali ya kupunguza msongamano wa wafungwa, usalama, udhibiti wa madawa ya kulevya na Takukuru;
-Kila Wizara iandike kueleza mafanikio katika wizara yake, ifanye tathmini ili kuhifadhi kumbukumbu kwa vizazi vya baadaye.

Alichokisema Rais Kikwete ni sawa lakini kuna jambo moja la kushangaza: ni kwa nini Kikwete aitishe semina elekezi mjini Dodoma wakati alishatembelea wizara zote? Kwa nini hakuelekeza mambo hayo huko huko kwenye wizara zao wakati alipozitembelea?

Inashangaza pia kwa rais ambaye ndiye mwenyekiti wa CCM, chama kilicho kwenye harakati za kujivua gamba la ufisadi kwa kuwatosa viongozi wenye tuhuma za ufisadi na matumizi mabaya ya pesa za Watanzania, kwamba yeye haoni kama huu nao ni aina nyingine ya ufisadi kwa kutumia pesa za Watanzania vibaya!

Inasikitisha sana kuona nchi yetu inavyoendeshwa na kuhujumiwa na watu wachache tuliowapa dhamana ya kulinda rasilimali zetu. Watu ambao wanatumia kodi za wananchi wanyonge kwa kile wanachokiita “Semina Elekezi”.

Sielewi hii maana yake ni nini hasa? Au maana yake ni kwamba wananchi masikini waendelee kuteseka kwenye umasikini wakati wakubwa wao kila siku wanafikiria jinsi ya kutumia fedha za umma?

Semina hii pia imeniacha na maswali mengi: je, ni kweli wateule hawa wa rais ni watu wasioelewa majukumu na kazi zao? Je, wale waliopata semina elekezi kule Ngurudoto mara tu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza amewaweka kwenye fungu lipi?

Pia najiuliza kama rais alishafanya tathmini ya semina elekezi ya Ngurudoto ili kujua mapungufu na faida zake kabla hajatoa semina nyingine?

Nafikiri mapendekezo haya ya rais yangeenda sambamba na kuliangalia upya Baraza la mawaziri ambalo kwa mtazamo wangu ni kubwa na halina kazi za kufanya. Mfano Waziri wa Maji, Waziri wa Kilimo na Ushirika, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Waziri wa Mazingira, Waziri wa Ardhi Nyumba na Makazi, bado sijaelewa mipaka yao ya kazi ili wasiingiliane kwenye majukumu yao. Labda kwenye hili rais alipaswa kuliweka sawa ili kuepuka migongano.

Mfano kama kuna eneo lina mgogoro wa wakulima, wafugaji na mbuga za wanyama ina maana wote watatu wawepo?

No comments:

Post a Comment